Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Israel yashambulia maeneo ya Hezbollah kusini mwa Lebanon

Ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi ya angani kusini mwa Lebanon, yakilenga ghala la silaha la Hezbollah na kiwanda cha kutengenezea silaha.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi, Yusuf Jumah and Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo tukutane tena hapo kesho.

  2. Habari za hivi punde, Bunge la Ghana laidhinisha muswada tata unaopinga mapenzi ya jinsi moja,

    Bunge la Ghana limepitisha kwa kauli moja muswada tata wa kupinga mapenzi ya jinsia moja ambao unaamuru kifungo cha miaka 3 jela kwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja na kifungo cha miaka mitano kwa kuendeleza shughuli za LGBTQ+.

    Sheria hiyo imekosolewa vikali kwa kukiuka haki za watu wachache wa jinsia moja nchini humo.

    Ghana ni nchi ya hivi karibuni ya Afrika kutunga sheria ya kupinga mapenzi ya jinsi moja baada ya Uganda. Sheria hiyo mpya inatoa adhabu kali, hadi kifungo cha miaka 10, kwa kuchapisha nyenzo zinazolenga watoto na kupiga marufuku shughuli za ufadhili.

    Pia inawahimiza raia wa Ghana kuripoti kwa polisi, wakati waandishi wa habari wanaweza kuwa hatarini ikiwa ripoti zinachukuliwa kuwa za kuunga mkono mapenzi ya jinsi moja na watu wa jamii ya LGBTQ +.

    Mswada huo uliwasilishwa katika bunge la Ghana mnamo Agosti 2021 lakini ulikosolewa sana.

    Wale wanaopinga sheria hiyo wanasema sheria hiyo itakiuka haki na uhuru wa watu wachache wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja.

    Lakini wanaounga mkono mswada huo wanasema utasaidia kuhifadhi maadili ya familia ya Ghana. Sheria hiyo inaanza kutekelezwa baada ya rais Nana Akufo Addo kutia saini.

  3. Beatrice Munyenyezi: Mwendeshamashtaka aomba mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari Rwanda afungwe maisha,

    Beatrice Munyenyezi alishtakiwa kwa makosa ya uhalifu yakiwemo mauaji ya kimbari na uchochezi wa wa ubakaji dhidi ya wanawake wakati wa mauaji ya kimbari katika mji wa Butare kusini mwa Rwanda.

    Munyenyezi alifukuzwa nchini Marekani mwaka wa 2021 kwa kosa la kusema uongo kwa mamlaka ya uhamiaji. Munyenyezi anakana mashtaka na kuomba aachiliwe.

    Wakili wake Bw. Bruce Bikotwa alisema mashahidi hao wamekuwa na kauli zinazokinzana katika maelezo yao mahakamani. Kuna shahidi aliyesema kuwa ‘’ Munyenyezi hakuwa mjamzito wakati wa mauaji ya kimbari ‘’wakili amesema huo ni uongo kwani wana hati inayoonyesha wakati alipojifungua mapacha kama uthibitisho kuwa alikuwa mjamzito wakati wa mauaji ya kimbari.

    Ni wakati baadhi ya mashahidi walisema wakati wa mauaji ya kimbari, Mshtakiwa alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rwanda kilichopo Butare, mawakili wake walieleza kuwa alifukuzwa Shule ya Sekondari ya Gitwe kwa kuwa alikuwa mjamzito na baadaye akajiunga na shule iitwayo CEFOTEC iliyoko katika mji huo wa kusini ambako alisomea kwa mihula miwili kabla ya mauaji ya kimbari kuanza.

    Mawakili wake waliiomba mahakama kubatilisha ushahidi dhidi yake kwa sababu ulikuwa "msingi wa hadithi za uwongo".

    Upande wa mashtaka ulisema kuwa ushahidi dhidi ya Munyenyezi ni halali na kubainisha jukumu lake katika kuwaua Watutsi katika mji wa Butare. Miongoni mwao walikuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rwanda ambacho alikuwa jirani nao.

