Urusi yatoa masharti ya kusitisha vita Ukraine

Urusi imesema kuwa inaweza kusitisha operesheni "wakati wowote" ikiwa Ukraine itatimiza masharti ya Urusi.

Moja kwa moja

  1. Polisi Kenya yawasaka waendesha boda boda waliomshambulia nusu uchi mwanamke Nairobi

    Bodaboda

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Polisi nchini Kenya wameanzisha msako mkali kwa waendesha bodaboda walionaswa kwenye kamera wakimshambulia dereva wa mjini Nairobi.

    Katika video hiyo ya kutisha, mwanamke huyo anaonekana akipiga mayowe huku akijaribu kujinasua kutoka kwenye mikono ya wanaume hao ambao walikuwa wakijaribu kumvua nguo huku wengine wakiamuru atolewe ndani ya gari.

    Genge hilo lilimmuweka nusu uchi mwakamke huyo.

    Inadaiwa kuwa gari aliyokuwa anaendesha mwanamke huyo ilihusika kwenye ajali iliyohusisha mwendesha pikipiki, au boda boda, kama wanavyojulikana nchini Kenya.

    Video hiyo imezua taharuki nchini humo. Wakenya mtandaoni wametaka hatua zichukuliwe na wanaharakati wakiishutumu serikali kwa kuruhusu uvunjaji wa sheria kuongezeka miongoni mwa waendesha pikipiki.

    Inaelezwa kuwa waendesha bodaboda huendesha bila tahadhari na mmoja wao anapohusika kwenye ajali wengine hujitokeza kwa wingi na kuwashambulia na kuwatisha waendesha magari.

    Mwaka 2020, kundi la waendesha pikipiki lilinaswa kwenye kamera likimshambulia dereva katika barabara kuu ya Thika baada ya kuripotiwa kumpiga mwenzao.

  2. Tanzania yazungumza na Urusi ili kuwaondoa kwa usalama raia wake walioko Ukraine

    Ukraine

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tanzania imesema imezungumza na Urusi kuhusu wanafunzi wake wanaosoma katika chuo kikuu cha Ukraine karibu na Kharkiv, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

    Ubalozi wa Tanzania mjini Moscow sasa umewataka raia wake wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Sumy State mashariki mwa Ukraine kuelekea kwenye mpaka wa Urusi, kwa mujibu wa gazeti la kibinafsi la Mwananchi.

    "Taarifa kutoka ubalozi wa Tanzania... alitoa wito kwa wanafunzi hao kuelekea Sudja ambako watapokelewa na jeshi la Urusi," ripoti hiyo imesema.

    "Kutoka Sudja, watasafirishwa na jeshi kwenda Belgorod [nchini Urusi] ambako watakaribishwa na maafisa kutoka ubalozi wa Tanzania mjini Moscow kwa ajili ya kufanya maandalizi kabla ya kurejea nyumbani Tanzania," ilisema taarifa hiyo.

    "Ubalozi pia umewashauri wanafunzi kuondoka chuoni hapo kwa makundi na kubeba bendera ya Tanzania kwa ajili ya utambulisho wakati wakipita katika ukanda salama," ilisema ripoti hiyo.

    Tangazo la ukanda (njia) salama limekuja baada ya mazungumzo ya kidiplomasia na Urusi, ripoti hiyo imesema.

    Televisheni ya binafsi ya ITV ilichapisha taarifa hiyo kutoka ubalozi wa Tanzania mjini Moscow. Haikufahamika mara moja ni wanafunzi wangapi wa Tanzania walioko Sumy. Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa zaidi ya wanafunzi 400 wa Kitanzania huko Odesa na 200 huko Kyiv tayari wamefanikiwa kuondoka Ukraine.

  3. Mpatanishi wa Ukraine ataka kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya raia

    Wakati duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine ikianza, mjumbe wa Ukraine Mykhailo Podolyak ameitaka Urusi kusitisha mashambulizi dhidi ya raia.

    Katika ujumbe wa Twitter, anasema: "Katika dakika chache, tutaanza kuzungumza na wawakilishi wa nchi ambayo inaamini sana vurugu kubwa dhidi ya raia ni hoja. Kuthibitisha kwamba hii sio kesi."

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  4. Habari za hivi punde, Urusi yatoa masharti ya kusitisha vita Ukraine

    Rais wa Urusi Vladimir Putin

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi imesema kuwa inaweza kusitisha operesheni "wakati wowote" ikiwa Ukraine itatimiza masharti ya Urusi.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Ukraine lazima itambue Crimea kama Urusi, na Donetsk na Luhansk kama mataifa huru.

    Mbali na hayo, Peskov anasema Ukraine lazima irekebishe katiba yake na kukataa madai ya kuingia katika kambi yoyote (kama vile Nato, kwa mfano).

    Anaongeza kuwa Urusi itamaliza "kuondoa jeshi" kwa Ukraine, na ikiwa masharti haya yatatimizwa hatua za kijeshi za Urusi "zitakoma mara moja".

    Msemaji wa Kremlin amesisitiza kuwa Urusi haitaki kutoa madai yoyote zaidi ya eneo nchini Ukraine.

  5. Rais wa Ukraine atoa wito wa vikwazo zaidi dhidi ya Urusi

    Volodymyr Zelensky

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky atoa wito wa vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.

    Akizungumza katika mkutano wake wa kila siku, Zelensky anasema uvamizi unaoendelea unaonesha kwamba "Urusi haijaacha mipango yake dhidi ya Ukraine" - kwa hivyo, anaongeza, "tunahitaji kifurushi kipya cha vikwazo".

    Zelensky ametoa wito wa "kususia uuzaji nje wa Urusi, haswa kukataliwa kwa bidhaa za mafuta kutoka Urusi". Anaongeza kuwa hatua hizi kali "zinaweza kuitwa zuio, au maadili tu".

  6. Mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Ukraine kukutana

    Sergei Lavrov

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba siku ya Alhamisi mjini Antalya, Uturuki.

    Mkutano huo unafanyika huku Urusi ikiendelea na uvamizi wake nchini Ukraine.

    Ukraine inasema mashambulizi ya roketi yameendelea kwenye maeneo ya makazi katika miji kadhaa, na kwamba mji mkuu wa Kyiv unaweza kukabiliwa na mashambulizi ya kila namna.

    Mazungumzo ya awamu ya tatu kuanza hivi karibuniAwamu ya tatu ya mazungumzo inatarajiwa kufanyika kati ya wapatanishi wa Ukraine na Urusi katika muda wa saa chache.

    Sasa tumesikia zinatarajiwa kuanza saa 16:00 saa za Kyiv (14:00 GMT), kulingana na maafisa wa Ukraine

  7. Marekani na washirika 'tayari kukabiliana na tishio lolote' - Blinken

    Antony Blinken

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, ambaye yuko kwenye ziara nchini Lithuania, anasema Urusi imejaribu "kudhoofisha demokrasia ya Lithuania na kusababisha mgawanyiko kwa mashambulizi ya mtandao na habari za upotoshaji ''.

    Pia anasema Marekani na nchi mwenyeji wake "zimeungana katika azimio letu la kusimama na Ukraine", huku uvamizi wa Urusi ukifikia siku yake ya 12.

    Marekani ilikuwa ikiimarisha "ulinzi wetu wa pamoja", anasema, hivyo Marekani na washirika wako tayari "kukabiliana na tishio lolote" - ikiwa ni pamoja na kutuma vikosi vingine 7,000 vya Marekani huko Ulaya, na kuweka upya vingine "kuipa nguvu Nato ". Katibu Blinken alisisitiza dhamira "takatifu" ya Marekani kwa kifungu cha 5 cha Nato - "shambulio dhidi ya mtu mmoja ni shambulio kwa wote" - akisisitiza: "Tutalinda kila nchi iliyo kwenye mwamvuli wa Nato."

  8. Zelensky aapa kuwaadhibu wanaofanya ukatili dhidi ya Ukraine

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Volodymyr Zelensky amesema kila mtu atakayefanya ukatili dhidi ya raia wa Ukraine ataadhibiwa.

    Amesema raia wa Ukraine hawatasamehe au kusahau, na kuwashutumu wanajeshi wa Urusi waliovamia na kufanya mauaji ya makusudi.

    "Hakutakuwa na mahali pa utulivu Duniani kwako. Isipokuwa kaburi," rais alisema. Maafisa wa Ukraine wanasema Urusi inalenga shabaha kwa raia kote nchini, zikiwemo hospitali, vitalu na shule.

    Lakini Urusi inakanusha kuwalenga raia, ikisema kuwa inatekeleza "operesheni maalum ya kijeshi" dhidi ya "wazalendo wa Kiukreni" na "Wanazi mamboleo".

    Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Olha Stefanishyna aliiambia BBC kwamba, baada ya "upinzani mkali" kutoka kwa jeshi la Ukraine, kulikuwa na "operesheni kubwa" ya Urusi dhidi ya raia.

    Siku ya Jumapili pekee, familia ya watu wanne waliuawa wakati vikosi vya Urusi vilipofyatua makombora kwa watu waliokuwa wakikimbia mzozo katika mji wa Irpin, kaskazini-magharibi mwa Kyiv.

    Na katika mji wa bandari wa Mariupol, uhamishaji ulioahidiwa ulifutwa siku za Jumamosi na Jumapili huku kukiwa na mashambulizi mapya.

    Baraza la jiji nchini humo lilisema uvamizi wa makombora wa Urusi ulifanya harakati salama za uhamishaji zisiwezekane. Urusi imevilaumu vikosi vya Ukraine.

    Unaweza kusoma

  9. Maelfu wakamatwa kwenye maandamano Urusi

    Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa kwenye maandamano mjini Moscow siku ya Jumapili

    Chanzo cha picha, EPA

    Zaidi ya watu 4,300 wamekamatwa katika maandamano ya kupinga vita kote Urusi siku ya Jumapili, mashirika ya kutetea haki za binadamu na mamlaka ya Urusi yanasema.

    Watu wapatao 1,700 walizuiliwa huko Moscow pekee, shirika la habari la Ria linaripoti, likinukuu wizara ya mambo ya ndani.

    Kundi la haki za OVD-Info linasema kamata kamata hiyo ilifanyika katika miji 53.

    Ingawa maandamano yamezidi kuzuiliwa katika miaka ya hivi karibuni, mikutano mingi imefanyika kote Urusi tangu uvamizi huo.

    Katika siku 11 zilizopita, zaidi ya watu 10,000 walizuiliwa kwenye maandamano, OVD-Info inasema.

    Maria Kuznetsova, msemaji wa OVD-Info, aliliambia shirika la habari la Reuters kutoka Tbilisi nchini Georgia. "Tunaona maandamano makubwa leo - hata katika miji ya Siberia, ambapo ni mara chache tuliona idadi kama hiyo ya kukamatwa."

  10. Kinachojiri Ukraine

    Vifaru

    Chanzo cha picha, Getty Images

    • Urusi inasema inafungua njia mpya za kibinadamu katika miji mingi ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Kyiv, siku ya Jumatatu ili kuruhusu raia kuondoka - inakuja siku chache baada ya majaribio kama hayo huko Mariupol kushindwa baada ya kuendelea kwa makombora kutoka kwa vikosi vya Urusi wakati wa saa zilizokubaliwa za kusitisha mapigano, kulingana na Ukraine.
    • Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameishutumu Urusi kwa mauaji ya raia, baada ya shambulio la Urusi Jumapili huko Irpin kuua familia changa.
    • Maafisa wa ulinzi wa Ukraine wanadai kuwa vikosi vyao vimeuteka tena mji wa mashariki wa Chuhuiv
    • Kumekuwa na mashambulizi mapya ya Urusi kwenye mji wa bandari wa kusini wa Mykolaiv
    • Uingereza imesema itatoa $100m ya ziada (£74m) kwa Ukraine kusaidia serikali kuendelea wakati wa uvamizi wa Urusi.
    • Bei ya mafuta imepanda hadi kiwango cha juu zaidi tangu 2008 baada ya Marekani kusema kuwa inajadili vikwazo vinavyowezekana kwa usambazaji wa Urusi na washirika wake.
  11. Habari za hivi punde, Urusi kusitisha mashambulizi ili kuruhusu raia kuondoka Ukraine

    Vifaru

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi itatoa nafasi ya huduma ya kibinadamu katika miji mingi ya Ukraine Jumatatu ili kuruhusu raia kuondoka, vyombo vya habari vya serikali vinaripoti.

