Iran: Lango la Hormuz halitafunguliwa hadi Marekani itakapoondoka
Msemaji wa jeshi la Iran, Mohammad Akraminia, amesema kufunguliwa tena kwa Mlango-bahari wa Hormuz kunategemea kuondoka kwa vikosi vya Marekani katika eneo hilo.
Muhtasari
- Papa aonekana kwa mara ya kwanza tangu upasuaji
- Wagonjwa waliofungwa minyororo waokolewa Afrika Kusini
- Kenya yathibitisha mgonjwa wa tatu wa Ebola
- Iran: Hormuz haitafunguliwa kabla ya Marekani kuondoka
- China yaitaka Israel kusitisha 'upanuzi' wa makazi Ukingo wa Magharibi
- Urusi yaimarisha juhudi za kidiplomasia kuhusu mgogoro wa Iran
- Mlipuko wa Ebola wa DRC waenea hadi jimbo jipya linalopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati
- Wafanyakazi saba hawajulikani walipo baada ya shambulio la droni pwani ya Romania
- Martinez aomba radhi, Man United yampiga faini
- Polisi wa Ubelgiji wapekua nyumba za ndugu wa Rais Tshisekedi wa DRC
- Infantino aomba radhi, lakini uongozi wake FIFA watiliwa shaka
- Tazama: Ndege isiyo na rubani ya Urusi ikigonga duka kubwa mjini Odesa Ukraine
- Mwanamume alizuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Ujerumani akiwa na sanduku iliyojaa nyoka
- Afisa wa Saudi Arabia atoa shutuma kali dhidi ya Iran kuhusu Wahouthi
- Trump asema hatatumia silaha za nyuklia dhidi ya Iran
- Mvulana awauwa kwa risasi watoto watatu na mwalimu katika shule ya msingi Marekani
Moja kwa moja
Na Faidha Ngaga, Dinah Gahamanyi & Ambia Hirsi
Papa aonekana kwa mara ya kwanza tangu afanyiwe upasuaji wa mapafu

Chanzo cha picha, Reuters
Papa Leo XIV ameonekana kwa mara ya kwanza hadharani tangu afanyiwe upasuaji wa mapafu, baada ya Vatican kutoa picha zikimuonyesha akiongoza Misa akiwa hospitalini.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 aligundulika kuwa na saratani ya mapafu kufuatia upasuaji aliofanyiwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma Jumanne. Vatican ilieleza kuwa upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio bila matatizo yoyote.
Picha zilizotolewa Ijumaa zilimuonyesha Papa huyo mzaliwa wa Chicago akiwa amevaa joho la kijani na akiongoza ibada mbele ya madhabahu ya muda katika wodi ya hospitali.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican, Papa Leo alishiriki Misa pamoja na madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa hospitali, huku akiwashukuru kwa huduma na uangalizi wanaoendelea kumpatia.
Siku ya Ijumaa, madaktari wa Papa walisema vipimo vya afya vilionyesha maendeleo mazuri na ya kutia moyo tangu afanyiwe upasuaji wa mapafu.
Kwa mujibu wa madaktari hao, picha za eksirei ya kifua zimeonyesha kuwa pafu lililofanyiwa upasuaji linaendelea kupona vizuri.
Vatican ilieleza kuwa sehemu ya chini ya pafu la kulia la Papa iliondolewa ili kuhakikisha ugonjwa huo unaondolewa kikamilifu na kuongeza uwezekano wa kupona kwa mafanikio.
Soma zaidi:
Wagonjwa waliofungwa minyororo waokolewa Afrika Kusini

Chanzo cha picha, Idara ya Maendeleo ya Jamii
Mchungaji na mkewe wamekamatwa nchini Afrika Kusini baada ya watu zaidi ya 200 kupatikana wakizuiliwa katika kituo cha urekebishaji tabia kinachoshukiwa kuendesha shughuli zake kinyume cha sheria katika jimbo la Mpumalanga. Baadhi ya watu hao walikuwa wamefungwa minyororo, huku wengine wakionekana kuwa na majeraha mwilini.
Kituo hicho, kilichokuwa kinaendeshwa ndani ya kanisa, kilibainika wakati wa operesheni ya maafisa wa usalama iliyofanyika siku ya Alhamisi. Mamlaka zilisema zilishuhudia hali duni na zisizo za kibinadamu, huku baadhi ya waliokuwa wakihifadhiwa hapo wakikuta wamefungwa minyororo na wengine wakiwa na vidonda mwilini.
Wanandoa hao wamefunguliwa mashtaka ya utekaji nyara, huku polisi wakisema huenda mashtaka mengine yakaongezwa kadiri uchunguzi unavyoendelea. Kufikia sasa, hawajatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo.
Miongoni mwa waliookolewa ni msichana aliye na umri wa miaka 16 na mvulana wa miaka 11, ambao walikuwa wamewekwa katika chumba kimoja pamoja na watu wazima.
Mamlaka zinasema vituo haramu vya urekebishaji tabia vimeongezeka nchini humo katika miaka ya hivi karibuni, sambamba na kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kulevya.
Mwaka jana, Idara ya Maendeleo ya Jamii ilitangaza kuwa iligundua zaidi ya vituo 100 vya aina hiyo vikifanya kazi bila kibali katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Chanzo cha picha, Idara ya Polisi Afrika Kusini
Kenya yathibitisha mgonjwa wa tatu wa Ebola

Kenya imethibitisha kisa cha tatu cha ugonjwa wa Ebola baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 65, ambaye alikuwa amewekwa karantini kutokana na kukaribiana na wagonjwa wawili wa kwanza, kubainika kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mwanamke huyo, ambaye ni ndugu wa karibu wa wagonjwa hao wawili, alipata homa, maumivu ya koo na udhaifu wa mwili akiwa bado chini ya uangalizi wa afya. Baada ya kutengwa kwa ajili ya matibabu, alifanyiwa vipimo vilivyothibitisha kuwa ameambukizwa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Sampuli zake zilithibitishwa na Maabara ya Kitaifa ya Marejeo ya Virusi pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya (KEMRI).
Wizara ilisema mgonjwa huyo amehamishiwa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza (IDU), ambako anaendelea kupatiwa matibabu na uangalizi maalumu.
Mamlaka za afya zilisema maambukizi hayo yaligunduliwa mapema kwa kuwa alikuwa tayari akifuatiliwa kama mmoja wa watu waliokaribiana na wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa. Hali hiyo imewezesha kuanza matibabu kwa haraka na kupunguza hatari ya ugonjwa huo kusambaa kwa wengine.
Wizara pia ilieleza kuwa mgonjwa wa pili anaendelea vizuri na anaonyesha mwitikio mzuri kwa matibabu.
Hadi sasa, watu 130 waliokaribiana na wagonjwa wa Ebola wametambuliwa, huku 127 kati yao wakipatikana na kuwekwa karantini. Juhudi zinaendelea kuwatafuta watu watatu waliosalia.
Mamlaka zimeonya kuwa visa vingine vinaweza kujitokeza miongoni mwa watu walio katika karantini kabla ya kipindi cha ufuatiliaji kumalizika, lakini vimesisitiza kuwa vitabainika na kushughulikiwa kwa haraka.
Wakati huohuo, Kenya imeimarisha uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaowasili kutoka nchi 10 zinazotajwa kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya Ebola. Nchi hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Angola, Zambia, Ethiopia, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wasafiri kutoka nchi hizo watalazimika kujaza fomu ya kidijitali ya ufuatiliaji wa afya kabla ya kupanda ndege na kuwasilisha msimbo wa QR kwa maafisa wa afya wanapowasili nchini. Aidha, ndege zote zinazotoka katika nchi hizo zitafanyiwa uchunguzi wa ziada wa afya katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Kenya ili kuzuia kuingia na kuenea kwa ugonjwa huo nchini.
Ebola ni nini?
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi.
Virusi vya Ebola kwa kawaida huambukiza wanyama, hasa popo wa matunda, lakini milipuko kwa binadamu wakati mwingine huanza pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa.
Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu
Maelezo zaidi
Raia wawili wa Bangladesh wanyongwa Saudi kwa 'vitendo vya aibu' msikitini

Chanzo cha picha, Getty Images
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema kuwa raia wawili wa Bangladesh, mwanamume na mwanamke, wamehukumiwa kifo na kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya kile kilichoelezwa kama "vitendo vya aibu" ndani ya msikiti katika mji mtakatifu wa Makka.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), likinukuu taarifa ya Wizara hiyo, mwanamume huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nazrul Islam Abdul Basir na mwanamke Siti Akhtar walikabiliwa na mashtaka ya kufanya vitendo hivyo ndani ya moja ya misikiti ya Makka.
Baada ya tukio hilo, maafisa wa usalama waliwakamata wawili hao na kuwafikisha mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yao.
Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema mahakama iliwapata na hatia na kuwahukumu adhabu ya kifo, ikizingatia uzito wa kosa hilo, mazingira ya tukio, pamoja na kile ilichokitaja kuwa ukiukwaji wa utakatifu na heshima ya msikiti.
Kwa mujibu wa maafisa wa Saudi Arabia, hukumu hiyo ilikatiwa rufaa, lakini Mahakama ya Juu ilitupilia mbali ombi hilo na kuidhinisha uamuzi wa mahakama ya awali.
Baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria, amri ya kifalme ilitolewa kuruhusu utekelezaji wa hukumu, ambao ulitekelezwa Jumatano, Oktoba 14.
Pia unaweza kusoma:
Iran: Hormuz haitafunguliwa kabla ya Marekani kuondoka

Chanzo cha picha, Reuters
Msemaji wa jeshi la Iran, Mohammad Akraminia, amesema kufunguliwa tena kwa Mlango-bahari wa Hormuz kunategemea kuondoka kwa vikosi vya Marekani katika eneo hilo, akionya kuwa endapo vitaendelea kuwepo, Iran itaviondoa kwa nguvu.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Akraminia alisema kuondoka kwa Marekani kungefungua njia ya kuimarishwa kwa usalama wa kikanda na kurejesha utulivu katika usafiri wa baharini pamoja na biashara ya kimataifa.
"Ikiwa Marekani itaondoka katika eneo hili, Mlango-bahari wa Hormuz utafunguliwa, usalama wa pamoja utaimarishwa kwa ushiriki wa mataifa ya eneo hili, na uchumi wa dunia utafaidika. Ikiwa haitaondoka, tutaifukuza," alisema.
Akraminia pia aliishutumu Marekani kwa kuchangia hali ya ukosefu wa usalama katika eneo la mashariki mwa Hormuz na kuwataka waendeshaji wa meli kutumia njia maalumu iliyotengwa na vikosi vya Iran, akidai kuwa ndiyo njia salama zaidi kwa sasa.
Kauli hizo zinatolewa wakati mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara ndani na karibu na Mlango-bahari wa Hormuz yakiongezeka, hali iliyosababisha kupungua kwa shughuli za usafirishaji katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara duniani.
Takwimu za kampuni ya ufuatiliaji wa meli ya Kepler zinaonyesha kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita meli tano pekee za mizigo zilipita katika njia hiyo siku ya Jumamosi, huku hakuna meli iliyorekodiwa kupita siku iliyofuata. Wiki moja kabla, meli 31 zilikuwa zimepita eneo hilo.
Wakati huo huo, Marekani inaendelea kuimarisha shinikizo dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran. Ripoti ya Reuters, ikinukuu kampuni ya takwimu za nishati ya Vortexa, ilisema usafirishaji wa mafuta ghafi ya Iran kwa njia ya bahari ulifikia sifuri mwezi Oktoba wakati taarifa hiyo ilipochapishwa.
Awali, viongozi wa Iran walieleza kuwa kufunguliwa tena kwa Mlango-bahari wa Hormuz kunategemea kutimizwa kwa masharti ya Tehran katika juhudi za kumaliza mvutano wake na Marekani.
Mlango-bahari wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa nishati, ukipitisha takribani asilimia 20 ya biashara ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa duniani, jambo linaloufanya kuwa kitovu muhimu cha biashara ya kimataifa.
Soma zaidi:
China yaitaka Israel kusitisha 'upanuzi' wa makazi Ukingo wa Magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, ameitaka Israel kusitisha kile alichokiita upanuzi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi na kubadili sera zake katika eneo hilo.
Akizungumza na Rais wa Israel, Isaac Herzog, pembezoni mwa mkutano uliofanyika Azerbaijan, Wang alisema suala la Palestina linaendelea kuwa moja ya migogoro mikubwa ambayo haijapatiwa suluhu ya haki.
China imeendelea kusisitiza kuwa suluhisho la mataifa mawili ndilo njia sahihi ya kumaliza mzozo wa Israel na Palestina, huku ikijaribu kujiimarisha kama mpatanishi katika migogoro ya Mashariki ya Kati.
Katika kauli yake ya hivi karibuni, Wang alisema kipaumbele cha sasa kinapaswa kuwa kufunguliwa kikamilifu kwa njia za kuingiza misaada ya kibinadamu Gaza na kuzuia kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika eneo hilo.
Beijing pia imekuwa ikijitahidi kuhimiza maridhiano ya kisiasa miongoni mwa Wapalestina na kuunga mkono juhudi za kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo.
Soma zaidi:
Urusi yaimarisha juhudi za kidiplomasia kuhusu mgogoro wa Iran

Chanzo cha picha, EPA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, anatarajiwa kuzuru Tehran Jumatatu ijayo kwa mazungumzo na mwenzake wa Iran, Abbas Araghchi, katika hatua inayoashiria kujitosa kwa Moscow katika jitihada za kutafuta suluhu ya mzozo wa Iran.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, mazungumzo hayo yataangazia hali ya sasa ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati na masuala mengine muhimu ya kikanda.
Ziara hiyo inafuatia ushiriki wa Lavrov katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) nchini Bahrain, kabla ya kuelekea Tehran kwa mazungumzo na viongozi wa Iran.
Hatua hiyo inakuja wakati Urusi ikijitokeza kama mmoja wa wadau muhimu katika juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano unaoihusisha Iran. Hivi karibuni, Kremlin ilisema Rais wa Marekani, Donald Trump, aliunga mkono ushiriki wa Moscow katika kutafuta njia za kumaliza mgogoro huo wakati wa mazungumzo yake ya simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Kwa mujibu wa Kremlin, katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Oktoba 9, Putin alimweleza Trump msimamo wa Iran kuhusu njia zinazowezekana za kutatua mgogoro huo, baada ya kuyajadili na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian.
Putin pia alisisitiza kuwa pendekezo la Urusi la kuhamishia nje urani ya Iran iliyoboreshwa kwa kiwango cha juu bado lipo mezani, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya suluhu ya kidiplomasia inayoweza kusaidia kupunguza mvutano uliopo.
Ziara ya Lavrov mjini Tehran inatazamwa kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za Urusi kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kikanda wakati juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro wa Iran zikiendelea.
Pia unaweza kusoma:
Mlipuko wa Ebola wa DRC waenea hadi jimbo jipya linalopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati

Chanzo cha picha, Reuters
Mlipuko unaoendelea wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeenea hadi jimbo jipya linalopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, maafisa wawili wa afya wamesema , na kusababisha changamoto mpya kwa mamlaka zinazojitahidi kuudhibiti.
Ubangi Kaskazini(North Ubangi) linakuwa mkoa wa nane kuathiriwa na mlipuko wa aina ya Bundibugyo ya Ebola, ambao ulitangazwa katikati ya Mei na umekuwa mlipuko wa pili kwa ukubwa wa Ebola kuwahi kurekodiwa, huku visa zaidi ya 9,000 na vifo zaidi ya 4,000 vikithibitishwa.
Maafisa walisema visa viwili vimethibitishwa huko North Ubangi. Havijatangazwa rasmi na mamlaka za Kongo.
Mkoa wa Ituri unabaki kuwa kitovu cha mlipuko ingawa visa vimeongezeka hivi karibuni katika mkoa wa Kivu Kaskazini .
Visa pia vimethibitishwa katika majimbo ya Kivu Kusini, Tshopo, Haut-Uele, Bas-Uele na Ubangi Kusini.
Afisa wa afya huko North Ubangi aliiambia Reuters siku ya Alhamisi kwamba kumekuwa na mfululizo wa vifo vinavyoshukiwa hivi karibuni katika eneo la migodi katika eneo la afya la Wapinda, karibu na mpaka na Bas-Uele, na kusababisha sampuli kuchunguzwa katika maabara ya mkoa na mjini Kinshasa.
Unaweza pia kusoma:
Wafanyakazi saba hawajulikani walipo baada ya shambulio la droni pwani ya Romania

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mamlaka za Romania zinasema kuwa operesheni ya kutafuta na kuokoa watu inaendelea katika bahari yenye mawimbi makali, ikihusisha boti na helikopta. Wafanyakazi saba kati ya 12 hawajulikani walipo baada ya shambulio la droni kusababisha meli ya kemikali kuwaka moto karibu na pwani ya Romania, Alhamisi asubuhi, kwa mujibu wa mamlaka za wanamaji.
Meli hiyo ya Wine Trader, iliyokuwa na bendera ya San Marino, ilikuwa kilomita 24 mashariki mwa mdomo wa Mto Danube, karibu na eneo la Sulina, iliporipoti milipuko na moto.
Rais wa Romania, Nicușor Dan, alithibitisha kuwa Wine Trader na meli nyingine ya kubeba kemikali katika eneo hilo, Yara J, zilikuwa zimeshambuliwa kwa droni. Shambulio dhidi ya Yara J lilitokea Jumatano.
Meli ya Wine Trader haikuwa na mzigo wowote wakati wa shambulio hilo.
Moscow ilisema meli mbili za mizigo zilizokuwa zikielekea bandari ya Odesa nchini Ukraine, zikiwa na mizigo ya kijeshi, zilishambuliwa. Hata hivyo, haikutaja majina ya meli hizo.
Usiku kucha, kundi kubwa la droni za Urusi liligunduliwa karibu na eneo la tukio, jirani na Kisiwa cha Snake cha Ukraine.
Pwani ya magharibi ya Bahari Nyeusi imekumbwa na mfululizo wa mashambulizi ya droni katika siku za hivi karibuni.
Jumanne, meli mbili za kibiashara zilishambuliwa kwa droni kusini zaidi, katika pwani ya Bulgaria, nchi jirani na Romania. Moja ya meli hizo ilizama, huku wafanyakazi 11 wakiripotiwa kutoweka.
Bulgaria ilisema inashuku Urusi kuhusika na shambulio hilo na kumwita mwakilishi wa kidiplomasia wa nchi hiyo kwa maelezo.
Mamlaka za Romania zimesema kuwa operesheni ya kutafuta na kuokoa wafanyakazi waliopotea wa meli ya Wine Trader inaendelea.
Helikopta mbili aina ya Black Hawk na boti mbili za uokoaji zimetumwa kushiriki katika operesheni hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania imetoa video inayoonyesha mojawapo ya helikopta hizo ikiruka juu ya meli hiyo.
Unaweza kusoma pia:
Martinez aomba radhi, Man United yampiga faini

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mkataba wa Martinez na Manchester United unamalizika msimu ujao wa kiangazi Beki wa Manchester United, Lisandro Martinez, ameomba radhi baada ya kutoa kauli za kuikosoa klabu kufuatia kipigo dhidi ya Atletico Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Baada ya mchezo huo, Martinez alisema alitarajia kuona uwekezaji mkubwa zaidi katika kikosi cha Manchester United na mchango mkubwa zaidi kutoka kwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Jason Wilcox. Kauli hizo zilionekana kuhoji namna klabu ilivyojiandaa kuimarisha timu.
Hata hivyo, baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa klabu pamoja na kocha Michael Carrick, beki huyo wa Argentina alifafanua kuwa alitoa kauli hizo kwa msukumo wa hisia baada ya kipigo hicho. Alisema hasira na kufadhaika vilichangia maoni yake, huku akisisitiza kuwa ana imani kamili na wachezaji wenzake, benchi la ufundi na wafanyakazi wote wa klabu katika juhudi za kuirejesha Manchester United kwenye mafanikio.
Katika taarifa, Martinez alisema maumivu ya kushindwa yalimfanya kueleza hisia zake kwa wakati na kwa njia ambayo haikuwa sahihi, na hivyo akaomba radhi kwa kauli zake.
Wakati huohuo, Manchester United ilimchukulia hatua za kinidhamu kwa kumpiga faini kutokana na matamshi hayo.
Akitoa tathmini yake kuhusu hali ya sasa ya klabu hiyo, nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, alisema mazingira ndani ya timu yanaashiria sintofahamu na ukosefu wa mwelekeo, akiyaelezea kama "vurugu tupu"
Unaweza pia kusoma:
Polisi wa Ubelgiji wapekua nyumba za ndugu wa Rais Tshisekedi wa DRC

Chanzo cha picha, Getty Images
Polisi nchini Ubelgiji Jumatano wamevamia nyumba za ndugu na washirika kadhaa wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, katika uchunguzi wa tuhuma za utakatishaji fedha zinazohusishwa na mapato ya sekta ya madini, kwa mujibu wa mawakili wawili waliowasilisha malalamiko hayo.
Misako hiyo inaongeza shinikizo kwa Tshisekedi, ambaye anakabiliwa na changamoto za kiusalama mashariki mwa Congo, ambako uasi wa kutumia silaha sasa unaongozwa na mtangulizi wake, Joseph Kabila. Aidha, nchi hiyo inakabiliwa na mlipuko hatari wa Ebola na ukosoaji unaoongezeka kutoka kwa upinzani kuhusu madai kwamba anapanga kuwania muhula wa tatu wa urais.
Serikali ya Congo pia imekuwa ikijitahidi kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini nchini humo. Congo ina baadhi ya akiba kubwa zaidi duniani ya shaba, kobalti na madini mengine ya kimkakati, lakini sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa kwa muda mrefu na tuhuma za ufisadi.
Mwanasheria wa Ubelgiji Bernard Maingain na mwanasheria wa Congo anayeishi Ufaransa, Hervé Diakese, wanaowakilisha kundi la mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka jimbo la Katanga, kusini mwa Congo, linalojulikana kama DESC/RDC, walisema misako hiyo ilifanyika katika mfumo wa uchunguzi ulioanzishwa baada ya mashirika hayo kuwasilisha malalamiko mjini Brussels.
“Malalamiko yaliyowasilishwa nchini Ubelgiji yanahusu kunyakuliwa kwa rasilimali na raia wa Ubelgiji na utakatishaji wa fedha zilizotokana na ubadhirifu wa mapato ya madini na rasilimali zinazomilikiwa na jamii za wenyeji, jambo lililoidhuru serikali ya Congo,” alisema Diakese.
“Fedha hizo zimewawezesha waliohusika kuendeleza maisha ya kifahari kupita kiasi ikilinganishwa na kipato ambacho wangeweza kukipata kihalali,” aliongeza.
Malalamiko hayo yaliwasilishwa nchini Ubelgiji mwaka 2025 kwa sababu baadhi ya watu waliotajwa katika kesi hiyo ni raia wa Ubelgiji wanaoishi nchini humo.
Msemaji wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Shirikisho la Ubelgiji alithibitisha kuwa polisi walifanya misako katika anwani kadhaa mjini Brussels na vitongoji vyake vya kaskazini na kusini, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa utakatishaji fedha ulioanzishwa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na mashirika yasiyo ya kiserikali mwaka 2025.
Hata hivyo, msemaji huyo alikataa kuthibitisha iwapo watu waliolengwa na misako hiyo ni ndugu wa Tshisekedi.
Msemaji wa rais wa Congo alikataa kutoa maoni kuhusu suala hilo.
Diakese alisema malalamiko hayo hayawalengi tu watu wa familia ya karibu ya Tshisekedi, bali pia watu wengine wanaohusishwa na mzunguko mpana wa washirika wa rais huyo.
Unaweza pia kusoma:
Infantino aomba radhi, lakini uongozi wake FIFA watiliwa shaka

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ameomba radhi kwa Baraza la FIFA kufuatia dosari katika mawasiliano na mashauriano kuhusu mpango wa Fifa Forward Enterprise (FFE), uliopendekeza kuhamisha sehemu ya haki za kibiashara za FIFA kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa Baraza la FIFA wamesema msamaha huo haujajibu maswali muhimu yaliyopo. Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha England (FA) na Makamu Rais wa FIFA, Debbie Hewitt, amesema Infantino anapaswa kuweka wazi nyaraka zote zinazohusiana na mpango huo na kutoa majibu ya kina kuhusu masuala yaliyozua utata.
Hewitt alisisitiza kuwa ikiwa Infantino hatafanya hivyo, atakuwa ameshindwa kuonyesha sifa zinazostahili kwa kiongozi wa FIFA. Aliongeza kuwa uwazi kuhusu mpango wa FFE na maamuzi mengine yenye utata ndani ya FIFA ni muhimu ili kurejesha imani ya viongozi wa soka duniani.
Kwa upande wake, Infantino amesema FFE ilikuwa pendekezo tu na si uamuzi uliokuwa umekamilika, akiahidi kuyajibu maswali yaliyosalia kwa maandishi.
Wakati huohuo, UEFA imeendelea kuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa Infantino, ikisisitiza kuwa nyaraka zote zinazohusiana na mpango huo zinapaswa kuwekwa wazi ili kubaini kilichotokea na kama kulikuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu.
Unaweza pia kusoma:
Mwanamume alizuiwa kwenye uwanja wa ndege wa Ujerumani akiwa na sanduku iliyojaa nyoka

Chanzo cha picha, German Customs
Mwanamume mmoja amesimamishwa katika Uwanja wa Ndege wa Cologne Bonn nchini Ujerumani baada ya kujaribu kuingiza mijusi na nyoka wenye sumu zaidi ya 90 kwa njia ya magendo.
Maafisa wa forodha walisema kwamba mhudumu huyo wa zima moto huyo raia wa Mexico mwenye umri wa miaka 45 alionekana "mwenye wasiwasi sana" alipojaribu kupitia njia ya kizuizi cha upekuzi bila kutangaza chochote kutoka uwanja wa ndege.
Walimfanyia kipimo cha dawa za kulevya mwanaume huyo ambaye alipatikana na cocaine -kabla ya kuendelea kukagua sanduku lake la nguo.
Hawakupata dawa yoyote, lakini walipata nyoka na mijusi, waliofichwa kwenye chupa za shampoo na krimu, vyombo vya plastiki na soksi.
"Wenzangu uwanja wa ndege wamezoea sana linapokuja suala la zawadi katika masanduku, lakini hatujawahi kuwa na nyoka 37 wenye sumu hai na mijusi 55 kutoka Mexico hapo awali," alisema Jens Ahland, msemaji wa ofisi ya forodha ya Cologne.
Baadhi walikuwa wakiwekwa "katika hali mbaya", Ahland alisema. Wengine walifariki wakati wa safari kutoka Mexico City kupitia Istanbul.
Mwanamume huyo, ambaye jina lake halijatajwa, aliwaambia maafisa kwamba alikuwa amewarudisha wanyama hao kama msaada kwa rafiki yake Mbrazil.
Alikataliwa kuingia Ujerumani na akarudi Istanbul kwa ndege.
Unaweza pia kusoma:
Tazama: Ndege isiyo na rubani ya Urusi ikigonga duka kubwa mjini Odesa Ukraine
Maelezo ya video, Ukraine: Wakati droni ya Urusi ilipopigajengo la maduka ya bidhaa mbali mbali Odesa Video ya CCTV iliyothibitishwa na BBC inaonyesha wakati ambapo ndege isiyo na rubani ilishambulia duka kubwa katika mji wa Mayaky katika eneo la Odesa nchini Ukraine.
Ndege hiyo isiyo na rubani inaweza kuonekana ikiruka juu ya paa la duka kubwa la Tavria na kulipuka wakati wa mgongano.
Watu watatu walijeruhiwa katika shambulio hilo, kulingana na Rais Volodymyr Zelensky, ambaye ameilaumu Urusi kwa shambulio hilo.
Vita vya Urusi nchini Ukraine viko katika mwaka wake wa tano, ambavyo vimekuwa vikiendelea tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine mnamo Februari 2022.
Unaweza pia kusoma:
Afisa wa Saudi Arabia atoa shutuma kali dhidi ya Iran kuhusu Wahouthi

Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia ameishutumu Iran kwa kuwatia moyo Wahouthi wa Yemen kutekeleza mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Saudi Arabia. Alisema Tehran inaendelea kulipa kundi hilo vifaa, mafunzo na usaidizi.
"Iran inaendelea kuwapa silaha, kuwafunza, na kuwaunga mkono wanamgambo wa Houthi, jambo ambalo linakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," Raed Karimli, naibu waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia anayehusika na diplomasia ya umma, alisema Alhamisi wakati wa mkutano wa mtandaoni na waandishi wa habari.
Aliongeza: "Tunaamini kwamba ongezeko la mashambulizi ya Wahouthi katika hatua hii ya mzozo linahimizwa na Iran."
Afisa huyo wa Saudi Arabia alisema nchi yake bado ina uhusiano na Iran, lakini Tehran haionekani kuwa tayari kufanya makubaliano ili kufikia suluhisho.
"Kwa ujumla, bado haionekani kwamba Wairan wako tayari kufanya makubaliano muhimu ili kufikia suluhisho," alisema.
Bw. Karimli pia aliwashutumu Wahouthi kwa kukataa kushiriki katika mazungumzo yaliyopendekezwa na Saudi Arabia nchini Oman katika wiki za hivi karibuni, huku mapigano yakizidi.
"Mwanzoni mwa awamu hii wakati mvutano ulipokuwa ukiongezeka, tuliwaomba wafanye mkutano huko Muscat, mji mkuu wa Oman, lakini walikataa," alisema.
Kulingana na afisa huyo wa Saudi Arabia, huo ulikuwa ndio mawasiliano ya mwisho kati ya pande hizo mbili, ambayo yalifanyika wiki kadhaa zilizopita.
Wakati huo huo, msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, Turki al-Maliki, alizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mashambulizi ya Wahouthi kwenye Uwanja wa ndege wa imataifa wa Mfalme Khalid huko Riyadh na operesheni za kijeshi za muungano huo dhidi ya kundi hilo.
Alisema Wahouthi wamejaribu kulenga viwanja vya ndege kadhaa, vituo vya mafuta na bandari nchini Saudi Arabia.
Bw. Maliki alisema mashambulizi hayo kwenye Uwanja wa Ndege wa King Khalid yalifanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani 10, makombora na silaha zingine.
Unaweza pia kusoma:
Trump asema hatatumia silaha za nyuklia dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty
Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatatumia silaha za nyuklia dhidi ya Iran.
Katika mahojiano na Newsmax, pia alisema kwamba hafikirii kutuma wanajeshi wa ardhini wa Marekani nchini Iran.
"Hatutatumia silaha za nyuklia. Hatuhitaji," Trump alisema.
Pia alijadili kile kinachoitwa "Mama wa Mabomu Yote," ambacho CNN iliripoti kinaweza kuzingatiwa kutumika katika mashambulizi yanayowezekana. Trump alisema ni bomu lenye nguvu sana, lakini si silaha ya nyuklia.
"Ni bomu kubwa sana, lakini si la nyuklia," alisema.
Trump pia alisema Marekani inaweza kuanzisha shambulio jingine dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, ikiwemo eneo la Koh Kalang.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Trump alisema kwamba Marekani iko katika mazungumzo na Urusi na China ili kupunguza silaha za nyuklia.
Unaweza pia kusoma:
Mvulana awauwa watoto watatu na mwalimu kwa risasi katika shule ya msingi Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Kijana wa miaka 16 amewapiga risasi watoto watatu na mwalimu katika shule ya msingi katika jimbo la Oregon nchini Marekani kabla ya kuuawa na mtu aliyekuwa karibu, kulingana na polisi.
Mshukiwa huyo, ambaye jina lake halijatajwa, alilazimisha kuingia katika Shule ya Msingi ya Silver Rail katika jiji la Bend kwa nguvu siku ya Alhamisi alasiri na kufyatua risasi kwenye milango iliyofungwa, polisi wanasema.
Mkuu wa Polisi wa Bend, Mike Krantz, alisema kijana huyo alipigwa risasi na kufa na mwanajamii ambaye "alimfuata shuleni hapo na kumshambulia".
Watoto watatu waliouawa walikuwa na umri wa miaka mitano, minane na 11. Mwalimu mmoja wa miaka saba na mwalimu wa miaka 54 walipelekwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya, polisi walisema. Haijulikani wazi kama mshambuliaji huyo alikuwa na uhusiano wowote na shule hiyo.
"Tumeshangazwa na kuvunjika moyo na mkasa huu usio na maana," Steven Cook, afisa mkuu wa utawala wa wilaya ya shule ya eneo hilo, alisema katika taarifa.
"Hakuna maneno yanayoweza kuelezea vya kutosha huzuni ambayo jamii yetu inapitia."
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu kwa matangazo haya ya mubashara ya leo Ijumaa tarehe 16.10.2026, shukran kwa kuwa nasi.



















