Rais wa kwanza wa Namibia afariki akiwa na umri wa miaka 95

Rais wa kwanza wa Namibia huru, Sam Nujoma, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 katika mji mkuu wa Windhoek, kiongozi wa sasa wa nchi hiyo ametangaza.

Muhtasari

  • 'Fedha za USAID hazitumiki ipaswavyo', asema Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani
  • Trump: 'Israel haitaishambulia Iran iwapo tutafikia makubaliano'
  • Bondia afariki wiki baada ya kushindwa katika pigano
  • Aukana uraia wa Ufaransa ili kugombea urais Ivory Coast
  • Zaidi ya watu 50 wameuawa katika shambulio la kuvizia Mali
  • Israeli yatarajiwa kujiondoa Netzarim huku Netanyahu akiapa kuiangamiza Hamas
  • Misri na Jordan zalaani kauli ya Israel ya kutaka kuazishwa taifa la Palestina huko Saudi Arabia
  • Rais wa kwanza wa Namibia afariki akiwa na umri wa miaka 95

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu na Rashid Abdalla

  1. 'Fedha za USAID hazitumiki ipaswavyo', asema Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty images

    Mshauri wa Usalama wa Taifa nchini Marekani Mike Waltz amezungumza na NBC News kufuatia tangazo la Rais Donald Trump la kukata ufadhili wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID).

    Serikali ya Marekani imetangaza kusitisha ufadhili wa miradi ya misaada kwa siku 90 huku ikifanya "mapitio" ili kuhakikisha ufadhili huo unawiana na vipaumbele vya Rais Trump - hatua ambayo imekosolewa na wataalamu wengi wa afya duniani.

    Waltz alisema kuwa "fedha hizo zinatolewa ili ziwafakie wanaohitaji usaidizi ", akiongeza kuwa "kati ya wakandarasi wakubwa, wakandarasi wadogo, na wakandarasi wa ndani, fedha hizo hazitumiki ipaswavyo".

    "Tunahitaji kuangalia kwa makini (USAID). Tunahitaji kupiga hatua haraka," alisema, akiongeza kuwa lengo lao ni "kurekebisha" na "kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatolewa kulingana na sera ya kigeni ya rais Trump.

  2. Habari za hivi punde, Trump: 'Israel haitaishambulia Iran iwapo tutafikia makubaliano'

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump aliliambia gazeti la New York Post kwamba angependa kufanya makubaliano na Iran na kwamba "tukifanya makubaliano, Israel haitawashambulia kwa mabomu.

    "Bw. Trump alisisitiza kwamba anataka makubaliano na "angependelea" kuliko kuishambulia Iran.

    Rais wa Marekani alisema hatataja mada za uwezekano wa mazungumzo na Iran: "Sipendi kuwaambia nitawaambia nini. Si jambo zuri."

    Bw. Trump alisema anatumai “wangeamua kutofanya kile wanachofikiria kufanya kwa sasa.

    Maneno haya ya Rais wa Marekani yanakuja wakati ambapo wasiwasi umeongezeka kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kuelekea katika uzalishaji wa silaha.

    Kiongozi wa Iran amekataa wazi mazungumzo na Marekani.

  3. Bondia aliyemshinda Mtanzania afariki wiki baada ya kushindwa katika pigano

    .

    Chanzo cha picha, BBC Sport

    Bondia wa uzani wa Super-feather John Cooney, 28, amefariki dunia baada ya kushindwa na Nathan Howells wa Wales mjini Belfast Jumamosi iliyopita.

    Bondia huyo wa Ireland alipatwa na tatizo la kutokwa na damu kwenye ubongo na kufanyiwa upasuaji wa kupunguza shinikizo kwenye ubongo wake kufuatia pambano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Ulster.

    Galway man Cooney alipimwa na timu ya madaktari kwenye ulingo kabla ya kutolewa nje kwa machela na kupelekwa katika Hospitali ya Royal Victoria huko Belfast.

    "Ni kwa huzuni kubwa kwamba tunapaswa kutangaza kwamba baada ya wiki moja ya kupigania maisha yake John Cooney ameaga dunia kwa huzuni," MHD Promotions ilisema kwa niaba ya familia ya Cooney.

    "Bw na Bibi Cooney na mchumba wake Emmaleen wangependa kuwashukuru wafanyikazi katika Hospitali ya Royal Victoria ya Belfast ambao wamefanya kazi bila kuchoka kuokoa maisha ya John na kwa kila mtu ambaye ametuma ujumbe wa msaada na sala.

    "Alikuwa mwana, kaka na mshirika anayependwa sana na itatuchukua maishani kusahau jinsi alivyokuwa wa pekee. RIP John 'The Kid' Cooney." Pambano hilo lilisitishwa katika raundi ya tisa ikiwa ni mara ya kwanza kwa Cooney kutetea taji lake la uzito wa juu wa Celtic.

    Bondia huyo wa Galway alishinda taji la Celtic kwa ushindi wa raundi ya kwanza dhidi ya Liam Gaynor mnamo Novemba 2023 kwenye uwanja wa 3Arena huko Dublin, kwa kadirio la ushindi wa kulipiza kisasi wa Katie Taylor dhidi ya Chantelle Cameron.

    Cooney kisha alitumia mwaka mmoja nje ya ulingo akiuguza jeraha la mkono kabla ya kurejea kwa kishindo na kumshinda Tampela Maharusi wa Tanzania Oktoba 2024 jijini London.

  4. Aukana uraia wa Ufaransa ili kugombea urais Ivory Coast

    c

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Tidjane Thiam, rais wa PDCI (Chama cha upinzani Cote d'Ivoire), akizungumza wakati wa mkutano huko Soubre, Ivory Coast, Juni 22, 2024.

    Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa benki ya Credit Suisse, Tidjane Thiam ameukana uraia wake wa Ufaransa ili kutimiza masharti ya kushiriki katika uchaguzi wa urais wa Ivory Coast mwezi Oktoba.

    Mwaka 2023, Thiam alichaguliwa kuwa kiongozi wa PDCI, moja ya vyama vikuu vya upinzani nchini Ivory Coast, na kumfanya kuwa mgombea wake.

    Katika video iliyowekwa kwenye mtandao wa Facebook siku ya Ijumaa, Thiam alisema amewasilisha ombi la kurudisha hati yake ya kusafiria ya Ufaransa, ili kubaki kuwa raia wa Ivory Coast pekee wakati wa uchaguzi.

    "Ninasisitiza upya ahadi yangu ya kufanya kazi kwa ajili ya mabadiliko ya kweli nchini Ivory Coast, ili hali ya maisha ya watu wa Ivory Coast iboreke. Hilo ndilo tunalopigania," alisema.

    Thiam, 62, aliwahi kuwa waziri nchini Ivory Coast chini ya Rais wa zamani Henri Konan Bedie. Aliondoka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi baada ya kuondolewa madarakani kwa Bedie katika mapinduzi ya kijeshi ya 1999 na kufanya kazi katika kampuni ya ushauri ya McKinsey, na kampuni ya bima ya Aviva and Prudential, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Credit Suisse mwaka 2015.

    Alirejea Ivory Coast na kuingia katika kinyang'anyiro cha uongozi cha chama cha PDCI - chama cha rais wa kwanza wa nchi hiyo, Felix Houphouet Boigny.

    Rais Alassane Ouattara, 83, ameashiria kuwa atagombea muhula wa nne, uamuzi ambao huenda ukakabiliwa na upinzani kutoka vyama vya upinzani, ambavyo vilipinga kugombea kwake muhula wa tatu mwaka 2020.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Zaidi ya watu 50 wameuawa katika shambulio la kuvizia Mali

    f

    Chanzo cha picha, HRW

    Zaidi ya watu 50 wameuawa karibu na mji wa kaskazini-mashariki mwa Mali wa Gao siku ya Ijumaa baada ya washambuliaji waliokuwa na silaha kuvizia msafara uliokuwa ukilindwa na jeshi lake, amesema afisa wa eneo hilo na wakaazi.

    Shambulio hilo lilitokea karibu na kijiji cha Kobe, karibu kilomita 30 (maili 19) kutoka Gao katika eneo ambalo makundi ya Islamic State na Al Qaeda yamekuwa yakifanya shughuli zao kwa zaidi ya muongo mmoja, na kuikosesha utulivu Mali na majirani zake Burkina Faso na Niger.

    "Watu waliruka kutoka kwenye magari ili kukimbia. Kulikuwa na raia wengi waliokufa na waliojeruhiwa," afisa wa eneo hilo alisema siku ya Jumamosi, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na wasiwasi wa usalama.

    Takribani miili 56 ilirikodiwa katika hospitali ya Gao, amesema afisa huyo, na kuongeza kuwa pia kulikuwa na idadi isiyojulikana ya wanajeshi majeruhi.

    Jeshi la Mali halijasema chochote hadi sasa.

    Mkazi wa Gao pia amesema karibu 50 waliuawa na magari kuchomwa. Mashambulizi mabaya yamekuwa ya mara kwa mara, na jeshi linalazimika kusindikiza magari ya raia karibu kila siku, amesema mkazi huyo.

    Uasi huo ulianza katika eneo kame la kaskazini mwa Mali kufuatia uasi wa watu wa Tuareg waliotaka kujitenga mwaka 2012. Wanamgambo hao wa Kiislamu wameenea katika nchi nyingine katika eneo maskini la Sahel kusini mwa Sahara.

    Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuchangia mgogoro wa kibinadamu ambapo zaidi ya watu milioni 3.2 wameyakimbia makazi yao kufikia Januari, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Wanajeshi wa Israel waondoka kwenye ukanda uliogawanya Gaza mara mbili huku Netanyahu akiapa kuiangamiza Hamas

    d

    Chanzo cha picha, Anadolu

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa "kuiangamiza" Hamas na kuwarudisha mateka wote baada ya duru ya tano ya mabadilishano ya wafungwa na mateka siku ya Jumamosi.

    "Tutawaangamiza (Hamas) na kuwarejesha mateka wetu," Netanyahu alisema katika taarifa yake ya video, akiwaelezea wanamgambo hao kama "wanyama" baada ya mateka watatu kuachiliwa huko Gaza mapema Jumamosi, wakionekana wamekonda na kulazimishwa kuzungumza jukwaani.

    Nao wafungwa 183 wa Kipalestina waliachiliwa, wakiwemo 72 wenye vifungo vya maisha na vifungo virefu na wafungwa 111 kutoka Gaza, waliachiwa huru siku ya Jumamosi.

    Shirika la habari la AFP likinukuu chanzo cha habari cha Hamas limeripoti kwamba kwa mujibu wa makubaliano ya kusitisha mapigano, "wapatanishi waliiarifu Hamas jana usiku kwamba vikosi vya Israel vitaanza kuondoka kwenye Barabara ya Salah al-Din siku ya Jumapili na kuondoa vizuizi vya kijeshi katika barabara hiyo na barabara itafunguliwa tena katika pande zote mbili kwa shughuli za raia na magari."

    Baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa, Israel iliruhusu magari kupita katika kituo cha ukaguzi cha kijeshi kwenye eneo la Netzarim kwenye Barabara ya Salah al-Din baada ya kupekuliwa na kusimamiwa na wanausalama kutoka kampuni mbili binafsi za Misri na Marekani.

    Gazeti la Israel la Haaretz pia limesema jeshi la Israel litaondoka kikamilifu "kwenye eneo lote la Netzarim, ambalo linaanzia mashariki mwa Ukanda wa Gaza hadi magharibi mwake."

  7. Misri na Jordan zalaani kauli ya Israel ya kutaka kuanzishwa taifa la Palestina huko Saudi Arabia

    tr

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na wanahabari baada ya mkutano na Spika wa Bunge la Marekani Mike Johnson, katika Ikulu ya Marekani, Februari 7, 2025.

    Matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwenye Channel 14, Alhamisi iliyopita kuhusu kuanzishwa kwa taifa la Palestina nchini Saudi Arabia imekataliwa na watu wengi za katika ulimwengu wa Kiarabu, hasa Jordan na Misri.

    "Wasaudi wana uwezo wa kuanzisha taifa la Palestina nchini Saudi Arabia, wanamiliki ardhi kubwa huko," Netanyahu alinukuliwa na gazeti la Jerusalem Post.

    Kwa mujibu wa gazeti hilo, Netanyahu alijibu swali kuhusu sharti la Saudi Arabia la kuwa na uhusiano na Israel, ni lazima kuundwe taifa la Palestina, akisema "hatafikia makubaliano ambayo yatahatarisha usalama wa taifa la Israel."

    Kauli ya Netanyahu inakuja baada ya kauli ya Rais Donald Trump wa Marekani wakati wa mkutano wake mjini Washington, ambapo rais huyo alipendekeza kuwahamishia wakazi wa Gaza hadi Misri na Jordan na Gaza kuchukuliwa na Marekani, jambo ambalo nchi hizo mbili (Misri na Jordan) zimelikataa vikali.

    Wizara ya Mambo ya nje ya Jordan imelaani matamshi ya Netanyahu katika taarifa yake iliyotolewa Jumapili, Februari 9, 2025, ikielezea matamshi ya Israel ya kutaka kuanzishwa taifa la Palestina nchini Saudi Arabia kama "wito wa uchokozi."

    Msemaji wa wizara hiyo, Sufyan Al-Qudah, alisema "serikali ya Israel inaendelea na sera zake za uchochezi na matamshi ambayo yanakiuka sheria za kimataifa.”

    Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ililaani siku ya Jumamosi matamshi ya Israel kuhusu kuanzisha taifa la Palestina katika ardhi ya Saudia, ikiyataja kuwa “ya kutojali."

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema katika taarifa yake "kauli ya Israel dhidi ya Ufalme wa Saudi Arabia ni uvunjaji wa sheria na ukiukaji wa kanuni zote za kidiplomasia."

    Wizara hiyo imesisitiza katika taarifa yake kwamba "usalama wa Ufalme wa Saudi Arabia na mamlaka yake ni mstari mwekundu ambao Misri haitaruhusu kukiukwa.

    Pia unaweza kusoma:

  8. .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rasi wa zamani wa Namibia San Nujoma aanga dunia

    Rais wa kwanza wa Namibia huru, Sam Nujoma, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 katika mji mkuu wa Windhoek, kiongozi wa sasa wa nchi hiyo ametangaza.

    Nujoma aliongoza vita vya muda mrefu vya kudai uhuru kutoka kwa Afrika Kusini mwaka 1990 baada ya kusaidia kupatikana kwa vuguvugu la ukombozi la Namibia lililojulikana kama South West Peoples' Organization (Swapo) miaka ya 1960.

    Baada ya uhuru, Nujoma alikua rais mwaka 1990 na aliongoza nchi hadi 2005.

    Nujoma alikuwa amelazwa hospitalini kwa muda wa wiki tatu zilizopita kutokana na ugonjwa ambao "hakuweza kupona", Rais wa Namibia Nangolo Mbumba alisema katika taarifa yake akitangaza kifo hicho kwa "huzuni na masikitiko makubwa".

    Aliongeza: "Baba yetu mwanzilishi aliishi maisha marefu na yenye matokeo ambayo alitumikia kipekee watu wa nchi yake anayoipenda."

    Nujoma alistaafu kama mkuu wa nchi mwaka 2005, lakini aliendelea kukiongoza chama hicho kabla ya kung'atuka mwaka 2007 kama rais wa chama tawala cha Swapo baada ya kukiongoza kwa miaka 47.

  9. Natumai hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja