Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Uchaguzi Zambia 2021: Raia wanapiga kura katika uchaguzi wenye ushindani mkali

Mamilioni ya raia wa Zambia wanapiga kura leo, Alhamisi katika uchaguzi mkuu wa rais huku hali ya kiuchumi ikiwa imezorota.

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya matangazo yetu ya moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Ujerumani ina wasiwasi kuwa maelfu walichomwa maji ya chumvi, badala ya chanjo

    Mamlaka kaskazini mwa Ujerumani zimewataka watu zaidi ya 8,000 kurudia kupata chanjo ya virusi vya corona kwasababu muuguzi anashukiwa kuwachoma watu maji ya chumvi badala ya chanjo iiyokusudiwa.

    Polisi wanachunguza kitendo hicho cha mhudumu wa afya katika kituo cha chanjo mjini Friesland, karibu na pwani ya bahari ya kaskazini.

    Awali watu sita pekee waliaminika kuchomwa maji hayo yenye chumvi yasiyo na madhara, mwezi Machi na Aprili.

    Wengi wao ni wa umri wa zaidi ya miaka 70- walio katika hatari ya kupata maambukizi ya janga la corona.

    Inspekta Peter Beer, amenukuliwa na Süddeutsche Zeitung, akisema mwanamke mmoja wa miaka 40 amekuwa ''akishirikisha watu taarifa za kutamausha'' kwenye mitandao ya kijamii, akikosoa serikali kuweka masharti yenye nia ya kudhibiti kuenea kwa virusi.

    Redio ya mji huo ya NDR imesema watu 8,557 wametakiwa kurudi vituoni kurudia chanjo, na mpaka sasa watu 3,600 wameweka miadi ya kurejea tena kwenye chanjo.

    Mwezi Aprili muuguzi huyo aliwapa maji ya chumvi watu sita kuficha ukweli kuwa aiangusha mkebe wa chanjo sakafuni.

    Lakini uchunguzi wa polisi ulibainisha kuwa watu wengi zaidi walipewa maji ya chumvi badala ya chanjo ya Pfizer/BioTech.

    Mashahidi zaidi wanahojiwa na hadi sasa hakuna mashtaka yoyote yaliyoripotiwa katika kesi hiyo.

    Ujerumani imekuwa na maandamano mengi ya kupinga chanjo.

  3. Rais wa Madagascar alivunja baraza la mawaziri

    Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amelivunjilia mbali baraza lake la mawaziri.

    Ofisi yake haikutoa sababu, lakini Jumapili Bw Rajoelina alisema kutakuwa na hali ya kushindwa ndani ya serikali - "kama katika timu ya mpira wa miguu" - mabadiliko yangehitajika.

    Kufutwa kwa baraza hilo kumekuja baada ya ripoti za njama iliyofeli ya kumuua rais ambaye ni kiongozi wa zamani wa mapinduzi huko Madagascar.

    Zaidi ya washukiwa 20 - wakiwemo 12 kutoka kwenye jeshi - wamekamatwa. Bwana Rajoelina alikua rais wa kisiwa hicho miaka miwili iliyopita - baada ya mzozo wa kisheria uliogubika uchaguzi huo.

  4. Uchaguzi Zambia: Joho la bafuni lapata umaarufu katika kituo cha kupiga kura

    Ikiwa unatarajia kuepuka foleni kusubiri kwa muda mrefu kupiga kura nchini Zambia ilibidi uamke mapema.

    Mwenzetu Kennedy Gondwe katika mji mkuu, Lusaka, alimwona mtu mmoja ambaye alikuwa na haraka sana kwamba hakuvaa vizuri.

    Chimwemwe Chuwa anasema alichelewa kugundua kuwa muda wa kupiga kura umefika kuwahi foleni ilimbidi afike kwenye kituo cha kupiga kura akiwa na joho la bafuni na malapa, pamoja na kufanya hivyo bado aliendelea kusubiri:

    Mpiga kura mwingine, Charles Masompe , alivaa gauni la kuhitimu elimu ya chuo kikuu.

    Baadaye alituma video kwenye mtandao wake wa twitter akishangiliwa katika kituo cha kupigia kura baada ya kuruhusiwa kuruka foleni:

  5. Waasi wa Oromo wakubali kujiunga na vikosi vya Tigray

    Kikosi cha waasi wa Oromo Liberation Army (OLA) cha Ethiopia kimesema kimekubaliana na muungano wa kijeshi na vikosi vya Tigray kutoka kaskazini mwa nchi hiyo kupigana na serikali.

    Wapiganaji wa TPLF hawajatoa taarifa kuhusu makubaliano hayo lakini msemaji wa kikundi hicho alithibitisha makubaliano hayo kwa shirika la habari la Bloomberg.

    Serikali ilivitaja vikundi vyote kama washirika ya ugaidi mnamo Mei.

    Ushirikiano kati ya vikosi vya OLA na vikosi vya Tigray unaweza kuweka shinikizo zaidi kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

    Serikali si tu imepambana na vikosi vya Tigray - bali pia inakabiliwa na msururu wa mizozo katika sehemu tofauti za nchi.

    Huko Oromia - nyumbani kwa kabila kubwa zaidi nchini humo na mahali ambapo Waziri Mkuu Abiy Ahmed anatoka - ilibidi apigane na Jeshi la Ukombozi la Oromo.

    Kundi ambalo linashinikiza kujitenga kwa jamii ya Oromo, limekuwa na mafanikio madogo ya kijeshi, lakini limefanya sehemu za mkoa kutokuwa na utulivu sana.

    Hivi karibuni, serikali ya shirikisho imekabiliwa na msururu wa vipigo kaskazini mwa Ethiopia na kupoteza eneo kwa waasi wa Tigray.

    Ilisitisha makubaliano ya pamoja ya usitishaji mapigano na kulitaka jeshi la kitaifa na washirika wake kumaliza uharibifu uliosababishwa na Tigray People's Liberation Front mara moja

  6. Riek Machar wa Sudani Kusini afanya mazungumzo ya kusitisha mapigano

    Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, inasema amepokea simu kutoka kwa majenerali ambao waliasi wiki iliyopita kutoka kwa mrengo wa kijeshi wa Vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan (SPLM-IO).

    Jenerali Johnson Olony alimfahamisha Bw Machar juu ya kukubali kwa kikundi chao kusitisha vita, mkurugenzi wa mawasiliano wa SPLM-IO alisema.

    Bwana Machar alisisitiza hitaji la kusuluhisha kwa amani tukio lililotokea Magenis katika Jimbo la Upper Nile, mkurugenzi huyo aliongeza.

    Mwisho wa wiki iliyopita mapigano kati ya pande hizo mbili yalishuhudia wanajeshi wasiopungua 34 wakiuawa kutoka pande zote mbili, kulingana na vyombo vya habari vya nchini humo.

    Mkurugenzi wa mawasiliano wa SPLM-IO Puok Baluang amesema Bw Machar na Jenerali Olony walikubaliana kudumisha mawasiliano.

    BBC haikuweza kuthibitisha habari hii kwa kujitegemea kwani mawasiliano na mrengo ulioasi hayakupatikana.

    Mapema wiki iliyopita, majenerali watatu kutoka SPLM-IO walitangaza kwamba wamemwondoa madarakani Machar na nafasi yake kukaliwa na Mkuu wa zamani wa wafanyikazi, Jenerali Simon Gatwech Dual na walitaka Bw Machar ajiondoe kwenye nafasi yamakamu wa kwanza wa rais.

    Lakini Bw Machar alisema jaribio la kumwondoa liliungwa mkono na "waharibifu wa amani".

  7. Rais wa Malawi awafuta kazi waziri na mkuu wa watumishi

    Rais wa Malawi Lazarus Chakwera amewafuta kazi waziri wa nishati na mkuu wake wa watumishi ambao wanakabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

    Wawili hao na afisa mwingine mmoja - Enock Chihana, mshirika katika usimamizi wa Tonse Alliance – walikamatwa siku ya Jumatatu kwa madai ya kuhusika na zabuni ya mafuta ya nchi hiyo.

    Waliripotiwa kujaribu kushawishi jinsi kandarasi ya usambazaji wa mafuta itakavyotolewa.

    Nafasi ya waziri Newton Kambala haijajazwa baada ya kufutwa kwake.

    Majukumu ya wizara ya nishati yamehamishiwa ofisi ya rais.

    Mrithi wa mkuu wa watumishi wa umma Chris Chaima Banda pia hajatajwa wakati tangazo la kufutwa kwake lilipotolewa.

    Bw. Kambala na Bw. Banda hawajatoa tamko lolote kuhusiana na suala hilo.

    • Lazarus Chakwera: Rais wa Malawi 'aliyebishana na Mungu'
    • Lazarus Chakwera: Kutoka kuongoza makanisa ya Walokole mpaka kushinda Urais wa Malawi
  8. Takribani watu 52 wapoteza maisha kutokana na mafuriko nchini Niger

    Takriban watu 52 wamekufa katika mafuriko ya Niger huku 34 wakijeruhiwa na maelfu wakipoteza nyumba zao, viongozi wanasema.

    Hii ni pamoja na watano waliokufa kati ya Jumanne na Jumatano baada ya mvua kubwa katika mji mkuu wa Niamey, na kusababisha uharibifu mkubwa na kusababisha mamia kukosa makazi.

    Zaidi ya nyumba 4,000 na vibanda 200 vilianguka na mifugo 800 ilisombwa na maji, kulingana na ripoti ya Ufuatiliaji wa Huduma ya Ulinzi wa Raia.

    Mikoa kadhaa ya nchi imeathiriwa na mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwanzo wa Juni.

    Mji mkuu ni miongoni mwa miji iliyoathiriwa zaidi - na mvua ya milimita 144 ilirekodiwa kati ya Jumanne na Jumatano.

    Watu wasiopungua 70 walipoteza maisha kutokana na mafuriko nchini Niger mwaka jana na wengine 350,000 waliathirika.

  9. Taliban yauteka mji wa kumi mkuu wa mkoabaada ya kuingia Ghazni

    Taliban wameuchukua mji muhimu wa Ghazni, mji mkuu wa mkoa wa 10 kuwaangukia wanamgambo hao chini ya wiki moja.

    Ghazni ni mji ulioko kwenye barabara kuu ya Kabul-Kandahar, ikiunganisha ngome za wapiganaji kusini na mji mkuu Kabul.

    Kuchukua Ghazni kunafikiriwa kuongeza uwezekano kwamba hatimaye Taliban inaweza kuuteka mji wa mkuu wa Kabul

    Karibu theluthi moja ya miji mikuu ya mikoa 34 ya nchi hiyo sasa iko chini ya udhibiti wa Taliban.

    Wanamgambo hao wamekuwa wakiidhibiti miji hiyo kwa kasi, tangu majeshi ya Marekani na washirika wake yaondoke nchini humo baada ya miaka 20.

    Mapigano makali pia yaliripotiwa katika jiji la Kandahar Jumatano. Taliban wanadai kuchukua jela la jiji, ingawa hili halijathibitishwa.

  10. Watu 69 wafariki wakijaribu kuzima moto Algeria

    Algeria imetangaza siku tatu za maombolezo kitaifa kuanzia leo Alhamisi baada ya watu wapatao 69 kufariki kutokana na moto ulioanzia maeneo ya msituni.

    Wahanga wa ajali hiyo ya moto wakiwemo wanajeshi 28, wote wamekufa wakiwa wanajaribu kupambana kuuzima moto huo. Msitu wa mlima wa Kabylie ulioko magharibi mwa Algiers ndio uliathirika zaidi.

    Picha za kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha jinsi moto ulivyoteketeza maeneo ya mlimani, wanyama na moshi ukiwa unaonekana katika maeneo mbalimbali.

    Joto kuongezeka na upepo mkali ulichochea moto kuwaka ingawa serikali inawalaumu watu wanaochoma moto mapori. Watu kadhaa wamekamatwa lakini kukiwa hakuna ushahidi dhidi yao.Haijawekwa wazi nini kilipelekea kukamatwa kwao.

  11. Muungano wa kutetea haki za binadamu Tanzania wakosoa kusistishwa kwa leseni ya oparesheni ya gazeti la Uhuru

    Muungano wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania (THRDC) umekosoa hatua ya serikali kufuta leseni ya oparesheni ya gazeti la Uhuru kwa siku 14 kwakuchapisha habari za uwongo .

    Muungano huo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari umesema mkurugenzi wa huduma ya idaraya Habari hakufafanua Iwapo uamuzi huo ulichukuliwa baada ya gazeti hilo kupewa nafasi ya kujitetea ama upande wake kusikilizwa.

    THRDC imesema vipengee vya sheria iliyotegemewa kuchukua uamuzi huo vinatumika kinyume cha sheria kwasababu iliwasilisha kesi katika mahakama ya haki ya afrika mashariki ili virekebishwe lakini serikali ya Tanzania haikutii agizo la mahakama hiyo ili kuirekebisha sheria ya huduma ya Habari ambayo muungano huo umesema inatumikakubana uhuru wa kujieleza nchini Tanzania

    Taarifa hiyo iliyotiwa saini na mratibu wa kitaifa wa THRDC Onesmo Olengurumwa pia imeihimiza serikali kutii maelekezo ya mahakama ya EACJili kuhakikishasheria ya huduma za Habari inaambatana na matakwa ya mkataba wa EAC ambao Tanzania ilisaini kwa nia njema .

    Hapo jana Chama cha Mapinduzi-CCM kiliwasimamisha kazi viongozi watatu wa gazeti la Uhuru pamoja na kusimamisha uchapishaji wa gazeti hilo kwa muda wa siku saba.

    Miongoni mwa waliosimamishwa kazi ni pamoja na mkurugenzi mtendaji, mhariri mtendaji na mhariri wa zamu.

    Daniel Chongolo, ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, hatua hiyo imekuchuliwa baada ya gazeti hilo kuchapisha taarifa ambazo zinadai kwamba rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema hana nia ya kuwania urais mwaka 2025.

    Awali, chama hicho kilitoa taarifa inayoonesha kusikitishwa na taarifa hiyo.

    Katibu huyo mkuu alikiri kutokea kwa kosa hilo katika uchapishaji wa gazeti hilo mama la CCM katika toleo lake la tarehe 11 Agosti, katika habari yake kuu ukurasa wa mbele, inayosema, “Sina Wazo Kuwania urais 2025-Samia.”

    Chongolo aliongeza kusema kuwa bodi ya wakurugenzi pia imeunda tume itakayochunguza sababu za kutokea kwa tukio hilo.

    Taarifa iliyotolewa na Chama hicho tawala ambacho ni miongoni mwa vyama vikongwe barani Afrika, imesema gazeti hilo limepotosha mahojiano aliyofanya Rais na BBC.

    Maelezo zaidi:

  12. Marufuku ya Twitter kuondolewa Nigeria hivi karibuni

    Waziri wa Habari nchini Nigeria Lai Mohammed ameeleza mikakati ambayo imewekwa na serikali ili kuondoa kizuizi kilichowekwa kwenye utumiaji wa mtandao wa kijamii ujulikanao kwa jina la Twitter.

    Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari baada ya kikao cha wajumbe kilichofanyanyika Jumatano mjini Abuja , ambapo kikao hicho kilijumuisha makampuni mabalimbali ya mitandao ya kijaamii na kuwa wameshapata suluhisho litakalo saidia pande zote mbili.

    Aliwasilisha mikakati mbalimbali iliyotolewa na serikali katika kuondoa kizuizi cha kufungia mtandao wa Twitter nchini Nigeria ambapo moja wapo ni kusajili mtandao huo nchini humo na kulipia kodi iliyopangwa na serikali na pia kuajiri wazawa wa nchi hiyo.

    Lakini bwana Mohammed ameeleza kuwa mikakati imeweka vizuri ili kuondoa tofauti kati ya serikali ya Nigeria na mtandao wa twitter hivi karibuni.

    Serikali ya Nigeria ilifungia twitter mwanzoni wa mwezi wa sita baada ya kuondoa maoni ya Muhammadu Buhari katika mtandao huo kwa madai kuwa alichokisema rais ni kinyume na sera za mtandao huo.

    Hata hivyo serikali ya Nigeria ilisema kufungiwa kwenye Twitter haikuwa kutokana na kuondolewa kwa ujumbe wa rais lakini ilikuwa ni kwa ajili ya usalama wa taifa na umoja. Wanaharakati walikosoa katazo hilo na kusema hakuna uhuru wa kujieleza.

    Licha ya marufuku hayo kuwepo kwa zaidi ya miezi miwili, Wanaigeria wengi wamekuwa wakiendelea kutumia mtandao huo kwa kutumia mfumo wa VPN.

  13. Wakenya walalamika mitandaoni kuhusu mapokezi ya wanariadha wa Olimpiki huku wale wa Uganda wakipokelewa ‘kifahari’

    Kuishindia nchi yako medali yoyote kwenye mashindano ya kimataifa ni fahari kubwa sana kwa mtu yeyote.Wanariadha ni miongoni mwa watu ambao kazi zao huziletea nchi zao fahari.