    Usitishaji huo wa mapigano utafanyika kuanzia saa 10:00 kwa saa za huko kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, huku njia za uokoaji zikiwekwa katika mji mkuu wa Kyiv, pamoja na Kharkiv, Mariupol na Sumy.

    Miji yote hii kwa sasa iko chini ya operesheni kubwa ya uvamizi wa Urusi.

    Maafisa wa Kiukreni bado hawajathibitisha hili.

    Mwishoni mwa juma, juhudi mbili za kufungua njia ya kuruhusu raia kuhama kutoka Mariupol kusini-mashariki mwa nchi hiyo zilisambaratika.

    Maafisa wa Ukraine walisema hii ni kwa sababu Urusi iliendelea kuushambulia mji huo wakati wa saa zilizokubaliwa za kusitisha mapigano.

    Raia wataelekea Belarus na Urusi

    Njia za uokoaji zilizotangazwa na shirika la habari la RIA Novosti la Urusi zinaonesha raia wataweza kuondoka hadi Urusi na Belarus.

    Njia ya kutoka Kyiv itaongoza hadi kwa mshirika wa Urusi Belarus, na raia kutoka Kharkiv watapita njia inayoelekea Urusi.

    Njia ya kutoka miji ya Mariupol na Sumy itaelekea miji mingine ya Ukraine hadi Urusi, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

    Unaweza pia kusoma

  12. Waafrika walionaswa wanywa theluji iliyoyeyushwa Ukraine

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wanafunzi wa Nigeria, Ghana na Somalia ni miongoni mwa mamia ya raia wa kigeni waliokwama katika mji wa kaskazini-mashariki wa Sumy nchini Ukraine ambao umekuwa ukishikiliwa na majeshi ya Urusi kwa siku kadhaa.

    Hakuna chakula sokoni, mashine za benki hazifanyi kazi na wanafunzi wanakunywa theluji iliyoyeyushwa baada ya kukosa maji.

    Mwanafunzi wa Kihindi, Vipin Yadav, ambaye ni sehemu ya kundi lililokwama katika jiji hilo, anakadiria takriban wanafunzi 1,300 wa kigeni bado wamenaswa huko - ikiwa ni pamoja na watu kutoka Bangladesh, Pakistan na Uturuki.

    Katika mahojiano kwa njia ya simu, Bw Yadav aliambia mwandishi wa BBC Danny Aeberhard kwamba hakuna chakula kwa muda wa siku nne hadi tano zilizopita.

    Serikali za Nigeria na Ghana zimekuwa zikiwarudisha nyumbani raia wao wanaokimbia mzozo nchini Ukraine. Vikundi vya kwanza vilirudi nyumbani wiki iliyopita.

    Zaidi ya wanafunzi 1,000 wa Ghana walikuwa wakiishi Ukraine hadi Urusi ilipovamia nchi hiyo. Taifa hilo la Afrika Magharibi hadi sasa limefanya misheni mbili za kuwarejesha makwao.

    Nigeria inatarajiwa kuwahamisha raia 5,000 waliovuka kutoka Ukraine hadi nchi jirani za Romania, Poland na Hungary.

    Unaweza pia kusoma

  13. Vikosi vya Ukraine vinadai kutwaa tena Chuhuiv

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa ulinzi wa Ukraine wanadai kuwa vikosi vyao vimeuteka tena mji wa mashariki wa Chuhuiv.

    Katika taarifa kuhusu operesheni iliyotumwa kwenye Facebook Jumapili usiku, Mkuu wa jeshi la Ukraine alisema kwamba vikosi vya Kyiv viliuteka mji huo kutoka kwa wanajeshi wa Urusi na kuvisababishia hasara kubwa vikosi vya Moscow wakati wa vita.

    Maafisa wa Ukraine pia walidai kuwa makamanda wawili wa ngazi za juu wa Urusi waliuawa wakati wa vita vya kuwania mji huo, ambao una idadi ya watu wapatao 31,000.

    BBC haiwezi kuthibitisha madai haya kwa uhuru.

    Chuhuiv iko katika eneo la kimkakati karibu maili 23 kutoka mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine Kharkiv, ambao umekuwa chini ya mashambulizi ya makombora makubwa kutoka kwa vikosi vya Urusi kwa zaidi ya wiki.

    Unaweza pia kusoma

  14. Bei ya mafuta yapanda hadi kiwango cha juu zaidi tangu 2008

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bei ya mafuta imepanda hadi kiwango cha juu zaidi tangu 2008 baada ya Marekani kusema kuwa inajadili vikwazo vinavyowezekana kwa bidhaa za Urusi na washirika wake.

    Brent crude - alama ya kimataifa ya mafuta - ilipanda hadi zaidi ya $139 kwa pipa, kabla ya kurudi chini hadi chini ya $130.

    Masoko ya nishati yametikiswa katika siku za hivi karibuni kutokana na hofu ya usambazaji iliyosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Wateja tayari wanahisi athari ya gharama ya juu ya nishati kadiri bei ya mafuta na bili za za majumbani zinavyoongezeka.

    Masoko ya hisa barani Asia yalishuka siku ya Jumatatu, huku kampuni za Nikkei za Japan na Hang Seng huko Hong Kong zikishuka kwa zaidi ya 3%.

    Siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema utawala wa Biden na washirika wake wanajadili vikwazo vya usambazaji wa mafuta ya Urusi.

    Baadaye, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi alisema baraza hilo "linachunguza" sheria ya kupiga marufuku uagizaji wa mafuta ya Urusi na kwamba Bunge la Congress wiki hii lilinuia kupitisha msaada wa $10bn (£7.6bn) kwa Ukraine ili kukabiliana na uvamizi wa kijeshi wa Urusi.

    "Kwa sasa Bunge linachunguza sheria dhabiti ambazo zitatenga zaidi Urusi kutoka kwa uchumi wa kimataifa," Bi Pelosi alisema katika barua.

    Maoni hayo yametolewa huku shinikizo zikiongezeka kwa Ikulu ya White House na mataifa mengine ya Magharibi kuchukua hatua kali dhidi ya Moscow kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

    Vikwazo vya mafuta vya Urusi vitakuwa ongezeko kubwa katika kukabiliana na uvamizi wa Ukraine na kunaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia.

    "Wakati Marekani inaweza tu kusukuma marufuku ya uagizaji wa mafuta kutoka Urusi, Ulaya haiwezi kumudu kufanya hivyo. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba [kiongozi wa Urusi Vladimir] Putin, ikiwa atasukumwa ukutani, anaweza kuzima usambazaji wa gesi Ulaya, kukata njia ya nishati barani," Vandana Hari katika shirika la ushauri la masoko ya nishati Vanda Insights aliambia BBC.

    Unaweza pia kusoma

  15. Haya hapa unayofaa kujua ….

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ikiwa unajiunga nasi, haya ndiyo ambayo huenda umekosa wakati uvamizi wa Urusi nchini Ukraine unapoingia siku yake ya 12:

    • Seneta Marco Rubio, mgombea wa ngazi ya juu zaidi wa Republican katika Kamati ya Ujasusi ya Seneti, aliiambia CNN Jumapili kwamba kuweka eneo la kutopaa ndege juu ya Ukraini bila shaka kutamaanisha "kuanzisha Vita vya Tatu vya Dunia"

    • Maafisa wa ulinzi wa Uingereza wamesema wanaamini kuwa vikosi vya Urusi vilipata mafanikio kidogo zaidi katika muda wa saa 48 zilizopita, huku wanajeshi wake wakikabiliwa na upinzani mkali wa Ukraine na usaidizi duni wa vifaa.

    • Lakini makamanda wa Ukraine wameonya kwamba vikosi vya Urusi vimekuwa vikijipanga upya na vinajiandaa kufanya mashambulizi ya kila namna kwenye mji mkuu Kyiv.

    • Vikosi vya Moscow vimekuwa vikishambulia kwa nguvu miji ya pembezoni mwa jiji na kusambaza tena tanki za mafuta zilizohamishwa kutoka Belarusi kwa ajili ya kujiandaa kwa shambulio hilo, maafisa walisema.

    • Katika mji wa kusini-mashariki wa Mariupol, mashambulizi ya makombora ya Urusi yameua makumi ya watu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaonya wanajeshi wa Moscow kwamba vikosi vyake vitamfuatilia mwanajeshi yeyote atakayefanya uhalifu wa kivita hadi kaburini.

    • Vikwazo vya kiuchumi vinaendelea kulenga uchumi wa Moscow, huku Netflix, American Express, KPMG na PricewaterhouseCoopers zikiwa miongoni mwa kampuni kuu za hivi punde zaidi kusitisha huduma nchini Urusi.

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imeripotiwa kumpa Zelensky simu salama ya moja kwa moja hadi kwa Biden

    Timu za kijasusi za Marekani zinaripotiwa kufanya kazi ili kukatiza mashambulizi ya kidijitali ya Urusi na mawasiliano, gazeti la New York Times linaripoti.

    Kulingana na gazeti la Times, wafanyakazi wa Kamandi ya Mtandao ya Marekani iliyoko Marekani na Ujerumani wanatoa taarifa za kijasusi kutoka kwa picha za satelaiti na miingiliano ya kielektroniki kwa wanajeshi wa Ukraini ndani ya "saa moja au mbili" baada ya kukusanywa.

    Marekani pia imempatia Rais wa Ukraine Zelensky vifaa vya mawasiliano vilivyosimbwa kwa njia fiche, na kumwezesha kumpigia simu Biden kwa njia salama, linaripoti Times. Siku ya Jumamosi, Zelensky alipiga simu ya dakika 35 na Biden.

    Siku ya Alhamisi, katibu wa habari wa Ikulu ya White House, Jen Psaki alisema Marekani ilikuwa ikishiriki taarifa za kijasusi na Ukraine "katika muda halisi". Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa.

  16. Urusi inajitayarisha kushambulia Kyiv, Ukraine inasema

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maafisa wa ulinzi wa Ukraine wameonya kuwa Urusi inatayarisha vikosi vyake kufanya mashambulizi ya kila namna kwenye mji mkuu wa Kyiv.

    Taarifa ya Jenerali wa jeshi la Ukraine ilisema kuwa vikosi vya Moscow vimeanza kukusanya rasilimali kwa ajili ya kushambulia mji huo, huku vifaru na vitengo vya askari wa miguu vikiwa vinasonga mbele kuelekea mji wa karibu wa Irpin kuweka msingi.

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa makamanda wa Urusi wamekuwa wakivipatia vikosi vyao mafuta yaliyosafirishwa kutoka Belarus kupitia eneo la kutengwa la Chernobyl.

    Kwingineko, maafisa waliripoti kuwa jeshi la Urusi lilikuwa likielekeza nguvu zake katika kuzunguka miji ya mashariki ya Kharkiv, Chernihiv, Sumy na mji wa kusini wa Mykolayiv.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi inaripotiwa kuwaajiri mamluki wa Syria

    Urusi inawaajiri Wasyria wenye ujuzi katika mapigano ya mijini kupigana nchini Ukraine huku Moscow ikijiandaa kwa mapigano makali ya barabara hadi mtaa katika harakati zake za kuteka miji mikubwa ya Ukraine, maafisa wa Marekani wameliambia jarida la Wall Street Journal.

    Maafisa wa kijasusi walikataa kueleza chapisho hilo ni wapiganaji wangapi wamekubali kujiunga na vita, lakini wakasema baadhi yao tayari wamesafiri hadi Urusi na wanajiandaa kutumwa Ukraine.

    Kulingana na chapisho huko Deir Ezzor, Syria, Urusi imetoa wafanyakazi wa kujitolea kutoka nchi hiyo mishahara ya kati ya $200 na $300 "kwenda Ukraine na kufanya kazi kama walinzi" kwa miezi sita kwa wakati mmoja.

    Maafisa huko Moscow wanasemekana kuamini kutumwa kwa wapiganaji waliopata uzoefu kwa zaidi ya muongo mmoja wa vita vya mijini katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria kunaweza kuongeza nguvu katika vita vyao vya kunyakua miji muhimu ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wa Kyiv.

    Maveterani wa kijeshi wa Israel wameripotiwa kujitokeza kupigania Ukraine.

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja leo Jumatatu tarehe 7 Machi 2022.Tutakupa taarifa kutoka sehemu mbali mbali duniani.