"Siku elfu moja ni muda mrefu sana kizuizini," anasema Nick Coyle.
Anazungumzia kilichokuta mpenzi wake, mwandishi wa habari wa Australia Cheng Lei, ambaye bado anazuiliwa katika gereza la China.
Maelezo kuhusu mashtaka dhidi yake bado yamewekwa siri na hajahukumiwa.
Kama marafiki na familia nyingine za Bi Cheng, Bw Coyle anasema hailewi kwa nini Cheng anapitia madhila kama haya.
"Nitoa wito kwa mamlaka husika nchini China kutatua hali hii mbaya haraka iwezekanavyo," anaiambia BBC.
Cheng Lei alikuwa akifanya kazi kama mwandishi wa taarifa za biashara katika kituo cha televisheni cha taifa cha China cha CGTN alipokamatwa ghafla na maafisa wa usalama wa serikali tarehe 13 Agosti 2020, na baadaye kushutumiwa kwa "kutoa siri za serikali nje ya nchi kinyume cha sheria".
Miezi yake sita ya kwanza alizuiliwa katika kifungo cha upweke, akidhibitiwa vikali ingawa alihojiwa bila kuwa na wakili.
Tangu wakati huo, amekuwa akizuiliwa pamoja na wafungwa wengine.
Kesi yake ilifanyika faraghani mwezi Machi mwaka jana.
Balozi wa Australia nchini China Graham Fletcher alinyimwa kuingia mahakamani.
Lakini hukumu yake imeahirishwa mara kwa mara.
Juhudi za BBC kuwasiliana na maafisa wa kwa Mahakama ya Beijing, ambako kesi yake ilifanyika, hazikufaulu.
Bw Coyle - mtendaji mkuu wa zamani wa Chama cha Wafanyabiashara wa China-Australia - sasa ameondoka Beijing lakini anaendelea kufuatilia suala hilo kutoka ng'ambo wa ajili ya kuachiwa kwake.
Wizara ya mambo ya nje ya China imejaribu kupunguza wasiwasi wa kimataifa kuhusu kesi hiyo.