Je, Urusi itaishambulia NATO?

Chanzo cha picha, Getty Images
Uwezekano wa kuingilia kijeshi kwa Urusi katika eneo la nchi mwanachama wa NATO hali ambayo Moscow imekanusha vikali kuwa inapanga kuitekeleza umevutia tena umakini wa vyombo vya habari katika miezi ya hivi karibuni.
Mnamo tarehe 5 Oktoba 2026, gazeti la Financial Times liliripoti kuwa Estonia ilikuwa ikisogeza vikosi vyake karibu na mpaka wa Urusi kutokana na hofu ya uwezekano wa shambulio kutoka Moscow.
Mnamo tarehe 24 Septemba 2026, Shirika la Ujasusi wa Kijeshi la Denmark lilionya kuhusu "hatari ndogo lakini inayoongezeka" kwamba Urusi inaweza kupeleka idadi ndogo ya askari katika nchi jirani mwanachama wa NATO katika miezi ijayo.
Poland na Jamhuri ya Czech pia zimeonyesha wasiwasi kuhusu uwezekano wa vikosi vya Urusi kuingia katika eneo la mwanachama wa NATO au kufanya shambulio la anga.
Wakati huo huo, maafisa wa Moscow wameendelea kuionyesha Urusi kama mwathirika wa upanuzi wa NATO na kuishutumu jumuiya hiyo kwa nia ya kuizingira au kuzuia njia ya kufikia Kaliningrad, eneo la Urusi lililotengwa na ardhi kuu ya nchi hiyo na linalopakana na Bahari ya Baltic.
Hivyobasi tunauliza ni kwa kiasi gani tishio la shambulio la Urusi dhidi ya NATO ni halisi?
Msimamo wa Moscow ni upi?
Viongozi wakuu wa Urusi wamekanusha mara kwa mara mpango wowote wa kushambulia NATO.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema katika mkutano wa kila mwaka wa wataalam wa sera za kigeni wa Valdai karibu na Moscow kwamba Urusi "haina nia ya kushambulia mtu yeyote; sio 2029, sio 2030, sio 2050."
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Aliendelea kushutumu Ulaya kwa kujaribu kugeuza mawazo kutoka kwa matatizo ya nyumbani kwa kuchochea hofu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Urusi na NATO huku kukiwa na "hali ya uchumi na siasa inayozidi kuwa mbaya."
Wakati huo huo, Putin alionya tena kwamba Urusi ingetumia "silaha zote ilizonazo" iwapo NATO ingeshambulia.
Akijibu swali kutoka kwa mchambuzi wa Kirusi Fyodor Lukyanov kuhusu mazoezi ya kijeshi ya NATO katika Bahari ya Baltic na "vitisho" dhidi ya Kaliningrad, alisema: "Iwapo kutatokea shambulio la moja kwa moja [kutoka NATO] dhidi ya Shirikisho la Urusi katika hali hii dhidi ya Kaliningrad, lakini labda pia maeneo mengine suala la Urusi kutumia silaha zote ilizonazo bila shaka litakuwa ajenda ya haraka na isiyoepukika."
Kauli za Putin zilikuja siku chache baada ya ubalozi wa Urusi nchini Ireland kuishutumu NATO kwa kupanga "zingirio la anga na majini" dhidi ya Kaliningrad eneo la Urusi lililotengwa na ardhi kuu ya nchi hiyo na kuzungukwa na mataifa mengine na kusema kuwa Urusi iko tayari kulilinda eneo hilo kwa silaha za nyuklia iwapo itabidi.
Maafisa wengine wa Urusi kwa kiasi kikubwa wameunga mkono msimamo huo huo.
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alielezea ripoti kuhusu uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi wa Urusi katika nchi mwanachama wa NATO kama "habari ya kutisha," na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema kuwa Moscow "imeshasema mara kwa mara kwamba haina nia ya kuishambulia Ulaya."
Urusi inafanya nini katika eneo la Bahari ya Baltic?
Maafisa wa Urusi pia hawajatangaza hadharani mabadiliko yoyote katika msimamo wa kijeshi wa nchi hiyo dhidi ya NATO, ingawa Kikosi cha Majini cha Urusi katika Bahari ya Baltic kimefanya mazoezi kadhaa katika miezi ya hivi karibuni.
Mapema mwezi Agosti 2026, kikosi hicho kilifanya mazoezi yaliyohusisha vitengo vya makombora , huku timu za kukabiliana na hujuma zikifanya mazoezi ya kulinda kambi ya majini dhidi ya shambulio la adui lililoigizwa.
Mnamo tarehe 3 Oktoba 2026, United Shipbuilding Corporation, kampuni kubwa zaidi ya ujenzi wa meli nchini Urusi, ilitangaza kuwa nyambizi ya "Veliky Loki" ilifanya zoezi la kurusha kombora la torpedo.
Wakati huo huo, mshirika wa Urusi, Belarus, ilifanya mazoezi ya amri na maafisa wa ngazi ya juu yaliyodumu kwa siku nne karibu na mipaka yake na Lithuania na Poland kuanzia tarehe 15 hadi 18 Septemba 2026.
Mazoezi hayo yalifanyika karibu na njia ya Suwalki (Suwalki Pass), kipande cha ardhi kando ya mpaka wa Poland na Lithuania ambacho kinatenganisha Belarus na Kaliningrad.
Je, Urusi itashambulia NATO?
Wataalamu wengine wa masuala ya Urusi wanaona kuwa mgogoro wa moja kwa moja na NATO, hasa katika eneo la Baltic, unawezekana na hata una uwezekano mkubwa wa kutokea.
Kwa mfano, mchambuzi wa masuala ya kisiasa Vladimir Pastukhov alisema mnamo Septemba 2026 kwamba mtazamo wake ulikuwa umebadilika katika miezi sita iliyopita na kwamba sasa anaona shambulio dhidi ya mataifa ya Baltic kuwa jambo "lenye uwezekano mkubwa."
Pastukhov alisema kuwa ingawa migogoro ya sasa ya Moscow nchini Ukraine inafanya shambulio kama hilo kuonekana kutowezekana kwa mtazamo wa kimantiki pekee, imani za kiitikadi za Putin zinafanya hatua hiyo kuwa "hatua inayofuata yenye uwezekano mkubwa zaidi."
Hata hivyo, huu si mtazamo unaoshikiliwa na wengi.
Wachambuzi wengi, akiwemo mchambuzi maarufu wa masuala ya kijeshi Ruslan Levev, wanaona kuwa shambulio kamili la Urusi dhidi ya NATO halina uwezekano mkubwa wa kutokea "katika miaka michache ijayo," wakisema kuwa Moscow tayari inakabiliwa na changamoto ya kupeleka vikosi vya kutosha nchini Ukraine.
Wakati huo huo, wachambuzi pia wanachunguza uwezekano wa operesheni ndogo zaidi za Urusi katika mataifa ya Baltic.
Sergei Auslander, mwandishi wa habari za ulinzi anayeishi Israel, anaamini kuwa kuingia kwa vikosi vya Urusi kwa kiwango kidogo kuna "uwezekano mkubwa kidogo" kuliko uvamizi kamili.
Alipendekeza hali ambapo Urusi inaweza kuteka eneo la kilomita za mraba kadhaa ndani ya ardhi ya Estonia kwa kisingizio fulani, au kuchukua hatua ya uchochezi kwa lengo la "kuwalinda wakazi wanaozungumza Kirusi wa Narva," mji ulioko Estonia kwenye mpaka na Urusi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, lengo kuu ni kupima mwitikio wa NATO
Wataalamu kutoka mradi wa uchambuzi wa "Re:Russia" walisema mnamo Machi 2026 kwamba operesheni ndogo ingehitaji nguvu kidogo na huenda isilenge sana kuteka eneo, bali kupima mshikamano wa NATO na kusababisha migawanyiko miongoni mwa wanachama wake.
Makala hiyo pia ilidokeza kuwa shambulio la aina hiyo huenda lisiwe hatua inayofuata ya mzozo wa baada ya vita vya Ukraine, bali sehemu ya mzozo wa sasa.
Makala hiyo ilisema: "Kushindwa kwa Moscow kufikia malengo yake nchini Ukraine, iwe kijeshi au kidiplomasia, kunaweza kuilazimisha kuiwekea Ulaya shinikizo kwa kutumia tishio la vita kamili vya kijeshi na kuilazimisha kutoa masharti nafuu katika makubaliano ya kumaliza vita vya Ukraine."
Hata hivyo, si wachambuzi wote wanaoona shambulio dogo kama chaguo la kimantiki kwa Kremlin, wakionya kuwa mkakati kama huo unaweza kuleta matokeo kinyume na yaliyotarajiwa.
Gazeti la Nezavisimaya Gazeta liliandika mnamo Julai 2026 kwamba dhana ya "kupima uthabiti wa NATO" inaleta matokeo mabaya kwa upande unaoifanya tangu mwanzo, likisema kuwa hatua kama hiyo inaweza kwa vitendo kusababisha muungano huo kuimarika zaidi na kuleta mwitikio mkali.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Anton Barbashin, katika mahojiano ya Septemba 2026 na chombo cha habari cha Meduza chenye makao yake Latvia, pia alihoji mantiki ya kwamba shambulio dhidi ya Ulaya lingeweza kusababisha migawanyiko ndani yake.
Badala yake, alidai kuwa mashambulizi ya Urusi katika ardhi ya Ulaya yanaweza kuleta matokeo kinyume, na kusababisha ongezeko kubwa la matumizi ya ulinzi kote barani humo.
Pia alisema kuwa "kuzidi kuwa na msimamo mkali katika hatua za Urusi dhidi ya nchi za Magharibi" kunaweza kusababisha "kuporomoka kabisa" kwa ushirikiano wake na washirika muhimu kama vile China, nchi ambayo Urusi inaitegemea sana—au kwa maneno mepesi, inayoitegemea "kupita kiasi."
