    Lakini je,nchi zinafaa kurejesha vipi shukrani ama upendo kwa wale wanaoziletea fahari na hasa katika mashindano makubwa kama ya Olimpiki?

    Basi ndio kwasababu baadhi ya wakenya mitandaoni waliiponda serikali yao kwa kutojishughulisha na makaribisho kabambe ya wanariadha wa nchi hiyo walioshinda medali za dhahabu ,fedha na shaba.

    Nchini Kenya mshindi wa rekodi ya dunia Eliud Kipchoge alirejea nchini kwake kimya kimya bila hata shamrashamra kama zilizoandaliwa kwa wanariadha wa Uganda waliopokelewa na rais wa nchi yao Yoweri Museveni.

    Rais Museveni alitangaza kwamba wanamichezo wa Uganda wanaoshinda dhahabu katika michezo ya bara, Jumuiya ya Madola au Olimpiki watakuwa wakilipwa mshara wa shilingi milioni tano za Uganda.

    Museveni alisema aliwakabidhi washindi wote wa medali magari na pia kuahidi kuwajengea wazazi wao nyumba.

    Alikuywa akizungumza baada ya kuwapokea Joshua Cheptegei (mshindi wa dhahabu na fedha ), Peruth Chemutai (mshindi wa dhahabu), Jacob Kiplimo (shaba )Halima Nakaayi na Winnie Nanyondo, miongoni mwa wengine walioshiriki mashindano ya olimpiki.

    Licha ya Kenya kumaliza ya 19 duniani ya kwanza Afrika,kulikuwa na kimya katika uwanja wa ndege na wengi wa watumiaji wa mitandao ya kijamii waliilaumu wizara ya michezo kwa kutofanya maandalizi yoyote kuwalaki kishujaa wanariadha wake.

  14. Milionea wa Urusi akiri kumuua kwa kumpiga risasi mwanaume ‘aliyedhani kuwa ni dubu’

    Mwanasiasa milionea katika Mashariki ya Mbali ya Urusi amekiri kumuua mtu ambaye anasema alidhani ni dubu .

    Igor Redkin, 55, amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari vya Urusi kwamba alikuwa amesikia kulikuwa na dubu kwenye jalala la takataka katika kijiji cha Ozernovsky huko Kamchatka.

    Alitaka kumtisha mnyama huyo na alifyatua risasi, lakini baadaye "aligundua kuwa mkazi wa eneo hilo alijeruhiwa katika eneo lililo karibu wakati huo huo," alisema.

    Mwanaume huyo wa miaka 30 ambaye alipigwa risasi baadaye alikufa hospitalini.

    Kesi ya jinai ilifunguliwa dhidi ya milionea huyo wiki iliyopita.

    Bwana Redkin ndiye mmiliki mwenza wa biashara kadhaa kubwa katika peninsula ya Kamchatka na ameelezewa kama mmoja wa maafisa tajiri wa umma wa Urusi.

    Alisema "alikuwa ameshafanya uamuzi na alikuwa tayari kukubali adhabu ambayo mhakama itaamua".

    Tangu wakati alipoondoka chama cha Rais Vladimir Putin cha United Russia.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Urusi, mwanasiasa huyo atatumikia miezi miwili chini ya kifungo cha nyumbani wakati wa uchunguzi.

  15. Raia wa Zambia wanapiga kura katika uchaguzi wenye ushindani mkali

    Mamilioni ya raia wa Zambia wanapiga kura leo, Alhamisi katika uchaguzi mkuu wa rais huku hali ya kiuchumi ikiwa imezorota.

    Polisi na wanajeshi wanafanya doria nchi nzima katika vituo vya kupigia kura na idadi kubwa ya waangalizi wa kimataifa watakuwa wakifuatilia mchakato huo.

    Rais Edgar Lungu anawania kutawala kwa muhula wa pili huku akikabiliana na ushindani mkubwa kutoka kutoka kwa Hakainde Hichilema, mgombea wa chama kikuu ya upinzani nchini humo.

    Huku wapiga kura wengi wakiwa wanataka hali ya uchumi kuboreshwa na fursa za ajira kupatikana. Tume ya uchaguzi nchini Zambia imehaidi uchaguzi wa uwazi na haki.

  16. Habari na karibu katika ukurasa wa matangazo ya moja kwa moja ya BBC Swahili leo ikiwa Alhamisi 12.08.2021