Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Rabsha zarindima Kampala baada ya Bobi Wine kukamatwa

Mgombea wa urais kupitia chama cha upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amekamatwa akiwa kwenye kampeni.

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio nakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja kwa hii leo. Mola akiridhia kesho pia ni siku. Kwaheri.

  2. Ndege aina ya Boeing 737 iliyosababisha ajali yaruhusiwa kuanza tena safari za abiria

    Mkuu wa Mamlaka ya Safari za Anga Marekani (FAA), Steve Dickson, ametia saini agizo linaloruhusu ndege aina ya Boeing 737 kuanza tena safari zake kwa abiria.

    Bwana Dickson alisema ana uhakika wa asilimia 100 juu ya usalama wa ndege hizo ambazo zilipigwa marufuku kusafiri baada ya kutokea kwa ajali mbili za abiria nchini Indonesia na Ethiopia, na kusababisha vifo kwa watu 346.

    Uamuzi huo wa Mamlaka ya Safari za Anga Marekani (FAA), unamaanisha kuwa ndege hizo zinaweza kuanza tena safari za abiria kufikia mwisho wa mwaka huu.

    Mamlaka hiyo imetoa wito marubani kupewa mafunzo zaidi ili waweze kutumia kwa ubora wa juu kifaa kipya cha usalama kilichowekwa kwenye ndege aina ya Boeing 737.

    Aidha, wamiliki wa ndege ya Boeing wamefurahishwa na hatua ya FAA na kusema kuwa imejifunza kutokana na makosa yake yaliyotokea awali.

    Pia unaweza kusoma zaidi:

  3. Marekani kuondoa wanajeshi wake Afghanistan na Iraq

    Wajumbe wa Republicans na washirika wa Marekani wameonesha wasiwasi wao baada ya kutangazwa kuwa Marekani itaondoa wanajeshi wake katika nchi za Afghanistan and Iraq.

    Marekani itaondoa wanajeshi wapatao 2,500 kutoka nchi zote hizo mbili kufikia katikati ya mwezi Januari, Wizara ya Mambo ya Nje imethibitisha.

    Rais Donald Trump kwa kipindi kirefu amekuwa akitaka majeshi ya Marekani kurejea nyumbani na amekosoa muingilio wa Marekani kwa nchi za nje.

    Hata hivyo, mkuu wa shirika la Nato ameonya kuwa hatua hiyo huenda ikawa na athari mbaya huku kiongozi wa Bunge la Seneti Mitch McConnell akitaja mpanga huo kama "makosa makubwa".

    Bwana Trump bado hajakiri kuwa alishindwa na mpinzani wake Joe Biden na hatua ya kurejea nyumbani kwa wanajeshi imepangiwa kufanyika siku tano kabla ya Bwana Biden kuingia madarakani Januari 20, 2021.

    Rais mteule Joe Biden, pia naye amesema kuwa "amechoshwa na vita vya Afghanistan ambavyo vimedumu kwa muda mrefu lakini pia kuna haja ya kumaliza vita hivyo kwa njia ya uwajibikaji na kwa namna ambayo inahakikisha ulinzi dhidi ya vitisho kwa nchi yetu na tusiwe na haja ya kurejea tena huko".

    Timu ya mpito ya Biden bado haijasema lolote kuhusiana na tangazo la mpango huo.

    Nchini Iraq idadi ya wanajeshi wa Marekani itapunguzwa kwa 500 hadi 2,500 huku idadi ya maafisa wa Marekani nchini Afghanistan ikipungua kutoka 4,500 hadi 2,500.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Rabsha zarindima Kampala baada ya Bobi Wine kukamatwa

    Mgombea wa urais kupitia chama cha upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amekamatwa akiwa kwenye kampeni.

    Bobi Wine amekamatwa katika eneo la Luuka mashariki mwa nchi hiyo alikokuwa anafanya kampeni kulingana na ujumbe wa mtandao wa Twitter uliotumwa na wasaidizi wake.

    Kulingana na taarifa za gazeti la Daily Monitor, Bobi Wine alikuwa amepangiwa kuhutubia wafuasi wake katika eneo hilo.

    Polisi imeshtumiwa kwa ukiukaji wa hatua za kukabiliana na ugonjwa wa corona kama vile kufanya mikutano ya hadhara kama ilivyoagizwa na tume ya uchaguzi, kulingana na gazeti hilo.

    Aidha, Polisi wamekuwa wakikabiliana na wafuasi wa Bobi Wine baada ya kukamatwa kwa mgombea huyo wa urais.

    Kulingana na gazeti la Daily Monitor, maandamano yalianza muda mfupi baada ya wafuasi wake kupata taarifa kuwa Bobi Wine amekamatwa.

    Inspekta jenerali wa polisi nchini humo Martin Okoth Ochola ameonya wagombea urais na wanaharakati wengine wa kisiasa pamoja na wagombea wengine dhidi ya kukiuka miongozi ya Tume ya Uchaguzi wakati kampeni zinaendelea kushika kasi.

    Raia nchini Uganda watapiga kura katika uchaguzi mkuu kumchagua rais pamoja na wabunge Januari 14.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Nabii milionea Shepherd Bushiri ajisalimisha kwa polisi

    Nabii milionea Shepherd Bushiri na mke wake Mary wamejisalimisha kwa polisi katika eneo lao la nyumbani baada ya kukwepa masharti ya dhamana nchini Afrika Kusini.

    Wanandoa hao wamejisalimisha katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe, Jumatano asubuhi kulingana na mwanahabari wa BBC Nomsa Maseko.

    Awali mwezi huu, waliachiwa kwa dhamana na mahakama moja nchini Afrika Kusini baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ulaghai na utakatishaji wa pesa.

    Awali, muhubiri huyo alisema kuwa alitaka kutakasa jina lake.

    Jumamosi, Nabii Bushiri aliwaambia wafuasi wake katika mitandao ya kijamii kuwa uamuzi wake wa kukiuka masharti ya dhamana ni kwasababu alipokea vitisho vya kifo.

    Muhubiri huyo pia alishtumu Afrika Kusini kwa kushindwa kuwapa ulinzi.

    Afrika Kusini ilikuwa imeanza mchakato wa kutaka wawili hao warejeshwe nchini humo na Jumatatu ikatoa kibali cha kukamatwa kwao.

  6. Polisi Kenya watambua wezi wa watoto

    Polisi nchini Kenya imesema kuwa imebaini mtandao unaohusika na wizi wa watoto katika jiji la Nairobi.

    Sakata hii imebainika baada ya kipindi cha uchunguzi cha BBC Africa Eye kupeperushwa hewani ambacho kilionesha uhalifu unaotendeka katika maeneo mbalimbali na hospitali za umma.

    Maafisa watatu wa matibabu wa hospitali za umma wamekamatwa na polisi imedokeza kuwa bado kuna wengi ambao wanatafutwa.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Inspekta Generali wa polisi Hillary Mutyambai, ilisema uchunguzi na taarifa kutoka kwa washirika umeonesha maafisa waandamizi wa matibabu ndio wanaohusika kwa kiasi kikubwa na wizi wa watoto.

    Taarifa hiyo ilisema hospitali za umma na makao ya watoto ndani ya jiji la Nairobi pia vinahusika katika sakata hiyo.

    Inspekta Mutyambai ameagiza makamanda wa polisi mjini Nairobi kufanya uchunguzi mara moja katika hospitali za umma na za kibinafsi pamoja makazi ya watoto.

    Agizo hilo linakuja siku mbili tu baada ya kipindi cha BBC Afrika Eye kupeperusha makala iliyoweka wazi jinsi mitandao haramu inavyofaidika na wizi wa watoto ambao huuzwa hata kwa pesa kidogo tu kiasi cha dola 450 za Marekani.

  7. WHO: Ebola imekwisha DRC

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa sasa nchi hiyo imeondokana na ugonjwa wa Ebola baada ya siku zaidi ya 40 bila kuripotiwa kwa ugonjwa huo.

    Mlipuko wa hivi karibuni kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ulikuwa wa tatu katika kipindi cha miaka miwili.

    Lakini chanjo na tiba zilizobuniwa wakati wa majanga yaliyotangulia sasa hivi zinatoa matumaini kwa wagonjwa.

    Tangu mwaka 2018, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa Ebola kufuatana.

    Mwanzoni mwa mwezi Juni, wagonjwa kadhaa walipatikana na ugonjwa huo katikati mwa eneo la Mbandaka.

    Watu 130 waliambukizwa ugonjwa huo huku 55 kati yao wakifariki dunia.

    Visa vya ugonjwa huo eneo la Mbandaka vilibainika wakati mlipuko wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo unakaribia kufikia ukomo wake.

    Zaidi ya watu 2,000 wamekufa kutokana na ugonjwa huo katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri kwa zaidi ya miaka miwili.

    Huo ulikuwa mlipuko wa pili mkubwa zaidi duniani.

    Shirika la Afya Dunian - WHO, limeidhinisha chanjo iliyotolewa na kampuni ya dawa ya Merk ambayo imetolewa kwa watu 400,000 kote nchini humo.

    Mwezi uliopita, Shirika la Dawa nchini Marekani limeidhinisha dawa ya Inmazeb kama tiba ya Ebola, baada ya kufanyiwa majaribio huko Congo.

  8. Chanjo dhidi ya corona kutoka China yaonesha mafanikio

    Chanjo ya Covid-19 kutoka China imeonesha ufanisi katikati ya majaribio, watafiti wamesema.

    Kuna chanjo kadhaa zilizobuniwa China na zingine tayari zimeanza kutumika.

    Kulingana na watafiti, chanjo ya Sinovac Biotech ilionesha matokeo chanya kwa haraka katika uimarishaji wa kinga mwili kwa karibu watu 700.

    Tangazo hilo linawadia baada ya chanjo zilizobuniwa Ulaya na Marekani kusemekana kuwa na mafanikio katika hatua ya mwisho ya majaribio.

    Chanjo tatu zilizotengenezwa Marekani, Ujerumani na Urusi zote zimetoa data inayoonesha ufanisi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa makumi ya maelfu ya watu.

    Malezo zaidi:

  9. Viongozi wa Al- Shabaab wapigwa marufuku kuingia Marekani

    Marekani imewawekea vikwazo viongozi wawili waandamizi wa kundi la kigaidi la Al-Shabab waliohusika na utekelezaji wa shambulio la kigaidi katika kambi ya jeshi nchini Kenya.

    Afisa mmoja wa jeshi la Marekani na wanakandarasi wawili waliuawa mnamo mwezi Januari katika shambulio lililtokea kambi ya Simba kisiwa cha Manda.

    Hilo lilikuwa shambulio la kwanza kutekelezwa na kundi la Al-Shabab dhidi ya jeshi la Marekani nchini Kenya.

    Wizara wa Mambo ya Nje Marekani imesema kuwa imewatambua Abdullahi Osman Mohamed na Maalim Ayman katika orodha ya magaidi wa kimataifa.

    Taarifa kutoka wizara hiyo imesema Bwana Mohamed ni mtaalamu mwandamizi wa vilipuzi wa kundi la Al-Shabab na kiongozi wa mausala yao ya mawasiliano huku Bwana Ayman akihusishwa na kupanga shambulizi lililotokea katika kambi ya Simba.

    "Raia wa Marekani wamepigwa marufuku kujihusisha na shughuli za muamala za aina yoyote na Mohamed and Ayman. Mali zao nchini Marekani zimezuiwa," Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Makataa ya siku tatu ya kujisalimisha kwa vikosi vya Tigray yakamilika

    Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema kuwa oparesheni ya kijeshi dhidi ya vikosi vya waasi kaskazini mwa Tigray inaingia katika awamu ya mwisho.

    Abiy Ahmed amesema kuwa siku tatu za kujisalimisha zilizotolewa kwa vikosi vya Tigray sasa zimekamilika.

    Inasemekana kuwa mamia ya watu wamefariki dunia katika kipindi cha karibu wiki mbili kwasababu ya mapigano kati ya waasi na jeshi.

    Pia watu takriban 27,000 wanakadiriwa kutorokea Sudan.

    Ethiopia imesema kuwa vikosi vyake vimeingia katika eneo la kaskazini mwa Tigray na sasa hivi vimefika eneo la mji wa Mekelle.

    Pia inasemekana wanamgambo wa Tigray wamekita kambi katika mji mwingine wa Alamata.

    Raia wengi wamelazimika kuhama makazi yao huko Tigray ndani ya wiki mbili tangu kuanza tena kwa vita.

    Mratibu wa misaada ya dharura, Mark Lowcock, amesema kuwa watu hao wanataabika kwa ukosefu wa chakula na mafuta lakini pia kukatizwa kwa mawasiliano eneo hilo kunamaanisha kwamba msaada wa kibinadamu hauwezi kufikika.

    Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limeonya uwezekano wa kutokea kwa athari zaidi za kibinadamu.

    Maelezo zaidi:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 18/11/2020.