Manny Pacquiao: Nyota wa ndondi anayewania urais Ufilipino

Philippine Senator and boxer Manny Pacquiao

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Manny Pacquiao ni bondia pekee aliyeshinda ubingwa wa dunia mara nane

Nyota wa masumbwi kutoka nchini Ufilipino Manny Pacquiao atangaza nia ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaofanyika mwakani.

Kundi dogo ndani ya chama tawala cha PDP-Laban kimeonesha utayari wa kumtaka kupeperusha bendera.

Ukiachana na kazi yake ya masumbwi, Bw Pacquiao, 42, ni seneta katika bunge la Ufilipino.

Kwasasa Ufilipino inaongozwa na Rais Rodrigo Duterte ambaye amezuiliwa kugombea muhula mwingine.

Pacquiao ambaye anashindanishwa na Christopher "Bong" Go, lakini Bwana Go anasema hataki kumrithi Bw Duterte.

Ikiwa bado chama chake kinaonesha nia ya kumpendekeza Bw Go, lakini bado wanaendelea kumshawishi ili afikirie tena uamuzi wake, kukataa kwake uteuzi huo kumesababisha maoni kwamba binti wa Rais Duterte anaweza kujiunga naye kwa nafasi hiyo.

Haijulikani ni yupi kati ya vikundi vipi vya PDP-Laban vitakavyotambuliwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kwa uchaguzi wa 2022.

Je itakuwa kazi rahisi kwa Pacquiao kuingia Ikulu?

bondia

Chanzo cha picha, Getty Images

Disemba 2020 aliukwaa urais wa chama cha Rais Duterte, cha PDP-Laban, na anaonekana kuitumia fursa hiyo ingawa kwa muda mfupi kujiweka sawa kwenye uchaguzi ujayo.

Na Bondia huyo anaonekana kama mtu muhimu kwenye siasa za nchi hiyo . Kuna wakati Duterte, alitoka hadharani na kusema bondia huyo anamuona kama "rais ajaye wa Ufilipino".

Duterte, kikatiba anaruhusiwa kuwania kipindi kimoja cha miaka 6, na inaelezwa huenda akakutana na mkono wa sheria atakapoachia madaraka, kutokana na tuhuma mbalimbali.

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) inamtuhumu Rais huyo kwa uhalifu dhidi ya binadamu, na kwamba mahakama hiyo huenda ikaamuru akamatwe.

Watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakimpinga rais huyo hasa kupitia vita yake dhidi ya dawa za kulevya" , ambao pia wameeleza watamshitaki kwa tuhuma hizo hizo, mara tu baada ya kutoka madarakani na kukosa kinga ya kushitakiwa.

Sara Duterte, binti wa Rais Duterte anayepigiwa chapuo la kuwania urais wa
Maelezo ya picha, Sara Duterte, binti wa Rais Duterte anayepigiwa chapuo la kuwania urais wa Ufilipino

Kwa sababu hana uwezo wa kuwania awamu nyingine, Duterte alisema anataka kuwania umakamu wa rais, na kwa namna anavyoonekana angependa nafasi ya urais iende kwa mmoja wa watu wa familia yake na labda ikishindikana kwa watu wake wa karibu sana, ili kuendelea kuwa salama na tuhuma zinazomkabili akiamini atalindwa na rais.

"Rais ana wasiwasi na mtu yeyote ambaye sio binti yake akiwania urais na kushinda, Rais anajua kwamba atashitakiwa kwenye mahakama ya ICC," alisema Puentevella.

Hofu hii huenda ikamnyima usingizi Pacquiao, anayeutaka urais na huenda ikawa ni kikwazo kikubwa , kwa sababu Ras Duterte ana nguvu kubwa na mbinu za kufanya analoweza ili jambo lake litimie.

"kwa sasa anataka kuhakikisha kuwa, haendi jela, kwa hivyo hakuna mtu wa kumsaidia hilo isipokuwa ni binti yake tu."