Trump asema yuko tayari kukutana na Putin na Xi kujadili kupunguza silaha za nyuklia

Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kushiriki mkutano wa pande tatu na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping, kufuatia taarifa kwamba Putin amependekeza mkutano maalumu kujadili mustakabali wa Ukraine.
Hata hivyo, Trump amesema mkutano huo hautajikita katika suala la Ukraine, bali katika kutafuta njia za kuondoa au kupunguza idadi ya silaha za nyuklia duniani.
Trump amesema, kwa maoni yake, Urusi imeshughulikia suala la Ukraine kwa njia inayofaa.
Taarifa kuhusu pendekezo la Putin, iliyoripotiwa na gazeti la Wall Street Journal, imezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya na kulaaniwa vikali nchini Ukraine.
Trump pia amerejea kumkosoa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akisema huenda wakati umefika wa mtu mwingine kuongoza mazungumzo ya kutafuta amani.
Wakati huohuo, vita kati ya Ukraine na Urusi vinaendelea. Mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa watu wanne waliuawa katika mashambulizi ya Urusi usiku uliopita.
Watu watatu waliuawa katika eneo la Kyiv, huku mwingine akipoteza maisha katika mji wa Zaporizhzhia. Watu wengine 11 walijeruhiwa.
Mashambulizi hayo yalitokea baada ya Rais Zelensky kutangaza kuwa Ukraine itaendelea kushambulia miundombinu ya mafuta ya Urusi, kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi yanayoendelea kulenga mitambo ya umeme nchini Ukraine.
Soma Pia:





























