Arnold Schwarzenegger alikamatwa katika uwanja wa ndege wa
Ujerumani kwa madai ya kushindwa kutangaza saa ya kifahari aliyokuwa akipanga
kuipiga mnada kwa ajili ya kutoa misaada.
Muigizaji huyo wa Hollywood alizuiliwa kwa saa tatu katika
uwanja wa ndege wa Munich siku ya Jumatano.
Uchunguzi wa madai ya kukwepa kulipa kodi ulianzaiswa baada
ya kubainika kwamba saa hiyo ilinuiwa kuuzwa ndani ya Umoja wa Ulaya (EU).
Kulingana na sheria za Umoja wa Ulaya, mtu yeyote anayefika
na "pesa au vitu fulani vya thamani" zaidi ya €10,000 (£8,580) lazima
atangaze.
Hata hivyo, chanzo kiliiambia CBS News, mshirika wa BBC wa
Marekani, kwamba Schwarzenegger hakuulizwa kujaza fomu ya kutangaza alichobeba.
Muigizaji, mwanasiasa na mwanaharakati huyo wa mabadiliko ya
hali ya hewa hatimaye aliweza kulipa kodi, lakini tu baada ya kukabiliana na matatizo kadhaa.
Baada ya mashine ya kadi kutofanya kazi, iligundulika kuwa
benki ya karibu ilikuwa imefungwa na ukomo wa kutoa ATM ulikuwa chini sana,
ikimaanisha kuwa mzee huyo wa miaka 76 alilazimika kusubiri mashine mpya ya
kadi kuletwa na maafisa wa forodha, chanzo kilisema.
Msemaji wa muigizaji huyo aliliambia gazeti la udaku la
Ujerumani Bild kwamba tukio hilo la uwanja wa ndege lilikuwa "mzaa uliojaa
makosa, lakini ungweza kutengeneza filamu ya kuchekesha ya polisi ".
Bild ilisema "alichukua tukio hilo kwa utulivu" na
picha iliyochapisha ilionyesha Schwarzenegger akitabasamu akipiga picha na
kushikilia kisanduku cha saa na barua inayosema " ni ya Austria".
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, saa hiyo
ilitengenezwa maalum kwa ajili ya nyota ya Terminator na mtengenezaji wa saa wa
kifahari Audemars Piguet, ambaye hutengeneza saa ambazo zinaweza kuuzwa kwa
mamia ya maelfu ya dola.
Saa hiyo ilisemekana kupigwa mnada katika chakula cha jioni
cha kuchangisha fedha kwa ajili ya The Schwarzenegger Climate Initiative huko
Kitzbuhel, Austria, takriban kilomita 89 (maili 55) kutoka Munich, baadaye siku
ya Alhamisi.
Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hafla hiyo,
inayotarajiwa kufanyika katika hoteli ya nyota tano ya Stanglwirt, ilisema
"kazi za sanaa, maonyesho yaliyotiwa saini, na uzoefu kutoka kwa ulimwengu
wa michezo na filamu" zitauzwa.
Orodha ya mnada wa saa hiyo, iliyopatikana na Bild, ilisema
ni moja kati ya 20 zilizopo, na itajumuisha "picha ya Arnold katika pozi
lake la kitambo lenye maneno 'Arnold Classic'". Bei ya kuanzia ya mnada
ilikuwa €50,000.