Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kinara wa mapinduzi ajitangaza kuwa Kiongozi wa Niger

Jenerali Abdourahmane Tchiani amelihutubia taifa akieleza sababu za mapinduzi hayo.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Rais wa Kenya alaani mapinduzi ya kijeshi nchini Niger

    Rais wa Kenya William Ruto amelaani mapinduzi ya yaliyokea nchini Niger.

    Alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum na kurejeshwa kama mkuu wa nchi aliyechaguliwa kidemokrasia:

    Msemaji wa Ikulu ya Kenya ameshirikisha katika mtandao wa Twitter video ya taarifa ya Bw Ruto:

  3. Urusi yaombwa kufufua mkataba wa nafaka wa Ukraine katika mkutano wa kilele

    Rais wa Misri amemuomba Rais wa Urusi Vladmir Putin kufufua upya mkataba wa nafaka wa Ukraine katika mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika unaondelea.

    Abdel Fattah al-Sisi alisema ni "muhimu" mpango huo kufufuliwa na kutafuta suluhu ya dharura ya usambaza wa nafaka katikanchi maskini zaidi za Afrika.

    Urusi ilijiondoa katika mpango huo wiki iliyopita na tangu wakati huo imeshambulia kwa mabomu bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine.

    Bw Putin anasema nchi za Magharibi hazijazingatia matakwa yake katika mpango huo na kutoa nafaka ya Urusi kwa nchi sita za Kiafrika.

    Alisema Urusi itapeleka nafaka hiyo bure.

    Misri ni mnunuzi mkuu wa nafaka kupitia njia ya Bahari Nyeusi na iko katika hatari kubwa ya kupanda kwa bei ya chakula duniani.

    Kujibu Bw Putin alisisitiza kuwa kupanda kwa bei za vyakula kulitokana na makosa ya sera za nchi za Magharibi ambayo yalitangulia vita na Ukraine.

    Pia alidai mpango wa nafaka haukutilia maanani usafirishaji wa nafaka kwa nchi maskini zaidi na kuongeza kwa Urusi iko tayari kutoa nafaka yake ili kusaidia kuepusha "mgogoro wa chakula duniani".

    Urusi inaweza kutoa tani 25-50,000 za nafaka bila malipo kwa mataifa ya Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo, alisema.

    Nchi hizi sita zote ni washirika wa Urusi mbali na Somalia, ambayo inakabiliwa na janga kubwa la kibinadamu.

  4. Ndege za kijeshi za Sudan zaharibiwa na wapinzani mjini Khartoum

    Ndege za kivita zimeharibu ndege tatu za kijeshi katika kambi ya anga ya Wadi Seidna kaskazini mwa mji mkuu, Khartoum, vyanzo vya jeshi vimethibitisha.

    Uwanja huo wa ndege unatumiwa na wanajeshi kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Vikosi vya waasi (RSF), ambavyo askari wake wana kambi katika maeneo mengi ya makazi ya miji mitatu inayounda Greater Khartoum, Bahri, Khartoum na Omdurman, ambayo iko kwenye ukingo wa Mto Nile.

    Kambi ya anga ya Wadi Seidna pia ilitumiwa na serikali za kigeni kuwahamisha raia wao muda mfupi baada ya mzozo wa kikatili wa kuwania madaraka kati ya jeshi na waasi wa RSF kuzuka katikati ya mwezi Aprili.

    Vijosi vya RSF lirusviha makombora kutoka ukingo wa mashariki wa Mto Nile huko Bahri kuelekea Wadi Saeedna upande wa magharibi wa mto siku ya Alhamisi.

    Vyanzo hivyo vilikanusha kuwa kuna mtu yeyote aliuawa au kujeruhiwa - kama ilivyodaiwa na RSF - lakini vilithibitisha kwamba ndege, baadhi ya zile zilizotumiwa katika mashambulizi ya anga, zimeharibiwa.

    Ni shambulio la kwanza kubwa la RSF kwa jeshi katika wiki kadhaa. Kutulia kwa mashambulizi yao kumeambatana na safari iliyofanywa na naibu kiongozi wa RSF kwenda Chad na nchi nyingine kadhaa kutafuta uungwaji mkono.

    Naibu kamanda Abdul Rahim Hamdan Dagalo ni nduguye kiongozi wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Dagolo, anayejulikana kama "Hemedti".

    Chad inapakana na eneo la magharibi la Sudan la Darfur, ambako RSF ina asili yake katika wanamgambo mashuhuri wa Janjaweed ambao walipigana kikatili na waasi na kushutumiwa kwa mauaji ya kikabila mapema miaka ya 2000.

    Hata hivyo, mashambulizi ya anga na mizinga katika mji mkuu wa jeshi yameendelea - na roketi sasa zikirushwa usiku.

    Ikizingatiwa kuwa vikosi vya RSF viko katika maeneo ya makazi, mara nyingi ni raia ambao wanauawa katika mashambulio haya.

  5. Mahakama ya Kenya yapitisha utekelezaji wa sheria tata ya nyongeza ya kodi

    Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imeamua kuwa sheria ya nyongeza ya kodi inayokumbwa na utata inaweza kutekelezwa.

    Sheria hiyo imezusha maandamano makali ya upinzani na wafuasi wake, na kusababisha vifo vya watu 30.

    Wakosoaji wa sheria hiyo wanasema itapandisha gharama ya maisha, hivyo kufanya maisha kuwa magumu zaidi kwa mamilioni ya Wakenya wanaojizatiti kujikimu.

    Sheria iliyoidhinishwa na Rais William Ruto mwezi Juni inapandisha Ushuru wa VAT kwa bidhaa za mafuta kutoka asilimia 8 hadi 16.

    Pia inatanguliza ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5 utakaolipwa na waajiri na waajiriwa.

    Uamuzi wa mahakama ya rufaa unaipa hazina idhini ya kuanza kukusanya ushuru huo mpya.

    Huenda uamuzi huo ukazua maandamano zaidi ya upinzani.

    Soma:

  6. Kiongozi wa Wagner akaribisha mapinduzi ya Niger katika ujumbe wa sauti

    Kiongozi wa mamluki wa Wagner, Yevgeny Prigozhin, amekaribisha mapinduzi ya kijeshi nchini Niger, kulingana na ujumbe wa sauti ambao haujathibitishwa.

    Niger imekuwa mshirika mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo wa kijihadi katika eneo la Afrika Magharibi.

    Marekani na Ufaransa, ukoloni wa zamani zina kambi za kijeshi katika nchi hiyo yenye utajiri wa madini ya uranium.

    Ujumbe wa sauti ambao haujathibitishwa kutoka kwa Bw Prigozhin ulioibuka kwenye mtandao wa Telegram inayohusishwa na kundi hilo, ikisema kuwa mapinduzi hayo yalikuwa yamechelewa.

    Kulingana na shirika la habari la Reuters, mzungumzaji huyo alikuwa na matamshi ya lugha ya Kirusi na sauti kama mkuu huyo wa Wagner.

    "Kilichotokea Niger si chochote zaidi ya mapambano ya watu wa Niger dhidi ya wakoloni, ambao walijaribu kuweka sheria zao za maisha," shirika la habari la AFP linamnukuu akisema.

    "Ili kudumisha mfumo wao halisi wa utumwa katika maeneo ya mataifa haya, wanapeleka vikosi mbalimbali za kigeni, ambavyo vinafikia maelfu ya askari."

    Aliendelea kusifu "ufanisi" wa Wagner, akielezea maelfu ya wapiganaji wake "wanaweza kurejesha utulivu na kukabiliana na magaidi, kuwazuia wasidhuru raia", AFP inaripoti.

    Kutolewa kwa ujumbe wa sauti kuliendana na kuchapishwa kwa picha kwenye Telegram zinazomuonyesha Bw Prigozhin huko St Petersburg katika mkutano wa kilele wa Afrika na Urusi.

    Alionekana akipeana mkono na Balozi Freddy Mapouka, afisa mkuu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

    Ni mara ya kwanza kuthibitishwa kuonekana kwa Bw Prigozhin nchini Urusi tangu Wagner walipohindwa kufanya uasi wao dhidi ya Urusi mwezi Juni.

    Wagner ina mkataba wa usalama nchini CAR na kupitia mtandao wake wa makampuni yanayodaiwa kufanya biashara huko katika migogoro ya madini na mbao, pamoja na kutengeneza bia na vodka.

    Kundi hilo la mamluki pia liko nchini Mali, ambako linaaminika kuwa na wanajeshi wapatao 1,000 ambao wameshutumiwa kutekeleza ukatili.

    Kutumwa kwao mwezi Disemba 2021 kulifuatia kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya utawala wa kijeshi wa Mali na Ufaransa, na kusababisha ukoloni wa zamani kuwaondoa wanajeshi wake wa kukabiliana na ugaidi.

    Kulingana na Reuters, kiongozi huyo wa Wagner alisikika kwenye video iliyotolewa mapema mwezi huu akiwaambia wapiganaji wake, ambao sasa wamehamishwa Belarus, kwamba wanapaswa kuimarisha nguvu zao kwa "safari mpya ya Afrika".

    Pia unaweza kusoma:

  7. Jenerali wa jeshi la Niger ajitangaza kuwa kiongozi mpya

    Jenerali Abdourahmane Tchiani amejitangaza kuwa kiongozi mpya wa Niger baada ya mapinduzi makubwa.

    Jenerali Abdourahmane ambaye pia anajulikana kama Omar Tchiani, aliongoza mapinduzi ambayo yalianzaJumatano wakati kitengo cha walinzi wa rais alichoongoza kilimkamata kiongozi wa nchi.

    Hii inatatiza kipindi cha kwanza cha mpito cha amani na kidemokrasia nchini Niger tangu ijinyakulia uhuru wake mwaka 1960.

    Rais Mohamed Bazoum anadhaniwa kuwa katika afya njema, na bado anashikiliwa na walinzi wake.

    Haya hapa kuna mambo matano tunayojua kumhusu:

    • Jenerali Tchiani, 62, amekuwa akiongoza kitengo cha walinzi wa rais tangu 2011.
    • Kikosi cha wanajeshi 700 kilianzishwa na mtangulizi wa rais aliyepinduliwa Mahamadou Issoufou kulinda dhidi ya utekaji wa kijeshi.
    • Alihusishwa na jaribio la mapinduzi ya 2015 dhidi ya Bw Issoufou.Kesi iliyofuata kortini mnamo 2018 ilimuondolea makosa ya kuhusika
    • Alipandishwa cheo hadi kuwa jenerali mwaka wa 2018 na Bw Issoufou
    • Kabla ya kuchukua mamlaka ya kijeshi,Rais Bazoum alikuwa amepanga kumuondoa jenerali huyo kama sehemu ya mabadiliko aliyokuwa akiyafanya kwa vikosi vya usalama, gazeti binafsi la Niger la L'Enqueteur linaripoti.

    Maelezo zaidi:

  8. Urusi inatathmini mpango wa amani wa Ukraine uliopendekezwa na Afrika - Putin

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ameliambia kundi la viongozi wa Afrika kwamba anaheshimu pendekezo la amani nchini Ukraine ambalo walilitoa mwezi uliopita.

    Katika siku ya pili ya mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika mjini St Petersburg, Bw Putin alisema atauchunguza mpango huo "kwa makini".

    Kiongozi huyo wa Urusi pia alisema nchi yake imefuta deni la thamani ya dola bilioni 23 kwa nchi za Afrika.

    Hakutaja nchi wala hakutaja muda uliohusika.

    iongozi wa Kiafrika pia waliambiwa kwamba Urusi ilikuwa na nia ya ushirikiano zaidi wa kijeshi.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Utawala mpya wa kijeshi nchini Niger wapiga marufuku maandamano ya umma

    Wizara ya mambo ya ndani ya utawala mpya wa kijeshi nchini Niger imepiga marufuku maandamano yote ya umma baada ya wafuasi wa mapinduzi hayo kuchoma moto makao makuu ya chama cha rais aliyepinduliwa.

    Polisi walirusha vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliovamia makao makuu ya chama cha PNDS Tarraya, ambako watu pia walikuwa wakipiga mawe na kuchoma magari.

    "Maandamano ya umma kwa nia yoyote yamepigwa marufuku hadi ilani nyingine itakapotolewa.

    Serikali itahakikisha kwamba sheria inatekelezwa,” ilisema taarifa ya wizara ya mambo ya ndani.

    "Vitendo hivi, vilivyofanywa na watu wasioheshimu utawala wa sheria, vinajumuisha vitendo vya uharibifu na uovu na havitavumiliwa," iliongeza.

    Wizara hiyo imevitaka vyombo vya usalama kulinda raia na mali zao.

    Maelezo zaidi

  10. Umaja wa Mataifa wasitisha shughuli za kibinadamu nchini Niger

    Umoja wa Mataifa unasema kuwa umesitisha shughuli zake za kibinadamu nchini Niger, baada ya wanajeshi kutangaza kumpindua rais mteule wa nchi hiyo.

    Unasema zaidi ya watu milioni nne nchini humo kwa sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti Rais wa Niger Mohamed Bazoum, ambaye anazuiliwa na maafisa wa kijeshi.

    Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema Rais Bazoum alizungumza na Rais Emmanuel Macron mapema siku ya Ijumaa na kumwambia kwamba "anafikika" na "afya njema".

    Unaweza pia kusoma:

    • Mapinduzi Niger: Makao makuu ya chama tawala yashambuliwa baada ya Rais Bazoum kuondolewa madarakani
    • Wanajeshi wa Niger watangaza mapinduzi kwenye televisheni ya taifa
  11. Prigozhin: Bosi wa Wagner aonekana Urusi katika mkutano wa Afrika

    Kiongozi wa Wagner, Yevgeny Prigozhin alipigwa picha huko St Petersburg wakati wa mkutano wa kilele wa Afrika na Urusi wiki hii.

    Alionekana akipeana mkono na Balozi Freddy Mapouka, kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

    Picha hiyo iliwekwa kwenye mtandao wa Facebook na Dmitri Syty, ambaye inasemekana anasimamia shughuli za Wagner huko CAR.

    Ni mara ya kwanza kuthibitishwa kuonekana kwa Bw Prigozhin nchini Urusi tangu Wagner kushindwa kufanya uasi mwezi Juni.

    Mkutano wa Prigozhin na Mapouka ulifanyika katika hoteli ya Trezzini Palace huko St Petersburg, BBC ilithibitisha.

    Mkutano huo unafuatia kuonekana kwa Prigozhin huko Belarus wiki iliyopita. Video kwenye chaneli yaTelegram inayoendeshwa na kundi la Wagner inamwonyesha akiwakaribisha wapiganaji na kuelezea matukio ya hivi karibuni kuhusu vita vinavyoendelea Ukraine kama "fedheha".

    Pia, ameeleza kwamba Wagner inaweza kujiunga tena na vita hapo baadaye.

  12. DRC yawatuhumu wanajeshi wa Rwanda kwa uvamizi wa mpakani

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewashutumu wanajeshi wa Rwanda kwa kuvuka mpaka na kuingia katika ardhi yake.

    Jeshi la Congo lilitoa taarifa kuelezea madai ya uvamizi katika jimbo la Kivu Kaskazini kama uchokozi usiovumilika.

    lilisema wanajeshi wa Rwanda wamelazimishwa kurejea mpakani.

    Rwanda haijatoa tamko lolote kuhusiana na tuhuma hizo, lakini mara kwa mara imekuwa ikikana tuhuma za uvamizi wowote ndani ya ardhi ya DRC.

    Awali ilikanusha shutuma za serikali ya DRC kwamba inaunga mkono kundi la waasi linalojulikana kwa jina la M23, ambalo limefanya mashambulizi mengi mashariki mwa nchi hiyo.

    Taarifa zaidi kuhusu DRC:

    • Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo
    • Makundi ya waasi bado yanahatarisha maisha ya watu wa mashariki mwa Jamuhuri ya Congo
    • Jumuiya ya Afrika Mashariki, majeshi na mustakabali wa amani DRC
    • Link
  13. Vita vya Ukraine: Kyiv yadai mafanikio huku mapigano yakichacha kusini

    Jeshi la Ukraine linasema kuwa limepata mafanikio katika mapigano kusini mashariki mwa Ukraine, huku maafisa wa nchi za Magharibi wakizungumzia kuhusu mapigano makali yanayoendelea.

    Katika video iliyochapishwa na Rais Zelensky, wanajeshi wa Ukraine walisema wamekichukua kijiji cha Staromaiorske.

    Kijiji hicho, kilichopo kilomita 150 (maili 90) mashariki mwa mji wa Zaporizhzhia, kilikombolewa kwa milio mikubwa ya risasi na mashambulizi ya angani, lilisema jeshi.

    Ukraine haijathibitisha kwamba imeimarisha mashambulizi yake ya kukabiliana na hali hiyo.

    Lakini Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema mashambulizi ya Ukraine "yameongezeka" sana.

    Aliwaambia waandishi wa habari huko St Petersburg hawakuwa na mafanikio: "Majaribio yote ya kukabiliana na mashambulizi yalisizimwa, na adui alirudishwa nyuma na hasara kubwa."

    Kiongozi wa wanamgambo wanaoungwa mkono na Urusi Aleksandr Khodakovsky alipingana na kauli ya Bw Putin, akisema Ukraine ilikuwa imeishambulia Staromaiorske kwa siku kadhaa na kupata mafanikio, ikishikilia maeneo na kusonga mbele.

    Rais Zelensky alichapisha video ya wanajeshi wakiwa wamenyenyua bendera ya Ukraine katika kijiji hicho na Waziri wa Ulinzi Hanna Maliar alisema sasa "wanaendelea kusafisha makazi".

    Vita vya Ukraine: Taarifa zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  14. Inasikitisha kwamba Ubelgiji ilimkataa balozi Karega - msemaji wa serikali ya Rwanda

    Serikali ya Rwanda "inasikitika" kwamba Vincent Karega aliteuliwa kuwa balozi nchini Ubelgiji na kwamba uamuzi huu sio mzuri kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, limeripoti gazeti la New Times nchini humo.

    Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alinukuliwa Jumatano na gazeti la New Times linalounga mkono serikali akisema: "Inasikitisha kuona kwamba serikali ya Ubelgiji inaonekana imekubali shinikizo la serikali ya DRC na [propaganda] ya makundi ya waasi, ambao pia waliamua kutangaza uamuzi huo mapema".

    BBC imejaribu kuwasiliana na serikali ya Rwanda kuhusu uamuzi huo wa Ubelgiji, hadi sasa haijawezekana.

    Katika ujumbe wake wa barua pepe, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji, Nicolas Fierens Gevaert, aliiambia BBC siku ya Alhamisi kwamba nchi yake itazungumza kuhusu hilo kupitia njia za kidiplomasia.

    Alisema: "Ubelgiji itatoa taarifa kupitia njia za kidiplomasia. Masuala hayo yatashughulikiwa kupitia njia za utawala. Tunatumai kuwa na uhusiano wa amani na wenye kujenga na Rwanda."

    Karega, mwenye umri wa miaka 60, alitarajiwa kuchukua nafasi ya balozi Dieudonné Sebashongore, ambaye aliiwakilisha Rwanda nchini Ubelgiji tangu 2020.

    Serikali ya Rwanda inawatuhumu watu wa familia ya Jambo Asbl, mmiliki wa tovuti ya Wanyarwanda wanaoishi Ubelgiji, wakiwemo wale ambao wazazi wao walikuwa na nguvu katika serikali ya Rwanda kabla ya chama tawala cha RPF kutwaa mamlaka mwaka 1994, kuwa ni waasi wa mauaji ya halaiki. Wamekuwa wakipinga shutuma hizo.

  15. Kenya: Serikali yasema huduma zake za mtandaoni E-Citizen zimerejea baada ya jaribio la mashambulio ya kimtandao

    Huduma za kawaida zimeanza tena kwenye jukwaa la huduma za serikali la e-Citizen kufuatia kukatizwa kwa mfumo uliochochewa na jaribio la kushambulia mtandaoni.

    Wakenya jana walikosa huduma kama vile ya ununuzi wa umeme, kufanya miamala kwa njia ya M-pesa, huduma za benki za kidigitali na huduma za serikali zinazotolewa kwa njia ya kidigitali kupitia e-Citizen kufuatia shambuliola mtandao lililolenga taasisi za umma na za kibinafsi, linalodaiwa kutekelezwa na watu wanaojiita Anonymous Sudan.

    "Usumbufu huo wa muda ulisababishwa na jaribio la uvamizi wa kimtandao kwenye jukwaa la huduma za serikalikwa njia ya mtandao E_ Citizen kupitia mbinu ya Distributed Denial of Service (DDoS), ambayo ilihusisha kufurika kwa mfumo lengwa na utumaji mkubwa wa taarifa kutoka kwenye vyanzo vingi wakati mmoja.

    Jukwaa lilijaa taarifa na hivyo watumiaji halisi kushindwa kupata huduma kwa urahisi.

    ‘’Shambulio hilo halionyeshi tu kwamba tumezungukwa na watendaji wenye nia mbaya, ndani na nje ya nchi, lakini pia linathibitisha harakati za serikali za kuchukua hatua kali za usalama wa mtandao kulinda miundombinu yetu ya habari muhimu na data dhidi ya vitisho kama hivyo’’, alisema Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa katika taarifa yake.

    Awali, maafisa wa serikali walikuwa wamekanusha madai kwamba jukwaa la e-citizen lilikuwa limedukuliwa, wakisema kuwa walifanikiwa kuzuia majaribio ya kujaza mfumo huo kupita kiasi, jambo ambalo lilisababisha jukwaa hilo kusababisha usumbufu kwa watumiaji wake.

  16. Mapinduzi nchini Niger: Bendera ya Urusi yaonekana miongoni mwa wanaounga mkono mapinduzi

    Baadhi ya wafuasi wa kundi la waasi nchini Niger walifanya maandamano nje ya bunge la huku wakiwa wamebeba bendera za Urusi.

    Baadaye baadhi ya waandamanaji walishambulia makao makuu ya chama cha rais aliyepinduliwa Mohamed Bazum na kuyachoma moto.

    Urusi imeyaita mapinduzi hayo nchini Niger kuwa ni hatua ya kupinga katiba.

    Urusi, pamoja na nchi nyingine, zimetoa wito wa kuachiliwa huru kwa rais Bazum aliyeondolewa madarakani, ambaye anashikiliwa na wapiganaji hao.

    Kwa sasa haijulikani ni nani anayesimamia nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

    Kamanda wa jeshi alijitokeza kuunga mkono wapiganaji, kwa maneno yake, ili ‘’kulinda umoja wa majeshi’’

    Serikali yenyewe haijatangaza nani anaongoza.

    Tangazo la usiku wa manane la kuondolewa kwa rais huyo lilirudiwa kwenye televisheni ya taifa, likiingiliana na muziki wa kizalendo na mistari kutoka Koran.

    Kipindi cha habari, ambacho kwa kawaida hupeperushwa wakati wa chakula cha mchana, hakikutangazwa wakati huo.

    Hata hivyo, katika mji mkuu wa Niger, Niamey, maduka na masoko yalifunguliwa tena katika muda wa kawaida, na wafuasi wa kundi hilo waliingia mitaani asubuhi.

    Mamia ya watu walikusanyika nje ya jengo la bunge. Baadhi walipeperusha bendera huku wengine wakibeba mabango yaliyoandikwa "Ufaransa chini!" na "Kambi za kigeni!".

    naweza pia kusoma:

    • Jinsi Urusi inavyochukua nafasi ya Ufaransa katika makoloni yake ya zamani ya Kiafrika
    • Mtandao wa Wagner barani Afrika unakabiliwa na mustakabali usio na uhakika
    • Fahamu ni kwanini kumekuwa na mapinduzi na majaribio mengi ya mapinduzi Afrika
  17. Tutatuma nafaka kwa nchi za Afrika bila malipo – Putin

    Rais Vladimir Putin wa Urusi ameeleza nia yake ya kutuma nafaka katika mataifa sita ya Afrika bila malipo.

    Putin alisema hayo katika mkutano kati ya Urusi na nchi za Afrika mjini St Petersburg.

    Katika mkutano huo rais Putin alisema katika miezi michache ijayo wataanza kutuma nafaka bure.

    Haya yanajiri baada ya Urusi kujiondoa katika makubaliano ya Bahari Nyeusi na Ukraine mapema mwezi huu.

    Putin alisema kuwa Urusi iko tayari kujaza upungufu wowote wa nafaka unaosababishwa na Ukraine.

    Alisema na kuongeza kuwa Urusi iko tayari kusambaza nafaka kwa nchi sita za Afrika katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo.

    Alisema, "Katika muda wa miezi mitatu hadi minne ijayo, Urusi itatuma tani 25,000 hadi 50,000 za nafaka kwa kila nchi.

    Nchi hizo ni Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Afrika ya Kati, na Eritrea.

    Putin alisema, "Tutahakikisha pia kwamba hazinatumwa bure bila kulipa ada yoyote ya usafirishaji."

  18. Mwanafunzi nchini Mauritania ashtakiwa kwa kukufuru kuhusu karatasi za mtihani

    Mamlaka ya Mauritania imemshtaki mwanafunzi wa shule ya usekondaei kwa kukufuru kutokana na karatasi ya mtihani wa kuigiza aliyowasilisha.

    Mwanafunzi huyo wa kike mdogo alikamatwa wiki iliyopita kwa madai ya kutomheshimu Mtume Muhammad, mwanzilishi wa Uislamu.

    Ikiwa atapatikana na hatia, anaweza kuhukumiwa kifo bila uwezekano wa kukata rufaa.

    Mauritania imeimarisha sheria zake za kufuru katika miaka ya hivi majuzi, na kuondoa kipengele kinachoruhusu wahalifu kuepuka kifo ikiwa wataonyesha majuto.

    Hata hivyo, hakujakuwa na hukumu ya kunyongwa kwa kufuru nchini kwa zaidi ya miaka 30.

    Mwanafunzi huyo alikamatwa tarehe 18 Julai katika mji wa kaskazini-magharibi wa Atar kwa tuhuma za "kutoheshimu na kumdhihaki Mtume" na kutumia mitandao ya kijamii "kudhoofisha () maadili matakatifu ya Uislamu", afisa kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka wa umma katika mji mkuu, Nouakchott, aliliambia shirika la habari la AFP.

    Maelezo ya kina kuhusu kile alichodaiwa kuandika hayakutolewa.

    Familia ya mwanafunzi huyo baadaye ilitoa taarifa kwa gazeti la pan-Arabic Al-Quds al-Arabi ambapo waliomba msamaha, wakisema alikuwa na matatizo ya afya ya akili.

  19. Kevin Durant anasema 'kila mtu hutumia' bangi katika NBA

    Nyota wa mpira wa vikapu Kevin Durant amesema kuwa kamishna wa NBA aliweza kunusa harufu ya bangi alipokuwa akishawishi – kumalizika kwa marufuku ya ligi dhidi ya bangi.

    "Alinusa harufu nilipoingia ndani, kwa hivyo sikulazimika kusema mengi, unajua ninachosema?" Durant alisema katika mahojiano.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 aliongeza kuwa dawa hiyo inatumika sana kwenye ligi "ni kama mvinyo kwa wakati huu".

    Wachezaji wa NBA hawaruhusiwi tena kutumia bangi.

    Ligi hiyo na muungano wake, Chama cha Kitaifa cha Wachezaji wa Mpira wa Kikapu, walitia saini makubaliano mapya ya mazungumzo ya pamoja mwezi uliopita ambayo yataondoa dawa hiyo kwenye orodha yake ya dawa zilizopigwa marufuku.

    Mabadiliko hayo ya sera yalileta sifa kutoka kwa rapper Snoop Dogg, ambaye alisifu "faida zake za kiafya na jinsi inavyoweza kusaidia kupunguza tembe zote ambazo wamepewa na sindano".

    Wacheza hawajafanyiwa majaribio ya matumizi ya bangi tangu msimu wa ligi wa 2019-2020.

    Durant, mshambuliaji wa Phoenix Suns na mmoja wa wafungaji bora katika historia ya NBA, alikuwa miongoni mwa wale ambao binafsi walimshawishi kamishna wa NBA Adam Silver katika mkutano wa kusimamisha ligi kama adhabu kwa matumizi ya dawa hiyo.

  20. Tuna Mali: Wizara ya ulinzi ya Marekani yatuma barua pepe kwa mshirika wa Urusi kwa bahati mbaya

    Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeanzisha uchunguzi baada ya barua pepe zenye taarifa za siri kutumwa kwa mshirika wa karibu wa Urusikutokana na kosa la kimaandishi.

    Barua pepe hizo zilikusudiwa kutumwa kwa jeshi la Marekani, ambalo linatumia jina la siri la ".mil".

    Lakini walisahau herufi 'i', na hivyo ujumbe ulikwenda badala yake katikataifa la Afrika Magharibi la Mali.

    Maafisa wa ulinzi wanasema barua pepe hizo hazikuwa na habari zinazoweza kuathiri usalama wa utendakazi.

    "Tumeanzisha uchunguzi baada ya idadi ndogo ya barua pepe kutumwa kimakosa kwenye barua isiyo sahihi," msemaji wa Wizara ya ulinzi ya Marekani aliliambia shirika la habari la PA. "Tuna uhakika hawakuwa na taarifa yoyote ambayo inaweza kuathiri usalama wa uendeshaji au data ya kiufundi."

    Msemaji huyo aliongeza kuwa taarifa zote nyeti zinazotumiwa na idara ya serikali "zilishirikishwa kwenye mifumo iliyoundwa ili kupunguza hatari ya upotoshaji".

    "Wizara ya ulinzi mara kwa mara hukagua michakato yake na kwa sasa inafanya mpango wa kazi ili kuboresha usimamizi wa habari, kuzuia upotevu wa data, na udhibiti wa habari nyeti," msemaji huyo alisema.

    Mapema mwezi huu, iliibuka kuwa mamilioni ya barua pepe za kijeshi za Marekani pia yalitumwa nchini Mali, kwasababu za hitilafu sawa ya uandishi.

    Baadhi ya barua pepe hizo ziliaminika kuwa na taarifa nyeti zikiwemo nywila, rekodi za matibabu na ratiba za maafisa wakuu.

    Mali ilikuwa moja ya nchi sita za Kiafrika zilizoahidiwa kupelekewa nafakabila malipo na Rais wa Urusi Vladimir Putin baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya Bahari Nyeusi na Ukraine mapema mwezi huu.

    Jeshi la wanamaji la Urusi lilizuia bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine kufuatia uvamizi wake Februari 2022, na kukamata tani milioni 20 za nafaka ambazo zilikusudiwa kuuzwa nje ya nchi na kusababisha uhaba wa chakula katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika.

    Mali pia ni mshirika wa karibu wa Urusi kwa sababu mamluki wa Wagner wa Moscow wametumwa nchini humo kupigana pamoja na jeshi dhidi ya wanajihadi.

    Mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema waziri wa ulinzi wa Mali, mkuu wa jeshi la anga na naibu mkuu wa majeshi watawekewa vikwazo kwa kuratibu uenezi wa Wagner katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Jinsi Urusi inavyochukua nafasi ya Ufaransa katika makoloni yake ya zamani ya Kiafrika
    • Mtandao wa Wagner barani Afrika unakabiliwa na mustakabali usio na uhakika
    • Fahamu ni kwanini kumekuwa na mapinduzi na majaribio mengi ya mapinduzi Afrika