Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Vikosi vya Yemen vyashambuliana vikali na wanamgambo wa Houthi mpakani mwa Saudi Arabia

Vikosi vya serikali ya Yemen na kundi la Wahouthi vimeendelea kufanya mashambulizi makali katika maeneo mbalimbali ya Yemen na mpakani mwa Saudi Arabia.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Trump asema yuko tayari kukutana na Putin na Xi kujadili kupunguza silaha za nyuklia

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kushiriki mkutano wa pande tatu na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping, kufuatia taarifa kwamba Putin amependekeza mkutano maalumu kujadili mustakabali wa Ukraine.

    Hata hivyo, Trump amesema mkutano huo hautajikita katika suala la Ukraine, bali katika kutafuta njia za kuondoa au kupunguza idadi ya silaha za nyuklia duniani.

    Trump amesema, kwa maoni yake, Urusi imeshughulikia suala la Ukraine kwa njia inayofaa.

    Taarifa kuhusu pendekezo la Putin, iliyoripotiwa na gazeti la Wall Street Journal, imezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya na kulaaniwa vikali nchini Ukraine.

    Trump pia amerejea kumkosoa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akisema huenda wakati umefika wa mtu mwingine kuongoza mazungumzo ya kutafuta amani.

    Wakati huohuo, vita kati ya Ukraine na Urusi vinaendelea. Mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa watu wanne waliuawa katika mashambulizi ya Urusi usiku uliopita.

    Watu watatu waliuawa katika eneo la Kyiv, huku mwingine akipoteza maisha katika mji wa Zaporizhzhia. Watu wengine 11 walijeruhiwa.

    Mashambulizi hayo yalitokea baada ya Rais Zelensky kutangaza kuwa Ukraine itaendelea kushambulia miundombinu ya mafuta ya Urusi, kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi yanayoendelea kulenga mitambo ya umeme nchini Ukraine.

    Soma Pia:

  2. Ronaldo asimamishwa kuichezea timu ya taifa ya Ureno kwa siku 30 na kutozwa faini

    Cristiano Ronaldo amesimamishwa kuichezea timu ya taifa ya Ureno kwa siku 30 na kutozwa faini ya euro 255 na Shirikisho la Soka la Ureno (FPF), baada ya kuondoka kambini mwa timu hiyo kufuatia kutokubaliana na kocha Jorge Jesus.

    Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41 na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, aliondoka kambini Julai 9 akiwa amekasirishwa na kutochezeshwa katika mechi ya Ureno dhidi ya Norway. Aidha, alikuwa amearifiwa kuwa hangeanza katika kikosi cha kwanza cha Ureno kwenye mechi iliyofuata dhidi ya Denmark.

    Ronaldo alisema aliamua kuondoka kwa sababu Jorge Jesus hakuheshimu makubaliano waliyokuwa wamefikia. Alimtuhumu kocha huyo kwa kusaliti imani aliyokuwa amemwekea.

    Kwa upande wake, kocha huyo wa Ureno amekanusha kuwapo kwa makubaliano yoyote na Ronaldo, lakini amesema mlango wa kurejea kikosini ulikuwa wazi wakati wowote mchezaji huyo alipotaka kujiunga tena na timu hiyo.

    Ronaldo, ambaye ameshinda tuzo ya Ballon d'Or mara tano, ndiye mchezaji mwenye idadi kubwa zaidi ya mechi za kimataifa katika soka la wanaume, akiwa ameichezea Ureno mara 146.

    Soma pia:

  3. Mshauri wa Zelensky: Waukraine wanakufa kutokana na kupungua kwa ushirikiano wa kijasusi wa Marekani

    Raia wa Ukraine wameuawa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa tahadhari zisizo sahihi kutoka Marekani kuhusu mashambulizi ya Urusi, kwa mujibu wa mmoja wa washauri wakuu wa Rais Volodymyr Zelensky.

    Serhii “Flash” Beskrestnov aliiambia BBC kuwa baadhi ya watu wameuawa katika mashambulizi hayo kwa sababu hakukuwa na muda wa kutosha wa kuwaonya wananchi kuhusu mashambulizi ya makombora ya balistiki.

    “Ni hatari... Nafikiri hili ni jambo baya sana... Watu wameuawa,” alisema.

    Mshauri huyo pia alisema kuwa vikwazo vinavyoweka mipaka kwa Ukraine kutumia huduma ya intaneti ya satelaiti ya Starlink bado vinaendelea kutekelezwa.

    Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imesema kuwa hakuna mabadiliko yaliyofanyika katika ushirikiano wa kijasusi kati ya Washington na Kyiv.

    Wiki iliyopita, Ukraine ilitangaza kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani. Hatua hiyo ilijiri huku mvutano kati ya Kyiv na utawala wa Rais Donald Trump ukiongezeka kutokana na mkataba wenye utata wa kuingiza mafuta ya Urusi nchini Marekani, hali iliyozorotesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

    Licha ya Washington kukanusha kuwa kumekuwa na mabadiliko yoyote, baadhi ya watu nchini Ukraine wanahisi kuwa changamoto hizo zinahusiana na mvutano huo.

    Jumatatu asubuhi, Zelensky aliandika kwenye mtandao wa X kuwa mji mkuu wa Kyiv ulikabiliwa na mashambulizi mawili ya makombora ya balistiki usiku uliotangulia.

    “Usiku uliopita, makombora mawili ya balistiki yalishambulia mji mkuu. Shambulizi moja halikutanguliwa na tahadhari yoyote, huku jingine likiwa na tahadhari ya muda mfupi sana kiasi cha kutowawezesha watu kupata hifadhi kwa wakati,” aliandika.

    Soma pia:

  4. Ethiopia yaionya Eritrea dhidi ya kuunga mkono makundi ya upinzani

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ameionya Eritrea na kuwatishia kuwakabili na majibu makali iwapo itaendelea kuunga mkono makundi ya upinzani nchini Ethiopia, akiitaja serikali ya Eritrea kuwa “mjumbe wa uharibifu”.

    Katika mahojiano ya hivi karibuni kwa lugha ya Kitigrinya yaliyorushwa na televisheni ya taifa, Abiy amesema Eritrea imegeuka kuwa chombo kinachotumiwa na maadui wa Ethiopia.

    Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umedorora kwa kiasi kikubwa, huku uhusiano wa kidiplomasia ukikatika na mvutano ukiendelea kuongezeka. Ethiopia imeishutumu Eritrea kwa kuyaunga mkono makundi yenye silaha yanayopinga serikali yake na kuhusika katika mzozo unaoendelea kaskazini mwa Ethiopia. Eritrea imekanusha madai hayo.

    Mzozo wa kidiplomasia ulizidi kuongezeka baada ya Ethiopia kutangaza kufungwa kwa ubalozi wake mjini Asmara, mji mkuu wa Eritrea, tarehe mosi Oktoba 2026, na kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea. Eritrea ilijibu kwa kuchukua hatua kama hizo, na hatimaye kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ethiopia.

    Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Abiy amesema nchi zinazoiunga mkono Eritrea hazitaweza kuikinga na matokeo ya vitendo vyake.

    “Ninaamini kwa dhati kuwa wale wanaoiunga mkono Eritrea hawawezi kufanya zaidi ya kuipatia risasi, wala hawawezi kutatua matatizo ya Eritrea,” amesema, bila kutaja nchi au wahusika aliokuwa akiwazungumzia.

    Abiy pia ameishutumu Eritrea kwa kuchagua kuwa “uwanja wa michezo wa maadui” badala ya kuwa mshirika katika maendeleo ya kikanda.

    “Hata hivyo, ikiwa itaendelea kupuuza wito wetu, hatari itakuwa kubwa sana,” ameonya.

    Waziri mkuu huyo pia amekosoa hali ya ndani ya Eritrea, akidai kuwa serikali ya nchi hiyo imeshindwa kuweka maendeleo kuwa kipaumbele.

    “Kabla ya uhuru, miji ya Eritrea ilikuwa hai na yenye maendeleo. Leo hii, hata hivyo, imegeuzwa kuwa vijiji,” amesema.

    Abiy ameongeza kuwa Waeritrea wengi wamepoteza fursa za kiuchumi tangu nchi hiyo ipate uhuru, akisema changamoto zinazowakabili zimetokana na kushindwa kwa serikali katika utawala.

    “Watu wa Eritrea, ambao ni wachapakazi na wakarimu, wamekuwa ishara ya uhamiaji na maisha ya dhiki. Mtu akiuliza kwa nini hali hii imetokea, ni kwa sababu serikali iliacha kuwekeza katika maendeleo na ujenzi wa taasisi, na badala yake ikawa chombo cha maadui wa Ethiopia,” amesema.

    Soma Pia:

  5. Jeshi la Iran ladai kudungua droni ya Marekani

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) ladai kuilenga droni ya kijeshi ya Marekani

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne asubuhi, Oktoba 19, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema kuwa droni ya kijeshi ya Marekani aina ya MQ-9 Centcom "ilizuiwa na kuharibiwa" katika anga juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, droni hiyo ilidunguliwa kwa kutumia mfumo mpya wa kisasa wa ulinzi wa anga wa kikosi hicho, ukiwa chini ya usimamizi wa mtandao wa pamoja wa ulinzi wa anga wa Iran.

  6. Miji ya Ufaransa yawa tulivu usiku kucha baada ya amri za kutotoka nje

    Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesema kuwa utekelezaji wa amri maalum za kutotoka nje katika maeneo mbalimbali umechangia kuwepo kwa utulivu usiku uliopita, kufuatia wikendi iliyoshuhudia ghasia na uporaji katika sehemu kadhaa za nchi.

    Amri hizo zilianzishwa katika maeneo ya katikati ya jiji la Paris, ikiwemo Place de la République, ambako waandamanaji walikuwa wamekusanyika mwishoni mwa wiki, pamoja na eneo la biashara la Les Halles.

    Hatua nyingine za kuzuia mikusanyiko na kudhibiti harakati za vijana pia ziliwekwa katika miji ya Marseille, Bordeaux, Nice na Lyon kusini mwa Ufaransa, pamoja na Lille na miji mingine ya kaskazini.

    Lecornu aliwashukuru maafisa wa polisi na askari wa Gendarmerie kwa kusimamia na kutekeleza hatua hizo za usalama, akisema zimechangia kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika.

    Aidha, amesema uamuzi kuhusu kuendelea au kutekelezwa kwa amri nyingine za kutotoka nje usiku wa Jumanne utafanywa kulingana na hali ya usalama katika kila eneo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Lecornu alisema maamuzi hayo yatafanywa "moja kwa moja katika maeneo husika" na mamlaka za mikoa pamoja na mameya wa serikali za mitaa kulingana na mahitaji ya kila eneo.

  7. Lissu ateuliwa hatua ya mwisho na Bunge la Ulaya katika tuzo ya Sakharov

    Bunge la Ulaya limetangaza orodha ya wagombea watatu wa mwisho wa Tuzo ya Sakharov ya Haki za bindamu 2026, kwa kutambua mchango wao katika kutetea haki za binadamu, uhuru na demokrasia.

    Walioteuliwa kufika hatua ya mwisho ni:

    • Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na maafisa wake
    • Tundu Lissu wa Tanzania
    • Taraneh Rahimi na Romina Rahimi wa Iran

    Tuzo ya Sakharov hutolewa kila mwaka kwa watu binafsi au mashirika yanayojitokeza kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi duniani kote.

    Kila mwaka, Bunge la Ulaya hutunuku Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo kwa watu binafsi au mashirika yanayoonyesha ujasiri wa kipekee katika kutetea haki za binadamu, demokrasia na uhuru wa msingi duniani.

    Mwaka 2025, tuzo hiyo ilitolewa kwa Andrzej Poczobut, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa jamii ya Wapolandi nchini Belarus, pamoja na Mzia Amaglobeli, mwandishi wa habari kutoka Georgia na mwanamke wa kwanza kutambuliwa kama mfungwa wa kisiasa nchini humo tangu taifa hilo lipate uhuru wake.

    Kwa upande wa tuzo ya mwaka 2026, kamati za Mambo ya Nje na Maendeleo za Bunge la Ulaya zinatarajiwa kupigia kura orodha ya wagombea watatu wa mwisho tarehe 19 Oktoba mjini Strasbourg. Baadaye, Mkutano wa Marais wa Bunge la Ulaya utaamua mshindi wa tuzo hiyo tarehe 22 Oktoba 2026.

    Unaweza kusoma;

  8. Maafisa 13 wa uhifadhi na usalama wakamatwa baada ya vifo vya watu wanne Tanzania

    Polisi nchini Tanzania wamewakamata maafisa 13 wa uhifadhi na usalama kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha watu wanne waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa pikipiki katika wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, kaskazini-magharibi mwa nchi.

    Tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:00 asubuhi GMT Jumamosi katika kijiji cha Kanyamika, kando ya barabara ya Muleba-Biharamulo, takribani kilomita 140 kutoka mpaka wa Tanzania na Uganda.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, watuhumiwa hao ni pamoja na askari watatu wa Hifadhi ya Taifa, (TANAPA), askari sita maalumu wa misitu kutoka Tanzania Forest Services (TFS) na maafisa wanne wasaidizi wa usalama.

    Polisi wamesema uchunguzi unaendelea ili kubaini mazingira halisi yaliyosababisha tukio hilo la vifo.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, doria za maafisa hao zilikutana na watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa pikipiki 10 ndani ya hifadhi ya misitu. Inadaiwa kuwa watu hao walikataa kukamatwa na kujaribu kuwanyang'anya silaha maafisa hao.

    “Watu hao walikataa kujisalimisha na walijaribu kuwanyang'anya maafisa silaha, hali iliyosababisha mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu wanne,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

    Polisi walieleza kuwa walikamata pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa na mapanga matano, miongoni mwa vielelezo vingine. Pia walipata bunduki tatu aina ya AK-47 na gari la serikali lililokuwa limeharibiwa, huku vioo vya mbele na vya pembeni vikiwa vimevunjwa.

    Kamanda Chatanda aliwataka wananchi kuzingatia sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapokutana na polisi au mamlaka nyingine za utekelezaji wa sheria.

    Taarifa hiyo imezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya wananchi wamehoji iwapo wahusika watawajibishwa na kama matokeo ya uchunguzi yatawekwa wazi kwa umma.

    Mwezi Agosti mwaka huu, polisi waliwakamata askari watatu wa hifadhi kaskazini mwa Tanzania baada ya mtu mmoja kufariki na mwingine kujeruhiwa katika eneo la uhifadhi ambako walidaiwa kuingia kinyume cha sheria.

    Kwa muda mrefu, mashirika ya haki za binadamu nchini Tanzania yamekuwa yakieleza wasiwasi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na operesheni za utekelezaji wa sheria katika maeneo ya uhifadhi wa mazingira.

  9. Tetesi za soka Jumanne: Liverpool, Manchester United wamuweka Nmecha kwenye rada zao

    Liverpool na Manchester United ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazomfuatilia kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Felix Nmecha.

    Liverpool inatajwa kumuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa pauni milioni 84, kama mbadala wa Alex Scott wa Bournemouth na England.

    Kiungo wa Argentina Emiliano Buendía yuko karibu kukubaliana mkataba mpya na Aston Villa baada ya mazungumzo kuonesha maendeleo mazuri.

    Mlinzi wa kulia wa England Trent Alexander-Arnold anadaiwa kutafakari mustakabali wake Real Madrid kutokana na kutoridhishwa na muda mdogo wa kucheza. Klabu yake ya zamani ya Liverpool ni miongoni mwa timu zinazomfuatilia.

    Kuondoka kwa mshambuliaji chipukizi wa England mwenye umri wa miaka 16, JJ Gabriel, kutoka Manchester United kunatajwa kuwa karibu kutokea. Real Madrid imewasilisha ofa kubwa kwa mchezaji huyo, huku Barcelona na Bayern Munich nazo zikivutiwa naye.

    Manchester United pia inamfuatilia mlinzi wa pembeni wa Brazil mwenye umri wa miaka 23, Wesley, anayeichezea Roma, kabla ya uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la Januari.

    Winga wa England mwenye umri wa miaka 18, Rio Ngumoha, ameondoa uvumi wa kuhamia Arsenal na kusema mazungumzo ya kuongeza mkataba wake na Liverpool yanaendelea vizuri.

    Mlinzi wa zamani wa Real Madrid na Hispania, Sergio Ramos, anaangalia uwezekano wa kurejea Ulaya na La Liga, huku Getafe ikionesha nia ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40.

    Manchester United inaweza kulazimika kushindana na Juventus endapo itataka kumteua kocha wa Italia Antonio Conte kuchukua nafasi ya Michael Carrick, iwapo kocha huyo wa United ataachishwa kazi.

    Unaweza kusoma;

  10. Mkosoaji wa Rais wa Rwanda aliyekuwa uhamishoni apatikana akiwa amekatwa kichwa

    Aliyekuwa Sajenti Meja wa Jeshi la Rwanda, ambaye baadaye alijulikana kwa kuwa mkosoaji wa wazi wa Rais Paul Kagame, amepatikana akiwa amekatwa kichwa nchi jirani ya Uganda.

    Robert Kabera, mwenye umri wa miaka 50, alikimbia Rwanda baada ya kushtakiwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, ambayo aliyakanusha. Aliomba hifadhi nchini Uganda akidai kuwa alikuwa akifuatiliwa kwa misingi ya kisiasa.

    Msemaji wa Polisi wa Uganda, Kituuma Rusoke, alisema Jumatatu kwamba kichwa cha Kabera bado hakijapatikana. Mwili wake ulipatikana na wakazi wa eneo moja lililo pembezoni mwa mji wa Kampala mwishoni mwa wiki.

    Serikali ya Rwanda haijatoa tamko rasmi kuhusu mauaji hayo. Wakosoaji kadhaa wa Kagame wameuawa, ndani ya Rwanda na pia nje ya nchi.

    Mjane wake, Jeanne d'Arc Rwigema Uwizeye, aliiambia BBC idhaa ya Maziwa Makuu kwa ujumbe wa maandishi kwamba sasa ana hofu kuhusu usalama wa familia yake.

    “Inatisha. Nahisi kama nimechanganyikiwa. Mimi na watoto wangu hatuna usalama,” alisema.

    Kwa mujibu wa familia yake, Kabera alikuwa amesafiri kwenda kukagua eneo la ujenzi lililoko takribani kilomita 45 kutoka Kampala kabla ya kuuawa.

    Kabera alikuwa amejijengea umaarufu kama mwanamuziki na mtayarishaji wa maudhui kwenye YouTube. Kituo chake cha YouTube kilikuwa na zaidi ya wafuasi 144,000 na zaidi ya video 800, nyingi zikiwa zikimkosoa Kagame na utawala wake.

    Likizungumzia taarifa za kuuawa kwake, kundi la upinzani lililo uhamishoni la Rwanda National Congress (RNC) lilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa uwazi ili wale wote waliohusika na mauaji hayo wafikishwe mbele ya sheria.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, RNC ilisema:

    "Leo, familia yake inaomboleza, sauti yake imezimwa, na Wanyarwanda wanaoishi uhamishoni wanakabiliwa na swali la kutisha: tunaweza kuwa salama wapi?"

    Kifo chake kimeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wapinzani na wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni katika mataifa mbalimbali.

    Mwaka 2014, Patrick Karegeya, aliyekuwa mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya Rwanda na mmoja wa waanzilishi wa RNC, alipatikana amefariki katika chumba chake cha hoteli mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

    Tukio la kuuawa kwa Kabera limeibua tena mijadala kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda waliopo nje ya nchi, huku mashirika ya haki za binadamu na makundi ya upinzani yakitaka uchunguzi huru ufanyike ili kubaini waliohusika na tukio hilo.

  11. Vikosi vya Yemen vyashambuliana vikali na wanamgambo wa Houthi mpakani mwa Saudi Arabia

    Vikosi vya serikali ya Yemen na kundi la Wahouthi vimeendelea kushambuliana vikali katika maeneo mbalimbali ya Yemen na mpakani mwa Saudi Arabia, huku taarifa zikieleza kuwepo kwa makumi ya waliouawa na kujeruhiwa.

    Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na pande hizo mbili, vikosi vya serikali vilitekeleza mashambulizi dhidi ya ngome na maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi, huku vikidai kufanikisha operesheni kadhaa za kijeshi na kusababisha hasara kubwa kwa wapiganaji wa kundi hilo.

    Kwa upande mwingine, Wahouthi walitangaza kuwa walifanya mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya kijeshi na miundombinu ndani ya Saudi Arabia.

    Kundi hilo lilidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa sahihi na yalifanikiwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

    Taarifa kutoka pande zote zinaonesha kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo na majeraha ya watu kadhaa, wakiwemo wapiganaji na wanajeshi, ingawa idadi kamili ya waliopoteza maisha haijathibitishwa kwa uhuru.

    Mapigano haya yanaonesha kuendelea kwa mzozo wa muda mrefu nchini Yemen, ambao umesababisha maelfu ya vifo, mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa kibinadamu, na kuathiri utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.

    Unaweza kusoma;

  12. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo