Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi imesema shambulio la Siku ya Krismasi dhidi ya Ukraine lilifanikiwa
Jeshi la anga la Ukraine linasema liligundua makombora 184 na ndege zisizo na rubani, na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya nishati nchini kote.
Muhtasari
- Wanne wauawa na makombora ya Ukraine huko Kursk
- Hatua za jeshi 'zilichochea' mauaji ya mateka sita na Hamas - Israel
- Makumi ya watu wafariki katika ajali ya ndege ya abiria nchini Kazakhstan
- Zelensky alitaja shambulio la siku ya Krismasi dhidi ya Ukraine la 'kinyama
- Urusi yafanya mashambulizi makubwa ya makombora dhidi ya miundombinu ya kawi Ukraine
- Watu watatu wameuawa kwa kupigwa risasi huku watu wenye silaha wakishambulia hospitali ya Haiti
- Mji alikozaliwa Yesu hauna raha wakati wa Krismasi
- Urusi Ilishambulia Ukraine kwa ndege 60 zisizo na rubani, 36 ziliangushwa
- Kiongozi wa upinzani Msumbiji aapa kujiapisha kuwa rais
- Denmark yaimarisha ulinzi wa Greenland baada ya Trump kurudia hamu ya Marekani kutaka kukidhibiti kisiwa hicho
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu
Wanne wauawa na makombora ya Ukraine huko Kursk
Watu wanne wameuawa na wengine watano kujeruhiwa na makombora ya Ukraine katika mji wa Lgov kwenye mkoa wa Kursk nchini Urusi, kulingana na kaimu gavana wa eneo hilo.
Alexander Khinshtein anasema jengo la ghorofa tano, majengo mawili ya makazi ya ghorofa moja, na saluni ya urembo ya ghorofa moja yaliharibiwa.
Anaongeza kuwa "wimbi la mlipuko" liliharibu sehemu ndogo ya bomba la gesi lilipua madirisha katika nyumba za jirani, na kuharibu magari kadhaa.
Sehemu za eneo la Kursk zinakaliwa na Ukraine kufuatia shambulio lake la kuvuka mpaka mapema Agosti.
Hatua za jeshi 'zilichochea' mauaji ya mateka sita na Hamas - Israel
Uchunguzi uliofanywa na jeshi la Israel umegundua kuwa vitendo vya vikosi vyao vya ardhini huenda vilichochea mauaji ya mateka sita huko Gaza mwezi Agosti na Hamas.
Ilisema "shughuli za wanajeshi wake" katika eneo hilo, ingawa ni za taratibu na zenye kuzingatia tahadhari, zilikuwa na ushawishi wa kimazingira kwa uamuzi wa magaidi wa kuwaua mateka sita".
Uchunguzi huo pia uligundua kuwa wanajeshi hao hawakujua uwepo wa mateka hao walipoanza operesheni yao katika eneo la Rafah. Miili ya mateka ilipatikana baadaye.
Mauaji hayo yalisababisha hasira nchini Israel, huku mamia kwa maelfu wakiingia barabarani na kuitaka serikali kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, wanajeshi wa Israel walipata miili hiyo kwenye handaki katika eneo la Tal al-Sultan huko Rafah. Wanajeshi walisema waliuawa kabla tu ya wanajeshi kuwafikia.
Uchunguzi ulisema kwamba mkuu wa jeshi la Israel "alihitimisha kuwa hili lilikuwa tukio la uchungu na la kusikitisha, na matokeo magumu sana ya mauaji ya kikatili ya mateka sita yaliyotekelezwa na Hamas".
Soma zaidi:
Makumi ya watu wafariki katika ajali ya ndege ya abiria nchini Kazakhstan
Makumi ya watu wamefariki baada ya ndege ya abiria kuanguka iliyokuwa na takriban watu 70 nchini Kazakhstan, maafisa wa eneo hilo wamesema.
Mamlaka nchini Azerbaijan, ambako ndege hiyo ilianzia, wanasema kulikuwa na manusura takriban 30.
Ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan J2-8243 ilishika moto ilipokuwa ikijaribu kutua kwa dharura karibu na mji wa Kazakh wa Aktau.
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea Grozny nchini Urusi lakini ililazimika kutua kwa sababu ya ukungu, shirika hilo la ndege liliambia BBC.
Kulikuwa na abiria 62 na wahudumu 5 kwenye ndege ya Embraer 190, wizara ya uchukuzi iliripoti.
BBC imewasiliana na Azerbaijan Airlines na Embraer kwa maoni.
Zelensky alitaja shambulio la siku ya Krismasi dhidi ya Ukraine la ‘kinyama’
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amejibu hivi punde tu shambulio la Siku ya Krismasi la Urusi nchini Ukraine:
"Kila shambulio kubwa la Urusi huchukua muda kuandaliwa. Kamwe sio uamuzi wa ghafla. Ni chaguo la kufahamu sio tu la malengo, lakini pia la wakati na tarehe.
"Leo, Putin alichagua Krismasi kwa makusudi kutekeleza shambulio. Ni nini kinachoweza kuwa unyama zaidi? Zaidi ya makombora 70, yakiwemo ya balestiki, na zaidi ya ndege mia moja zisizo na rubani. Walengwa ni sekta yetu ya nishati. Wanaendelea kupigania kukatika kwa umeme nchini Ukraine. .
"Kwa mujibu wa takwimu za awali, watetezi wetu walifanikiwa kuangushi zaidi ya makombora 50 na sehemu kubwa ya ndege zisizo na rubani. Kwa bahati mbaya, kuna sehemu zilizoathiriwa katika mikoa kadhaa. Wafanyakazi wa kawi wanafanya kazi kurejesha usambazaji wa umeme haraka iwezekanavyo.
"Asante kwa kila mtu ambaye kwa sasa anaifanyia kazi nchi, ambaye yuko kwenye mstari wa vita , ambaye analinda anga yetu. Tuendelee kutoa huduma ya kiwango cha juu. Uovu wa Urusi hautavunja Ukraine na kuharibu Krismasi."
Urusi yafanya mashambulizi makubwa ya makombora dhidi ya miundombinu ya kawi Ukraine
Miji ya Ukraine imeshambuliwa kwa kiasi kikubwa asubuhi ya siku ya Krismasi kutoka kwa makombora ya masafa marefu ya Urusi.
Waziri wa nishati German Galushchenko alisema: "Adui anafanya mashambulizi makubwa kwenye mfumo wa nishati kwa mara nyengine."
Alisema vikwazo vya upatikanaji wa umeme vimewekwa ili kukabiliana na mashambulizi hayo. Milipuko kadhaa ilitikisa Kharkiv, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ukraine.
Kulikuwa na taarifa za awali kutoka kwa viongozi wa eneo hilo kuhusu majeraha. Jiji la Dnipro pia liliripotiwa kushambuliwa.
Watu watatu wauawa kwa kupigwa risasi huku watu wenye silaha wakishambulia hospitali ya Haiti
Takriban watu watatu wamefariki wakati watu wenye silaha nchini Haiti walipowafyatulia risasi waandishi wa habari, polisi na maafisa wa afya wakati wa mkutano wa kutangaza kufunguliwa tena kwa hospitali kubwa ya umma nchini humo.
Wanahabari wawili na afisa wa polisi wameripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi, huku wengine wakijeruhiwa katika shambulio la Jumanne katika hospitali kuu katika mji mkuu Port-au-Prince.
Kituo hicho cha matibabu kilikuwa kimetekwa tena na serikali ya Haiti mnamo Julai, baada ya kukaliwa na kuharibiwa na magenge.
Muungano wa genge la Viv Ansanm, ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya jiji, limekiri kutekeleza shambulio hilo
Picha zilizochapishwa mtandaoni zinaonekana kuonyesha watu kadhaa wakiwa wamejeruhiwa au kufariki ndani ya jengo hilo.
Wanahabari walikuwa wakisubiri kuwasili kwa Waziri wa Afya Lorthe Blema wakati ufyatuaji risasi ulipoanza.
Waandishi wa habari Markenzy Nathoux na Jimmy Jean waliuawa wakati wa shambulio hilo, Robest Dimanche, msemaji wa Online Media Collective, aliliambia shirika la habari la AFP.
Waandishi wengine wa habari walijeruhiwa, aliongeza.
Afisa mmoja pia aliuawa, msemaji wa polisi Lionel Lazarre aliambia AFP.
"Ilionekana kama sinema mbaya," Dieugo André, mwandishi wa picha ambaye alishuhudia vurugu hizo, alinukuliwa akisema na The Haitian Times.
"Nina damu ya waandishi wa habari kadhaa waliojeruhiwa kwenye nguo zangu."
Katika video ya mtandaoni inayodai shambulio hilo, muungano wa genge la Viv Ansanm ulisema haujaidhinisha kufunguliwa tena kwa hospitali hiyo, ambayo waliikalia na kuharibu mnamo Machi.
Mkuu wa baraza la mpito la rais wa Haiti, Leslie Voltaire, alisema: "Tunatoa pole kwa familia zote za wahasiriwa, haswa kwa Polisi wa Kitaifa wa Haiti na vyama vyote vya waandishi wa habari.
Mji alikozaliwa Yesu hauna raha wakati wa Krismasi
Mji mdogo wa Bethlehem katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa una sababu nzuri ya kujiona kuwa mji mkuu wa Krismasi lakini mwaka huu haujisikii hivyo.
Kuna wageni wachache sana wakati ambao kwa kawaida ni wakati wa kilele wa sherehe hizo. Hakuna mapambo ya kawaida ya barabarani au mti mkubwa wa Krismasi mbele ya Kanisa la Nativity, liliojengwa juu ya mahali ambapo inaaminika kwamba Yesu alizaliwa.
Sherehe za hadhara za Krismasi zimefutwa kwa mwaka wa pili kwa sababu ya vita huko Gaza. Wakristo wa Palestina wanahudhuria tu sherehe za kidini na mikusanyiko ya familia.
"Huu unapaswa kuwa wakati wa furaha na sherehe," asema Mchungaji Dkt Munther Isaac, mchungaji wa Kilutheri. "Lakini Bethlehem ni mji wa huzuni katika mshikamano na ndugu zetu huko Gaza."
Katika kanisa lake, tukio la Kuzaliwa kwa Yesu linaonyesha mtoto Yesu akiwa amelala kwenye rundo la vifusi. Katika kuelekea Krismasi, ibada ya maombi iliangazia hali mbaya ya Gaza.
"Ni vigumu kuamini kwamba Krismasi nyingine imetujia na mauaji hayajakoma," Isaac alisema katika mahubiri yake yenye maneno makali. "Watoa maamuzi wameridhika na kuacha jambo hili liendelee. Kwao, Wapalestina ni watu wasiofaa."
Israel inakanusha vikali tuhuma za mauaji ya halaiki huko Gaza na majaji katika mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa bado hawajatoa uamuzi katika kesi ya madai ya mauaji ya halaiki, iliyoletwa na Afrika Kusini.
Habari za hivi punde, Urusi yaishambulia Ukraine kwa ndege 60 zisizo na rubani
Jeshi la Urusi liliishambulia Ukraine kwa ndege 60 zisizo na rubani aina ya Shahed na aina nyingine za ndege zisizo na rubani, Jeshi la Wanahewa la Ukraine limeripoti.
Ndege 36 zisizo na rubani zilidunguliwa, ndege zisizo na rubani 23 "zilipotea".
Mikoa ya Poltava, Sumy, Kharkiv, Kiev, Chernihiv, Zaporizhia, Dnepropetrovsk na Khmelnytsky ilishambuliwa.
Kiongozi wa upinzani Msumbiji aapa kujiapisha kuwa rais
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Msumbiji, Venâncio Mondlane, ametangaza kuwa atajiweka kuwa rais tarehe 15 Januari baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa urais yaliomuonesha .
Tangazo lake lilikuja huku wafuasi wake wakifanya maandamano yenye ghasia kote nchini kutaka kusitishwa kwa utawala wa miaka 49 wa chama cha Frelimo.
Mji mkuu wa Maputo ulikuwa umesalia kuwa mahame usiku wa mkesha wa Krismasi, na karibu biashara zote zimefungwa na watu kukaa nyumbani ili kuepuka kunaswa katika machafuko mabaya zaidi katika jiji hilo tangu Frelimo ilipojitawala wakati wa uhuru mwaka 1975.
Ofisi za Frelimo, vituo vya polisi, benki na viwanda vimeporwa, kuharibiwa na kuchomwa moto kote nchini. Tangu Jumatatu, takriban watu 21 wameuawa katika machafuko hayo, waziri wa mambo ya ndani alisema mapema siku ya Jumanne.
Denmark yaimarisha ulinzi wa Greenland baada ya Trump kurudia hamu ya Marekani kutaka kukidhibiti kisiwa hicho
Serikali ya Denmark imetangaza ongezeko kubwa la matumizi ya ulinzi kwa kisiwa cha Greenland, saa chache baada ya Rais mteule wa Marekani Donald Trump kurudia nia yake ya kutka kulinunua eneo la Arctic.
Waziri wa Ulinzi wa Denmark Troels Lund Poulsen alisema kifurushi hicho kilikuwa "kiasi cha mabilioni ya krone, au angalau $1.5bn (£1.2bn).
Alielezea muda wa tangazo hilo kama "kejeli ".
Siku ya Jumatatu Trump alisema umiliki na udhibiti wa kisiwa hicho kikubwa ni "lazima" kwa Marekani.
Greenland, eneo linalojiendesha la Denmark, ni nyumbani kwa kituo kikubwa cha anga za juu cha Marekani na ni muhimu kimkakati kwa Marekani, kikiwa katika njia fupi zaidi kutoka Amerika Kaskazini hadi Ulaya.
Kina hifadhi kubwa ya madini.
Poulsen alisema kifurushi hicho kitaruhusu ununuzi wa meli mbili mpya za ukaguzi, ndege mbili mpya zisizo na rubani na za masafa marefu na timu mbili za ziada za mbwa.
Pia itajumuisha ufadhili wa kuongeza wanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Arctic katika mji mkuu wa Nuuk na uboreshaji wa mojawapo ya viwanja vya ndege vitatu vya raia vya Greenland ili kushughulikia ndege za kivita za F-35.
"Hatujawekeza vya kutosha katika Arctic kwa miaka mingi, sasa tunapanga uwepo wa nguvu zaidi," alisema.
Waziri wa ulinzi hakutoa kiwango cha ufadhili huo, lakini vyombo vya habari vya Denmark vilikadiria kuwa karibu krone bilioni 12-15.
Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya Trump kusema kwenye jukwaa lake la mtandao wa kijamii la Truth Social: "Kwa madhumuni ya Usalama wa Taifa na Uhuru Duniani, Marekani inahisi kuwa umiliki na udhibiti wa Greenland ni jambo la lazima kabisa."
Natumai hujambo leo ikiwa siku kuu ya Krisimasi na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja