'Mtashuhudia ndege za Israel juu ya anga ya Tehran' - Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel anasema nchi yake inalenga "kuzuia tishio la pande mbili" kutoka Tehran, yaani, "makombora ya nyuklia na balestiki"
Muhtasari
- Papa Leo atoa wito wa kuwepo kwa busara na mazungumzo kati ya Israel na Iran
- Jeshi la Israel lasema limewaua wanasayansi tisa wa masuala ya nyuklia wa Iran
- Iran yaonya kuwa italenga vituo vya Uingereza, Marekani na Ufaransa iwapo vitaikingia kifua Israel
- Idadi ya vifo kwenye ajali ya ndege ya India yafikia 270
- Katibu mkuu wa UN atoa wito kwa Iran na Israel kukomesha mashambulizi
- China yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran
- Israel inaendelea na mashambulizi dhidi ya Iran, jeshi lasema
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga
'Mtashuhudia ndege za Israel juu ya anga ya Tehran' - Netanyahu

Chanzo cha picha, GPO
Waziri mkuu wa Israel anasema nchi yake inalenga "kuzuia tishio la pande mbili" kutoka Tehran, yaani, "makombora ya nyuklia na balestiki" na anasema Israel imefikia malengo yake.
"Hatuwezi wa kuwaacha kujenga uwezo wa kuzalisha makombora 20,000, hivyo tumechukua hatua kuharibu uwezo wao wa uzalishaji, na hivyo ndivyo IDF inafanya sasa."
Anaongeza: "Tumetengeneza njia kuelekea Tehran. Katika siku za usoni karibu sana, utaona ndege za Israel, Jeshi la anga la Israel, marubani wetu, juu ya anga ya Tehran."
Unaweza kusoma;
Papa Leo atoa wito wa kuwepo kwa busara na mazungumzo kati ya Israel na Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku ya Jumamosi Papa Leo ameziomba mamlaka za Iran na Israel "busara" baada ya mashambulizi ya anga kati ya nchi hizo mbili kuua watu kadhaa na kuwalazimisha raia kukimbilia makazi salama, huku akitoa wito kwa mataifa hayo kufuata njia ya mazungumzo.
Leo, katika moja ya wito wake wenye nguvu zaidi wa kusisitiza amani tangu achaguliwe kuwa papa wiki tano zilizopita, aliwaambia waumini katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwamba anafuatilia hali hiyo kwa "wasiwasi mkubwa."
Katika wakati huu muhimu, ninatamani sana kuleta tena wito wa kuwepo kwa uwajibikaji na busara,” alisema papa.
"Ahadi ya kujenga dunia salama zaidi isiyo na tishio la silaha za nyuklia, lazima ishughulikiwe kupitia njia za heshima na mazungumzo ya dhati, ili kujenga amani ya kudumu kwa haki, kirafiki, na maslahi ya pamoja," alisema.
"Hakuna mtu anayepaswa kutishia uwepo wa mwingine," alisema Leo. "Ni jukumu la kila nchi kuunga mkono suala la amani, kuanzisha njia za maridhiano na kuhimiza suluhisho linalohakikisha usalama na heshima kwa wote."
Israel ilfanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran mapema siku ya Ijumaa, ikilenga makamanda, maeneo ya kijeshi na maeneo ya silaha za nyuklia katika kile ilichokiita "shambulio la kujikinga" ili kuizuia Iran kuendeleza mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Iran, ambayo inakanusha kuwa shughuli zake za kurutubisha madini ya uranium ni sehemu ya mpango wa siri wa silaha, ilijibu kwa kurusha makombora kwa wingi kuelekea Israel, na kuua takribani watu wawili na kuwajeruhi kadhaa.
Jeshi la israel lasema limewaua wanasayansi tisa wa masuala ya nyuklia wa Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema limewaua wanasayansi na wataalamu tisa wa nyuklia wa Iran.
Hapo awali, jeshi la Israel lilisema liliwaua sita katika wimbi la kwanza la mashambulizi dhidi ya Iran usiku wa Alhamisi.
Israel sasa inasema kuwa wanasayansi hao tisa waliuawa “mwanzoni mwa operesheni.”
Kwa mujibu wa ripoti kutoka shirika la habari la Reuters, Kwa upande mwingine, afisa wa kijeshi wa Israel amesema maeneo ya nyuklia ya Esfahan na Natanz yameharibiwa kwa kiwango kikubwa katika mashambulizi hayo.
Afisa huyo ameiambia Reuters kuwa maeneo zaidi ya 150 nchini Iran yameshambuliwa. Amesema kuwa ndege zisizo na rubani na makombora mengi yaliyorushwa kuelekea Israel yamezuiliwa.
Unaweza kusoma;
Iran yaonya kuwa italenga vituo vya Uingereza, Marekani na Ufaransa iwapo vitaikingia kifua Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Iran imezionya Marekani, Uingereza na Ufaransa kutoisaidia Israel kukomesha mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Tehran, kulingana na shirika la habari la Reuters likinukuu vyombo vya habari vya serikali ya Iran.
Ripoti zinasema kuwa Tehran italenga vituo vya kijeshi na meli zilizoko katika eneo hilo ikiwa nchi hizo tatu zitaiunga mkono Israel.
Waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema "Tehran itaungua" ikiwa Iran itaendelea kurusha makombora.
Katika maoni yaliyotolewa wakati wa tathmini na maafisa wa kijeshi, Katz anasema: "Dikteta wa Iran anawageuza raia wa Iran kuwa mateka na kuunda ukweli ambao wao, haswa wakazi wa Tehran, watalipa gharama kubwa kwa shambulio la jinai dhidi ya raia wa Israel."
Unaweza kusoma;
Idadi ya vifo kwenye ajali ya ndege ya India yafikia 270

Chanzo cha picha, EPA
Idadi ya vifo kwenye ajali mbaya ya ndege ya shirika la ndege la India imeongezeka hadi 270 siku ya Jumamosi, huku familia zikiwa na huzuni na hasira kutokana na kucheleweshwa kukabidhiwa miili ya wapendwa wao ambayo iliteketea vibaya katika ajali hiyo iliyotokea katika jiji la Ahmedabad, magharibi mwa India.
Ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyokuwa na watu 242 ndani yake ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick nchini Uingereza, ilianza kushuka ghafla sekunde chache baada ya kuruka siku ya Alhamisi na kusababisha mlipuko mkuwa wa moto pale ilipogonga majengo yaliyo chini, katika kile kinachotajwa kuwa janga baya zaidi la ndege duniani katika kipindi cha muongo mmoja.
Takribani miili 270 imetolewa kutoka eneo la ajali ya ndege, alisema Dhaval Gameti, rais wa Chama cha Madaktari Wanafunzi katika Chuo cha udaktari cha B.J., alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Ni mtu mmoja tu kati ya abiria na wahudumu 242 waliokuwemo kwenye ndege hiyo ndiye aliyenusurika, huku wengine wote wakifariki dunia baada ya ndege hiyo kugonga bweni la chuo kikuu cha udaktari wakati ilipokuwa ikianguka.
Ndugu wenye wasiwasi wamekuwa wakingoja nje ya hospitali moja mjini Ahmedabad kukusanya miili ya wapendwa wao waliofariki kwenye ajali hiyo, huku madaktari wakifanya kazi kwa muda wa ziada kuchukua sampuli za meno kutoka kwa marehemu kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi wa vinasaba (DNA)
Miili mingi katika ajali hiyo iliteketea vibaya kwa moto, na mamlaka zinatumia sampuli za meno kufanya uchunguzi wa utambuzi.
Jaishankar Pillai, daktari wa uchunguzi wa vinasaba wa meno, aliwaambia waandishi wa habari siku ya Ijumaa kuwa tayari walikuwa na rekodi za meno za wahanga 135 walioteketea kwa moto, ambazo zinaweza kulinganishwa na kumbukumbu za awali za meno za waathirika, picha za mionzi au rekodi nyingine.
Unaweza kusoma;
Katibu mkuu wa UN atoa wito kwa Iran na Israel kukomesha mashambulizi

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku mashambulizi yakiendelea katika eneo hilo, kundi kubwa la viongozi wa dunia linatoa wito wa kupunguza na kujizuia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Iran na Israel kukomesha "ogezeko" la mashambulizi.
''Mashambulizi ya Israeli katika maeneo ya nyuklia ya Iran.Kombora la Iran lililoshambulia Tel Aviv. Ni wakati wa kuacha. Amani na diplomasia lazima ziwepo," anasema kwenye chapisho kwenye X.
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anasema alizungumza na Rais wa Israel Isaac Herzog kuhusu hali inayoendelea. "Nilisisitiza haki ya Israel ya kujilinda na kuwalinda watu wake. Wakati huo huo, kuhifadhi utulivu wa kikanda ni muhimu," anasema kwenye X, akiongeza kuwa amezitaka pande zote "kuchukua hatua kwa kujizuia zaidi".
Unaweza kusoma;
China yalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
China inalaani "ukiukaji wa Israel wa mamlaka, usalama na uadilifu wa ardhi ya Iran", mjumbe wa Umoja wa Mataifa Fu Cong alisema katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa saa chache zilizopita.
Beijing "ina wasiwasi mkubwa" juu ya athari mbaya ya hali ya sasa katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran, aliongeza, akiitaka Israel kuacha mara moja hatua zote za kijeshi ili kuepuka kuongezeka zaidi.
Fu pia alisema kuwa haki ya Iran ya "matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kama mtia saini wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia inapaswa kuheshimiwa kikamilifu".
China ni mshirika mkuu wa Tehran, hasa katika nishati na miundombinu.
Mwezi Machi, China iliwakaribisha naibu mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Urusi mjini Beijing, ambapo walijadili suala la nyuklia la Iran na kuhimiza vikwazo dhidi ya Iran viondolewe.
Unaweza kusoma;
Israel inaendelea na mashambulizi dhidi ya Iran, jeshi lasema

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema kuwa linaendelea na mashambulizi ya anga katika maeneo ya Iran.
Katika taarifa fupi iliyotumwa kwa Telegram, IDF ilisema kwamba "Jeshi la anga la Israel linaendelea kulenga shabaha ili kuondoa vitisho nchini Iran".
Taarifa hiyo ilichapishwa pamoja na video inayoonesha picha za maonyo ya angani.
Hatua hii inakuja zaidi ya saa 24 baada ya shambulio la awali la Israel kwenye kambi za kijeshi za Iran, ambalo liliua makamanda watatu wa kijeshi wa Iran, kulingana na IDF.
Tangu wakati huo Iran imeanzisha mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel hadi Jumamosi asubuhi.
Unaweza kusoma;
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu
