Serikali yafikiria kumuondoa Andrew katika orodha ya urithi wa ufalme
Serikali ya Uingereza inafikiria kutunga sheria ya kumuondoa Andrew Mountbatten-Windsor katika orodha ya urithi wa ufalme.
Waziri wa Ulinzi Luke Pollard aliiambia BBC kuwa hatua hiyo, ambayo itamzuia Andrew kuwa Mfalme ni “jambo sahihi kufanya”, bila kujali matokeo ya uchunguzi wa polisi.
Kwa sasa Andrew, ndugu wa Mfalme, bado ni wa nane katika orodha ya kurithi kiti cha ufalme licha ya kuvuliwa hadhi na majukumu ya kifalme mwaka jana, kufuatia shinikizo kubwa kuhusu uhusiano na mfadhili wake na mtu aliyedaiwa kujihusisha na watoto kimapenzi, Jeffrey Epstein.
Alikamatwa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu katika ofisi ya umma na kuachiwa chini ya uchunguzi, akikanusha makosa yote.
Pollard alisema serikali imekuwa ikifanya kazi na kasri la Buckingham kuzuia hali ya Andrew “kurithi kiti cha ufalme”, lakini akasisitiza hatua hiyo inapaswa kusubiri hadi pale uchunguzi wa polisi utakapo kamilika.
Pendekezo hilo litahitaji kupitishwa na Bunge na kuidhinishwa na Mfalme, pamoja na kuungwa mkono na nchi 14 za Jumuiya ya Madola ambako Charles III ni mkuu wa jumuiya ya madola.
Mara ya mwisho orodha ya urithi kubadilishwa na sheria ya Bunge ilikuwa mwaka 2013, huku mwaka 1936 ikiwa mara ya mwisho mtu kuondolewa rasmi kufuatia kujiuzulu kwa Edward VIII.
Baadhi ya wabunge wa vyama vya Liberal Democrats na SNP wameunga mkono wazo hilo, huku wengine wakisema ni suala la kusubiri matokeo ya uchunguzi.
Kasri la Buckingham halijatoa maoni rasmi kuhusu mpango huo.
Soma pia: