Australia imetangaza mpango wa kununua silaha kutoka kwa raia baada ya shambulio la ufukwe wa Bondi, tukio baya zaidi la ufyatuaji risasi wa halaiki nchini humo katika miongo kadhaa.
Mpango huo ni mkubwa zaidi tangu mauaji ya Port Arthur mwaka 1996, ambapo watu 35 waliuawa na baadaye Australia ikaweka sheria kali za kudhibiti silaha.
Watu 15 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa Jumapili, baada ya washambuliaji wawili wanaodaiwa kuhamasishwa na itikadi ya Islamic State kufyatua risasi katika tamasha la Wayahudi lililofanyika katika ufuo maarufu wa Bondi.
Polisi wamesema shambulio hilo, ambalo limetangazwa kuwa la kigaidi, lilitekelezwa na baba na mwanawe.
Naveed Akram, mwenye umri wa miaka 24, ameshtakiwa kwa makosa 59, yakiwemo mashtaka 15 ya mauaji na kosa la kutekeleza kitendo cha kigaidi.
Baba yake, Sajid, aliuawa wakati wa tukio hilo.
Siku moja baada ya shambulio, baraza la mawaziri la kitaifa lilikubaliana kukaza zaidi sheria za umiliki wa silaha.
Waziri Mkuu Anthony Albanese alisema kwa sasa kuna zaidi ya silaha milioni nne nchini Australia, idadi iliyo kubwa kuliko ilivyokuwapo mwaka 1996.
Alisema mmoja wa washambuliaji alikuwa na leseni halali ya silaha na alimiliki bunduki sita, jambo lililoibua maswali kuhusu sababu ya mtu anayeishi katika vitongoji vya jiji kuwa na silaha nyingi kiasi hicho.
Kamishna wa Polisi wa Shirikisho, Krissy Barrett, alisema mpango wa kununua silaha ni hatua muhimu katika kupunguza idadi ya silaha mikononi mwa raia.
Mpango huo utanunua silaha zisizohitajika, zilizopigwa marufuku na silaha haramu, kwa ufadhili wa pamoja kati ya serikali ya shirikisho na majimbo.
Serikali inatarajia kukusanya na kuharibu mamia ya maelfu ya silaha. Pia kumekubaliwa kuweka kikomo cha idadi ya silaha anazoweza kumiliki mtu mmoja, kudhibiti utoaji wa leseni, kuainisha aina za silaha zinazoruhusiwa kisheria, na kufanya uraia wa Australia kuwa sharti la kupata leseni ya silaha.
Hatua za kuanzisha daftari la kitaifa la silaha zitaongezwa kasi, huku wasimamizi wa silaha wakipewa taarifa bora za kijasusi kuhusu uhalifu.
Polisi wa New South Wales wamesema wanaume saba waliokuwa wakishukiwa kwa misimamo mikali wataachiliwa, lakini wataendelea kufuatiliwa.
Polisi hawajathibitisha kuwepo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati yao na shambulio la ufukwe wa Bondi, ingawa eneo hilo lilikuwa miongoni mwa maeneo waliyopanga kutembelea.
Kamishna wa Polisi wa NSW, Mal Lanyon, alisema ingawa tishio halikujulikana wazi, uwezekano wa tukio la vurugu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba polisi hawakuwa tayari kuhatarisha usalama wa umma.