Biden asema ameamua jinsi Marekani itakavyojibu shambulio la Jordan

Rais hakufafanua, lakini aliongeza: "Sidhani tunahitaji vita vingine zaidi Mashariki ya Kati."

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Rais Ruto asema polisi kutumwa Haiti karibuni licha ya uamuzi wa mahakama

    .

    Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya

    Maelezo ya picha, Rais William Ruto

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya amemshutumu Rais William Ruto kwa kupanga kukaidi uamuzi wa mahakama dhidi ya kutumwa kwa polisi nchini Haiti.Ekuru Aukot, ambaye wiki jana alifaulu kupinga kutumwa kwa ujumbe huo mahakamani, anasema rais anaweza tu kupeleka jeshi na sio polisi.

    Mahakama ilisema ujumbe huo haukuwa halali.Bw Ruto alisema Jumanne ujumbe huo unaweza kuendelea “wiki ijayo” iwapo makaratasi yote yatafanyiwa kazi ili kukidhi mahitaji ya mahakama.Novemba mwaka jana, bunge la Kenya liliidhinisha kutumwa kwa maafisa 1,000 kuongoza kikosi cha kimataifa nchini Haiti, ambapo magenge yanajaribu kupanua udhibiti wao wa maeneo.

    Lakini wiki jana, jaji alisema Baraza la Usalama la Kitaifa la Kenya, ambalo linaongozwa na rais, halina mamlaka ya kupeleka polisi wa kawaida nje ya nchi.Iliongeza kuwa baraza hilo linaweza tu kupeleka wanajeshi, sio polisi, kwa misheni za kulinda amani kama vile Haiti.

    Mahakama pia ilisema lazima kuwe na makubaliano ya usawa kati ya nchi hizo mbili kabla ya kutumwa.Akitoa uamuzi huo, Jaji Chacha Mwita alisifu pendekezo la Kenya la kupeleka polisi nchini Haiti, lakini akasema linahitaji kutekelezwa kwa mujibu wa sheria.

    Akizungumza kando ya mkutano wa kilele wa Italia na Afrika mjini Rome, Bw Ruto Jumanne aliambia shirika la habari la Reuters kwamba alitarajia ombi litakuja hivi karibuni ambalo lingekidhi matakwa ya mahakama ya Kenya.

    "Mpango uko mbioni. Misheni hiyo ni wito mkubwa kwa ubinadamu," aliongeza.Alipoulizwa ikiwa kulikuwa na juhudi kwa Haiti kupata ombi hilo muhimu, Bw Ruto alisema: "Hakika."

    "Haiti wameandika rasmi, sio leo, miezi kadhaa iliyopita," aliongeza.

    Korir Sing'oei, afisa mkuu katika wizara ya mambo ya nje ya Kenya, katika msururu wa machapisho kwenye X, alisema kuwa kutumwa kwa polisi nje ya nchi hakutakuwa kinyume na katiba ikiwa kutafanywa chini ya mpango wa maelewano baina ya nchi hizo mbili.

    Lakini Bw Aukot anasema kutumwa kunahitaji zaidi ya makubaliano ya pande mbili kati ya nchi hizo mbili.

    "Thamini hekima ya Jaji Mwita kuhusu 'huduma' na 'nguvu'. Kulingana na sheria na katiba, huwezi kupeleka huduma ya polisi nje ya Kenya," Bw Aukot alichapisha kwenye X, akimshutumu afisa huyo wa maswala ya kigeni kwa kupotosha rais.

    Wakati wa mahojiano hayo ya Jumanne, Bw Ruto alisisitiza kuwa hiyo ilikuwa operesheni ya polisi badala ya operesheni ya kijeshi.

    Serikali ya Kenya ilisema itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

    Marekani ilisema wiki jana kwamba inaunga mkono nia ya serikali ya Kenya kupinga uamuzi huo.

    Lakini upinzani wa Kenya Jumanne uliionya Marekani dhidi ya kuingilia masuala ya ndani ya Kenya.

    Haijabainika ni lini serikali ya Kenya ingewasilisha rufaa hiyo mahakamani na ikiwa nchi nyingine zilizoahidi kutuma vikosi vidogo ili kuimarisha ujumbe wa kimataifa zitazingatia kwenda peke yao.

    Miongoni mwa waliopanga kutuma vikosi ni Bahamas, Antigua na Barbuda, huku Marekani ikiahidi $200m (£158m) kusaidia kutuma ujumbe huo.

    Mjumbe wa Umoja wa Mataifa alisema wiki iliyopita kwamba ghasia za genge la Haiti zimefikia "hatua mbaya", na karibu vifo 5,000 viliripotiwa mwaka jana.

  2. Habari za hivi punde, Serikali imelitangaza kanisa la Paul Mackenzie kuwa kundi la uhalifu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa mambo ya ndani nchini kenya Kithure Kindiki ametangaza kwamba kanisa la Good News International Ministries la muhubiri Paul Mackenzie kuwa kundi la uhalifu..

    Katika taarifa yake aliyoitoa Jumatano, Kindiki alisema tamko hilo ni kwa mujibu wa Kifungu cha Sheria ya Kuzuia Uhalifu wa Kupangwa.

    Kifungu kilichotajwa kinaeleza kwamba “endapo Waziri ana sababu za msingi za kuamini kuwa kikundi fulani kinajihusisha na uhalifu wa kupangwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria hii, anaweza, kwa ushauri wa Kamishna wa Polisi, kwa notisi, kutangaza kwamba ni kundi la uhalifu kwa madhumuni ya Sheria hii.

    "Kifungu cha (2) kinasema kwamba "Mtu yeyote ambaye hakuridhika na uamuzi wa Waziri chini ya kifungu hiki anaweza kuomba Mahakama Kuu ili kusuluhishwa ndani ya siku ishirini na moja tangu tarehe ya kuchapishwa kwa amri."

    Waziri huyo na maafisa wake yuko katika eneo la Shakahola, Kaunti ya Kilifi, eneo linalomiliki dhehebu linaloshukiwa kuhusika na vifo vya zaidi ya watu 400 vilivyotokea kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.

    Kesi za mahakama zinazomkabili Mchungaji Mackenize na washtakiwa wengine 94 zimebaini kuwa nyenzo za DNA kutoka miili 429 kwa ajili ya uchunguzi zimezuiwa kutokana na kuoza kwa miili 360, na kufanya zoezi la uchunguzi wa maiti kuwa gumu, lenye gharama kubwa, na lilichokuwa muda mrefu.

    Washukiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 238 yanayowakabili yakiwemo ugaidi na itikadi kali.

    Wamekana mashtaka yote.Mackenzie na washtakiwa wenzake ambao wamekaa rumande kwa miezi kadhaa, wataendelea kusalia rumande kufuatia ombi la upande wa mashtaka la kutaka kuendelea kuwazuilia hadi kukamilika kwa upelelezi.

    Mwishoni mwa Disemba, mahakama ya Shanzu ilikubali ombi la upande wa mashtaka la kuongeza muda wa kuzuiliwa kwa washukiwa kwa siku 180 zaidi.

  3. Umaarufu wa Benjamini Netanyahu wazidi kushuka Israel - Kura ya Maoni

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

    Kura ya maoni ya hivi majuzi ya Israel inaonyesha kuendelea kupungua kwa umaarufu wa Netanyahu

    Kura ya maoni ya televisheni ya Israel ilifichua kuwa uungwaji mkono wa wananchi kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu umepungua zaidi katika wiki za mwisho za vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas huko Gaza, gazeti la Times of Israel liliripoti.

    Kura hiyo ya maoni iliyotangazwa na Idhaa 12 za Israel Jumanne jioni, ilisema iwapo uchaguzi mpya ungefanyika leo, chama cha National Unity Party, kinachoongozwa na Waziri Benny Gantz, kitapata idadi kubwa ya viti vya Bunge, na viti 37, vikifuatiwa na Chama cha Likud, kinachoongozwa na Netanyahu, chenye viti 18.

    Kura ya maoni iliongeza kuwa nyakati zijazo watapata viti 14, Shas watapata viti 10, na Yisrael Our Home na Jeshi la Kiyahudi watapata viti 8, kila moja.

    Wakati vyama vya Uzayuni wa Kidini na Meretz vitapata viti 4 kila kimoja. Chama cha Democratic Front for Peace and Equality kitapata viti vitano.

    Kwa ujumla, kura ya maoni ilionyesha kuwa muungano unaompinga Netanyahu utapata viti 68 kati ya 120 vya bunge la Knesset, huku Likud na washirika wake wakipata viti 47. Hii ni bila chama cha Democratic Front for Peace and Equality kujiunga na muungano wowote.

    Wakati wa kuchagua kati ya Benny Gantz na Benjamin Netanyahu kwa nafasi ya Waziri Mkuu, Gantz alipata kura za 41% ya washiriki wote, huku Netanyahu akipata 23%, ikilinganishwa na kura ya mapema mwezi huu, ambayo matokeo yake yalikuwa 42% na 29. %, kwa mtiririko huo.

    Ingawa Gantz alimshinda Netanyahu, Netanyahu alikuwa maarufu zaidi kwa nafasi ya waziri mkuu kuliko kiongozi wa upinzani Yair Lapid, kwa 29% na 27%.

  4. Iran imetishia kulipa kisasi iwapo Marekani itaishambulia

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Kurdistan

    Washington inasema kwamba uamuzi wa kujibu mashambulizi katika kambi zake umechukuliwa, Lakini Iran inatishia kulipa kisasi.

    Mjumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeed Iran, alionya Jumatano kwamba Tehran itajibu madhubuti kwa shambulio lolote dhidi ya ardhi yake, maslahi, au raia nje ya nchi, kulingana na vyombo vya habari rasmi vya Iran

    Kauli ya Iran inakuja siku moja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza kuwa ameamua jinsi ya kujibu mashambulizi dhidi ya kambi ya Wamarekani huko Jordan, ambayo yalisababisha vifo vya wanajeshi watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

    Washington iliishutumu Iran na makundi washirika wake kwa shambulio hilo, na haikutoa maelezo yoyote kuhusu jibu la Marekani.

    Kamanda wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran alisema kuwa Iran itajibu tishio lolote kutoka kwa Marekani. Alifafanua, "Tunasikia vitisho kutoka kwa viongozi wa Marekani, na tunawaambia kwamba tayari wametujaribu na tunafahamiana, hivyo tishio lolote halitapita bila majibu."

    Wanajeshi kadhaa wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran waliuawa kufuatia shambulio la Israeli huko Syria, na uvamizi Jumatatu uligonga kituo cha ushauri wa jeshi la Iran kulingana na Shirika la Habari la Iran la Tasnim huko Syria, na kuua wawili, lakini balozi wa Iran huko Damascus alikanusha maelezo kuhusu lengo, na kusema kwamba waliokufa hawakuwa raia wa Iran .

    Mnamo Januari 15, Iran ilishambulia kile ilichoelezea kama "makao makuu ya kijasusi" ya Israeli katika makoa makuu yake ya jimbo la kurdistan nchini Iraq.

    Soma zaidi:

      .

      Chanzo cha picha, NURPHOTO

    • Video: Hatari! Tazama mjusi huyu alivyoepuka kuwa kitoweo cha nyoka

      Maelezo ya video, Tazama jinsi mjusi huyu alivyonusurika kifo kutoka kwa nyoka wenye njaa

      Mjusi mkubwa anayeishi baharini nusra awe chakula cha nyoka walio na njaa kisiwani Galapagos huko Fernandina.

      Macho ya nyoka hayaoni vizuri lakini yanaweza kuona kitu kinachotambaa.

      Mjusi huyo analazimika kuongeza kasi ili kutoroka na kufika kwa wenzake

    • Kampuni kubwa ya muziki duniani kuondoa mamilioni ya nyimbo zake kutoka TikTok baada ya mzozo wa malipo

      .

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Kampuni kubwa ya muziki duniani Universal Music inatazamiwa kuondoa mamilioni ya nyimbo zake kwenye TikTok baada ya kuvunjika kwa mazungumzo kuhusu malipo.

      Hatua hiyo ingemaanisha kuwa mtandao huo wa kijamii hautaweza tena kupata nyimbo za wasanii wakiwemo Taylor Swift, The Weeknd na Drake.

      Kampuni ya Universal Music ilishutumu TikTok kwa "uonevu" ikasema inataka kulipa "sehemu" ya malipo tovuti zingine za mitandao ya kijamii hufanya kwa ufikiaji wa orodha yake kubwa.

      TikTok ilisema Universal ilikuwa ikiwasilisha "simulizi ya uwongo".

      Kampuni za muziki hupata malipo ya mrabaha nyimbo zao zinapochezwa kwenye tovuti moja kwa moja na majukwaa ya mitandao ya kijamii.

      Ingawa TikTok - ambayo inamilikiwa na kampuni ya Kichina ya ByteDance - ina watumiaji zaidi ya bilioni moja, inachukua 1% tu ya mapato yote ya Universal, ilisema.

      Katika "barua ya wazi kwa jumuiya ya wasanii na watunzi wa nyimbo" Universal - ambayo inadhibiti takriban theluthi moja ya muziki duniani - ilidai kuwa "hatimaye TikTok inajaribu kujenga biashara inayotegemea muziki, bila kulipa thamani sawa kwa muziki".

      Universal Music pia ilisema kuwa pamoja na kushinikiza "fidia inayofaa kwa wasanii wetu na watunzi wa nyimbo", pia ilikuwa na wasiwasi kuhusu "kuwalinda wasanii binadamu dhidi ya athari mbaya za AI, na usalama wa mtandaoni kwa watumiaji wa TikTok"

      Kampuni hiyo ilisema itaacha kutoa leseni kwa TikTok mkataba wake utakapomalizika tarehe 31 Januari.

      Kujibu, TikTok ilisema: "Inasikitisha na kukatisha tamaa kwamba Universal Music Group imeweka mbele uchoyo wao dhidi ya masilahi ya wasanii na watunzi wao wa nyimbo.

      "Licha ya simulizi ya uwongo ya Universal, ukweli ni kwamba wamechagua kuachana na usaidizi mkubwa wa jukwaa lenye watumiaji zaidi ya bilioni ambalo hutumika kama chombo cha utangazaji bidhaa na ugunduzi bila malipo kwa talanta zao," iliongeza.

      Hii ni mara ya kwanza kwa Universal Music kuchukua hatua kubwa ya kuondoa nyimbo zake kutoka kwa jukwaa la kampuni ya teknolojia.

      Universal inashikilia nafasi kubwa katika tasnia ya muziki iliyorekodiwa ulimwenguni.

      Pia unaweza kusoma:

    • Kundi la wanamgambo wa Iraq lasitisha mashambulizi dhidi ya Marekani baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani

      .

      Chanzo cha picha, Reuters

      Kundi la wanamgambo wa Iraq wanaoshukiwa kufanya shambulizi la ndege zisizo na rubani nchini Jordan na kusababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani limesema kuwa limesitisha operesheni dhidi ya Marekani.

      Kataib Hezbollah, kundi linalofungamana na Iran ambalo lilijisifu kwa shambulio hilo siku ya Jumapili, lilisema ni "kuzuia aibu kwa serikali ya Iraq".

      Rais Joe Biden alisema ameamua jinsi ya kujibu shambulio hilo, lakini hakusema hatua ya Marekani itakuwaje.

      Marekani imedokeza jinsi inavyoweza kujibu na kusema inaweza kuwa hatua kwa hatua.

      Akipendekeza kwamba haitaanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Marekani, Katibu Mkuu wa Hezbollah Abu Hussein al-Hamidawi alisema katika taarifa yake Jumanne: "Tunapotangaza kusimamishwa kwa operesheni za kijeshi na usalama dhidi ya vikosi vya uvamizi - ili kuzuia aibu ya serikali ya Iraq - tutaendelea kuwatetea watu wetu huko Gaza kwa njia zingine."

      Wanajeshi hao watatu wa Marekani waliuawa kwenye mpaka wa Jordan na Syria na ndege isiyo na rubani ambayo iliripotiwa kutengenezwa nchini Iran, kulingana na CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani.

      Makumi ya wanajeshi zaidi walijeruhiwa katika shambulio hilo, ambalo lilitekelezwa wakati wanajeshi wa Marekani walikuwa wamelala kwenye vyumba vyao.

      Soma zaidi:

    • Habari za hivi punde, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan ahukumiwa tena miaka 14 jela kwa kesi tofauti

      .

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Imran Khan na mkewe Bushra Bibi wamehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela, siku moja baada ya waziri mkuu huyo wa zamani wa Pakistan kufungwa jela miaka 10.

      Khan, ambaye alifukuzwa na wapinzani wake kama Waziri Mkuu mnamo 2022, tayari anatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.

      Siku ya Jumanne alihukumiwa kifungo cha miaka 10 kwa kuvujisha siri za serikali, na Jumatano amehukumiwa mingine 14 katika kesi tofauti ya ufisadi.

      Khan amesema kesi nyingi dhidi yake zimechochewa kisiasa.

      .

      Chanzo cha picha, EPA

      Soma zaidi:

    • Vita vya Israel na Gaza: Umoja wa Mataifa waonya kuwa mfumo wa misaada unaweza kuporomoka ikiwa ufadhili wa UNRWA utazuiwa

      .

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa kuondolewa kwa ufadhili kwa shirika lake kuu la misaada huko Gaza kunaweza kusababisha "kuporomoka kwa mfumo wa kibinadamu".

      Walizungumza baada ya Marekani, Uingereza na nchi nyingine kusitisha ufadhili kwa madai ya jukumu la baadhi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas dhidi ya Israel.

      Umoja wa Mataifa umewafuta kazi wafanyakazi wake kadhaa kutokana na madai hayo.

      Ilisema uchunguzi kuhusu shirika lake la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, unaendelea.

      Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameelezea UNRWA kama "iliyoingiliwa na Hamas", akisema Israel "imegundua kwamba kulikuwa na wafanyakazi 13 wa UNRWA ambao walishiriki, ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, katika mauaji ya Oktoba 7".

      Lakini Marekani, mfadhili mkuu wa UNWRA, imesema inataka kuona shirika hilo la misaada likiendelea na kazi yake.

      "Hakuna mtoaji mwingine wa misaada ya kibinadamu huko Gaza ambaye anaweza kutoa chakula na maji na dawa kwa kiwango ambacho UNRWA inafanya," Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller alisema.

      "Tunataka kuona kazi hiyo ikiendelea ndiyo maana ni muhimu Umoja wa Mataifa ulichukulie kwa uzito jambo hili, wachunguze, kuna uwajibikaji kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na makosa."

      Katika shambulio la Oktoba 7, watu wenye silaha wa Hamas waliwauwa takriban watu 1,300 na kuchukua mateka wapatao 250.

      Israel ilianzisha mashambulizi dhidi ya Hamas kujibu na zaidi ya watu 26,700 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

      Soma zaidi:

    • Jaji azuia mpango wa malipo wa $56bn kwa Elon Musk 'usioeleweka'

      .

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Jaji katika jimbo la Delaware nchini Marekani amebatilisha mkataba wa malipo wa $55.8bn (£44bn) uliopewa Elon Musk mwaka wa 2018 na kampuni ya magari ya umeme ya Tesla.

      Kesi hiyo iliwasilishwa na mwanahisa ambaye alidai kuwa ni malipo ya juu sana.

      Jaji Kathaleen McCormick aliamua kwamba idhini ya bodi ya Tesla ya kifurushi cha malipo "ilikuwa yenye dosari kubwa."

      Kwenye ujumbe katika mtandao wa Xzamani ukijulikana kama Twitter, unaomilikiwa na Bw Musk, aliandika: "Usijumuishe kampuni yako katika jimbo la Delaware".

      Mpango huo wa malipo ulikuwa mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya kampuni, na kusaidia kumfanya Bw Musk kuwa mtu tajiri zaidi duniani.

      Wakati wa kesi iliyochukua wiki moja, wakurugenzi wa Tesla walibishana kuwa mpango huo ulifanywa ili kuhakikisha kuwa mmoja wa wajasiriamali mahiri duniani anaendelea kujitolea kwa kampuni.

      Lakini jaji aliamua kwamba Tesla na mawakili wa Bw Musk "hawakuweza kuthibitisha kwamba wanahisa walifahamishwa kikamilifu juu ya kura ya wenye hisa", na kwamba "ana uhusiano wa karibu na watu waliopewa jukumu la kufanya mazungumzo kwa niaba ya Tesla".

      "Ikizingatiwa kuwa hakimu aligundua kuwa Bw Musk ndiye anayesimamia bodi, ni vigumu kuhalalisha malipo kama haya," Brian Quinn, profesa katika Shule ya Sheria ya Chuo cha Boston, aliambia BBC.

      Katika uamuzi wa kurasa 201, Jaji McCormick aliita malipohayo" kiasi kisichoeleweka" na haikuwa haki kwa wenyehisa.

      Greg Varallo, wakili wa mwanahisa wa Tesla Richard Tornetta ambaye alileta kesi hiyo mnamo 2018, alisema ilikuwa "siku njema kwa watu wema," katika barua pepe iliyoripotiwa na shirika la habari la Reuters.

      Pia unaweza kusoma:

    • Hamas yasema inachunguza pendekezo la kusitishwa upya kwa mapigano Gaza

      A Palestinian woman and child, fleeing Khan Younis, sit along the road amid a move towards Rafah

      Chanzo cha picha, Reuters

      Hamas yasema inachunguza pendekezo la kusitishwa upya kwa mapigano GazaKiongozi wa kisiasa wa Hamas amethibitisha kuwa wanachunguza pendekezo jipya la kusitishwa kwa mapigano katika ukanda wa Gaza.

      Ismail Haniyeh alisema kuwa kundi hilo limealikwa kujadili mpangokazi wa Israel, Marekani, Qatar na Misri.

      Inaripotiwa kuwa zimependekeza kusitishwa mapigano kwa wiki sita, wakati ambapo kutakuwa na mabadilishano ya waliochukuliwa mateka kati ya Israel na Palestina.

      Haniyeh alisistiza kipaumbele cha Hamas ilikuwa ni mpango wa kudumu wa kusitisha vita na kujiondoka kabisa kwa Israel, lakini Waziri mkuu wa Israel alifutilia mbali uwezekano huo.

      Benjamin Netanyahu alisistiza kuwa mapigano hayataisha hadi watakapopata "ushindi kamili" ambao alisema utamaanisha kumaliza kabisa kundi la Hamas na kuachiliwa huru kwa walioshikwa mateka.

      Mzozo huo ulichochewa na shambulio la kuvuka mpaka ambalo halijawahi kushuhudiwa na watu wenye silaha wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,300 waliuawa na wengine wapatao 250 kuchukuliwa mateka.

      Zaidi ya watu 26,700 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

      Wakati wa usitishaji vita wa wiki nzima mwishoni mwa mwezi Novemba, mateka 105 wa Israel na wa kigeni waliachiliwa kwa kubadilishana na Wapalestina 240 waliokuwa wakishikiliwa katika jela za Israel.

      Israel inasema mateka 136 bado wanazuiliwa, ingawa karibu dazeni mbili kati ya hao wanakisiwa kuwa wamekufa.

      Soma zaidi:

    • Afcon 2023:Afrika Kusini yaishtua Morocco huku Hakimi akikosa kufunga penalti

      Teboho Mokoena celebrates scoring for South Africa against Morocco at Afcon 2023

      Chanzo cha picha, Getty Images

      Achraf Hakimi alikosa nafasi ya dakika za mwisho kusawazisha kwa mkwaju wa penalti huku Afrika Kusini ikiishangaza Morocco iliyokuwa na wachezaji 10 na kutinga robo fainali dhidi ya Cape Verde kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika 2023.

      Evidence Makgopa alifunga bao la kwanza dakika ya 57, aliponusurika baada ya kufanyiwa ukaguzi wa muda mrefu wa (VAR) na kuwafanya Bafana Bafana kuibuka na ushindi wa kushtukiza dhidi wa mabao mawili kwa nunge ya waliofuzu kwa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022.

      Hakimi alipewa nafasi nzuri ya kusawazisha wakati Mothobi Mvala alipoamuliwa kuwa ndiye aliyeuwahi mpira wa shuti wa Ayoub El Kaabi, lakini akapiga mkwaju wake wa penalti dakika ya 85 dhidi ya lango.

      Kiungo wa kati wa Manchester United, Sofyan Amrabat alitolewa nje dakika za lala salama kabla ya Teboho Mokoena kuukunja mpira wa faulo uliompita Bono kuthibitisha makali ya Afrika Kusini katika mechi hiyo.

      Mabingwa hao wa 1996 sasa watalenga kuimarika baada ya kuondoka kwenye robo fainali walipocheza fainali za hivi majuzi zaidi mwaka wa 2019, watakapomenyana na Blue Sharks ambao hawajashindwa siku ya Jumamosi (20:00 GMT) kwa kufuzu kwa hatua ya nne bora.

      Mali nayo iliishinda Burkina Faso 2-1.

      Pia unaweza kusoma:

    • Biden asema ameamua jinsi Marekani itakavyojibu shambulio la Jordan

      .

      Chanzo cha picha, Reuters

      Rais Joe Biden anasema ameamua jinsi Marekani itakavyojibu shambulizi la ndege zisizo na rubani lililosababisha kuuawa kwa wanajeshi watatu wa Marekani huko Jordan mwishoni mwa juma.

      Bwana Biden hakufafanua zaidi katika matamshi yake katika Ikulu ya White House, lakini aliongeza: "Sidhani tunahitaji vita vingine zaidi Mashariki ya Kati."

      Kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran wamedai kuhusika na shambulio hilo katika kambi ya kijeshi ya Marekani.

      Makumi ya wengine walijeruhiwa katika shambulio la Jumapili karibu na mpaka wa Syria.

      Shambulio hilo la ndege zisizo na rubani ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Marekani kuuawa na adui katika eneo la Mashariki ya Kati tangu vita vya Israel na Gaza kuanza tarehe 7 Oktoba.

      Alipoulizwa na wanahabari Jumanne asubuhi ikiwa ameamua jinsi ya kujibu shambulio hilo, Bw Biden alisema: "Ndiyo."

      Pia aliulizwa iwapo Iran inapaswa kulaumiwa. "Ninawawajibisha [Iran] kwa maana kwamba wanasambaza silaha kwa watu waliofanya hivyo," alisema.

      Hata hivyo, Iran imekanusha kuhusika kwa namna yoyote.

      Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la White House John Kirby alisema Marekani inaweza kuchukua "mbinu ya hatua kwa hatua".

      "Sio hatua moja tu, lakini uwezekano wa kuchukua hatua nyingi... kwa kipindi fulani," aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa kwenye ndege ya Air Force One kwa ajili ya safari ya Bw Biden ya kuhudhuria mkutano wa kuchangisha pesa za uchaguzi huko Florida.

      "Kanuni elekezi ni kuhakikisha kuwa tunaendelea kuharibu aina ya uwezo ambao vikundi hivi vinao na wanavyotumia dhidi ya askari wetu na vifaa vyetu," alisema.

      Bw Kirby aliongeza: "Rais atafanya anachopaswa kufanya ili kulinda wanajeshi wetu na vituo vyetu na kuangalia usalama wa taifa letu."

      Rais ana chaguzi kadhaa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi katika kambi na makamanda wanaoungwa mkono na Iran.

      Marekani inaweza pia kuwalenga makamanda wakuu wa Jeshi la Revolution Guard la Iran nchini Iraq au Syria.

      Soma zaidi:

    • Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 31/01/2024.