Benki ya Dunia yaahirisha kupigia kura ya mkopo wa elimu kwa Tanzania

Magufuli na Dkt Hafez Ghanem

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Maelezo ya picha, Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt Hafez Ghanem walifanya mazungumzo Ikulu, Dar es Salaam Novemba 2018
    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Africa, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Benki ya Dunia imeahirisha kupiga kura kuhusu mkopo wa dola milioni 500 kwa Tanzania zilizokuwa zikilenga miradi mbalimbali ya elimu.

Kura hiyo ilikuwa inatarajiwa kupigwa leo, lakini tayari kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya benki hiyo iidhinishe mkopo huo kwa Tanzania ama la.

Taarifa za kuahirishwa kwa kura hiyo imekuja siku chache baada ya shinikizo kutoka kwa wanaharakati wa Tanzania na wa kimataifa waliokuwa wakiitaka benki hiyo isitoe mkopo huo kwa serikali kutokana na kile walichokiita kuwa ni sera na sheria ya elimu ya kibaguzi.

Kwa mujibu wa nyaraka za Benki ya Dunia, pamoja na mambo mengine, mkopo huu ulikusudiwa kwenda kusaidia upatikanaji wa elimu bora na kwa urahisi kwa wanafunzi waliokuwa wanarudi shule baada ya kuwa wamepata ujauzito.

Lakini mradi huu wa elimu ulikuwa ni kupitia elimu mbadala na si katika mfumo rasmi.

Kipengele ndicho kinachozua utata kiliwasukuma wanaharakati wa Tanzania kuiandikia bodi ya utendaji ya Benki ya Dunia ikiwa benki hiyo itaipa Tanzania mkopo huo, kabla ya nchi hiyo haijaahidi kuondoa sera na kipengele cha sheria kinachowakataza wanafunzi wa kike kurudi shuleni baada ya kujifungua, basi benki itakuwa imekubaliana na sera na sheria hiyo ambayo wanaharakati wanaiita ya kibaguzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN la nchini Marekani, hakuna sababu rasmi iliyotolewa kuhusu kuahirishwa kwa kura hiyo japo inaripotiwa kuwa uongozi wa benki hiyo ulifanya kikao cha dharura na wanaharakati wa haki za binaadamu kutoka Tanzania na mashirika ya kimataifa jana Jumatatu.

Sheria ya elimu ya Tanzania imebeba kipengele za nidhamu ambacho kinaipa mamlaka uwezo wa kuwafukuza shuleni wasichana wanafunzi wanaogundulika kuwa na ujauzito.

Benki ya Dunia na Tanzania

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha, Ujumbe wa Benki ya Dunia ulikutana na ujumbe wa serikali ya Tanzania mwezi Novemba 2018 jijini Dar es Salaam juu ya mustakabali wa mkopo huo.

Katika baadhi ya shule nchini Tanzania, walimu ama na maofisa wengine wa shule wamekuwa wakiwapima ujauzito kwa lazima wanafunzi wasichana.

Kwa mujibu wa nyaraka za Benki ya Dunia, wanafunzi wa kike zaidi ya 5000 walisimamishwa masomo nchini Tanzania mwaka 2017 baada ya kukutwa na ujauzito.

Ruka X ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 1

Ruka X ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 2

Sheria inayowapa mamlaka shule kuwapima wasichana na kuwafukuza shule ikiwa watakutwa na ujauzito ni ile ya elimu ya mwaka 2002, ambayo ilitungwa kwanza miaka ya 1960.

Wanaharakati wa haki za mtoto wa kike wanadai kwamba hata kama sheria hii iliyopitwa na wakati imekuwepo kwa muda mrefu, ni wakati wa uongozi wa Rais Magufuli ambapo maofisa wengi wa elimu wamekuwa wakiitekeleza kwa bidi.

Rais Magufuli amewahi kuweka msimamo wake hadharani kwamba mwanafunzi anapopata ujauzito hataruhusiwa tena kurudi shuleni.

'Hakuna mwenye mimba atakayerudi shuleni. Amechagua hayo maisha ya mtoto, akalee vizuri mtoto",alisema Rais Magufuli.

Katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa serikali kuwapuuza wakosoaji na wanaotaka Benki ya Dunia kuinyima Tanzania mkopo huo.

"Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia alikuja hapa mwaka jana, na wanatoa pesa wakijua tuna misimamo gani na tunafanya nini, hao wengine ni wapiga kelele tu tu, wala msiwajibu", alisema Rais Magufuli.

Mustakabali wa mkopo huo umekuwa ukisuasua toka mwaka 2018 ambapo uongozi wa Benki ya Dunia ulikataa kupitisha mkopo huo (ambao awali ulikuwa dola milioni 300).