Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanajeshi 25 wauawa katika mlipuko wa bomu Somalia - Jeshi
Chanzo cha kijeshi cha Somalia kimeiambia BBC kwamba wanajeshi 25 wameuawa baada ya mwanamume mmoja kujilipua katika kambi ya Chuo cha Jale Siad
Moja kwa moja
Habari za hivi punde, Muungano wa upinzani Kenya waahirisha Maandamano ya Jumatano
Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya umesitisha maandamano ya kuipinga serikali yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kote nchini Jumatano wiki hii.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, muungano huo ulisema badala ya kuingia mitaani, watafanya "gwaride za mshikamano na mkesha kwa wahasiriwa wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali katika maeneo yote ya nchi."
Muungano huo umewahimiza wafuasi wake kujitokeza na kuwasha mishumaa na kuwawekea maua waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa hafla hiyo.
Azimio inasema hadi sasa, vifo 50 vimeripotiwa huku mamia ya wengine wakijeruhiwa na wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.
Idadi rasmi ya waliouawa katika machafuko hayo haijatolewa na serikali .
"Azimio imefanya uamuzi kwamba Jumatano, badala ya kwenda mitaani kwa maandamano ya amani kama ilivyotangazwa hapo awali, tutafanya maandamano ya mshikamano na mkesha kwa wahasiriwa wa ukatili wa polisi katika maeneo mbalimbali katika maeneo yote ya nchi," ilisema taarifa hiyo.
"Tunawahimiza Wakenya wajitokeze kuwasha mishumaa na kuweka maua katika kuwakumbuka na kuwaheshimu waathiriwa. ... tunawahimiza Wakenya kusali na kusoma majina ya waathiriwa wa ukatili wa polisi. Tutatoa orodha ya waathiriwa kwa wakati kwa ajili ya zoezi hilo."
Polisi waliovunja sheria kushtakiwa-Tume ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi Kenya
Tume ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi nchini Kenya, IPOA, inasema imewasilisha faili kadhaa kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP, ili kuwafungulia mashtaka maafisa wa polisi kwa kuvunja sheria wakati wa kukabiliana na waandamanaji nchini Kenya
Kwa wiki kadhaa sasa, Kenya imeshuhudia maandamano yanayoongozwa na upinzani nchini kupinga kupanda kwa gharama ya maisha, na polisi wamelaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na waandamanaji.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, shirika la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International liliripoti vifo vya watu zaidi ya 30, tangu kuanza kwa maandamano hayo.
Kamishna wa IPOA JM Waiganjo ameiambia BBC kwamba afisi yao imekuwa ikituma maafisa kisiri ili kujionea utendakazi wa polisi.
Hata hivyo waziri wa usalama wa ndani wa Kenya Kithure Kindiki ameshikilia kwamba polisi wataendelea kutumia kila mbinu inayofaa kukabiliana na wanaopora mali ya watu na kutekeleza uhalifu.Ameonya kwamba kuna wahalifu wanaohujumu usalama na uchumi wa nchi ambao wanatumia maandamano kutekeleza ouvu wao.
Kwingineko viongozi wa kanisa la katoliki nchini Kenya wamemtahadharisha rais William Ruto dhidi ya kusifia vitendo vya polisi wakati wanapokabiliana na waandamanaji .Wamehimiza kuwepo kwa mazungumzo kati ya pande hasimu za kiasiasa nchini Kenya ili kupata suluhisho kwa tofauti zilizoibuka kati ya serikali na upinzani .
Pingamizi zazidi kujitokeza katika mpango wa mikataba kati ya Tanzania na DP World
Mjadala juu makubaliano Kati ya Tanzania ya Serikali na Dubai kupitia kampuni ya DP World juu ya ustawishaji na uboreshaji wa utendaji kazi katika Bandari za Tanzania unaendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, huku pande mbili zinazotofautiana kwa hoja zikishikilia misimamo ya kuunga mkono ama kupinga makubaliano hayo.
Wale wanaopinga wanazidi kupaza sauti zao huku zahivi karibuni zaidi zikisikika jana Jumapili wakati viongozi kadhaa wa kisiasa ,wanasheria na viongozi wa dini walipofanya mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam.
Hoja za kupinga zimeendelea licha ya maelezo ya viongozi wa serikali kutetea makubaliano hayo huku Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni akitoa maelekezo ya wakosoaji wa mipango ya Taifa kushirikishwa.
Kwa kuzingatia hali hiyo mwanahabari wa BBC Scolar Kisanga amezungumza na Wakili Boniface Mwabukusi, ambaye ni mmoja watu wanaopinga mkataba huo na kwanza alimuuliza Changamoto hasa nini?
Serikali kwa upande wake inasema mambo mengi yanayoibuliwa na wakosoaji ikiwemo ukomo wa miaka ya uwekezaji yatapatiwa ufumbuzi katika mikataba mahsusi inayotarajiwa kuingiwa na mwekezaji huyo kabla ya kuanza kazi rasmi.
Unaweza pia kusoma
Waziri wa Ghana akamatwa baada ya kashfa ya pesa taslimu $1m
Waziri wa zamani wa Usafi wa Mazingira na Rasilimali za Maji wa Ghana Cecilia Dapaah amekamatwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Maalum (OSP) baada ya kuripotiwa wizi wa $1m (£780,000) pesa taslimu kutoka kwa nyumba yake.
Kulingana na OSP, waziri huyo wa zamani aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani siku ya Jumapili tarehe 22 Julai kwa "makosa yanayoshukiwa ya rushwa na ufisadi".
Raia wengi wa Ghana na wanaharakati wa kupinga ufisadi wamehoji ni vipi mtumishi wa umma anaweza kuwa na pesa nyingi hivyo kufichwa nyumbani kwao huku kukiwa na mzozo wa kiuchumi nchini Ghana.
"Bi Dapaah anahojiwa na Maafisa walioidhinishwa wa OSP," taarifa hiyo ilisema
Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo alikubali kujiuzulu kwake Jumamosi kufuatia malalamiko ya umma.
Pesa hizo zilifichuliwa baada ya wafanyakazi wake wawili wa nyumbani kushtakiwa kwa kuiba pesa taslimu $1m, pamoja na €300,000 na cedi milioni kadhaa za Ghana, pamoja na baadhi ya vitu vya kibinafsi.
"Ninaweza kusema kwa msisitizo kwamba takwimu hizo haziwakilishi kwa usahihi kile ambacho mimi na mume wangu tuliripoti kwa polisi, ninafahamu sana kuhusu uzito wa hadithi kama hizo karibu na mtu katika nafasi yangu," Bi Dapaah alisema.
"Nina nia ya kushirikiana kikamilifu na mashirika yote ya serikali ili kuwawezesha kubaini ukweli kikamilifu," aliongeza.
‘Walitaka kuweka silaha na dawa za kulevya katika boma la mwanangu’-Uhuru Kenyatta
Siku chache baada ya polisi kuvamia nyumba ya mwanawe Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, Jomo, Mkuu huyo wa zamani wa Nchi kwa mara nyingine amezungumza kuhusu kisa hicho akidai kuwa kulikuwa na mpango wa kumwekea bunduki na dawa za kulevya wakati wa operesheni ya Ijumaa usiku.
Wakati wa mkutano na wahariri wa habari mnamo Jumatatu, Bw Kenyatta pia alizungumzia madai ya kuhifadhi bunduki zinazodaiwa kushikiliwa na wanawe wawili, Jomo na Muhoho.
"Suala hili la bunduki limezingirwa na propaganda nyingi ili kugeuza mawazo kutoka kwa kile ambacho kimekuwa kikitokea nchini," aliwaambia waandishi wa habari
"Ninaamini walitaka kuweka dawa na bunduki katika boma la mwanangu."
Kenyatta aliyejawa na hasira anasema tukio hilo lilimuumiza.
"Nilienda kwa sababu ya simu ya dhiki kutoka kwa mwanangu; sikuwa mlevi, niliumia sana," alisema.
Rais huyo wa zamani anadai kuwa wanawe wawili wanamiliki bunduki sita kwa jumla, tatu kila mmoja, na kwamba bunduki zote zimesajiliwa kisheria.Alifafanua kuwa bintiye Ngina hamiliki bunduki.
Kulingana na Rais huyo wa zamani, hakuna hata mmoja wa wanawe ambaye amepokea amri ya kusalimisha silaha zake kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari na maafisa wakuu wa serikali.
Baada ya uvamizi wa nyumba ya mtoto wa rais huyo wa zamani ,serikali ilithibitisha kuvamia nyumba tatu katika eneo la Karen jijini Nairobi kutafuta bunduki 23 zinazodaiwa kutumika kutekeleza operesheni haramu nchini wakati wa maandamano ya kuipinga serikali .
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema vyombo vya usalama vimepewa jukumu la kupekua eneo hilo kama sehemu ya operesheni pana inayolenga kuwaondoa watu walio na silaha na viongozi wa magenge ya uhalifu yanayojulikana.
Kenyatta pia alifichua kuwa amelazimika kushiriki usalama wake na mamake, Mama Ngina Kenyatta, baada ya usalama wake kuondolewa wiki jana.
"Faida ambazo mama yangu anapata si kwa sababu yangu bali kwa sababu yeye ni Mama wa Kwanza wa zamani," alisema.
"Tumelazimika kuajiri walinzi wa kibinafsi." rais huyo wa zamani amesema
George Alagiah: Mwandishi mahiri wa habari wa BBC na msomaji habari afariki dunia
George Alagiah, mmoja wa waandishi wa BBC waliofanyakazi kwa muda mrefu na wanaoheshimika zaidi, amefariki akiwa na umri wa miaka 67, miaka tisa baada ya kugundulika kuwa na saratani.
Taarifa kutoka kwa wakala wake ilisema "alikufa kwa amani leo, akiwa amezungukwa na familia yake na wapendwa wake".
"George alipendwa sana na kila mtu aliyemfahamu, iwe ni rafiki, mfanyakazi mwenza au mwananchi.
"Alikuwa mtu wa kipekee. Mawazo yangu yako kwa wavulana na familia yake," alisema.
Alagiah alifariki mapema Jumatatu, lakini "alipigana hadi mwisho wenye uchungu", wakala wake aliongeza.
Mkurugenzi mkuu wa BBC Tim Davie alisema: "Katika BBC, sote tumehuzunika sana kusikia habari kuhusu George. Kwa wakati huu, tunaombea familia yake."
"George alikuwa mmoja wa waandishi wa habari bora na shupavu wa kizazi chake ambao waliripoti bila woga kutoka kote ulimwenguni na pia kuwasilisha habari bila dosari.
"Alikuwa zaidi ya mwandishi wa habari bora, watazamaji waliweza kuhisi wema wake, huruma na ubinadamu wa ajabu. Alipendwa na wote na tutamkosa sana."
Mswada wenye utata wapitishwa kuwa sheria huku maandamano yakiendelea Israel
Wabunge wa Israel wamepitisha kuwa sheria mswada wenye utata mkubwa licha ya maandamano makubwa yaliyolenga kuuzuia.
Sheria hiyo inaondoa mamlaka ya Mahakama ya Juu Zaidi kubatilisha hatua za serikali inazoziona kuwa zisizo na maana.
Ni ya kwanza katika msururu wa mageuzi yanayopingwa vikali yanayolenga kuzuia mamlaka ya mahakama kuidhinishwa.
Mageuzi hayo yaliyopangwa yamesababisha maandamano makubwa zaidi katika historia ya Israel, huku wapinzani wakionya kuwa yanaihatarisha Israel kama nchi yenye demokrasia.
Kwa upande wake, serikali inasema kuwa hatua hizo ni muhimu ili kurekebisha kukosekana kwa usawa katika mamlaka ambayo imesababisha mahakama kuingilia kati maamuzi ya kisiasa katika miongo ya hivi karibuni.
Jengo laporomoka na kusababisha vifo vya watu 33 Cameroon
Watu 33 wamefariki katika jiji kubwa la Cameroon baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka na kuangukia kwenye jengo jingine la makazi, wazima moto wamesema.
Tukio hili limetokea mapema Jumapili asubuhi katika mtaa wa Ange Raphaël wa Douala lakini sababu ya ajli hiyo bado haijafahamika.
Takriban watu 21 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa wanapokea matibabu katika hospitali ya karibu ya Laquintinie.
Msichana wa miaka mitatu ambaye alipelekwa hospitalini siku ya Jumapili alifariki baadaye.
Majirani waliofadhaika wamekuwa wakitafuta manusura kwenye vifusi pamoja na huduma za dharura.
Gavana wa mkoa, Samuel Dieudonné Ivaha Diboua, ametaka kuwatuliza watu - akisema hali imedhibitiwa na timu za uokoaji zitahakikisha hakuna mtu anayeachwa chini ya mabaki.
Afisa wa ngazi ya juu ameiambia BBC kuwa amesikitishwa sana kwamba maisha ya watu yamepotea licha ya hatua zilizopigwa katika miaka ya hivi karibuni kuimarisha usalama.
"Tumekuwa na furaha kutokumbwa na majanga kama hayo kwa muda sasa - hasa huko Douala ambako meya anajaribu kuleta utulivu," anasema Kizito Ngoa, mkuu wa Agizo la Wahandisi wa Ujenzi la Cameroon ambalo linadhibiti makazi nchini humo.
Tangu jengo kubwa la mwisho la Douala kuporomoka mwaka wa 2016, halmashauri ya jiji imekuwa ikizibomoa nyumba zinazoonekana kuwa hatarini kutokana na mafuriko au maporomoko ya ardhi, lakini jengo la ghorofa nne lililoporomoka siku ya Jumapili halikutengwa kwa ajili ya kubomolewa.
Wakazi waliambia wanahabari ilionekana kuwa mbovu lakini maafisa wa eneo hilo hawajathibitisha kilichosababisha ajali hiyo.
Katika taarifa ya Jumapili walimkumbusha yeyote anayetaka kujenga nyumba huko Douala kwamba lazima kwanza apate kibali rasmi na kisha na "kujenga tu muundo ulioidhinishwa".
Bw Ngoa anaambia BBC kwamba kushindwa kufuata sheria zilizowekwa ni mojawapo ya sababu kuu za kuporomoka kwa majengo kote nchini, na anasema gharama halisi ya mradi wa ujenzi inapaswa kuwekwa wazi kwa umma.
"Kuna hisia iliyoenea kwamba kila mtu anaweza tu kufanya kile anachotaka" na "ni wazi kuna hamu hii ya kuokoa pesa katika hatua zote za mradi".
Wakati mwingine wafanyakazi wa baraza wanashiriki katika hili, anasema, na vikwazo na maswali yanapotokea hayatangazwi vya kutosha.
Pia unaweza kutazama:
Wanajeshi 25 wauawa kwa mlipuko wa bomu Somalia - Jeshi
Chanzo cha kijeshi cha Somalia kimeiambia BBC kwamba wanajeshi 25 waliuawa wakati mwanamume mmoja alijitengenezea vilipuzi na kujilipua miongoni mwa wanajeshi waliokuwa wamepanga foleni katika kambi ya Chuo cha Jale Siad.
Hata hivyo, jeshi halijatoa maoni yoyote rasmi kuhusu tukio hilo.
Wengine 48 walisemekana kujeruhiwa na kupelekwa hospitalini mjini Mogadishu.
Mtu aliyejilipua alikuwa amevalia sare za kijeshi na aliingia kambini akiwa na utambulisho wa uongo, chanzo cha kijeshi ambacho hakikutaka kutajwa jina kimeiambia BBC.
Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab limesema kuwa mmoja wa wapiganaji wake ndiye aliyetekeleza shambulio hilo, na kusema kuwa wanajeshi 73 wameuawa na 124 wamejeruhiwa.
Pia unaweza kusoma:
Uingereza:Wanawake wawili wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja washinda kesi ya kuingizwa mbegu za kiume kwa njia isiyo ya asili
Wanawake wawili wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wameshinda kesi inayohusisha taratibu za matibabu ya uzazi wanaoielezea kama "ya ubaguzi".
Meghan na Whitney Bacon-Evans wote walitaka mapitio ya mahakama ya masharti tofauti kwa wapenzi wa jinsia moja wanaotafuta usaidizi wa uzazi kutoka kwa NHS.
Walitangaza kuwa wameondoa hatua walizochukua, wakisema walikuwa wamewasiliana na mamlaka ya afya ya Uingereza kuhusu kukabiliana na kile walichokiona kama ukosefu wa usawa.
Mamlaka ziliombwa kujibu maswali kuhusu kesi hiyo.
Wanawake hao wawili, waliojitokeza kwenye kipindi cha Say Yes To The Dress TV, walisema kwamba walitakiwa kufanyiwa majaribio 12 ya kuwezesha uzazi kwa njia isiyo ya asili kwa gharama zao wenyewe, kwa makumi ya maelfu ya pauni, ili kuwaruhusu kupokea usaidizi wa NHS.
Wanandoa wa jinsia tofauti ambao wamekuwa wakijaribu kwa miaka miwili kupata mimba wana haki ya kupokea matibabu moja kwa moja kwa gharama ya mamlaka ya afya, tunafurahi kutangaza kwamba kesi yetu imekamilika kwa ushindi, "Meghan na Whitney walisema katika chapisho la Instagram Jumamosi.
"Tunafutilia mbali hatua zetu, kwa kuwa Frimley Council (inayowakilisha mamlaka ya afya) inatambua hitaji la kusasisha sera yake ili kuondoa ukosefu wa usawa kati ya wapenzi wa jinsia moja ikilinganishwa na wapenzi wa jinsia tofauti."
"Pamoja na dhamira ya serikali ya kuondoa vizuizi vya kupata IVF kwa wapenzi wa jinsia moja mwaka wa 2023, hii inatufanya tuwe na matumaini makubwa kwa familia ya LGBTQ."
Soma zaidi:
Sadio Mane: Mshambuliaji wa Bayern Munich anazingatia ofa kutoka kwa Al-Nassr ya Saudi Arabia
MSHAMBULIAJI wa Bayern Munich, Sadio Mane anafikiria ofa ya kujiunga na klabu ya Al-Nassr ya Saudi Arabia Pro League.
Mane, 31, anaonekana kutofautiana na mabingwa hao wa Bundesliga baada ya kuwa na msimu mbaya wa kwanza kufuatia uhamisho wa pauni milioni 35 kutoka Liverpool msimu uliopita.
Ripoti zinaonyesha Bayern wako tayari kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal, huku meneja Thomas Tuchel akisema Mane "alikosa kuafikia matarajio".
Mane amezungumza na Al-Nassr lakini hakuna mpango wowote ambao umekubaliwa na klabu hiyo ya Saudia.
Iwapo Mane atahama, ataungana na fowadi wa zamani wa Manchester United Cristiano Ronaldo, huku aliyekuwa Devil Red Alex Telles na mchezaji wa kimataifa wa Croatia Marcelo Brozovic wote wakiwa wamejiunga na klabu hiyo msimu huu wa joto.
Baada ya kucheza vizuri Anfield ambapo alishinda Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Premia, Mane alihamia Ujerumani msimu uliopita wa joto akisema ulikuwa "wakati mwafaka kwa changamoto hii".
Lakini wakati wake huko umegeuka kuwa mbaya baada ya ripoti kuwa alimpiga mchezaji mwenzake Leroy Sane kufuatia kushindwa kwa Ligi ya Mabingwa na Manchester City mnamo Aprili ambapo aliondolewa kwenye kikosi na pia faini.
Mane aliichezea Bayern mechi 38 msimu uliopita, akifunga mabao 12, na bosi Tuchel aliongeza: "Hali ya ushindani ni ya juu sana, nafasi ya kuanzia si rahisi kwake.
"Mchezaji anajua hilo pia, anajua maoni yangu na maoni ya klabu."
Lori la mafuta lalipuka na kusababisha vifo vya watu wanane kusini magharibi mwa Nigeria
Takriban watu 8 wamethibitishwa kufariki kutokana na mlipuko wa lori la mafuta katika jimbo la Ondo Kusini Magharibi mwa Nigeria baada ya wakaazi kuchota mafuta kutoka kwa lori hilo lililopata ajali ya barabarani Jumapili usiku.
Kamanda wa polisi wa jimbo la Ondo amesema lori lililokuwa limepakia mafuta lilianguka kando ya barabara, na mafuta karibu yote yakimwagika kabla ya wakaazi kukimbilia eneo la tukio kuchukua mafuta.
"Lori hiyo ya mafuta ililipuka yenyewe na kuua watu 8 huku wengine wengi wakijeruhi ambao kwa sasa wanatibiwa hospitalini" msemaji wa Polisi aliambia BBC.
Wakaazi na walioshuhudia wanasema lori hilo lililipuka katika mtaa ulio karibu na kituo cha mafuta, na jengo la kanisa lakini hakuna aliyeathiriwa na moto huo.
Nigeria imerekodi ongezeko la karibu 400% la bei ya mafuta tangu Juni kufuatia kuondolewa kwa malipo ya ruzuku na Rais Bola Tinubu, hatua ambayo imezidisha gharama ya juu ya maisha na bei za bidhaa, lakini serikali inaamini inalenga kuokoa mapato na kurejesha fedha za ruzuku ya mafuta kwa sekta zingine.
Mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika huagiza zaidi ya 90% ya mahitaji yake ya mafuta kutokana na kutokuwa na uwezo wa kusafisha mafuta ghafi ndani ya nchi kwa sababu mitambo yake minne ya kusafisha mafuta haifanyi kazi.
Pia unaweza kusoma zaidi:
China: Watu 11 wafariki baada ya paa kuangukia timu ya mpira wa wavu ya wasichana
Watu 11 wamefariki baada ya paa la jumba la mazoezi la shule kaskazini-mashariki mwa Uchina kuporomoka lilipokuwa likitumiwa na timu ya mpira wa wavu ya wasichana, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.
Wengi wa waathiriwa ni watoto, walioshuhudia waliambia vyombo vya habari vya ndani ingawa hii bado haijathibitishwa rasmi.
Wazazi waliofadhaika wamekusanyika katika hospitali iliyo karibu kutafuta kujua hali ya wana wao.
Ni watu wanane pekee kati ya 19 waliokuwa ndani ya ukumbi wa mazoezi katika mkoa wa viwanda wa Heilongjiang walionusurika.
Polisi wamewazuilia wakuu hao katika kampuni ya ujenzi ya eneo hilo, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Wameshutumiwa kwa kutupa ‘perlite’, aina ya glasi ya volkeno, juu ya paa la ukumbi wa mazoezi wakati wakifanya kazi yao kwenye mradi wa jengo lililo karibu.
Madini hayo yalikuwa yamelowa maji ya mvua kufuatia mvua kubwa iliyonyesha, ambayo ilipelekea paa kuporomoka saa 15:00 kwa saa za huko (07:00 GMT).
Kocha wa timu ya voliboli ya wasichana ya shule ya sekondari alisikika akitoa majina ya wanafunzi huku timu za uokoaji zikipitia vifusi katika mji wa Qiqihar, iliripoti Radio ya Taifa ya China.
Wazazi wamewakosoa maafisa wa shule, wakisema kumekuwa na ukosefu wa mawasiliano sahihi kuhusu juhudi za uokoaji, ambazo zilidumu hadi Jumatatu asubuhi.
"Wananiambia binti yangu amefariki lakini hatukuwahi kumuona mtoto. Watoto wote nyuso zao zilikuwa zimetapakaa tope na damu walipopelekwa hospitalini. Niliomba, tafadhali nimtambue huyo mtoto. Itakuwaje kama huyo si mtoto wangu?," mtu mmoja alisema kwenye video ambayo imesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii.
"Je, [mamlaka] wamekuwa wakifanya nini saa nne, tano, au hata sita baada ya watoto kupelekwa hospitalini? ... Madaktari hawawasiliani nasi kuhusu jinsi uokoaji unavyoendelea.
"Tuna wazee nyumbani, tunahitaji [kuwasaidia] kujiandaa kiakili. Kuna madaktari, maafisa wa polisi na viongozi wengine wa serikali hapa. Lakini hatujasikia chochote kutoka kwako," alisema.
Watumiaji wengi kwenye mitandao ya kijamii nchini humo walijadili wasiwasi kutoka kwa baba huyo kwenye video hiyo, wakihoji jinsi polisi na maafisa kwenye eneo la tukio, wanavyowafanyia wazazi waliokuwa na wasiwasi.
"Je, watu hawana maana kwao?"aliandika mtumiaji mmoja mwenye hasira.
Wengine walihoji kwanza kwa nini perlite ilikuwepo kwenye paa la ukumbi wa mazoezi hapo.
"Gharama ya kuvunja sheria ni ndogo sana katika nchi hii, watu hawana heshima yoyote kwa sheria, hiyo ndiyo sababu kuu," mtumiaji mwingine aliandika.
Watu tisa wafariki katika ajali ya ndege Port Sudan - jeshi
Jeshi la Sudan linasema watu tisa wamefariki katika ajali ya ndege iliyotokea katika uwanja wa ndege wa Port Sudan.
Ilisema ndege ya kiraia ya Antonov ilipata hitilafu ya kiufundi ilipokuwa ikipaa.
Wanajeshi wanne walikuwa miongoni mwa waliofariki.Msichana mdogo anaripotiwa kunusurika kwenye ajali hiyo.
Zaidi ya watu milioni tatu wameyakimbia makazi yao tangu mapigano kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF yalipozuka katikati ya mwezi wa Aprili, huku mzozo huo ukiwa hauonyeshi dalili za suluhu.
'Mandonga afurahia kipigo Kenya kuzichapa tena na Mganda Jumamosi hii'
Bondia mwenye mbwembwe na tambo nyingi Karim Mandonga wa Tanzania amesema anafurahia matokeo ya pambano lake la mwishoni mwa wiki dhidi ya Daniel Wanyonyi wa Kenya licha ya kupoteza pambano hilo.
Akizungumza na NTV ya Kenya mara baada ya Pambano hilo Mandonga alisema " Siku ya leo naona ilikua bahati yake kunaliza raundi tu ndio bahati yake lakini hakuna siku nakosea, kwa sababu kama nakosea angenipiga KO(Knockout), mimi nmempiga yule KO".
Mandonga akaongeza " kwa hiyo mimi hakuna la kukosea naona mchezo ndivyo ulivyo, ukimaliza kuna matokeo matatu suluhu, kushinda au kushindwa, kwa hiyo mimi nimekubaliana na matokeo yalitokea leo (usiku wa kuamkia Julai 23,2023), nmefurahi sana kwa hiyo, ila tuangalie rematch (pambano la marudiano), tuone nini kinaendelea, ndani ya Kenya".
Katika Mapambo hilo la raundi 10 uzani wa Light heavyweight lililofanyika jijini Nairobi usiku wa kuamkia Julai 23,2023, Majaji wote watatu walimpa Wanyonyi ushindi.
Jaji George Athmani alimpa Wanyonyi alama 100-80, Jaji Wycliffe Marende 100-80, na Jaji Leonard Wanga 100-89.
Hili ni Pambano la pili kwa mabondia hao wa Afrika Mashariki kukutana, pambano la kwanza lililofanyika Januari 2023 huko huko Nairobi, Mandonga alimchapa Wanyonyi.
Wakati huo huo Julai 29,2023 Bondia huyo mkazi wa Morogoro anatarajiwa kupanda tena ulingoni kuzichapa na Mganda Moses Golola
Pambano hilo kwenye Usiku wa Vitasa litafanyika jijini Mwanza akiwa na ngumi mpya inayoitwa Ndukube.
Mandonga anasema ukipigwa ngumi hiyo kwa mkono wa kulia unageuka kichuguu na ukipigwa kwa mkono wa kushoto unapata fangasi.
Unaweza pia kusoma:
- Karim Mandonga: 'Katika watoto wangu wote huyu Shariff ndiye atakayekuwa mtu kazi'
- Mzaha mzaha tu Mandonga anauheshimisha mchezo wa ngumi Afrika Mashariki
DRC: Mwanajeshi akamatwa baada ya kuwapiga risasi na kuwaua watu 13
Askari ambaye aliwaua watu 13 nchini DRC alikamatwa jana mwendo wa saa nane mchana Msemaji wa Jeshi la Kongo alisema.
Luteni Jules Ngongo aliambia BBC kwamba mwanajeshi huyo anazuiliwa Kasenyi, kituo cha jeshi la wanamaji, katika Mkoa wa Ituri wenye matatizo. Askari huyo ambaye jina lake halikufahamika aliua watu 13 wakiwemo watoto 9 Jumamosi iliyopita katika kijiji cha Nyakova.
Wakazi wanasema mwanajeshi huyo alifyatua risasi wakati wa mazishi kwa sababu alikasirika kupata kuwa mwanawe alizikwa kabla ya kufika kijijini, kutoka uwanja wake wa vita.
Ni nini kilimchochea?
Majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini yamekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu 2021
Gazeti la Bunia-Actualité linaripoti kwamba askari huyo aliondoka eneo alilokuwa akifanya kazi na kwenda nyumbani baada ya kupata habari kwamba mwanae amefariki.
Inasemekana mwanae alifariki Alhamisi tarehe 20 na akazikwa Ijumaa jioni, bila baba yake kufika.
Mwanawe alidaiwa kufariki dunia kwa kifo cha kawaida baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Tchomia ambako alifariki dunia.
Baba aliporudi nyumbani na kumkuta mtoto wake amezikwa, alikasirika na kupiga risasi kati ya majirani waliofika kuifariji familia.
Radio Okapi inaripoti kuwa miongoni mwa wengine waliopigwa risasi na mwanajeshi huyo ni watoto wake wawili.
Luteni Ngongo anasema hilo ni suala la ‘kinidhamu’. Anasema askari huyu akikamatwa atashitakiwa mahakamani.
Mmiliki wa Twitter Elon Musk amesema anataka kuondoa nembo ya ndege ya Twitter, na badala yake kuweka "X".
Picha ya nembo mpya ya Twitter, X nyeupe kwenye iliyowekwa kwenye rangi nyeusi nyuma, imezinduliwa na afisa mkuu mtendaji wa Twitter, baada ya mmiliki wake Elon Musk kusema anataka kuondoa nembo ya ndege.
Katika ujumbe wake wa Twitter aliochapisha Jumatatu asubuhi, Linda Yaccarino alisema "X yuko hapa! Hebu tufanye hivi."
Bw Musk pia alibadilisha picha yake ya wasifu na kuweka nembo mpya na kuongeza "X.com" kwenye wasifu wake wa Twitter.
Kulingana na ripoti, anataka kuunda "super app" inayoitwa "X".
Siku ya Jumapili, bilionea huyo alisema anatazamia kubadilisha nembo ya Twitter, ambapo alituma ujumbe wa Twitter : "Na hivi karibuni tutaomba radhi kwa chapa ya Twitter na, pole pole, ndege wote."
Alisema pia kwamba nembo ya muda ingeonyeshwa moja kwa moja baadaye siku hiyo hiyo.
Bw Musk alichapisha picha ya "X" iliyopeperushwa kwenye Twitter, na baadaye katika mazungumzo ya sauti ya Twitter Spaces, alijibu "Ndiyo" alipoulizwa ikiwa nembo ya Twitter itabadilika, akiongeza kuwa "mabadiliko haya yalipaswa kufanyika muda mrefu uliopita".
Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Linda Yaccarino, aliandika kwenye jukwaa kwamba urejeshaji wa chapa hiyo ulikuwa fursa mpya ya kusisimua.
Bwana Musk alishutumiwa kwa biashara ya ndani na kundi la wawekezaji wa Dogecoin, ambao walidai kuwa alifaidika kutokana na kuongeza thamani ya Dogecoin.
Kampuni hiyo ilikosolewa na watumiaji na wenye masoko ya mitandaoni Bw Musk alipotangaza mapema mwezi huu kwamba kutakuwa na kikomo cha idadi ya jumbe za twitter kwa siku.
Vikomo vya kila siku vya jumbe za Twitter vilisaidia katika ukuaji wa jukwa la Threads la huduma pinzani zinazomilikiwa na kampuni ya Meta, ambazo zilikuwa na usajili zaidi ya milioni 100 katika siku tano za kuzinduliwa.
Masaibu ya hivi karibuni zaidi ya witter ilikuwa ni kesi iliyowasilishwa Jumanne ambayo ilidai kuwa kampuni hiyo inadaiwa angalau $500m (£388.7m) ya malipo ya kuwasimisha kazi wafanyikazi wake zamani.
Tangu Bw Musk alipoinunua, kampuni hiyo imepunguza zaidi ya nusu ya wafanyikazi wake.
Vita vya Ukraine: Urusi yasema itachukua udhibiti wa usafirishaji wa nafaka zinazokwenda Afrika kutoka Ukraine
Rais Putin alisema kuwa atasafirisha ngano moja kwa moja barani Afrika na ataichukua Ukraine.
‘’Urusi itaendelea na juhudi zake kubwa za kutoa usambazaji wa nafaka, bidhaa za chakula, mbolea na bidhaa nyingine kwa Afrika’’, Putin alisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Kremlin.
Nataka kutoa hakikisho kwamba nchi yetu ina uwezo wa kuchukua nafasi ya nafaka za Ukraine kwa misingi ya biashara na bila malipo.’’
Alisema hayo baada ya kujiondoa kwenye mkataba wa mauzo ya ngano uliojadiliwa na Umoja wa Mataifa.
Taarifa kutoka Moscow ilisema kuwa ngano itauzwa nje kwa bei ya chini. Kwa hivyo hii inamaanisha nini kwa Urusi na Afrika.
Operesheni ya kijeshi ya Moscow ilizuia bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine hadi makubaliano yaliyosimamishwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki na kutiwa saini Julai 2022 kuruhusiwa kuidhinisha usafirishaji wa nafaka muhimu.
Aidha Putin aliandika kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya Kremlin kuwa kuhusu sababu za kukataa kwa Moscow kurefusha mkataba wa nafaka uliosimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa na iliyoundwa kutatua tatizo la uhaba wa chakula lililojitokeza kwenye soko la dunia baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Hii ilitishia njaa katika baadhi ya nchi maskini zaidi duniani, zikiwemo zile za bara la Afrika.
Putin anadai kuwa mpango huo haukutimiza malengo yake, na nchi za Magharibi ziliutumia kujinufaisha kibiashara."Mkataba" huu, ambao uliwasilishwa hadharani katika nchi za Magharibi kama dhihirisho la kujali kwao na manufaa kwa Afrika, kwa kweli ulitumiwa bila aibu kutajirisha biashara kubwa za Marekani na Ulaya ambazo zilisafirisha na kuuza tena nafaka kutoka Ukraine," rais wa Urusi alisem
Kulingana naye, katika mwaka wa mpango huo, Ukraine iliuza nje "jumla ya tani milioni 32.8 za shehena, ambayo zaidi ya 70% ilienda kwa nchi zenye viwango vya juu na vya juu vya mapato ya kati, pamoja na Jumuiya ya Ulaya, wakati nchi kama Ethiopia, Sudan na Somalia, pamoja na Yemen na Afghanistan, zilichukua chini ya 3% ya jumla - chini ya tani milioni moja."
Wakati huo huo, Putin aliahidi kwamba Urusi "ina uwezo wa kuchukua nafasi ya nafaka ya Kiukreni kwa misingi ya kibiashara na bila malipo."
Hata hivyo, Ijumaa iliyopita Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths alisema wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama kwamba kujiondoa kwa Urusi kwenye mkataba wa nafaka "kuna uwezekano wa kutishia mamilioni ya watu kwa njaa na mbaya zaidi."
"Wengine watakosa lishe bora, wengine watakufa njaa, watu wengi watakufa kutokana na maamuzi haya," Griffiths alisema.
Ahirika la habari la Reuters linaeleza katika taarifa yake kuwa , Umoja wa Mataifa daima umeamini kuwa makubaliano ya kuuza nafaka ya Kiukreni nje ya nchi husaidia hasa nchi maskini zaidi, na kuchangia kushuka kwa bei ya vyakula - tangu Machi mwaka jana, imeshuka kwa zaidi ya 23%.
Wakati huo huo, mara tu baada ya mpango wa nafaka kukoma kufanya kazi, bei ya nafaka kwenye masoko ya dunia ilianza kupanda kwa kasi zaidi tangu uvamizi wa Urusi wa Ukraine mnamo Februari 2022.
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
Marufuku ya saluni ya Taliban: Wanawake wa Afghanistan wanaomboleza mwisho wa huduma iliyothaminiwa
Saluni za nywele na urembo kote Afghanistan zitafungwa katika wiki zijazo kwa amri ya Taliban.
Kufungwa kwao kutasababisha kupotea kwa kazi zinazokadiriwa kufikia 60,000.
Saluni zilikuwa zimeruhusiwa kuendelea kufanya kazi tangu Taliban kuchukua tena mamlaka miaka miwili iliyopita, lakini ilibadilisha msimamo wake mwezi uliopita.
Uamuzi huo zaidi unazuia nafasi wazi kwa wanawake wa Afghanistan, ambao tayari wamezuiliwa kuingia madarasani, kumbi za mazoezi na bustani.
Zarmina mwenye umri wa miaka 23 alikuwa katika saluni akipaka nywele zake rangi ya kahawia iliyokolea wakati habari za kufungwa kwa karibu zilipokuja.
"Mmiliki alipata mshtuko mkubwa na kuanza kulia. Yeye ndiye mlezi wa familia yake," mama huyo wa watoto wawili alisema.
"Sikuweza hata kutazama kioo wakati nyusi yangu inafanywa. Kila mtu alikuwa akitokwa na machozi. Kulikuwa kimya."
Neema na uzuri
Madina hufunika kichwa chake na kitambaa wakati anaondoka nyumbani. Mume wake tu na washiriki wa kike wa familia yake wanaweza kuona nywele zake za rangi.
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 anaishi Kabul, na anafuata kwa makini mitindo mipya ya urembo mtandaoni.
"Kila mwanamke ninayemjua anapenda kuboresha mtindo wake. Ninapenda mitindo ya hivi punde na kujipodoa."
Anasema kwenda saluni kumeweka ndoa yake safi.
“Mume wangu anapenda sana kuona nywele zangu zikiwa na rangi tofauti na kukatwa kwa mitindo tofauti.
"Kila mara hunipeleka kwenye saluni na kungoja kwa subira mlangoni," anasema kwa fahari.
"Anapongeza sura yangu ninapotoka, ambayo inanifanya nijisikie vizuri."
Matarajio yake yalikuwa kuwa wakili lakini Taliban walisimamisha wanawake kwenda chuo kikuu. Hajaweza kupata kazi kwani wanawake pia wamepigwa marufuku kutoka kwa majukumu mengine mengi.