    Munyenyezi anatuhumiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na mauaji, na kuwahimiza waliofanya mauaji kuwabaka wanawake na wasichana wa Kitutsi.

    nakanusha uhalifu huo na kusema kuwa anashutumiwa hasa kwa sababu ya familia ya mme wake.

    Upande wa mashtaka uliomba hukumu ya kudumu jela, na walalamikaji wataifuatilia.

    Akizungumzia kuhusu adhabu iliyoombwa na Munyenyezi alisema: “Naomba haki kutendeka akisema yeye siyo miongoni mwa wanaokana mauaji ya kimbari na wala hakuwa na jukumu lolote katika mauaji hayo.na kusisitiza kuwa ‘’kama familia ya mme wangu ilitenda dhambi nisiadhibiwe kwa dhambi zao’’.

    Munyenyezi, 54, aliolewa na Shalom Ntahobari, ambaye yeye na mama yake Paulina Nyiramasuhuko ambaye alikuwa Waziri wa Familia mwaka 1994 wote walifungwa Arusha, Tanzania baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mauaji ya kimbari.

    Hakimu alitangaza kuwa uamuzi wa kesi hiyo utatangazwa Machi 27.

  4. Thamani ya Bitcoin imeongezeka kwa siku ya tano mfululizo na kukaribia dola 60,000

    Thamani ya pesa ya mtandaoni Bitcoin imeongezeka kwa siku ya tano mfululizo na kufikia dola za kimarekani 59,000 kwa dola moja ya kimarekani. Ongezeko kama hilo halijawahi kutokea tangu Disemba 2021.

    Marekani hivi karibuni imetoa ruhusa kwa Bitcoin kutumika katika eneo maalumu la kibiashara - ili kuwezesha manunuzi katika soko la kawaida. Uamuzi huu unaruhusu makampuni ya uwekezaji kuwekeza mali katika Bitcoin.

    Kwa mujibu wa jukwaa la CoinGeco, thamani ya bitcoins katika mzunguko wa Februari ilikuwa zaidi ya dola bilioni 2000, ambayo haijawahi kutokea katika miaka miwili iliyopita.

    Thamani ya sarafu hii imeimarika kwa takriban 47% katika mwezi huu wa Februari.

  5. Israel yashambulia maeneo ya Hezbollah kusini mwa Lebanon

    Ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi ya angani kusini mwa Lebanon, yakilenga ghala la silaha la Hezbollah na kiwanda cha kutengenezea silaha.

    Ni baada ya Hamas ya Lebanon kurusha makombora katika vituo viwili vya kijeshi vya Israel kaskazini mwa Israel.

    Makabiliano ya karibu kila siku ya kurushiana makombora kati ya vikosi vya Israel na Hizbullah ambayo inaungwa mkono na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yameongezeka hivi karibuni, jambo ambalo limezusha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutanuka kwa mzozo huo.

  6. Mwanamfalme Harry apoteza pingamizi la Mahakama Kuu kuhusu viwango vya usalama wake Uingereza

    Mwanamfalme Harry amepoteza pingamizi la Mahakama Kuu dhidi ya serikali kuhusu kiwango cha usalama wake alipokuwa nchini Uingereza.

    Duke wa Sussex alishindwa kugeuza uamuzi wa mahakama ambao ulishusha hadhi yake ya usalama baada ya kuacha kazi ya kifalme.

    Mahakama Kuu iliamua kuwa uamuzi huo haukuwa kinyume cha sheria wala hauna mantiki.

    Mwanamfalme Harry atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo na "anatumai atapata haki", msemaji wa sheria alisema.

    Mawakili wake walikuwa wamepinga kuwa jinsi uamuzi huo ulivyofanywa haukuwa wa haki.

    Alianza kuikosoa hatua hiyo ya kisheria baada ya kuambiwa kuwa hatapewa tena kiwango sawa cha ulinzi unaofadhiliwa na umma akiwa nchini.

    Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema usalama wake katika ziara za Uingereza unapaswa kuamuliwa kwa msingi wa hali baada ya hali, na Jumatano ilisema "imefurahishwa" na matokeo ya mahakama.

    Wakijadili hoja yao dhidi ya ukosoaji wa Duke, mawakili wa Wizara ya Mambo ya Ndani waliiambia Mahakama Kuu kwamba Mwanamfalme Harry bado atakuwa na usalama wa polisi unaofadhiliwa na umma, lakini hii itakuwa "mipango ya kawaida, iliyoundwa mahsusi kwake", badala ya usalama wa moja kwa moja unaotolewa kwa familia ya kifalme wa wakati wote.

    Uamuzi huo unaweza kuwa na athari kwa ziara za baadaye za Duke nchini Uingereza, kwani hapo awali alisema kuwa kiwango cha chini cha usalama kimefanya iwe vigumu kuleta familia yake nchini humo.

  7. Mjane wa Alexei Navanly: Mume wangu hataona Urusi nzuri ya siku zijazo

    Mjane wa aliyekuwa mpinzani mkuu wa Rais Putin, Yulia Navalnaya ameliambia Bunge la Ulaya kwamba lazima wapigane na "genge hili la uhalifu" na anasema kwamba uchunguzi wa kifedha badala ya mbinu za kidiplomasia utakuwa muhimu.

    Anasema kwamba "makumi ya mamilioni ya Warusi" wanampinga Putin na hawapaswi kuteswa.

    Navalanaya anaongeza kuwa Putin lazima ajibu kwa kile alichofanya kwa Urusi, Ukraine na mumewe.

    "Putin lazima ajibu kwa kile alichoifanyia nchi yangu. Putin lazima ajibu kwa kile alichofanya kwa nchi jirani, mwenye amani. Na Putin lazima ajibu kwa kila kitu alichomfanyia Alexei," anasema.

    Akimalizia kwa kumuenzi Navalny, aliongeza: "Mume wangu hatawahi kuona jinsi Urusi nzuri ya siku zijazo itakavyokuwa, lakini lazima tuione. Na nitafanya kila niwezalo kutimiza ndoto yake, uovu huo utashindwa na mustakabali huu mzuri utakuja."

    Wabunge walimshangilia alipomaliza hotuba yake.

    'Kumshinda Putin haupaswi kuchoka'

    Alexei aliwaongoza watu licha ya vizuizi ambavyo Putin alimwekea wakati wa maisha yake, Navalnaya anaendelea.

    Alipokatazwa kwenye TV, aligeukia Youtube. Aliponyimwa kura alikuja na mkakati wa kukiondoa chama cha Putin.

    "Hata katika gulag (nfumo wa Usovietiwa kambi za vizuizi na magereza ya muda)ya Putin, Alexei aliweza kupitisha mawazo ya miradi ambayo ingefanya Kremlin kuwa na hofu," anasema.

    Navalnaya anasema kumshinda Putin kunahitaji kuwa mvumbuzi.

    Anaonya kwamba Putin hawezi kuumizwa na vikwazo au maazimio, au kwa misingi ya maadili na sheria.

    "Hili ndilo jibu la swali. Ikiwa kweli unataka kumshinda Putin, lazima uwe mvumbuzi. Na lazima uache kuchoka.

    "Huwezi kumuumiza Putin kwa azimio lingine au vikwazo vingine ambavyo havina tofauti na vilivyotangulia. Huwezi kumshinda kwa kudhani ni mtu wa kanuni na mwenye maadili na sheria.

    Unaweza pia kusoma:

    • Matukio: Kwa nini Navalny alikuwa mpinzani mkuu wa Putin?
  8. DRC: Umoja wa Mataifa waanza kuondoa kikosi chake MONUSCO

    Umoja wa Mataifa umeanza kuondoa vikosi vya kulinda amani vya MONUSCO Jumatano kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kukabidhi kituo cha kwanza cha Umoja wa Mataifa kwa polisi wa kitaifa, AFP imeshuhudia.

    Wakati wa sherehe rasmi katika kambi ya Kamanyola, karibu na mipaka ya Rwanda na Burundi, bendera za Umoja wa Mataifa na Pakistan, nchi za asili za walinda amani wanaosimamia amani zilibadilishwa na zile za DRC.

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetaka kuondolewa kwa wanajeshi hao licha ya wasiwasi wa Umoja wa Mataifa kuhusu ghasia zilizokithiri mashariki mwa nchi hiyo.

    Kinshasa inalichukulia jeshi la Umoja wa Mataifa kama lisilo na ufanisi katika kuwalinda raia dhidi ya makundi yenye silaha na wanamgambo ambao wamepiga mashariki mwa nchi hiyo kubwa kwa miongo mitatu.

    Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura mwezi Disemba ili kuharakisha matakwa ya Kinshasa ya kutaka kuondolewa kwa taratibu kwa ujumbe wa MONUSCO, ambao uliwasili mwaka 1999.

    Kikosi cha Umoja wa Mataifa kwa sasa kina wanajeshi 13,500 na polisi 2,000 katika majimbo matatu ya mashariki ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini.

    Kabla ya mwezi Mei, kikosi cha Umoja wa Mataifa kitaondoka katika kambi zake 14 katika jimbo hilo na kuvikabidhi kwa vikosi vya usalama vya DRC.

  9. Ghasia za wanamgambo zasababisha vifo vya watu 58,000 kaskazini mwa Msumbiji

    Zaidi ya watu 58,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na wimbi la mashambulizi ya wanamgambo yaliyorekodiwa katika jimbo la kaskazini mwa Msumbiji la Cabo Delgado mwezi Februari.

    "Katika taarifa yake ya kila wiki, shirika la ndani la serikali (Shirika la Kimataifa la Uhamiaji) lilisema kuwa mashambulizi hayo yaliyotokea kuanzia Februari 8 hadi Februari 25, hasa katika wilaya za Chiure na Macomia, yalisababisha vifo vya watu 54,534 na watu 2,626 mtawalia, hususan watoto (35,295)," TV Sucesso inayomilikiwa na watu binafsi iliripoti Jumanne.

    Mamlaka za eneo hilo zimesema wengi wa watu waliokimbia makazi yao walitafuta hifadhi katika jimbo jirani la Nampula huku wengine wakikimbilia katika mji mkuu wa Cabo Delgado, Pemba.

    Wilaya za kusini mwa Cabo Delgado zimerekodi ongezeko la shughuli za wanamgambo katika wiki chache zilizopita, huku vyombo vya habari vya ndani vikiiunganisha na kampeni ya "waue popote unapowapata" iliyoanzishwa na kundi la Islamic State mnamo Januari 4.

    Wakati huo huo, polisi wameelezea hali kwa sasa kama ya "utulivu lakini tete" na kuhakikisha kuwa vikosi vya usalama vinafanya kazi kurejesha amani katika eneo hilo.

  10. Tshisekedi 'alikubali kukutana na Kagame' – Angola

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasema kuwa Rais Félix Tshisekedi "amekubali kukutana na mwenzake wa Rwanda" katika mazungumzo yenye lengo la kusuluhisha vita mashariki mwa Kongo.

    Katika mtandao wa kijamii wa X, ofisi ya rais wa Congo inarudia maneno ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Tete António:

    "Rais Félix Tshisekedi amekubali kukutana na mwenzake wa Rwanda."

    Serikali ya Rwanda na serikali ya Angola hazikuwa zimetangaza chochote rasmi.

    Nchi mbalimbali ziliendelea kuwaomba viongozi wa nchi hizo wakutane na kujadili utatuzi wa mgogoro huo.

    Mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa akifanya kampeni, Tshisekedi alisema atazungumza tena na Kagame” tu mbele ya Mungu ambaye atatuhukumu sisi".

    DRC ilisema hayo baada ya mkutano wa saa tatu siku ya Jumanne mjini Luanda, kwa mwaliko wa mpatanishi, Rais wa Angola, João Lourenço, ambaye ni mpatanishi katika mzozo huo.

    Ofisi ya rais wa RD Congo inarudia maneno ya Waziri António akisema kwamba kitakachofuata ni kwamba utaratibu huo unafanya kazi katika ngazi nyingine kuhakikisha mkutano huo unafanyika.

    Mwezi huu nchini Ethiopia, Lourenço alikuwa amekutana na Rais wa Rwanda Paul Kagame na Tshisekedi, kila mmoja tofauti, kama ilivyoripotiwa na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kando na mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika.

    Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa wiki iliyopita, Tshisekedi alisema kuwa mtu pekee ambaye anataka kuzungumza naye ni Rais Kagame, kwamba hawezi kwenda kwenye mazungumzo na kundi la waasi la M23.

    Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) na DRC wanaishitumu Rwanda kwa kusaidia harakati ya M23 dhidi ya serikali ya Kinshasa, mashtaka ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.

    Serikali ya Rwanda na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa pia inaishutumu Congo kwa kufanya kazi na kundi la waasi wa Rwanda wanaoendesha harakati zao mashariki mwa Congo (FDLR), ambao Rwanda inadai walihusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na wenye hila dhidi ya serikali ya Rwanda. DRC pia inakanusha madai hayo.

  11. Tazama: Ndege ilivyoepuka kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Heathrow kwa sababu ya upepo mkali

    Ndege iliyokuwa ikiruka katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow ililazimika kuacha kutua wakati wa upepo mkali.

    Video inaonyesha ndege ya abiria ya British Airways ikiyumba-yumba na kukaribia njia ya kurukia ndege karibu upande mmoja, kabla ya kupaa tena.

    Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea London kutoka Berlin na ilifanikiwa kutua katika jaribio lake la pili.

  12. Nigeria yaanzisha tozo ya kila mwaka kwa wafanyakazi wa kigeni

    Nigeria imeanzisha ushuru wa lazima wa kila mwaka kwa mashirika yanayoajiri wafanyikazi kutoka nje, inayowahitaji kulipa $15,000 (£12,000) kwa watu wenye cheo cha mkurugenzi na $10,000 kwa vitengo vingine..

    Hatua hiyo inakusudiwa kuhimiza makampuni ya kigeni kuajiri wafanyakazi zaidi wa Nigeria.

    Wafanyikazi wa balozi za kidiplomasia na maafisa wa serikali hawatahitajika kulipa tozo hiyo.

    Rais Bola Tinubu ameonya kuwa ushuru huo haufai kutumika kuwakatisha tamaa wawekezaji watarajiwa.

    Alizungumza wakati akizindua kitabu cha Mwongozo cha Ushuru wa Ajira kwa Wageni (EEL) Jumanne, na kuongeza kuwa serikali inatarajia kuboresha mapato na ukuzaji.

    Alisema kuwa lengo lake lilikuwa kusawazisha fursa za ajira kati ya Wanigeria na wahamiaji kutoka nje.

    "Lengo ni kuziba mapengo ya mishahara kati ya wahamiaji kutoka nje na nguvu kazi ya Nigeria huku ikiongeza nafasi za ajira kwa Wanigeria waliohitimu katika makampuni ya kigeni nchini," alisema.

  13. Mauaji ya AKA: Washukiwa sita wakamatwa kwa mauaji ya rapa wa Afrika Kusini

    Washukiwa sita wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya rapa maarufu wa Afrika Kusini, Kiernan Forbes, maarufu kwa jina la AKA, na rafiki yake wa karibu, mpishi maarufu na mjasiriamali Tebello "Tibz" Motshoane.

    Wawili hao waliuawa kwa kupigwa risasi nje ya mkahawa mmoja mjini Durban mwaka mmoja uliopita, katika mauaji ambayo yaliwashangaza Waafrika Kusini.

    Polisi walisema wahusika walilipwa ili kumlenga AKA lakini hakuna nia iliyofichuliwa.

    Katika taaluma yake , alikuwa na nyimbo nyingi zikiwemo alizomshirikisha Burna Boy wa Nigeria.

    Washukiwa hao, wote wenye umri wa chini ya miaka 36, ​​wanatazamiwa kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.

    "Ilikuwa wazi kwamba AKA alifuatiliwa kutoka uwanja wa ndege na Tibz hakuwa mlengwa aliyekusudiwa katika mauaji kwenye Barabara ya Florida huko Durban," Luteni Jenerali Nhlanhla Mkhwanazi, kamishna wa polisi wa jimbo la KwaZulu-Natal, alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne usiku.

    "Tunajua walilipwa kwa hili," Luteni Jenerali Mkwananzi aliongeza.

  14. Nyimbo zaidi kutolewa TikTok kuhusiana na mzozo na Universal Music

    TikTok inasema imeanza kuondoa muziki zaidi kwenye jukwaa lake kuhusiana na mzozo unaoendelea kuhusu mirahaba na Universal Music Group (UMG).

    Programu hiyo tayari imezima nyimbo za wasanii waliosainiwa na lebo, lakini sasa inapaswa kufanya vivyo hivyo na waandishi pia.

    Hii inamaanisha kuwa video zinazoangazia nyimbo za wasanii kama vile Harry Styles na Adele, ambao wameandika na wasanii waliosainiwa na Universal, zinaweza kuzimwa hivi karibuni.

    TikTok inasema hadi 30% ya nyimbo inazoziita "nyimbo maarufu" zinaweza kupotea.

    Lakini makadirio mengine katika ya tasnia hiyo yanasema hadi 80% ya muziki wote kwenye TikTok unaweza kuzimwa .

    Hiyo ni kwa sababu ya kitu kinachoitwa "hakimiliki zilizogawanyika".Hatua inamaanisha ikiwa mtunzi aliyetia saini kwenye kitengo cha uchapishaji cha Universal Music amechangia hata sehemu ndogo kwenye wimbo, rekodi hiyo yote, kwa nadharia, itabidi ishushwe.

    Hiyo itajumuisha nyimbo za wasanii kwenye lebo zingine, zikiwemo nyimbo kuu mbili zilizosalia, Sony na Warner, na mamia ya watu huru.

  15. Ndoto ya mtoto anayekabiliwa na maradhi adimu nchini Tanzania

    Ally Kimara huenda sasa itatimia kupitia mpango maalumu unaomuwezesha kupata elimu yake akiwa nyumbani kutokana na hali yake kushindwa kufika katika maeneo ya shule rasmi.

    Kuendelea na masomo yake Ally,ni kutokana na mpango wa serikali ulioanzishwa Mapema mwaka 2023 ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalumu kuweza kupata fursa ya masomo.

    Pamoja na hali yake hiyo anasema iwe jua iwe mvua ni lazima aje kuwa Daktari siku za usoni

  16. Chad kuandaa uchaguzi wa kwanza tangu kumalizika kwa utawala wa kiraia

    Tume ya uchaguzi ya Chad imesema duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais itafanyika tarehe 6 Mei.

    Kura hizo za maoni zitaashiria mwisho wa kipindi kirefu cha mpito cha kijeshi ambacho kilianza mwaka 2021 baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu Idriss Deby Itno.

    Kulingana na kalenda ya uchaguzi iliyochapishwa Jumanne, duru ya pili ya upigaji kura itaandaliwa mnamo Juni, na matokeo ya mwisho yanatarajiwa Julai.

    Rais wa tume ya uchaguzi, Ahmet Bartchiret alisema ilikuwa ni lazima uchaguzi ufanyike kabla ya Oktoba 10, tarehe ambayo kipindi cha mpito cha kijeshi kinafaa kumalizika.

    Mahamat Idriss Deby amekuwa akiongoza nchi kwa karibu miaka mitatu sasa, licha ya ahadi ya awali ya kuondoka baada ya kipindi cha mpito cha miezi 18.

    Kipindi cha mpito kiliongezwa baadaye kwa miaka miwili, na hivyo kurefusha kukaa kwake madarakani.

    Mwezi uliopita, Chama cha Patriotic Salvation Movement (MPS) kilimtaja Deby kama mgombeaji wake katika uchaguzi wa urais, lakini bado hajatoa maoni yake rasmi kuhusu iwapo atagombea.

    Katiba mpya iliyopiga kura mwezi Disemba inamruhusu kusimama kama mgombea, na kuzua maswali kuhusu ahadi ya kukomesha utawala wa kijeshi.

  17. Wakili wa Navalny azuiliwa kwa muda mjini Moscow - ripoti

    Wakili wa kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny, aliyefariki gerezani mapema mwezi huu, amezuiliwa kwa muda mfupi mjini Moscow.

    Vyombo vya habari vya Urusi vilisema Vasily Dubkov alishikiliwa kwa "kukiuka utaratibu wa umma".

    Maafisa wa Urusi hawajathibitisha kukamatwa kwa wakili huyo.

    Lakini Bw Dubkov aliambia chombo cha habari cha Verstka kwamba aliachiliwa baadaye Jumanne.

    Bw Dubkov aliandamana na mamake Navalny hadi kwenye gereza la Arctic ambako alifariki tarehe 16 Februari.

    Mnamo Oktoba 2023, mawakili wengine wa Navalny - Vadim Kobzev, Igor Sergunin, na Aleksei Lipster - walikamatwa kwa mashtaka ya "itikadi kali".

    Mnamo Januari, Olga Mikhailova, wakili mwingine wa kiongozi wa upinzani, alisema alikuwa ameshtakiwa kwa uhalifu huo na aliamua kusalia uhamishoni.

    Mamlaka ya Urusi ilipiga marufuku Wakfu wa Kupambana na Ufisadi, shirika linaloongozwa na Navalny, kwa "itikadi kali" mnamo 2021.

    Mwili wa kiongozi huyo wa upinzani ulishikiliwa na wakuu wa magereza kwa zaidi ya wiki moja kufuatia kifo chake.

    Mama yake, Lyudmila Navalnaya, alisafiri hadi jela ya "Polar Wolf" ambako alifariki ili kuuchukua mwili wake, akiandamana na Bw Dubkov.

    Mwili huo ulikabidhiwa kwa mama yake siku nane baada ya kifo chake.

    Bi Navalnaya alisema alitishwa na mamlaka, ambao walitaka mwanawe azikwe kwa "kisiri".

    Pia unaweza kusoma:

  18. Makumi ya watu wafariki baada ya basi kutumbukia mtoni nchini Mali

    Watu 31 wamefariki baada ya basi kutumbukia mtoni nchini Mali siku ya Jumanne.

    Basi hilo lilikuwa likielekea nchi jirani ya Burkina Faso kutoka mji wa Kenieba nchini Mali wakati lilipoanguka kutoka kwenye daraja la mto Bagoe.

    Watu kumi walijeruhiwa - baadhi yao wakipata majeraha mabaya.

    Maafisa wa eneo hilo walisema huenda ajali hiyo ilitokana na "dereva kushindwa dereva kulidhibiti gari".

    Ajali hiyo ilitokea mwendo wa 17:00 saa za ndani (17:00 GMT).

    "Basi... lililokuwa likitoka wilaya ya Kenieba kuelekea Burkina Faso lilipoanguka kutoka kwenye daraja.

    Sababu inayowezekana ni dereva kupoteza udhibiti wa gari," wizara ya uchukuzi ilisema katika taarifa.

    Imeongeza kuwa waathiriwa ni pamoja na raia wa Mali na raia kutoka maeneo mengine ya Afrika Magharibi.

    Ajali za barabarani hutokea mara kwa mara nchini Mali kwa sababu ya miundo misingi duni ya barabara na magari yasiyo katika hali nzuri ambayo hubeba mizigo kupita kiasi.

    Mapema mwezi huu, watu 15 walifariki na 46 kujeruhiwa baada ya basi lililokuwa likielekea mji mkuu Bamako kugongana na lori, kulingana na shirika la habari la AFP.

  19. Netanyahu na Biden watofautiana kuhusu mzozo wa Israel Gaza

    Uungwaji mkono maarufu wa Israel nchini Marekani utasaidia kupigana "hadi ushindi kamili" dhidi ya Hamas, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema Jumanne.

    Katika taarifa, Bw Netanyahu alinukuu kura zinazoonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Wamarekani wanaunga mkono Israel katika mzozo wa Gaza.

    Matamshi yake yanakuja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuonya kuwa Israel iko hatarini kupoteza uungwaji mkono wa kimataifa katika vita hivyo.

    Maafisa wa Marekani wanasema wanafanyia kazi mpango unaowezekana wa kusitisha mapigano.

    Katika taarifa siku ya Jumanne, Bw Netanyahu alisema kuwa, tangu kuanza kwa mzozo huo, amekuwa akiongoza kampeni "kukabiliana na shinikizo la kimataifa la kumaliza vita kabla ya wakati na kuhamasisha uungaji mkono kwa Israeli."

    "Tuna mafanikio makubwa katika eneo hili," Bw Netanyahu aliongeza, akinukuu kura ya hivi majuzi ya Harvard-Harris iliyoonyesha kuwa 82% ya umma wa Marekani unaunga mkono Israel. "Hii inatupa nguvu zaidi ya kuendelea na kampeni hadi ushindi kamili."

    Siku ya Jumatatu, Bw Biden alisema Marekani inatarajia kuwa na usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza "ifikapo Jumatatu ijayo."

    Rais wa Marekani pia alipendekeza baadaye kwamba Israel inaweza "kupoteza uungwaji mkono kutoka duniani kote" ikiwa "itaendelea na serikali hii ya kihafidhina ya ajabu waliyo nayo".

    Pia unaweza kusoma:

  20. Washirika wa Nato wapinga wazo la Macron la kupeleka wanajeshi Ukraine

    Nchi kadhaa za Nato, zikiwemo Marekani, Ujerumani na Uingereza, zimefutilia mbali pendekezo la kupeleka wanajeshi wa ardhini nchini Ukraine, baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kusema "hakuna lisilowezekana".

    Bw Macron alisema "hakuna makubaliano" yaliyofikiwa juu ya kutuma wanajeshi wa mataifa ya Magharibi nchini Ukraine.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov ameonya kuhusu mzozo wa moja kwa moja ikiwa wanajeshi wa Nato watatumwa huko.

    Vikosi vya Urusi hivi karibuni vimepata mafanikio nchini Ukraine na Kyiv imeomba kwa dharura silaha zaidi.

    Bw Macron aliambia mkutano wa wanahabari Jumatatu jioni: "Hatupaswi kuwatenga kwamba kunaweza kuwa na hitaji la usalama ambalo linahalalisha baadhi ya vipengele vya kupelekwa.

    "Lakini nimekuambia kwa uwazi kabisa kile ambacho Ufaransa inashikilia kama msimamo wake, ambao ni utata wa kimkakati ambao ninasimama nao."

    Kiongozi huyo wa Ufaransa alikuwa akizungumza mjini Paris, ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa mgogoro wa kuunga mkono Ukraine, unaohudhuriwa na wakuu wa mataifa ya Ulaya, pamoja na Marekani na Canada.

    Uvamizi kamili wa Ukraine ulioanzishwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin sasa ni mwaka wa tatu, na hakuna dalili kwamba vita hiyo kubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia vinaweza kumalizika hivi karibuni.

    Kauli ya Bw Macron ilivutia hisia kutoka kwa nchi nyingine za Ulaya na wanachama wa Nato.

    Rais wa Marekani Joe Biden anaamini "njia ya ushindi" ni kutoa msaada wa kijeshi "ili wanajeshi wa Ukraine wawe na silaha na risasi wanazohitaji kujilinda", taarifa ya Ikulu ya White House ilisema.

    "Rais Biden amekuwa wazi kwamba Marekani haitatuma wanajeshi kupigana nchini Ukraine," iliongeza.

    Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema hakujakuwa na mabadiliko yoyote katika msimamo uliokubaliwa kuwa hakuna nchi yoyote ya Ulaya au nchi mwanachama wa Nato itakayotuma wanajeshi wake nchini Ukraine.

    Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alisema kuwa nchi hiyo haina mpango wa kupeleka wanajeshi wengi nchini Ukraine, zaidi ya idadi ndogo ya wafanyakazi ambao tayari wanatoa mafunzo kwa vikosi vya Ukraine.

    Maelezo zaidi: