China na Ufilipino zalaumiana huku meli zao zikigongana

Ajali hiyo ni tukio la hivi punde zaidi kwenye mzozo unaozidi kuongezeka katika maeneo ya Bahari ya China Kusini.

Muhtasari

  • China na Ufilipino zalaumiana huku meli zao zikigongana
  • Urusi inatafuta helikopta iliyopotea ikiwa na watu 22
  • Mtandao wa X wapigwa marufuku Brazil
  • Wanajeshi wa Ujerumani wanaondoka Niger
  • Zelensky amfuta kazi mkuu wa jeshi la anga la Ukraine
  • Shambulizi la Urusi lamuua msichana, 14, Ukraine
  • Marekani yalenga Islamic State nchini Iraq, 15 wauawa

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tumekamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. China na Ufilipino zalaumiana huku meli zao zikigongana

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    China na Ufilipino zimeshutumiana katika tukio la kugongana kwa meli za walinzi wa pwani katika eneo linalozozaniwa la Bahari ya China Kusini.

    Ufilipino imedai meli ya China "moja kwa moja na kwa makusudi" iligonga meli yake, huku Beijing ikiishutumu Ufilipino kwa "kuigonga" kwa makusudi meli ya Uchina.

    Mgongano wa Jumamosi karibu na eneo la Sabina ni wa hivi karibuni zaidi katika mzozo wa muda mrefu - na unaozidi kuongezeka - kati ya nchi hizo mbili juu ya visiwa na maeneo mbalimbali katika Bahari ya China Kusini.

    Ndani ya wiki mbili zilizopita, kumekuwa na matukio mengine matatu katika eneo moja yanayohusisha meli za nchi hizo mbili.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Urusi inatafuta helikopta iliyopotea ikiwa na watu 22

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Operesheni ya utafutaji na uokoaji imeanzishwa katika eneo la mashariki ya mbali nchini Urusi kufuatia kutoweka kwa helikopta iliyokuwa na watu 22 wengi wao wakiwa watalii.

    Helikopta ya Mi-8T ilipaa kutoka kituo cha karibu na volcano ya Vachkazhets katika rasi ya Kamchatka, wizara ya dharura ilisema Jumamosi.

    Eneo hilo ni kivutio maarufu cha watalii kwa mandhari yake nzuri na volkano hai.

    Maafisa wanasema helikopta hiyo ilitoweka kwenye rada muda mfupi baada ya kupaa, na kuongeza kuwa ukungu mkubwa unatatiza juhudi za waokoaji.

    Helikopta hiyo inayomilikiwa na Vityaz-Aero, ilikuwa ikisafiri kuelekea kwenye volkano hiyo.

    Ikiwa iliundwa wakati wa enzi ya Soviet, helikopta ya Mi-8 inasalia kuwa maarufu na inatumiwa sana nchini Urusi.

    Ilitoweka kutoka kwenye rada na wafanyikazi walishindwa kuwasiliana kuanzia saa 16:15 saa za eneo, gavana wa Kamchatka alisema.

    Chanzo cha wizara chenye kusimamia dharura kiliambia shirika la habari la serikali la Tass kwamba wafanyakazi wake hawakuripoti matatizo yoyote kabla ya kutoweka.

    Vladimir Solodov alisema ilikuwa na abiria 19 na wahudumu watatu.

    Msako wa angani uliendelea hadi usiku lakini kulikuwa hakuonekani vizuri.

    Soma zaidi:

  4. Mtandao wa X wapigwa marufuku Brazil

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mtandao wa X, uliojulikana zamani kama Twitter, amepigwa marufuku nchini Brazil baada ya kushindwa kutimiza makataa yaliyowekwa na jaji wa Mahakama ya Juu.

    Alexandre de Moraes aliamuru "kusitishwa mara moja na kikamilifu" kuendeshwa kwa mtandao huo wa kijamii hadi itii amri zote za mahakama na kulipa faini zilizopo.

    Mzozo huo ulianza mwezi Aprili, huku jaji akiamuru kufungwa kwa akaunti nyingi za X kwa madai ya kueneza habari potofu.

    Akijibu uamuzi huo, mmiliki wa X Elon Musk alisema: "Uhuru wa kujieleza ndio msingi wa demokrasia na hakimu bandia ambaye hajachaguliwa nchini Brazili anaiharibu kwa malengo ya kisiasa."

    X inasemekana kutumiwa na moja ya kumi ya wakazi milioni 200 wa taifa hilo.

    Kufikia Jumamosi asubuhi baadhi ya watumiaji walikuwa wameripoti kushindwa kuingia kwenye jukwaa hilo.

    X ilifunga ofisi yake nchini Brazil mapema mwezi huu, ikisema mwakilishi wake alitishiwa kukamatwa ikiwa hatatii amri ilizozitaja kama "udhibiti" - na kwamba ni kinyume cha sheria chini ya sheria za Brazil.

    Jaji Moraes alikuwa ameamuru kwamba akaunti za X zinazoshutumiwa kueneza habari potofu - lazima zizuiwe wakati zinaendelea kuchunguzwa.

    Aliongeza kuwa wawakilishi wa kisheria wa kampuni hiyo watawajibishwa ikiwa akaunti yoyote itafunguliwa tena.

    X imetishiwa kutozwa faini kwa kukataa kutii agizo hili, huku kampuni hiyo na Bw Musk wakiungana na wakosoaji nchini Brazil kumshutumu jaji huyo kuegemea mrengo

  5. Wanajeshi wa Ujerumani wanaondoka Niger, kuashiria mwisho wa operesheni ya Sahel

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ujerumani imewaondoa wanajeshi wake wa mwisho waliosalia katika eneo linalosimamiwa na Niger, hatua inayoashiria mwisho wa operesheni zake huko Sahel.

    Kuondoka kwao kulikamilika siku ya Ijumaa na kutangazwa na maafisa waandamizi wa jeshi la Ujerumani na Niger.

    Wanajeshi 60 wa Ujerumani na tani 146 za vifaa vilivyosafirishwa na ndege tano za mizigo zilitua Ujerumani Ijumaa usiku.

    Mnamo mwezi Mei, Niger ilikubali kuruhusu wanajeshi wa Ujerumani kuendelea kuendesha shughuli zao katika kambi yao ya wana anga huko Niamey hadi Agosti 31.

    Mazungumzo yaligonga mwamba kati ya pande zote mbili baada ya Niger kushindwa kuhakikisha kwamba majeshi ya Ujerumani nchini humo yangenufaika na kinga dhidi ya kufunguliwa mashtaka.

    "Kujiondoa kwao hakuashirii mwisho wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Niger na Ujerumani," maafisa kutoka nchi zote mbili walisema katika taarifa ya pamoja iliyosomwa, wakionyesha kujitolea kwao kudumisha uhusiano wa kijeshi.

    Hata hivyo, kauli hiyo ni tofauti kabisa na ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, ambaye alisema mwezi Julai kuwa hawawezi tena kushirikiana na Niger kwa sababu ya kukosekana kwa uaminifu.

    Ujerumani ilianza operesheni katika kambi yake ya wanajeshi wa anga huko Niamey mwaka wa 2016, na ilikuwa na wanajeshi takriban 3,200.

    Berlin pia ilichangia katika vita dhidi ya waasi katika nchi jirani ya Mali, kama sehemu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani ambao ulilazimika kutamatisha shighuli zake mwaka jana.

    Soma zaidi:

  6. Zelensky amfuta kazi mkuu wa jeshi la anga la Ukraine baada ya ajali ya F-16

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais Volodymyr Zelensky amemfuta kazi kamanda wa kikosi cha anga cha Ukraine huku kukiwa na mjadala kuhusu kuanguka kwa ndege mpya ya kivita ya F-16 yenye thamani kubwa nchini humo.

    Bw Zelensky hakutaja sababu ya kumfukuza kazi Luteni Jenerali Mykola Oleshchuk, lakini alisema ana jukumu la "kuwatunza wapiganaji wetu wote".

    Ndege hiyo aina ya F-16 iliyotengenezwa Marekani - mojawapo ya ndege kadhaa zilizotolewa mapema mwezi huu na washirika wa Magharibi wa Ukraine - ilianguka Jumatatu, na kumuua rubani.

    Ingawa ilitokea wakati wa msururu wa makombora ya Urusi, Ukraine ilisema chanzo cha ajali hiyo haikuwa matokeo ya moja kwa moja ya shambulio la adui, na Luteni Jenerali Oleshchuk alijipata akiwa matatani na baadhi ya wanasiasa kuhusu nani alaumiwe kwa hasara hiyo.

    Soma zaidi:

  7. Shambulizi la Urusi lamuua msichana, 14, Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Msichana mwenye umri wa miaka 14 ameuawa baada ya shambulio la bomu lililoongozwa na Urusi katika mji wa kaskazini-mashariki mwa Ukraine wa Kharkiv kushambulia uwanja wa michezo, maafisa wa eneo hilo wamesema.

    Takriban watu wengine sita waliuawa na 59 kujeruhiwa wakati jengo la makazi la ghorofa 12 liliposhambuliwa katika jiji karibu na mpaka wa Urusi.

    Picha zilionyesha miali ya moto na moshi mzito mweusi ukitoka sehemu ya juu ya jengo huku wazima moto wakiwabeba watu kuwapeleka maeneo salama.

    Rais Volodymyr Zelensky alitoa wito mpya kwa washirika wote wa kimataifa wa Ukraine kuiruhusu kulenga maeneo ndani ya Urusi ili kuzuia mashambulizi kama hayo.

    Ofisi yake ilisema kuwa vikosi vya Moscow vilirusha zaidi ya ndege 400 zisizo na rubani na makombora dhidi ya Ukraine katika muda wa wiki moja iliyopita.

  8. Marekani yalenga Islamic State nchini Iraq, 15 wauawa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imesema kuwa vikosi vyake vya kijeshi nchini Iraq vimewaua "wanachama" 15 wa Islamic State (IS) katika operesheni ya pamoja na Vikosi vya Usalama vya Iraq iliyolenga uongozi wa kundi hilo la wanamgambo.

    Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema imefanya operesheni hiyo ya pamoja magharibi mwa Iraq mapema Alhamisi.

    Wanajeshi wa Marekani na Iraq walikutana na wanachama wa IS wakiwa na "silaha nyingi, maguruneti na mikanda ya 'kujitoa mhanga'" ilisema katika taarifa.

    "Hakuna dalili ya vifo vya raia."

    Wakati huo huo vyombo vya habari vya Marekani vimewanukuu maafisa wa ulinzi wa Marekani wakisema kuwa wanajeshi saba wa Marekani wamejeruhiwa.

    Centcom haijatoa maoni yoyote kuhusu hili.

    Jeshi la Iraq lilisema katika taarifa yake ya awali kwamba "mashambulizi ya anga yalilenga maficho yao, ikifuatiwa na operesheni ya anga" katika eneo la "jangwa na mapango" nchini humo.

    "Maficho yote, silaha na vifaa vyao viliharibiwa, mikanda ya vilipuzi ililipuliwa kwa usalama na hati muhimu, karatasi za utambulisho na vifaa vya mawasiliano vilitwaliwa."

    Baraza la Usalama la Taifa hilo na Ikulu ya Marekani walielekeza BBC kwa Centcom kwa maoni.

    Centcom ilisema imelenga uongozi wa IS katika juhudi za "kuvuruga na kupunguza makali" uwezo wa kundi hilo katika kupanga na kushambulia Wamarekani, Wairaq na washirika ndani na nje ya eneo hilo.

    Kuna takriban wanajeshi 2,500 wa Marekani nchini Iraq kwa sasa, ingawa wamesalia huko kwa ajili ya "kushauri na kusaidia" tangu jeshi la Marekani lilipotangaza kumalizika kwa shughuli zake nchini humo mnamo Desemba 2021.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya kila siku ikiwa ni tarehe 31/08/2024