India na Pakistan zakubaliana kusitisha mapigano baada ya siku kadhaa za mashambulizi
Pakistan yafungua anga lake kwa ndege zote, huku India ikisema mapigano yamesitishwa
Muhtasari
- India na Pakistan zasitisha mapigano baada ya siku kadhaa za mashambulizi
- Mamluki na mpangaji mapinduzi Simon Mann afariki dunia
- Viongozi wa Ulaya na Trump wajadili mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30
- Afrika Kusini yakosoa mpango wa Marekani kukubali Waafrika wazungu kama wakimbizi
- 'Pakistan imejibu kwa usahihi' – Waziri Mkuu Sharif
- Zelensky akaribisha viongozi wa Ulaya Ukraine katika juhudi za kukomesha vita
- Familia za mateka zendelea kuwa na wasiwasi juu ya hatima ya wapendwa wao
- India inasema Pakistan ilitumia makombora ya masafa marefu kulenga ngome zake
- Pakistan yaanza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya India - Jeshi
Moja kwa moja
Na Asha Juma
Habari za hivi punde, India na Pakistan zakubaliana kusitisha mapigano baada ya siku kadhaa za mashambulizi

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya siku nne za mashambulizi kutoka kila upande, India na Pakistan zimekubali kusitisha mapigano. Kipi kilichotokea?
Donald Trump alikuwa wa kwanza kuashiria kusitishwa kwa mapigano, akiweka ujumbe wake mtandao wa Truth Social kwamba Marekani ilikuwa ni mpatanishi wa mazungumzo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Ishaq Dar alithibitisha kuwa nchi yake imekubali kusitisha mapigano. Aliviambia vyombo vya habari vya Pakistan kwamba zaidi ya "nchi 30" zilihusika katika mazungumzo ya diplomasia - ikiwa ni pamoja na Uturuki, Saudi Arabia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio.
Waziri wa Mambo ya Nje wa India Vikram Misri kisha alithibitisha kwamba India ilikuwa imekubali "kusimamisha ufyatuaji risasi na hatua zote za kijeshi ardhini, angani na baharini". Aliongeza kwa ufupi mkutano wa wanahabari kwamba usitishaji mapigano ulianza kutekelezwa kutoka 17:00 IST (12.30 BST).
Mwandishi wa BBC wa Asia Kusini Samira Hussain aliripoti kwamba India na Pakistan zitafanya tena mazungumzo siku ya Jumatatu.
Maafisa wa ulinzi wa India kisha wakafanya mkutano na waandishi wa habari huko New Delhi. Walisema wanakubali makubaliano hayo lakini watakua macho kutetea India kukiwa na haja ya kufanya hivyo.
Kutokana na tangazo hilo, Pakistan imefungua tena anga yake kwa ndege zote.
Soma zaidi:
Mamluki na mpangaji mapinduzi Simon Mann afariki dunia

Chanzo cha picha, AP
Afisa wa zamani wa Jeshi la Uingereza ambaye pia alikuwa mamluki Simon Mann, na alikuwa sehemu ya jaribio la mapinduzi nchini Equatorial Guinea mwaka 2004, alifariki dunia kutokana na mshtuko wa moyo alipokuwa akifanya mazoezi, marafiki walithibitisha.
Mann mwenye umri wa miaka 72 alijipatia mamilioni ya pauni kutokana na kulinda biashara katika maeneo yenye migogoro kabla ya kushiriki katika jaribio lililoshindwa la kumpindua mtawala wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Mann alihukumiwa kifungo cha miaka 34 jela kwa kuwa na silaha na kupanga njama ya kupindua serikali.
Mnamo 2009, komando huyo wa zamani alisamehewa, akaachiliwa na kupewa masaa 48 kuondoka nchini humo.
Njama hiyo ilikuwa ni jaribio la kumpindua Rais Teodoro Obiang Nguema - wakati huo Mann na washirika wake walisema lengo lilikuwa kumsimamisha kiongozi wa upinzani aliye uhamishoni Severo Moto.
Iligunduliwa baada ya polisi katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare kukamata ndege iliyokuwa imetoka Afrika Kusini.
Mann na wengine zaidi ya 60 walikamatwa, huku kukiwa na madai kwamba walikuwa mamluki.
Walisema walikuwa wakitoa ulinzi kwa mgodi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Viongozi wa Ulaya na Trump wajadili mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 30

Chanzo cha picha, PA Media
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer na viongozi wenzake wa Ulaya wamempigia simu Rais Trump kutoka Kyiv walipokuwa wakifanya mazungumzo ya amani kuhusu vita nchini Ukraine.
Baada ya mkutano wa mtandaoni wa muungano wa walio tayari, waziri mkuu, pamoja na Rais wa Ukraine Zelensky, Rais wa Ufaransa Macron, Kansela wa Ujerumani Merz na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, walimpigia simu Trump ili kumuarifu juu ya kuunga mkono pendekezo la Marekani.
Viongozi hao kwa pamoja wamejadili mipango ya kusitisha mapigano kwa siku 30 na Urusi kuanzia Jumatatu.
Soma zaidi:
Afrika Kusini yakosoa mpango wa Marekani kukubali Waafrika wazungu kama wakimbizi

Chanzo cha picha, EPA
Wazungu Afrika Kusini wakosoa mpango wa Marekani wa kuwapokea Waafrika weupe kama wakimbizi
Afrika Kusini imeikosoa Marekani huku ripoti zikiibuka zinazosema kuwa Marekani inaweza kupokea Waafrika wenye asili ya wazungu kama wakimbizi mapema wiki ijayo.
Waraka ulioonekana na mshirika wa BBC wa Marekani CBS unaelezea uwezekano wa kuhamishwa kama "kipaumbele" kwa serikali ya Rais Donald Trump, hata hivyo muda haujathibitishwa hadharani na Ikulu ya White House.
Katika taarifa iliyochapishwa Ijumaa, wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini ilielezea hatua hiyo inayodaiwa kuwa "ilichochewa kisiasa" na iliyoundwa kudhoofisha "demokrasia ya kikatiba" ya Afrika Kusini.
Mnamo Februari, Trump alielezea Waafrika kama waathiriwa wa "ubaguzi wa rangi" katika agizo kuu, na kuwapa fursa ya kuishi tena Marekani.
Mamlaka za Afrika Kusini zilisema hazitazuia kuondoka kwa wale waliochaguliwa kwa ajili ya makazi mapya, lakini walisema walikuwa wametafuta hakikisho kutoka kwa Marekani kwamba wawe wamechunguzwa na kuhakikiwa kikamilifu na wasiwe na mashtaka ya uhalifu yanayowasubiri.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa madai ya ubaguzi dhidi ya wazungu walio wachache nchini humo hayana msingi wowote, na kwamba takwimu za uhalifu hazionyeshi kwamba kuna kundi lolote lililolengwa katika vurugu za mashamba.
Soma zaidi:
'Pakistan imejibu kwa usahihi' – Waziri Mkuu Sharif

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif anasema jeshi la nchi hiyo limejibu "kwa usahihi" shambulizi la India huku mzozo kati yan chi hizo mbili ukiendelea kuongezeka.
"Leo, tumeijibu India kwa usahihi na kulipiza kisasi damu ya watu wasio na hatia," amesema katika taarifa.
Awali, jeshi la Pakistan lilisema lilikuwa limechukua hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya India baada ya kuishutumu Delhi kwa kurusha makombora katika vituo vyake vitatu vya anga.
Soma zaidi:
Zelensky akaribisha viongozi wa Ulaya Ukraine katika juhudi za kukomesha vita

Chanzo cha picha, Reuters
Viongozi wa Ulaya wako mjini Kyiv nchini Ukraine katika juhudi za usitishaji mapigano.
Mkutano huu unawadia baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kutangaza vikwazo vipya kwa kile Putin alichokiita “shadow fleet” hapo jana.
Neno hili linarejelea kundi la meli za mafuta za Urusi zenye kuhusishwa na vikwazo vya usafirishaji wa mafuta na gesi.
Akijibu, Zelensky alisema siku ya Ijumaa kwamba anashukuru Uingereza kwa "vikwazo vipya" vyenye uzito.
"Kila hatua ambayo inazuia uwezo wa Kremlin kufadhili vita vyake huleta amani karibu. Uingereza kwa mara nyingine tena inaonyesha mbinu ya uongozi," alisema.
Soma zaidi:
Familia za mateka zaendelea kuwa na wasiwasi juu ya hatima ya wapendwa wao

Chanzo cha picha, Hostages and Missing Families Forum
Familia za mateka wa Israel waliopelekwa Gaza katika mashambulizi ya Oktoba 7 wameelezea wasiwasi wao unaoongezeka juu ya hatima ya wapendwa wao, huku mashaka yakiongezeka kuhusu wangapi bado wako hai.
Familia moja ilisema mateka hao wako hatarini "kila siku" wanapoendelea kushikiliwa na Hamas.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema wiki hii "hakuna uhakika" juu ya hali ya mateka watatu kati ya 24 walioaminika kuwa hai hapo awali .
Alikuwa akijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumanne kwamba ni 21 tu kati ya wale waliochukuliwa mateka katika mashambulizi yanayoongozwa na Hamas ambao walikuwa bado hai.
BBC ilizungumza na familia mbili - ikiwa ni pamoja na kaka wa mateka aliyeachiliwa huru na Hamas mwaka huu - baada ya baraza la mawaziri la usalama la Israel kuidhinisha mashambulizi zaidi huko Gaza.
Netanyahu alisema mawaziri waliamua utekelezaji wa "operesheni kali" ya kusambaratisha Hamas na kuwaokoa mateka, na kwamba wakazi milioni 2.1 wa Gaza "watahamishwa, ili kuwalinda".
Familia moja iliambia BBC kuwa wanatumai wanajeshi hao watatumiwa tu kusaidia kwa lengo la kuwaachilia mateka hao, wala si kwa sababu nyinginezo.
India inasema Pakistan ilitumia makombora ya masafa marefu kulenga ngome zake

Chanzo cha picha, Getty Images
Kanali wa Jeshi la India Sofiya Qureshi, ameishutumu Pakistan kwa kutumia makombora ya masafa marefu kulenga vituo vya anga vya India.
Taarifa hiyo imetolewa saa chache baada ya Pakistan kuishutumu India kwa kulenga vituo vyake vitatu vya kijeshi kwa mashambulizi ya makombora.
Wakiwa katika mkutano, Waziri wa Mambo ya Nje wa India Vikram Misri anawaambia waliokusanyika:
"Nimesema katika matukio mengi ya awali, hatua za Pakistani ndio ambazo zimesababisha uchochezi na kuongezeka kwa mzozo huu.
Kamanda wa Jeshi la Wanahewa la India Vyomika Singh, amesema Pakistan ilifanya "vitendo vikali kwa kutumia vienezaji vingi vya vitisho" kuzunguka mpaka wa magharibi wa India.
Amesema Pakistan ilitumia silaha - ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani na makombora ya masafa marefu - "kulenga raia na miundombinu ya kijeshi".
"Ikijibu, India imejitetea ikisema imechukua hatua zenye kipimo na kuwajibika kutokana na uchochezi unaoongezeka kutoka upande wa Pakistani.
"Mapema asubuhi ya leo, kumekuwa na marudio ya vitendo vya uchokozi."
Soma zaidi:
Pakistan yaanza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya India - Jeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Televisheni ya taifa ya Pakistani na idara ya uhusiano wa umma ya jeshi zimesema kuwa mashambulizi dhidi ya India yameanzishwa, baada ya kuishutumu Delhi kwa kurusha makombora katika vituo vitatu vya ndege vya Pakistan.
Kwa mujibu wa Idara ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Pakistani (ISPR), Pakistan imeita mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi "Operesheni Banyan Marsus".
India haijatoa maoni yoyote kuhusu hatua hiyo.
Milipuko yatikisa hoteli
Mwanahabari Aamir Peerzada kutoka Srinagar, Kashmir inayosimamiwa na India amesema aliamshwa na milipuko miwili mikubwa huko Srinagar karibu 5:45 asubuhi kwa saa za eneo.
Dakika 20 hivi baadaye, milipuko mingine mitatu ikatokea.
Milipuko miwili ya kwanza ilitikisa hoteli yetu huko Srinagar.
Pakistan yafungwa anga lake kwa muda
Muda mfupi baada ya shambulizi kuripotiwa mwendo wa saa 03:15 saa za eneo - ambayo Pakistan inadai kuwa India ilishambulia kambi zake tatu za kijeshi - Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Pakistani imefunga anga lake hadi saa sita mchana.
Wakati huo huo, mamlaka ya viwanja vya Ndege ya India imetangaza kufunga viwanja vya ndege 32 kote kaskazini na magharibi mwa nchi hadi asubuhi ya tarehe 15 Mei.
Soma zaidi:
Hujambo, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja
