Watu 39 wafa baada ya jumba kulipuka Idlib Syria

Mlipuko waua watu 39 Syria
Maelezo ya picha, Mlipuko waua watu 39 Syria

Taarifa kutoka nchini Syria zinasema kuwa raia 39 wakiwemo watoto 12 wameuawa katika mlipuko ulioangusha jengo moja katika jimbo linalokaliwa Waasi la Idlib eneo la Sarmada.

Haijajulikana mara moja nini kilichosababisha mlipuko huo.

Ndani ya jumba hilo lililopuka imebainika kuwa kulikuwa kumehifadhiwa silaha mbalimbali na waliokuwemo wengi wao ni raia wa Syria ambao,wanatoka katika maaneo mbalimbali ndani ya taifa hilo.

Hatem Abu Marwan yeye ni mmoja wa watu ambao wapo na kikosi cha ulinzi cha Idlib.

"Ni mlipuko ambao chanzo chake hakifahamiki.Vikosi vya ulinzi kutoka Idlib na Aleppo vilipofika eneo la tukio vilishangazwa na uharibifu mkubwa katika jingo hili na madhara yaliyotokea. Jumba kubwa lililo jaa watu limesambaratika na kuwa dogo kama tofali".

Wakati huo huo waangalizi wa haki za binadamu wa Uingereza waliopo nchini Syria wanasema kuwa bado kuna watu kadhaa ambao hawajulikani walipo, huku wengine wakisema idadi ya waliokufa huenda ni kubwa Zaidi ya iliyotajwa.

Wengi waliokuwa wakiishi katika jumba hilo, lililobomoka wanaaminika kuwa ni familia za wapiganaji wenye msimamo mkali waliokimbilia katika mji wa Idlib kutoka maeneo mengine yanayodhibitiwa na vikosi vya serikali ndani ya Syria.