Kwaheri hadi kesho
Hapa ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja, tukutane kesho.
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waasi wa Syria wanasema wameudhibiti mji mkuu wa pili muhimu wa Hama, baada ya jeshi kuwaondoa wanajeshi wake huku kukiwa na mapigano makali.
Na Asha Juma & Rashid Abdallah
Hapa ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja, tukutane kesho.
Chakula pendwa cha Ivory Coast, attiéké - kinachotengenezwa kwa unga wa muhogo - kimeongezwa rasmi kwenye orodha ya Unesco ya urithi wa kitamaduni.
Attiéké hutengenezwa kutokana na mizizi ya mihogo iliyosagwa na ni chakula pendwa kwa kiamsha kinywa, chakula cha mchana, na chakula cha jioni.
Kwa kawaida huliwa na samaki wa kukaanga. Kilianza maeneo ya pwani ya Ivory Coast karne nyingi zilizopita, lakini sasa kinajulikana kote Afrika Magharibi.
Mjumbe wa Unesco wa Ivory Coast, Ramata Ly-Bakayoko, alikiambia kikao cha 19 kuhusu umuhimu wa kulinda turathi za kitamaduni huko Paraguay.
Sake ya Kijapani, kinywaji cha kilevi kinachotengenezwa kutokana na nafaka, pia kimeongezwa kwenye orodha mwaka huu.
Shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International limeishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza, jambo ambalo Israel inalikanusha vikali.
Kikundi hicho cha haki za binadamu chenye makao yake nchini Uingereza kilisema maudhui ya ripoti hiyo yametokana na "taarifa za udhalilishaji wa utu na mauaji ya halaiki" za maafisa wa Israeli, picha za kidijitali na ushuhuda wa mashahidi.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilielezea ripoti hiyo yenye kurasa 295 kama "ya uwongo kabisa na yenye msingi wa uongo", wakati jeshi la Israel lilisema madai hayo "hayana msingi kabisa na yameshindwa kujibu ukweli wa operesheni" inayoikabili.
Wakati haya yakijiri, madaktari wa ndani wanasema kuwa Wapalestina 50 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza.
Idadi kubwa zaidi ya watu waliuawa katika kambi ya al-Mawasi ya watu waliokimbia makazi yao, ambapo Israel inasema ilikuwa ikiwalenga wapiganaji wa Hamas.
Unaweza pia kusoma:
Waasi wa Syria wanasema wameudhibiti mji mkuu wa pili muhimu wa Hama, baada ya jeshi kuwaondoa wanajeshi wake huku kukiwa na mapigano makali.
Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu Hayat Tahrir al-Sham (HTS), Abu Mohammed al-Jawlani, alitangaza "ushindi" katika mji huo na kuapa kuwa "hakutakuwa na kisasi".
Hapo awali, kamanda wa waasi alisema wapiganaji wa HTS na washirika wao waliteka gereza na kuwaachilia wafungwa, huku jeshi likisema kuwa limetuma wanajeshi tena "kulinda maisha ya raia na kuzuia mapigano ya mijini".
Hama ni makazi ya watu milioni moja na iko kilomita 110 (maili 70) kusini mwa jiji la Aleppo, uliotekwa wiki iliyopita baada ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza kutoka ngome yao kaskazini-magharibi.
Pia unaweza kusema:
Katika tukio la vita vikubwa kama vile vya Ukraine, jeshi lililopo la Uingereza kwa nguvu zake za sasa litaangamizwa ndani ya miezi sita, hivyo ni muhimu kwa Uingereza kuunda kikosi kikubwa cha askari wa akiba. Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Alistair Carnes.
"Katika vita vikubwa - sawa na ile vya Ukraine - jeshi letu, kulingana na kiwango cha sasa cha hasara nchini Ukraine, litapoteza ndani ya miezi sita,” amesema naibu waziri Ulinzi, akizungumza katika Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi (RUSI) huko London.
Alistair Carnes, kanali mstaafu wa jeshi la majini, ameeleza kwamba anaamini Uingereza inahitaji kuongeza idadi ya askari wa akiba.
Novemba, Luteni Jenerali Rob Magowan, akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya House of Commons, alihakikisha kwamba jeshi liko tayari kupigana ikiwa litaamriwa, na hakuna mtu anayepaswa kufikiri kwamba ikiwa Urusi itashambulia nchi za NATO, basi Uingereza haitawasaidia.
Pia unaweza kusema:
Admirali Tony Radakin, afisa mkuu wa jeshi katika vikosi vya jeshi la Uingereza, ametoa hotuba yake ya kila mwaka katika kitengo cha watalaam RUSI na kusema, pamoja na mambo mengine, uwezo wa Urusi kutekeleza mashambulizi ya moja kwa moja au kuivamia Uingereza ikiwa nchi hizo mbili ziko vitani iko chini.
Mkuu huyo wa jeshi alisisitiza haja ya kuwa "wazi" kuhusu vitisho vinavyoikabili nchi hiyo.
Moscow inajua "jibu litakuwa kubwa," Radakin aliendelea. Lakini ni muhimu "kuweka nguvu na kuendelea kuimarisha" kizuizi cha nyuklia, na serikali kadhaa za Uingereza zimewekeza sana katika nyambizi na makombora ambayo yanaunda nguvu ya nyuklia ya Uingereza.
Sehemu hiyo ni ya akiba yetu ambayo Urusi inafahamu zaidi na ambayo ina athari kubwa kwa Putin," aliongeza.
Radakin alibainisha kuwa dunia inaingia katika "enzi ya tatu ya atomiki" ambapo idadi ya mamlaka yenye silaha za nyuklia itaongezeka.
Alisema, kuwa Urusi, China, Iran na Korea Kaskazini zitaongeza akiba zao za silaha za nyuklia au zitaendelea kujaribu kuzipata.
Kuhusu vita vya Ukraine, Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi alitaja kuonekana kwa maelfu ya wanajeshi wa Korea Kaskazini kwenye mipaka ya Ukraine kuwa tukio la kushangaza zaidi la mwaka.
Kulingana naye, “makumi ya maelfu zaidi yatafuata kama sehemu ya mapatano mapya.
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kutoka Iran Narges Mohammadi ameachiliwa kutoka jela kwa wiki tatu ili kupata matibabu, kulingana na wakili wake.
Mostafa Nili alisema maafisa walisimamisha kifungo cha jela cha mteja wake kwa ushauri wa daktari baada ya Bi Mohammadi kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe.
Familia yake na wafuasi wake wametaka aachiliwe huru, wakielezea kuachiliwa kwa muda ni "jambo dogo sana, na lililochelewa sana."
Mwanaharakati huyo wa haki za wanawake mwenye umri wa miaka 52 amekuwa akishikiliwa katika jela ya Evin ya Tehran tangu 2021.
Kufuatia kuachiliwa kwake kwa muda, video iliwekwa kwenye akaunti ya Instagram ya Bi Mohammadi ikimuonyesha akiwa ameketi kwenye machela baada ya kutolewa katika gari la wagonjwa.
Katika video hiyo, anapaza sauti "Mwanamke, Maisha, Uhuru" - kauli mbiu ya vuguvugu la maandamano ya 2022-2023 ambayo yalitikisa Iran.
Polisi wa jiji la New York wameanzisha msako wa kumtafuta mshukiwa aliyejifunika uso na kumuua kwa risasi, mkuu wa kampuni kubwa ya bima ya matibabu nchini Marekani, katika kile wachunguzi wanachoeleza kuwa ni "shambulio la kinyama, lakuvizia."
Mtendaji mkuu wa UnitedHealthcare, Brian Thompson aliuawa kwa kupigwa risasi mgongoni Jumatano asubuhi nje ya Hoteli ya Hilton huko Midtown Manhattan, ambapo alikuwa anatarajia kuzungumza kwenye mkutano wa wawekezaji baadaye siku hiyo.
Ni Baba wa watoto wawili mwenye umri wa miaka 50, alipelekwa hospitalini, ambako alitangazwa kufariki dakika chache baada ya shambulio hilo, maafisa wamesema.
Wachunguzi wamesema hawajui sababu ya mshambuliaji kufanya hivyo, na kutoweka eneo la tukio bila kuchukua mali yoyote ya mwathiriwa.
Polisi wametoa zawadi ya dola za Kimarekani 10,000 kwa atakayetoa taarifa za kupatikana kwake.
Mshindi mara tatu wa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki, Charlotte Dujardin amepigwa marufuku kwa mwaka mmoja na kutozwa faini ya pauni 8,886 kwa "kumchapa farasi kupita kiasi."
Kanda za video ziliibuka mwezi Julai za mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 39 akimpiga farasi mara kwa mara kwa mjeledi mrefu kwenye miguu yake, siku chache kabla ya kuanza kwa Olimpiki ya Paris 2024.
Marufuku hiyo ya kimataifa dhidi ya Dujardin, iliyotolewa na FEI - shirikisho la ulimwengu la michezo ya wapanda farasi.
Medali sita za Olimpiki za Dujardin zinazojumuisha medali tatu za dhahabu, fedha na shaba mbili ndizo nyingi zaidi za Mwana Olimpiki wa kike wa Uingereza.
Dujardin alijiondoa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, ambapo alipaswa kuwakilisha Timu ya GB, baada ya kukubali kuwa ndiye mtu aliyerekodiwa.
Pia unaweza kusoma:
Jimbo la kaskazini mashariki mwa India la Assam limepiga marufuku ulaji wa nyama ya ng'ombe katika maeneo ya umma ikijumuisha mikahawa na hafla.
Waziri Mkuu Himanta Biswa Sarma alisema siku ya Jumatano, kuwa huu ni upanuzi wa sheria ya awali iliyozuia uuzaji wa nyama ya ng'ombe karibu na maeneo fulani ya kidini kama mahekalu,
Lakini nyama bado inaweza kununuliwa kutoka katika maduka na kuliwa ndani ya nyumba au taasisi za kibinafsi katika jimbo hilo.
Ulaji wa nyama ya ng'ombe ni suala nyeti nchini India, kwani ng'ombe wanaheshimiwa na Wahindu, ambao wanajumuisha 80% ya wakazi wa nchi hiyo.
Majimbo kadhaa yanayotawaliwa na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) cha Waziri Mkuu Narendra Modi – ambacho kipo madarakani - yamekabiliana vikali na uchinjaji wa ng'ombe katika miaka ya hivi karibuni.
Takriban theluthi mbili ya majimbo 28 ya India, mengi yakiwa yanatawaliwa na BJP, yamepiga marufuku kwa sehemu au kikamilifu uchinjaji wa ng'ombe na ulaji wa nyama ya ng'ombe, ingawa ulaji wa nyama ya nyati ni halali katika baadhi ya maeneo haya.
Katika maeneo mengi ya India, vikundi vya Kihindu vinashutumiwa kutekeleza marufuku hiyo kupitia vurugu, mara nyingi hufanya mashambulizi mabaya kwa wauzaji wa nyama Waislamu na wafanyabiashara wa ng'ombe, ambao nyama ya ng'ombe ni chakula kikuu na cha bei nafuu.
Pia unaweza kusema:
Mahakama nchini Kenya imemtia hatiani mpiga picha kwa mauaji ya mwanaharakati wa LGBT, Edwin Kiprotich Kipruto, almaarufu Edwin Chiloba, ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa kwenye sanduku la chuma miaka miwili iliyopita.
Mahakama katika mji wa magharibi wa Eldoret iliamua kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kuwa Jacktone Odhiambo aliyekuwa akiishi na Chiloba ndiye alimuua.
Mwili wa Chiloba aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu, ulitupwa kando ya barabara mjini Eldoret.
Kenya ni jamii ya kihafidhina na mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria, adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka 14 jela, ingawa haijabainika iwapo kumekuwa na hatia yoyote.
Hakimu Reuben Nyakundi alisema ushahidi uliojumuisha vipimo vya DNA ulithibishisha mshtakiwa kuhusika na mauaji hayo. Ushahidi huo pia ulionyesha kuwa mshukiwa alimdhalilisha Chiloba kabla ya kumuua.
Uchunguzi wa maiti ulionyesha alikufa kutokana na kukosa oksijeni. Odhiambo atahukumiwa tarehe 16 Disemba.
Wizara ya Afya ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inatazamiwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ugonjwa usiojulikana ambao umeua takriban watu 79 katika jimbo la Kwango kusini-magharibi tangu Oktoba 24.
Wengi wa waliofariki ni watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 15.
Zaidi ya watu 300 walioambukizwa dalili za mafua ikiwa ni pamoja na: homa, maumivu ya kichwa, mafua pua na kikohozi, ugumu wa kupumua na upungufu wa damu.
Afisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika aliambia BBC kuwa "wametuma timu katika eneo la mbali kuchukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara".
Mamlaka nchini humo imewataka wakazi kuwa watulivu na waangalifu.
Waliwataka watu kunawa mikono kwa sabuni, kuepuka mikusanyiko ya watu wengi, na kuepuka kugusa miili ya marehemu bila wahudumu wa afya waliopata mafunzo.
Amnesty International imeshutumu taifa la Israel kwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika vita vya Gaza kwenye ripoti iliyochapishwa siku ya Alhamisi, madai ambayo viongozi wa Israel wameyakanusha mara kwa mara.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza limesema limefikia hitimisho hilo baada ya miezi kadhaa ya kuchambua matukio na kauli za maafisa wa Israel.
Amnesty ilisema kiwango cha kuzingatiwa kisheria cha uhalifu huo kilifikiwa, katika uamuzi wake wa kwanza kama huo wakati wa mzozo mkali uliohusisha utumiaji wa silaha.
Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948, uliotungwa kufuatia mauaji ya halaiki ya Wayahudi katika Mauaji ya halaiki ya Nazi, unafafanua mauaji ya halaiki kama "vitendo vilivyofanywa kwa nia ya kuharibu, kwa ujumla au kwa sehemu, kikundi cha kitaifa, kikabila, ubaguzi au kidini".
Israel imekanusha mara kwa mara shtaka lolote la mauaji ya halaiki, ikisema kuwa imeheshimu sheria za kimataifa na ina haki ya kujitetea baada ya shambulio la kuvuka mpaka la Hamas kutoka Gaza mnamo Oktoba 7, 2023 ambalo lilichochea vita.
Maafisa wa Israel hawakupatikana mara moja kutoa maoni yao kuhusu ripoti ya Amnesty International.
Soma hapa:
Bei ya Bitcoin kwa mara ya kwanza imepita zaidi ya $100,000, na kufikia rekodi mpya ya juu.
Kuongezeka kwa thamani ya sarafu ya kidigitali iliyo kubwa zaidi duniani kumechochewa na matumaini kwamba Rais mteule wa Marekani Donald Trump atapitisha sera ambazo zinapendelea mfumo wa sarafa za kidigitali.
Hatua hiyo ilifikiwa saa chache baada ya Trump kusema atamteua kamishna wa zamani wa Tume ya Usalama na Biashara Paul Atkins kusimamia udhibiti wa masoko ya hisa.
Hatua hiyo muhimu ya $100,000 ilichochea sherehe kwa wanaopedelea sarafu za kidigitali kote ulimwenguni.
Thamani ya Bitcoin inayobadilika-badilika mara kwa mara imevutia watu wengi, huku wanaoipendelea wakifurahia kwa kupita viwango vya awali vya bei.
Ushindi wa Trump katika uchaguzi wa mwezi uliopita ulikuwa kichocheo cha ongezeko la thamani ya Bitcoin hivi punde.
Rais mteule ameapa kuifanya Marekani kuwa "mji mkuu wa fedha ya kidigitali duniani" - mabadiliko ya ajabu ya hivi punde kutoka kwake ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo alikuwa anaita Bitcoin "utapeli."
Soma zaidi:
Jeshi la Israel linasema mwili wa mateka wa Israel anayeshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza umepatikana katika operesheni ya pamoja na idara ya usalama ya Shin Bet.
Taarifa ilisema Itay Svirsky, 38, ambaye alitekwa nyara kutoka Kibbutz Be'eri wakati wa shambulizi la Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israeli, "aliuawa akiwa utumwani na watekaji wake".
Hamas ilisema mwezi Januari kwamba Svirsky na mateka mwingine, Yossi Sharabi, 53, waliuawa wakati wa mashambulizi ya anga ya Israeli.
Hapo awali, jeshi lilisema uchunguzi ulihitimisha kwamba maelezo ya kina ya vifo vya mateka wengine sita waliopatikana wamefariki kwenye handaki huko Gaza mnamo mwezi Agosti ni kwamba walipigwa risasi na Hamas "karibu" na wakati wa shambulio la anga la Israeli.
Wanajeshi walipata miili ya Yagev Buchshtab, 35, Alexander Dancyg, 76, Avraham Munder, 79, Yoram Metzger, 80, Chaim Peri, 79, na Nadav Popplewell, mwenye umri wa miaka 51, mwenye uraia mara mbili wa Uingereza na Israeli, pamoja na wapiganaji sita wa Hamas, katika eneo la kusini la Khan Younis.
Jeshi lilisema "kuna uwezekano mkubwa" vifo vya mateka vilihusiana na mashambulizi ya Februari kwenye eneo la chini ya ardhi lililolenga makamanda wa Hamas.
Soma zaidi:
Ndege mzee zaidi duniani ametaga yai akiwa na umri wa takriban miaka 74, wanabiolojia wa Marekani wanasema.
Wisdom, ndege huyo alirekodiwa na Shirika la Huduma ya Samaki na Wanyamapori la Marekani (USFWS) katika Bahari ya Pasifiki pamoja na mwenzi wake wa hivi punde akitaga yai.
Ndege wa spishi hii kawaida huishi kwa miaka 12-40 tu, lakini Wisdom alitambulishwa mnamo 1956 alipokuwa na umri wa miaka mitano.
Mtoto wake wa mwisho alianguliwa mwaka wa 2021.
Inaaminika kwamba alikuwa na zaidi ya vifaranga 30 maishani mwake.
Shirika la USFWS lilisema kwenye mtandao wa X kwamba Wisdom alikuwa na mwenza wake mpya mwaka huu na kwamba mwenza wake wa awali Akeakamai hajaonekana kwa miaka kadhaa.
Pia unaweza kusoma:
Serikali ya Ufaransa imeporomoka baada ya Waziri Mkuu Michel Barnier kuenguliwa katika kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge walipiga kura kwa wingi kumtaka aondoke, miezi mitatu tu baada ya kuteuliwa na Rais Emmanuel Macron.
Viongozi wa upinzani walileta hoja hiyo baada ya Barnier kutumia madaraka maalum kupitisha bajeti yake ambayo haikuwa imepigiwa kura.
Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Ufaransa kuanguka kupitia kura ya kutokuwa na imani tangu mwaka 1962.
Hali hii inaongeza msukosuko wa kisiasa nchini Ufaransa, ambako tayari uchaguzi wa mapema uliofanyika msimu wa joto ulisababisha ukosefu wa wingi katika upande zote bungeni.
Wabunge walihitajika kupiga kura ya ndio au kutoshiriki, ambapo kura 288 zilihitajika ili pendekezo lipite. Jumla ya kura 331 zilipigwa kwa ajili ya pendekezo hilo.
Barnier sasa anapaswa kujiuzulu kwa serikali yake na bajeti iliyosababisha kuporomoka kwake imepitwa na wakati.
Hata hivyo, anatarajiwa kusalia kama Waziri Mkuu wa mpito hadi Macron apate mrithi wake.
Mrengo wa kushoto na wa kulia walipeleka mapendekezo ya kutokuwa na imani naye baada ya Barnier kulazimisha mageuzi ya usalama wa kijamii kwa kutumia amri ya rais, baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa kutosha.
Rais Macron, aliyerejea Ufaransa baada ya ziara rasmi Saudi Arabia, anatarajiwa kutoa hotuba ya kitaifa Alhamisi jioni.
Haathiriwi moja kwa moja na matokeo ya kura, kwani Ufaransa inampigia kura rais wake tofauti na serikali yake.
Macron alikuwa amesema hatajiuzulu vyovyote vile matokeo ya kura yatakavyokuwa.
Anatarajiwa kumteua waziri mkuu mpya haraka iwezekanavyo ili kuepusha aibu ya serikali isiyokuwapo – na zaidi, kwa sababu Rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuzuru Paris wikendi hii kwa ufunguzi wa kanisa kuu la Notre-Dame.
Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ambaye alitangaza sheria ya kijeshi ametakiwa kuondoka kwenye chama chake cha People's Power Party.
Kiongozi wa chama hicho Han Dong-hoon aliwaambia waandishi wa habari "amemtaka rais huyo kujiuzulu" kutoka kwa chama.
Hata hivyo chama hicho kimedokeza kuwa hakitaunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani iliyoletwa na upinzani.
Yoon amekubali kujiuzulu kwa waziri wa ulinzi Kim Yong-hyun, ambaye inasemekana ndiye aliyependekeza sheria ya kijeshi kwa rais.
Kim aliomba radhi kwa baraza la mawaziri hapo jana na kujiuzulu.
Maandamano zaidi na mikutano ya hadhara inafanyika kote nchini humo hii leo huku rais - ambaye sasa anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani naye - akitarajiwa kuomba msamaha.
Bunge linatazamiwa kupiga kura ya kumuondoa Yoon madarakani.
Soma zaidi: