Netanyahu hafanyi vya kutosha kupata makubaliano ya mateka wa Gaza-Biden

Vifo vyao vimesababisha maandamano makubwa nchini Israel kutoka kwa wale wanaokosoa jinsiNetanyahu anavyoshughulikia vita na mzozo wa mateka.

Muhtasari

  • Uingereza kusitisha mauzo ya baadhi ya silaha kwa Israel, waziri wa mambo ya nje atangaza
  • Kenya: KUPPET yasitisha mgomo wa walimu baada ya kukutana na TSC
  • Makubaliano ya kurudisha mateka walioko Gaza yako karibu, asema Biden
  • Ufaransa: Mwanamume ashtumiwa kwa kuajiri watu asiowajua kumbaka mkewe
  • Makombora ya Urusi yalenga Kyiv siku ya kwanza ya mwaka wa shule
  • Kukata tamaa kuligeuka kuwa hasira - mambo Israeli yanatokota
  • Mahakama ya Israel yaamuru kusitishwa kwa mgomo huku maandamano zaidi yakipangwa
  • Mpinzani kwa rais wa Tunisia akamatwa, yasema timu yake ya kampeni
  • Mshukiwa wa mauaji Kevin Kang'ethe arejeshwa Marekani kujibu mashtaka
  • Mfanyikazi wa zamani wa huduma ya watoto akutwa na hatia ya kuwadhulumu makumi ya wasichana
  • Nyangumi anayeshukiwa kuwa 'jasusi wa Urusi' apatikana amekufa karibu na Norway
  • Chanjo ya kwanza ya Mpox kupelekwa DRC
  • Mtunza wanyama ashambuliwa na chuimilia katika bustani Australia
  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yatahadharisha kuwepo kwa upepo mkali
  • 'Huu ni msimu wangu wa mwisho Liverpool' - Mo Salah
  • Maelfu ya waandamana Israel kushinikiza makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka
  • Takribani watu 41 wajeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Urusi mjini Kharkiv

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Kwaheri

    Na kufikia hapo tunafikisha tamati taarifa zetu za moja kwa moja hii leo.Tukutane tena kesho alfajiri panapo majaaliwa.Shukran

  2. Uingereza kusitisha mauzo ya baadhi ya silaha kwa Israel, waziri wa mambo ya nje atangaza

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Uingereza itasitisha baadhi ya mauzo ya silaha kwa Israel, waziri wa mambo ya nje David Lammy ametangaza.

    Bw Lammy alisema uamuzi huo unafuatia mapitio ya leseni za mauzo ya silaha za Uingereza, ambayo iligundua kuwa kuna "hatari ya wazi" kwamba zinaweza kutumiwa kufanya "ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu".

    Takriban leseni 30 kati ya 350 zitasitishwa, Bw Lammy alisema, akisisitiza kwamba "hili sio marufuku ya kawaida, hii sio vikwazo vya silaha".

    Alisema: "Ikikabiliwa na mzozo kama huu, ni wajibu wa kisheria wa serikali hii kupitia upya leseni za mauzo ya nje ya Uingereza.

    "Ni kwa masikitiko kwamba nalijulisha Bunge leo tathmini niliyoipata inaniacha siwezi kuhitimisha kitu kingine chochote isipokuwa kwamba kwa uuzaji wa silaha za Uingereza kwa Israeli, kuna hatari ya wazi kwamba zinaweza kutumika kufanya au kuwezesha kosa kubwa- ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu."

    Serikali imekuwa chini ya shinikizo kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Israeli wakati wa vita huko Gaza.

    Uingereza haitoi silaha kwa Israel moja kwa moja, lakini inatoa leseni za kuuza nje kwa makampuni ya Uingereza kuuza silaha kwa nchi hiyo.

    Bw Lammy aliiambia bunge kwamba baada ya kuibua wasiwasi wake mwenyewe akiwa upinzani, mara moja alizindua mapitio baada ya kuchukua madaraka na "kujitolea kushiriki hitimisho la ukaguzi".

    “Tumefuatilia kwa makini kila hatua ya mchakato ambao Serikali iliyopita ya Conservative ilianzisha, na niweke wazi kwanza kuhusu upeo wa mapitio hayo, Serikali hii si mahakama ya kimataifa.

  3. Kenya: KUPPET yasitisha mgomo wa walimu baada ya kukutana na TSC

    CHAMA cha Walimu wa Elimu ya Baada ya Shule ya Msingi (KUPPET) kimesitisha mgomo wa walimu ulioanza wiki jana baada ya maafisa kukutana na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) mnamo Jumatatu.

    Katibu Mkuu wa KUPPET Akelo Misori na Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia waliambia mkutano wa pamoja wa wanahabari kwamba mgomo huo ulisitishwa kusubiri masuala ambayo yatashughulikiwa na TSC.

    "Makubaliano ya pamoja yamelipwa, bima ya matibabu imerejeshwa na kuhusu masuala ya kupandishwa vyeo kwa walimu, TSC inatafuta pesa za kuwapandisha vyeo walimu wengi iwezekanavyo na inajadili kuhusu kuidhinishwa kwa walimu katika nafasi za kukaimu," Misori alisema.

    Hapo awali mgomo huo uliitishwa ili kushinikiza kutekelezwakwa makubaliano ya mazungumzo ya pamoja ya 2021-2025 (CBA).

    Huku serikali ikichukua hatua ya kutekeleza awamu ya pili ya CBA, KUPPET inashikilia kuwa nyongeza ya mishahara haitoshi kukidhi mahitaji ya walimu.

  4. Makubaliano ya kurudisha mateka walioko Gaza yako karibu, asema Biden

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekanini, Joe Biden anasemaMarekani iko karibu sana kufanikisha pendekezo jipya la kurudishwa mateka kati ya Israel na Hamas, huku kukiwa na ripoti kwamba litakuwa pendekezo la mwisho.

    Rais wa Marekani na Kamala Harris, makamu wake wa rais, wamekutana na wapatanishi katika Ikulu ya Marekani, katika juhudi za hivi pundi za kupata usitishaji vita huko Gaza na kurejea kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

    Katika hotuba yake katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu, Biden alimkosoa Benjamin Netanyahu, akisema haamini kuwa kiongozi huyo wa Israel anafanya vya kutosha ili kupata mapatano.

    Haya yanakuja baada ya Israel kupata miili sita ya mateka huko Gaza siku ya Jumamosi.

    Vifo vyao vimesababisha maandamano makubwa nchini Israel kutoka kwa wale wanaokosoa jinsiNetanyahu anavyoshughulikia vita na mzozo wa mateka.

  5. Ufaransa: Mwanamume ashtumiwa kwa kuajiri watu asiowajua kumbaka mkewe

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Taarifa hii ina maelezo ya kusikitisha.

    Mwanamume mmoja amefikishwa mahakamani nchini Ufaransa kwa kumpa mke wake dawa za kumlevya na kumbaka mara kwa mara na pia kupanga wanaume wengine kadhaa kumbaka.

    Mshtakiwa huyo, aliyetajwa kwa jina la Dominique P, mwenye umri wa miaka 71, anashtakiwa kwa kusajili watu asiowajua mtandaoni kuja nyumbani kwake na kumnyanyasa kingono mwathiriwa kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Mwanamke huyo alikuwa ametulia sana hata hakujua kuhusu unyanyasaji huo uliorudiwa, mawakili wake wanasema.

    Kesi hiyo imeitia hofu Ufaransa kwa ukubwa wa uhalifu huo wa kutisha .

    Polisi waligundua ubakaji 92 uliofanywa na wanaume 72. Hamsini walitambuliwa na kushtakiwa na wapo mahakamani pamoja na mume wa mwathiriwa.

    Mwathiriwa, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 72, alifahamu kuhusu unyanyasaji huo mwaka wa 2020 baada ya kufahamishwa na polisi.

    Kesi hiyo itakuwa "jambo la kutisha" kwake, alisema wakili wake Antoine Camus, kwani itakuwa mara ya kwanza kuona ushahidi wa video wa unyanyasaji huo.

    "Kwa mara ya kwanza, atalazimika kuishi kupitia ubakaji ambao alivumilia zaidi ya miaka 10," aliambia shirika la habari la AFP.

    Dominique P alichunguzwa na polisi baada ya tukio la Septemba 2020, wakati mlinzi alipomkamata akipiga picha kwa siri chini ya sketi za wanawake watatu katika kituo cha maduka.

    Polisi kisha walipata mamia ya picha na video za mke wake kwenye kompyuta yake ambapo alionekana kupoteza fahamu.

    Picha hizo zinadaiwa kuonyesha makumi ya mashambulizi katika nyumba ya wanandoa hao. Unyanyasaji huo unadaiwa kuanza mnamo 2011.

  6. Makombora ya Urusi yalenga Kyiv siku ya kwanza ya mwaka wa shule

    TH

    Chanzo cha picha, Reuters

    Urusi imerusha msururu wa makombora katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, saa chache kabla ya maelfu ya watoto kurejea shuleni kwa siku ya kwanza ya mwaka wa masomo.

    Meya, Vitali Klitschko, anasema kiwanda cha kutibu maji na mlango wa kituo cha metro kinachotumika kama makazi vilipigwa. Shule mbili na chuo kikuu pia ziliharibiwa.

    Kulingana na jeshi la Ukraine, makombora 22 ya baharini na ya anga yaliharibiwa na jeshi la anga.

    Mamlaka ya eneo hilo inasema watu watatu walijeruhiwa na vifusi kutoka kwa makombora yaliyoharibiwa.

    Kwa watoto wa shule katika mji mkuu, shambulio hilo la Jumatatu liliambatana na siku ya kwanza ya mwaka wa shule, siku ya sherehe nchini Ukraine.

    Walimu na wazazi walijaribu kuweka hali ya kawaida, huku muziki ukicheza huku wanafunzi wakitabasamu walikaribishwa na bahari ya maua.

    Mzazi mmoja, ambaye alijificha na bintiye nyumbani wakati wa shambulio la kombora kabla ya kumpeleka shuleni, alisema walikuwa wakionyesha kwa mara nyingine "kwamba taifa hili haliwezi kushindwa".

    "Watoto wanatabasamu, lakini unaweza kuona mkazo katika nyuso za walimu wao [ambao] wanabeba mzigo huu", aliiambia BBC.

    "Ninawashukuru sana kwa yote waliyofanya kuifanya kuwa likizo ya kweli kwa watoto."

    Kwa Yevheniia mwenye umri wa miaka 33, ambaye alikuwa akimpeleka shuleni bintiye mwenye umri wa miaka sita kwa mara ya kwanza, siku hiyo ilitawaliwa na hofu.

  7. Kukata tamaa kuligeuka kuwa hasira - mambo Israeli yanatokota

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Israeli inachemka.

    Mitaa ya Tel Aviv ilijaa waandamanaji tena asubuhi ya leo, wakifunga barabara kuu ya nchi hiyo, wakiiomba serikali kufanya zaidi kuwarudisha mateka wa Israel waliosalia.

    Jana usiku, katika mitaa hiyo hiyo, kukata tamaa kuligeuka kuwa hasira na vurugu.

    Habari za kushtua za Jumamosi kwamba miili sita ya mateka, ambao hapo awali walidhaniwa kuwa hai, ilipatikana kwenye handaki huko Rafah, zilichochea hasira kwa kushindwa kwa serikali kufikia makubaliano. Mpango ambao ungeweza kuwaokoa.

    Hatima ya mateka inasambaratisha nchi.

    Wengi hapa wanamshutumu waziri mkuu, Benjamin Netanyahu, kwa kurudia kuweka vikwazo katika makubaliano.

    Leo, kwa mara ya kwanza tangu vita kuanza, mgomo wa kitaifa umefanyika

    Uwanja mkuu wa ndege nchini humo ulikumbwa na machafuko kwa muda, huku safari za ndege zikichelewa au kuahirishwa na mizigo kutopakiwa. Mahakama iliamuru mgomo huo kumalizika muda mfupi uliopita.

  8. Israel: Wafanyikazi waliamrishwa kurudi kazini

    Wafanyikazi nchini Israel wameamrishwa kurejea kazini, anasema Arnon Bar-David, mkuu wa Histadrut, chama ambacho kiliandaa mgomo wa Jumatatu.

    Mapema leo mahakama ya leba ya Israel hapo awali iliamuru kwamba mgomo huo lazima umalizike saa 14:30 saa za ndani (12:30 BST) - mapema kabla ya kukamilika kwake.

  9. Mpinzani kwa rais wa Tunisia akamatwa, yasema timu yake ya kampeni

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Polisi nchini Tunisia wamemkamata mmoja wa wapinzani wawili walioidhinishwa kuchuana na Rais aliye madarakani Kais Saied katika uchaguzi wa mwezi ujao, timu ya kampeni ya mgombea huyo imesema.

    Ayachi Zammel alishikiliwa mapema Jumatatu kwa madai ya kughushi maelezo ya wanaomuunga mkono, Mahdi Abdel Jawad aliliambia shirika la habari la Reuters.

    Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini New York la Human Rights Watch, lilisema mwezi Agosti kwamba mamlaka imewaweka kando wagombea wanane watarajiwa katika uchaguzi wa Oktoba 6, kupitia mashtaka na vifungo.

    Wiki iliyopita, mahakama ya juu zaidi ya Tunisia ilisema wagombea watatu ambao walikuwa wamezuiwa kuwania na tume ya uchaguzi wanapaswa kurejeshwa.

    Kukamatwa kwa Zammel kunakuja huku Rais Saied aliye madarakani tangu 2019, ambaye amelisimamisha bunge na kumfuta kazi waziri mkuu, anakabiliwa na shutuma za kujaribu kupunguza idadi ya wanaoruhusiwa kugombea dhidi yake.

  10. Mshukiwa wa mauaji Kevin Kang'ethe arejeshwa Marekani kujibu mashtaka

    TH

    Chanzo cha picha, DCI Kenya

    Mshukiwa wa mauaji Kevin Kang'ethe amesafirishwa kutoka Kenya hadi Marekani kujibu mashtaka ya kumuua mpenzi wake Margaret Mbitu.

    Kupitia idhini ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga, Kang'ethe alifaulu kurejeshwa Jumapili na atakabiliwa na kesi mjini Boston Jumanne, Septemba 3.

    Katika taarifa yake kwa vyomba vya habari, DPP Ingonga alithibitisha dhamira yake ya kuunga mkono Marekani, hasa timu ya waendesha mashtaka wanapoendelea na awamu inayofuata ya kesi hiyo.

    Hapo awali Ingonga alikuwa amemhakikishia Mkurugenzi wa FBI Christopher Wray mnamo Juni 2024 kwamba ofisi yake ina nia ya kuhakikisha haki inatendeka.

    Kang'ethe anasakwa nchini Marekani kwa mauaji ya Mbitu, mwenye umri wa miaka 31 ambaye mwili wake uligunduliwa ndani ya gari katika uwanja wa ndege wa Boston Logan mnamo Novemba 2023. Mwathiriwa aliripotiwa kuwa mpenzi wake.

    Kisha mshukiwa alikimbilia Kenya na kujificha hadi alipokamatwa na mamlaka ya Kenya.

    Baada ya kukamatwa mwezi Januari na kupewa agizo la kuzuiliwa kwa siku 30 ili kuruhusu mamlaka kufanya uchunguzi zaidi, Kang'ethe alitoroka kwa njia ya kutatanishakutoka kwa Kituo cha Polisi cha Muthaiga.

  11. Mfanyikazi wa zamani wa huduma ya watoto akutwa na hatia ya kuwadhulumu makumi ya wasichana

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mfanyikazi wa zamani wa huduma ya kulea watoto nchini Australia amekiri kosa la kubaka na kuwadhulumu kingono makumi ya wasichana wadogo chini ya uangalizi wake kwa zaidi ya miaka 20.

    Ashley Paul Griffith, 46, alikiri kutenda makosa 307 katika vituo vya kulea watoto huko Brisbane na Italia kati ya 2003 na 2022, mahakama ya Queensland ilisikiza Jumatatu.

    Wengi wa waathiriwa wa Griffith walikuwa chini ya umri wa miaka 12, mahakama iliambiwa. Mshirika wa hakimu alichukua muda wa saa mbili kusoma mashtaka yote dhidi yake.

    Hapo awali polisi wamemuelezea Griffith kama mmoja wa washukiwa sugu wa kuwadhulumu watoto nchini Australia.

  12. Nyangumi anayeshukiwa kuwa 'jasusi wa Urusi' apatikana amekufa karibu na Norway

    th

    Chanzo cha picha, Helene O'Barry

    Nyangumi aina ya ‘beluga’ anayeshukiwa kupewa mafunzo ya kijasusi na Urusi amepatikana amefariki katika pwani ya Norway.

    Mwili wa mnyama huyo - kwa jina la utani Hvaldimir - ulipatikana ukielea karibu na mji wa kusini-magharibi wa Risavika na kupelekwa kwenye bandari ya karibu kwa uchunguzi.

    Nyangumi huyo alionekana kwa mara ya kwanza katika maji ya Norway miaka mitano iliyopita, akiwa na kamera ya GoPro iliyofungwa katika hatamu yenye maneno "Vifaa vya St Petersburg."

    Mwili wa Hvaldimir uligunduliwa mwisho wa wiki na Marine Mind, shirika ambalo limefuatilia mienendo yake kwa miaka mingi.

    Mwanzilishi wa Marine Mind, Sebastian Strand ameliambia shirika la habari la AFP, chanzo cha kifo hakijajulikana na mwili wa Hvaldimir haukuwa na majeraha yoyote.

    Anakisiwa kuwa na umri wa miaka 15, Hvaldimir hakuwa mzee kwa nyangumi aina ya Beluga, ambao maisha yao yanaweza kufikia miaka 60.

    Alikaribia boti za Norway kwa mara ya kwanza Aprili 2019 karibu na kisiwa cha Ingoya, karibu kilomita 415 (maili 260) kutoka Murmansk ambapo Meli ya Kaskazini ya Urusi iko.

    Kuonekana kwake kulisababisha uchunguzi wa shirika la ujasusi la ndani la Norway, ambalo baadaye lilisema kuna uwezekano nyangumi huyo amefunzwa na jeshi la Urusi kwani alionekana kuwazoea wanadamu.

    Urusi ina historia ya kutoa mafunzo kwa mamalia wa baharini kama vile pomboo kwa madhumuni ya kijeshi. Lakini haijawahi kujibu rasmi madai kwamba Hvaldimir huenda alifunzwa na jeshi lake.

  13. Chanjo ya kwanza ya Mpox kupelekwa DRC

    Dawa yapakwa kwenye uso wa mtoto mwenye mpox

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kituo Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa CDC kanda ya Afrika kimeithibitishia BBC kwamba chanjo ya kwanza ya Mpox itawasilishwa DRC wiki hii.

    Madaktari wanatarajiwa kuanza kutoa chanjo nchini humo,kitovu cha mlipuko huo ifikapo Ijumaa.

    Shule nchini DRC zinatarajiwa kufunguliwa leo baada ya likizo, huku wazazi wengi wakitarajiwa kuwaacha watoto wao nyumbani huku kukiwa na wasiwasi wa idadi kubwa ya watoto walioathirika.

    DRC inasema karibu wagonjwa 18,000 wa Mpox wamerekodiwa nchini humo, na vifo zaidi ya 600.

    Wakati huohuo Kenya imeimarisha taratibu kwa wasafiri wanaoingia baada ya kurekodi mgonjwa wa nne wa Mpox.

    Nchi hiyo itakusanya taarifa za mawasiliano kwa wote wanaowasili kutoka ng'ambo ili kusaidia kufuatilia mawasiliano iwapo kutatokea mlipuko.

    Unaweza kusoma;

  14. Mtunza wanyama ashambuliwa na chuimilia katika bustani Australia

    Chuimilia

    Chanzo cha picha, Dreamworld

    Mtunza chui aliyefunzwa amelazwa hospitalini akiwa na majeraha kwenye mkono wake baada ya kushambuliwa na mmoja wa wanyama hao katika bustani ya mandhari ya Australia.

    Huduma ya Ambulensi ya Queensland (QAS) inasema mwanamke huyo, ambaye ana umri wa miaka 40, yuko katika hali nzuri baada ya kupata majeraha na mikwaruzo alipokuwa akifanya kazi Dreamworld huko Queensland Gold Coast.

    "Hili lilikuwa tukio la pekee na la nadra, na tutafanya uchunguzi wa kina ipasavyo," kampuni hiyo ilisema katika taarifa.

    Mbuga hiyo maarufu ya mandhari, ambayo hutembelewa na karibu watu milioni mbili kila mwaka ni sehemu ya makazi ya chui tisa wa Sumatran na Bengal.

    QAS ilisema matabibu waliitwa kwenye eneo la tukio saa 09:01 kwa saa za ndani siku ya Jumatatu (23:01 GMT siku ya Jumapili) "kufuatia tukio hilo" na kwamba mwanamke huyo alipelekwa mara moja katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Gold Coast.

    "Yeye ni mmoja wa wahudumu wenye uzoefu na waandamizi huko Dreamworld... ni vyema kuona kwamba aliweza kuangaliwa na wafanyakazi wengine wa usaidizi huko," aliongeza.

  15. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yatahadharisha kuwepo kwa upepo mkali

    upepo

    Chanzo cha picha, EPA

    Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetahadharisha kuwepo kwa upepo mkali wa zaidi unaozidi kilomita 40 kwa saa.

    TMA imesema upepo huo unatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya kusini mwa bahari ya hindi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

    Maeneo mengine ya ukanda wa Pwani ya kaskazini mwa bahari ya hindi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

    Athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuahirishwa kwa baadhi ya shughuli za baharini na kuharibika kwa miundombinu ya bahari.

  16. 'Huu ni msimu wangu wa mwisho Liverpool' - Mo Salah

    Salah

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohamed Salah anasema ni "mwaka wake wa mwisho" ndani ya Liverpool na kwamba hakuna mtu katika klabu hiyo ambaye amezungumza naye kuhusu mkataba mpya.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye mkataba wake wa sasa huko Anfield unatarajiwa kuisha msimu ujao, alifunga bao katika ushindi wa 3-0 wa The Reds dhidi ya Manchester United Jumapili.

    Salah alisema baadaye alichukulia mechi hiyo kana kwamba ilikuwa ya mwisho kwake Old Trafford.

    "Nilikuwa naingia kwenye mchezo, nilikuwa nikisema, 'angalia, inaweza kuwa mara ya mwisho'," aliiambia Sky Sports.

    "Hakuna mtu katika klabu ambaye alizungumza nami kuhusu mikataba kwa hivyo nilikuwa kama, 'Sawa, ninacheza msimu wangu wa mwisho na kuona kitakachofanyika mwisho'.

    "Ninahisi niko huru kucheza soka, tutaona kitakachotokea mwaka ujao." Alipoulizwa kuhusu maoni ya Salah, meneja Arne Slot alisema: "Tuna ‘pengine’ nyingi. Kwa sasa yeye ni mmoja wetu na ninafurahi sana yeye kuwa mmoja wetu na alicheza vizuri sana.

    "Sizungumzii kuhusu mikataba kutoka kwa wachezaji lakini ninaweza kuzungumza kwa saa nyingi jinsi Mo alivyocheza leo."

    Mwezi Julai 2022, Salah alisaini mkataba mpya wa miaka mitatu, na kumfanya kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya klabu hiyo, akilipwa zaidi ya £350,000 kwa wiki.

  17. Maelfu ya waandamana Israel kushinikiza makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka

    Raia na polisi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelfu ya watu wamekusanyika kote Israel baada ya miili sita ya mateka wa Hamas katika Ukanda wa Gaza kupatikana na wanajeshi, na kusababisha ghadhabu ya kitaifa.

    Waandamanaji, wengi wakiwa wamevalia bendera za Israel walishuka Tel Aviv, Jerusalem na miji mingine, wakimtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na serikali yake kwa kutofanya vya kutosha kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka waliosalia waliochukuliwa na Hamas wakati wa shambulio la Oktoba 7.

    Maandamano ya Jumapili kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani, lakini umati wa watu ulivunja vizuizi vya polisi, na kuziba barabara kuu ya Tel Aviv.

    Haya yanajiri huku chama kikuu cha wafanyikazi nchini Israel, Histadrut, kilipoitisha mgomo mkuu wa nchi nzima siku ya Jumatatu, kushinikiza makubaliano kuhusu waliotekwa nyara.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema awali kwamba miili hiyo sita ilipatikana siku ya Jumamosi kwenye handaki la chini ya ardhi katika eneo la Rafah kusini mwa Gaza.

    Mateka hao walitambuliwa kuwa ni Carmel Gat, Eden Yerushalmi, Hersh Goldberg-Polin, Alexander Lobanov, Almog Sarusi na Mwalimu Sgt Ori Danino.

    IDF ilisema walikuwa wameuawa muda mfupi kabla ya wanajeshi wake kuwafikia siku ya Jumamosi.

    Hii ilizua maandamano ya Jumapili, huku umati wa watu wakishutumu serikali na Bw Netanyahu binafsi kwa kushindwa kuwaokoa mateka waliosalia.

    Unaweza kusoma;

  18. Takribani watu 41 wajeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Urusi mjini Kharkiv

    Athari za mashambulizi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takribani watu 41 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Urusi katika mji wa Kharkiv nchini Ukraine, maafisa wamesema.

    Mkuu wa mkoa Oleh Syniehubov alisema watoto watano walikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa na aliishutumu Moscow kwa "kulenga miundombinu ya kiraia pekee" katika jiji hilo.

    Miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa ni duka kubwa na uwanja wa michezo katika maeneo ambayo wakazi huenda kila siku, aliongeza.

    "Urusi kwa mara nyingine inaitisha Kharkiv, ikigonga miundombinu ya raia na jiji lenyewe," Rais Volodymyr Zelensky alisema kufuatia mashambulizi hayo.katika mji wa Kharkiv nchini Ukraine, maafisa wamesema.

    Bw Zelensky alirudia wito wake kwa washirika wa Magharibi "kuipa Ukraine kila kitu inachohitaji kujilinda".

    BwSyniehubov alisema takribani mashambulizi 10 tofauti ya Urusi yamerekodiwa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya makombora ya masafa marefu.

    Watu wanaweza kufunikwa na vifusi katika baadhi ya maeneo na shughuli za uokoaji zinaendelea, aliongeza.

    Kutoka kwenye video kadhaa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii za mashambulizi hayo, BBC Verify imepata shambulio moja kaskazini mashariki mwa kituo cha Kharkiv, kando ya Akademika Pavlova St, na maili nyingine tatu kusini ambazo zliharibu majengo ya Jumba la Michezo la jiji.

    Picha kutoka kwa kila shambulio ni pamoja na wakati wa athari na mlipuko kutokana na makombora.

    Shambulio hilo limetokea baada ya Ukraine kuanzisha wimbi la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani usiku kucha dhidi ya maeneo yaliyolengwa nchini Urusi, ambapo moto ulizuka katika vituo viwili vya nishati.

    Hakuna majeruhi au vifo vimeripotiwa na maafisa wa Urusi.

    Kulingana na wizara ya ulinzi ya Urusi, zaidi ya ndege 158 zisizo na rubani za Ukraine zililenga maeneo 15 ya nchi hiyo, ukiwemo mji mkuu wa Moscow.

    Jeshi la Urusi limesema ndege hizo zisizo na rubani zilinaswa na kuharibiwa.

    Unaweza kusoma;

  19. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu