Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Marekani yaituhumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa 2024

Marekani imewashtaki na kuwawekea vikwazo wasimamizi wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi na kuwawekea vikwazo watangazaji wanaohusishwa na Kremlin huku ikiishutumu Moscow kwa kampeni iliyoenea ya kuingilia uchaguzi wa rais.

Muhtasari

  • Ufaransa: Mwanamke aelezea alivyopewa dawa za kulevya na kubakwa
  • Mkurugenzi wa zamani jela kwa mauaji ya kimbari Rwanda
  • Mtu mwenye silaha auawa kwa kupigwa risasi karibu na ubalozi mdogo wa Israel
  • Michel Barnier ateuliwa na Macron kama Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa
  • Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC atetea kibali cha kukamatwa kwa Netanyahu
  • Nimempoteza mlezi, babake Cheptegei asema kuhusu kifo cha mwanae
  • Papa na imamu mkuu wa Indonesia watoa wito wa pamoja wa amani
  • Putin: Urusi "inawaondoa polepole" wanajeshi wa Ukraine kutoka eneo la Kursk
  • Mwanariadha wa Uganda, Rebecca Cheptegei afariki dunia baada ya kuchomwa moto
  • Mhandisi feki ahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela Afrika Kusini
  • Uingereza yatetea uamuzi wa vikwazo vya sehemu ya silaha kwa Israel
  • Binti wa Zuma kuolewa na mfalme Mswati 'kwa mapenzi'
  • Majeshi ya Israel hayataondoka katika mpaka Misri na Gaza
  • Marekani yaituhumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa 2024

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Ufaransa: Mwanamke aelezea alivyopewa dawa za kulevya na kubakwa

    Onyo: Simulizi hii ina maelezo ya kuhuzunisha tangu mwanzo.

    Mwanamke mmoja Mfaransa ambaye alibakwa na wanaume wasiojulikana zaidi ya miaka kumi baada ya kuwekewa dawa za kulevya na mumewe ili alale, alielezea mahakama siku ya Alhamisi unyanyasaji aliopitia.

    Gisèle Pélicot, mwenye umri wa miaka 72, alikuwa akitoa ushahidi siku ya tatu ya kesi hiyo huko Avignon, kusini-mashariki mwa Ufaransa, ya wanaume 51 - ikiwa ni pamoja na mume wake wa miaka 50, Dominique. Wote wanatuhumiwa kwa ubakaji.

    Nyaraka mbele ya mahakama zinaonyesha kuwa Dominique Pélicot, 71, alikiri kwa polisi kwamba alikuwa akiridhika kwa kutazama wanaume wengine wakifanya mapenzi na mke wake aliyepoteza fahamu.

    Washtakiwa wengi katika kesi hiyo wanapinga shtaka la ubakaji dhidi yao, wakidai kuwa walidhani walikuwa wakishiriki mchezo wa ngono wa kukubaliana.

    Hii ni kesi ambayo imeshtua Ufaransa, cha kushangaza zaidi ni kwamba kesi hiyo inasikilizwa hadharani.

    Akikumbuka kilichotokea mnamo mwezi Novemba 2020 alipoulizwa na polisi kufika kwenye mahojiano pamoja na mumewe, alisema.

    "Afisa wa polisi aliniuliza kuhusu maisha yangu ya ngono," aliambia mahakama. “Nilimwambia sijawahi kufanya mapenzi ya kubadilishana wenzi au watu watatu. Nikasema mimi ni mwanamke ambaye siwezi kumruhusu mwingine yeyote aniguse zaidi ya mume wangu.

    "Lakini baada ya saa moja ofisa alisema, 'Nitakuonyesha baadhi ya mambo ambayo hutafurahia. Alifungua faili na kunionyesha picha.

    “Sikumtambua yule mwanamume au mwanamke aliyelala kitandani. Ofisa huyo akaniuliza: 'Bibi, hiki ni kitanda chako na meza yako ya pembeni?'

    “Ilikuwa vigumu kujitambua nikiwa nimevalia kwa namna nisiyoijua. Kisha akanionyesha picha ya pili na ya tatu.

    “Nilimwomba aache kunionyesha. Sikuweza kuvumilia. Nilikuwa sijielewi kabisa kitandani kwangu, na mtu alikuwa akinibaka. Moyo wangu ulivunjika."

    “Yote tuliyokuwa tumefanya pamoja, yakapotea tu hivyo. Watoto wetu watatu, wajukuu saba. Tulikuwa wanandoa wa kupigiwa mfano.

  3. Mkurugenzi wa zamani jela kwa mauaji ya kimbari Rwanda

    Mahakama moja nchini Rwanda inayoshughulikia kesi za uhalifu wa mauaji ya kimbari imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela mkurugenzi wa zamani wa taasisi ya kilimo Venant Rutunga kwa kumkuta na hatia ya kuwa mshirika katika mauaji dhidi ya watutsi mwaka 1994.

    Rutunga alirejeshwa nchini Rwanda mwaka 2021 na mamlaka ya Uholanzi ili kujibu mashitaka ya mauaji ya kimbari ambayo anakanusha.

    Mahakama imesema kwamba wakati wa mauaji ya kimbari aliomba msaada wa wanajeshi waliotumwa kushika doria kwenye ofisi za taasisi hiyo na baadae wakafanya mauaji ya watutsi zaidi ya elfu 1 waliokuwa wamejificha eneo hilo na mengine jirani.

    Awali Katika vikao vya kesihiyo Venant Rutunga alisema yeye alileta wanajeshi hao kwa nia njema ya kulinda taasisi hiyo na kwamba kamwe hawezi kuwajibishwa kutokana na mauaji yaliyotekelezwa na wanajeshi hao.

    Leo mahakama imesema Daktari Rutunga hakumuua mtu yeyote kwa kutumia silaha lakini jukumu lake kubwa ni kuwaleta wanajeshi hao licha ya kufahamu kuwa wanakuja kutekeleza mauaji ya kimbari.

    Mahakama imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela.

    Jaji amesema angepewa kifungo cha maisha jela lakini kwamba mahakama imeamua kumpunguzia hukumu kutokana na mwenendo wake wakati wa kesi.

    Ana siku 30 za kukata rufaa na wakili wake Sebaziga Sophonie ameiambia BBC ‘’tuna siku 30 za kutafakari uwezekano na njia za kukata rufaa’’

    Soma zaidi:

  4. Mtu mwenye silaha auawa kwa kupigwa risasi karibu na ubalozi mdogo wa Israel

    Mwanaume mwenye silaha ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Ujerumani karibu na kituo cha Nazi na ubalozi mdogo wa Israel katika mji wa kusini wa Munich.

    Mwanamume huyo, aliyetambuliwa na polisi kama raia wa Austria mwenye umri wa miaka 18, aliuawa wakati wa kurushiana risasi na maafisa.

    Polisi walisema mwanamume mmoja alikuwa ameonekana katika eneo hilo akiwa amebeba bunduki ndefu.

    Ubalozi mdogo wa Israel ulikuwa umefungwa wakati huo kwa ajili ya ibada ya kumbukumbu ya miaka 52 ya shambulio la wanamgambo wa Kipalestina katika Michezo ya Olimpiki ya Munich mwaka 1972, ambapo wanariadha 11 wa Israel na afisa wa polisi waliuawa.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bavaria Joachim Herrmann alisema nia ya tukio hilo haikubanishwa mara moja lakini huenda lilihusishwa na maadhimisho hayo.

    Aliongeza kuwa "inawezekana" mtu mwenye silaha alikuwa amepanga kushambulia "taasisi ya Israeli".

    Polisi walisema hakukuwa na dalili zozote za washukiwa wengine katika tukio hilo la Alhamisi.

    Mkuu wa polisi wa Munich Thomas Hampel alisema mtu huyo alikuwa amejihami kwa bunduki ya zamani ya kuwinda.

    Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti kwamba awali alikuwa anajulikana na vyombo vya usalama kwa tuhuma za kuunga mkono makundi ya Kiislamu yenye vurugu, lakini polisi walikataa kuzungumzia ripoti hizo.

    Helikopta ya polisi ilizunguka eneo hilo na umma kutakiwa kutoweka picha za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii.

    Soma zaidi:

  5. Michel Barnier ateuliwa na Macron kama Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemteua Michel Barnier kama waziri mkuu karibu miezi miwili baada ya uchaguzi wa mapema Ufaransa kumalizika kwa mkwamo wa kisiasa.

    Bw Barnier, 73, ndiye mpatanishi mkuu wa zamani wa Umoja wa Ulaya wa Brexit na aliongoza mazungumzo na serikali ya Uingereza kati ya 2016 na 2019.

    Mwanasiasa huyo mzoefu wa chama cha mrengo wa kulia cha Republicans, amekuwa katika kisiasa kwa muda mrefu na kushikilia nyadhifa mbalimbali za juu, nchini Ufaransa na ndani ya EU.

    Sasa atalazimika kuunda serikali ambayo itaepusha Bunge la Kitaifa kugawanyika katika kambi tatu kubwa za kisiasa, zisizo na uwezo wa kuunda wingi wa moja kwa moja.

    Miaka mitatu iliyopita Bw Barnier alisema anataka kupambana na Rais Macron kuwa rais wa Ufaransa, akisema anataka kuweka kikomo na kudhibiti uhamiaji.

    Lakini alishindwa kuchaguliwa kuwa mgombea na chama chake.

    Bw Barnier anatazamiwa kuchukua nafasi ya Gabriel Attal, waziri mkuu mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuchaguliwa nchini Ufaransa, ambaye Rais Macron alimteua kwa mara ya kwanza kuwa waziri mkuu mapema mwaka 2024 na ambaye amekaa katika wadhifa wake kama kaimu tangu Julai.

    Uchaguzi wa Bw Macron wa waziri mkuu tayari umesababisha kutoridhika ndani ya chama cha mrengo wa kushoto cha New Popular Front (NFP), ambacho kilishinda viti vingi zaidi katika uchaguzi wa mapema wa Julai.

  6. Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC atetea kibali cha kukamatwa kwa Netanyahu

    Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ameambia BBC kwamba haki lazima itendeke baada ya kutafuta kibali cha kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo.

    Karim Khan alisema ni muhimu kuonyesha kwamba mahakama itashikilia mataifa yote kwa kiwango sawa kuhusiana na madai ya uhalifu wa kivita. Pia alifurahishwa na uamuzi wa serikali mpya ya Uingereza wa kuacha kupinga kutolewa kwa hati za kukamatwa kwake.

    "Kuna mabadiliko na ninafikiria ni ya muhimu kuhusiana na sheria ya kimataifa na serikali mpya. Na nadhani hilo linakaribishwa,” Bw Khan aliambia mwandishi wa BBC Nick Robinson.

    Pia ametoa vibali kwa viongozi watatu wa Hamas, wawili kati yao wakiwa wameuawa.

    Katika mahojiano mapana, alielezea kuwa ICC ilihitaji kuomba vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa pande zote mbili ili kuhakikisha watu duniani kote wanaona kuwa mahakama ilikuwa inatumia "sheria kwa usawa kulingana na viwango fulani vya kawaida".

    "Huwezi kuwa na mtazamo mmoja kwa nchi ambako kuna uungwaji mkono, iwe ni uungaji mkono wa Nato, Ulaya [na] nchi zenye nguvu nyuma yako, na mtazamo tofauti ambapo una mamlaka ya wazi," aliongeza.

    Soma zaidi:

  7. Nimempoteza mlezi, babake Cheptegei asema kuhusu kifo cha mwanae

    Mzee Joseph Cheptegei, babake marehemu mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei ameelezea masikitiko makubwa kwa kumpoteza binti yake huku akitaka haki itendeke.

    Cheptegei ambaye alikuwa akihutubia wanahabari katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret muda mfupi baada ya kupokea habari hizo alisema kuwa familia hiyo sio tu imempoteza binti mpendwa bali pia mlezi.

    "Nimepoteza binti ambaye amekuwa akisaidia kwa njia nyingi," alisema.

    Akitaja kifo hicho kuwa kichungu kwake, Cheptegei aliyeonekana kufadhaika alisema kama familia wamekuwa wakimtegemea, haswa katika kusaidia elimu ya wadogo zake.

    "Tuna watoto katika shule za sekondari na sijui ni jinsi gani tutakabiliana na changamoto hii ili kuhakikisha wanamaliza masomo yao," aliongeza.

    Pia alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kuharakisha uchunguzi na kuhakikisha mhalifu wa kitendo hicho cha kinyama anakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

    Ni lazima tukabiliane na ukatili wa kijinsia! Waziri wa michezo Kenya

    Wakati huo huo, waziri wa michezo nchini Kenya, Kipchumba Murkomen amemuomboleza mshikilizi wa Rekodi ya Wanawake Marathon Rebecca Cheptegei, akisema kifo chake ni hasara kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki.

    Murkomen katika taarifa aliotoa siku ya Alhamisi alisema kifo chake ni ukumbusho kwamba juhudi zaidi zinafaa kuwekwa ili kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

    Marehemu Cheptegei anasemekana alipata asilimia 80 ya majeraha ya moto baada ya anayedaiwa kuwa mpenzi wake kumwagia mafuta ya petroli mwilini mwake na kumchoma moto.

    Kuchomoka huko kuliharibu viungo vyake vingi vya mwili.

    Cheptegei aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi mjini Eldoret.

    Aliendelea kusema kuwa serikali ya Kenya imejitolea haki inatendeka kwa Rebecca.

    Cheptegei alikuwa na umri wa miaka 33 na amekuwa mwanariadha kwa zaidi ya miaka 15.

    Soma zaidi:

  8. Papa na imamu mkuu wa Indonesia watoa wito wa pamoja wa amani

    Papa Francis ameonya dhidi ya kutumia dini kuchochea migogoro katika siku yake ya mwisho ya ziara yake nchini Indonesia, sehemu ya kwanza aliofika katika ziara yake ya kuzunguka eneo la Asia Pacific.

    Katika msikiti wa Istiqlal katika mji mkuu wa Jakarta, Papa alitia saini tamko kuhusu maelewano ya kidini na ulinzi wa mazingira na imamu mkuu wa msikiti huo na kukutana na viongozi wa eneo hilo wa dini sita.

    Mzee huyo mwenye umri wa miaka 87 mapema Jumanne alianza ziara ya siku 11 katika eneo hilo, safari ndefu zaidi nje ya nchi kama papa.

    Baada ya kusherehekea misa mbele ya umati wa watu 80,000 unaotarajiwa katika uwanja mkuu wa kandanda wa Indonesia baadaye siku hiyo, atakwenda Papua New Guinea, Timor Leste na Singapore.

    Akizungumza katika msikiti huo - ambao ni mkubwa zaidi Kusini Mashariki mwa Asia - Siku ya Alhamisi, Papa alisema watu kutoka dini tofauti walipaswa kujua "sisi sote ni ndugu, wote ni mahujaji, sote tuko njiani kuelekea kwa Mungu, zaidi ya kile kinachotutofautisha".

    Ubinadamu unakabiliwa na "mgogoro mkubwa" unaoletwa na vita, migogoro na uharibifu wa mazingira, aliongeza.

    Indonesia ndiyo nchi yenye Waislamu wengi zaidi duniani na asilimia 3 tu ya milioni 275 ndio Wakatoliki.

    Indonesia ina dini sita zinazotambulika rasmi -- Uislamu, Uprotestanti, Ukatoliki, Ubudha, Uhindu, na Ukonfusimu.

  9. Habari za hivi punde, Putin: Urusi "inawaondoa polepole" wanajeshi wa Ukraine kutoka eneo la Kursk

    Wanajeshi wa Urusi wameongeza mashambulizi yao huko Donbass kutokana na mashambulizi ya Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk, Rais Vladimir Putin anasema mwezi mmoja baada ya uvamizi wa Ukraine dhidi ya Urusi kuanza.

    "Lengo la adui lilikuwa kutufanya tuwe na wasiwasi, kuzozana na kuhamisha wanajeshi kutoka eneo moja hadi jingine," Putin alisema, akizungumza katika Kongamano la Uchumi la Mashariki huko Vladivostok.

    Kulingana na yeye, Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine vilitarajia kuzuia shambulio huko Donbass, lakini "adui alishindwa.

    "Putin anadai kuwa mwezi mmoja baada ya kuanza kwa uvamizi huo, wanajeshi wa Urusi "walituliza hali" katika mkoa wa Kursk na kuanza "kusukuma polepole" Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine kutoka kwa ardhi ya Urusi.

  10. Mwanariadha wa Uganda, Rebecca Cheptegei afariki dunia baada ya kuchomwa moto Kenya

    Mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei amefariki Alhamisi alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali moja mjini Eldoret nchini Kenya kutokana na kushindwa kwa viungo vya mwili, Mkurugenzi wa Huduma za Kliniki katika kituo hicho Owen Menach amethibitisha.

    Cheptegei ambaye alishiriki katika Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu alidaiwa kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake wa zamani mjini Kitale Jumapili, na kusababisha mwili wake kuungua kwa asilimia 80 na hatimaye kufariki.

    Shirikisho la Riadha la Uganda (UAF) pia limethibitisha kuaga dunia kwa Cheptegei katika chapisho kwenye akaunti yao rasmi ya X, na kutaka haki itendeke likisema "aliangukiwa na vurugu za nyumbani."

    "Tuna masikitiko makubwa kutangaza kifo cha mwanariadha wetu Rebecca Cheptegei mapema leo asubuhi, ambaye alihusika na dhuluma za nyumbani.

    Kama shirikisho, tunalaani vitendo hivyo na tunaomba haki itendeke.

    Roho yake ipumzike kwa amani," lilisomeka chapisho hilo la wanariadha wa Uganda.

  11. Mhandisi feki ahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela Afrika Kusini

    Mwanaume mmoja ambaye alikuwa mhandisi mkuu katika kampuni ya reli ya abiria inayomilikiwa na serikali ya Afrika Kusini amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kughushi sifa zake.

    Mara baada ya kusifiwa kwa kazi yake ya mafanikio, Daniel Mthimkhulu alikuwa mkuu wa uhandisi katika Shirika la Reli la Abiria la Afrika Kusini (Prasa) kwa miaka mitano, akipata mshahara wa mwaka wa takribani rand 2.8m ($156,000; £119,000).

    Kwenye CV yake, mtu huyo mwenye umri wa miaka 49 alidai kuwa na sifa kadhaa za uhandisi wa mitambo, ikiwa ni pamoja na shahada kutoka Chuo Kikuu cha Witwatersrand kinachoheshimika nchini Afrika Kusini pamoja na udaktari kutoka chuo kikuu cha Ujerumani.

    Hata hivyo, mahakama ya Johannesburg ilielezwa kwamba alikuwa amemaliza tu elimu yake ya sekondari.

    Mthimkhulu alikamatwa Julai 2015 muda mfupi baada ya mtandao wake wa uwongo kuanza kusambaratika.

    Alikuwa ameanza kufanya kazi katika Prasa miaka 15 mapema, akipanda cheo na kuwa mhandisi mkuu, kutokana na sifa zake za kuhitimu.

    Mahakama pia ilielezwa jinsi alivyoghushi barua ya ofa ya kazi kutoka kwa kampuni ya Ujerumani, ambayo ilihimiza Prasa kuongeza mshahara wake ili shirika hilo lisimpoteze.

    Pia alikuwa mstari wa mbele katika mpango wa rand 600m kununua makumi ya treni mpya kutoka Uhispania, lakini hazikuweza kutumika Afrika Kusini kwani zilikuwa nyingi sana.

    "Mahakama ilizingatia uzito na kuenea kwa udanganyifu, hasara kubwa ya kifedha kwa Prasa na usaliti wa Mthimkhulu kwa uaminifu wa mwajiri wake," Bi Mjonondwane alisema. Katika mahojiano ya 2019 na mtangazaji wa ndani wa eNCA, Mthimkhulu alikiri kwamba hakuwa na Shahada ya Uzamivu.

  12. Uingereza yatetea uamuzi wa vikwazo vya sehemu ya silaha kwa Israel

    Uingereza imetetea uamuzi wake wa kusitisha baadhi ya mauzo ya silaha kwa Israel, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiutaja uamuzi huo kuwa wa "aibu".

    Netanyahu alisema kwenye mtandao wa kijamii kwamba uamuzi huo "utawapa ujasiri Hamas." Lakini Husam Zomlot, balozi wa Palestina nchini Uingereza, alielezea marufuku hiyo ya sehemu kama "hatua muhimu ya kwanza kuelekea Uingereza kutimiza majukumu yake ya kisheria chini ya sheria za Uingereza na kimataifa".

    Siku ya Jumatatu, Uingereza ilisitisha leseni zipatazo 30 kati ya 350 za kuuza silaha kwa Israel.

    Waziri wa Ulinzi wa Uingereza John Healey alisisitiza kuwa Uingereza itasalia kuwa "mshirika mkubwa" wa Israel, akiiambia BBC kwamba usalama wa Israel hautayumbishwa na uamuzi huo.

    Mawaziri wa serikali wanasema silaha hizo zinaweza kutumika Gaza kukiuka sheria za kimataifa.

    Amnesty International ya Uingereza ilisema hatua hizo ni "finyu sana".

    Wengine wamekosoa muda wa kutangazwa kwa mpango huo, ambao uliambatana na siku ya mazishi ya mateka sita waliouawa huko Gaza wiki iliyopita.

    "Ilikuwa uchungu sana kuona nyuso za mateka waliokufa," Healy aliiambia BBC, lakini akaongeza kuwa muda wa uamuzi "ulisukumwa na ukweli kwamba huu ni mchakato wa kisheria" huku kukiwa na hitaji la kuarifu bunge.

    Unaweza kusoma;

  13. Binti wa Zuma kuolewa na mfalme Mswati 'kwa mapenzi'

    Binti mwenye umri wa miaka 21 wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma anaolewa na mfalme wa Eswatini , msemaji wa utawala wa mwisho kabisa wa kifalme barani Afrika ameiambia BBC.

    Uchumba wa Nomcebo Zuma na Mfalme Mswati wa Tatu ulifanyika rasmi mapema wiki hii mwishoni mwa sherehe ya siku nane ya densi ya mwanzi, ibada ya kitamaduni ya wasichana inayofanyika kila mwaka.

    Mfalme huyo mwenye umri wa miaka 56 kwa sasa yuko katika mpango wa mitala na wake 11 na ameoa mara 15 kwa jumla.

    Msemaji wa Eswatini Alpheous Nxumalo alipuuzilia mbali pendekezo kwamba ndoa hiyo itakuwa muungano wa kisiasa.

    Bw Zuma, ambaye alikuwa rais wa Afrika Kusini kuanzia 2009 hadi 2018, na Mfalme Mswati tayari ni jamaa kupitia ndoa.

    Wakosoaji wanamtuhumu Mfalme Mswati, ambaye anatawala kwa amri na amekuwa kwenye kiti cha enzi kwa miaka 38, kwa kuishi maisha ya anasa na nyumba yake yenye wake wengi, huku wengi wa watu wake wakitaabika katika umaskini.

    Eswatini, ambayo hapo awali ilijulikana kama Swaziland, ina wakazi milioni 1.1 na mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya VVU.

  14. Majeshi ya Israel hayataondoka katika mpaka Misri na Gaza

    Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesisitiza tena kwamba majeshi ya Israel hayataondoka kwenye Ukanda wa Philadelphi, ukanda muhimu wa kimkakati kusini mwa Gaza kwenye mpaka na Misri.

    Aliviambia vyombo vya habari vya kigeni mjini Jerusalem kwamba yuko "wazi" kufikiria njia mbadala za kuwepo kwa wanajeshi wa Israel kwenye mpaka wa Gaza na Misri, kama sehemu ya makubaliano yoyote ya siku za usoni ya kusitisha mapigano, lakini hakuona hilo likifanyika.

    Bw.Netanyahu alidai kwamba wanajeshi wa Israel lazima wabaki ili kuzuia silaha na ikiwezekana mateka wa Israel kupitishwa kinyemela kuvuka mpaka.

    Hamas ilisema katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters kwamba uamuzi wa Bw Netanyahu kutojiondoa katika ukanda wa Philadelphi ni jaribio la kukwamisha makubaliano ya kusitisha mapigano, na kuongeza kuwa ni wakati wa kuweka shinikizo kwa Israel.

    Unaweza kusoma;

  15. Marekani yaituhumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa 2024

    Marekani imewashtaki na kuwawekea vikwazo wasimamizi wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi na kuwawekea vikwazo watangazaji wanaohusishwa na Kremlin huku ikiishutumu Moscow kwa kampeni iliyoenea ya kuingilia uchaguzi wa rais.

    Wizara ya sheria, serikali na hazina ilitangaza hatua zilizoratibiwa Jumatano "kukabiliana vikali" na shughuli zinazodaiwa.

    Mwanasheria Mkuu Merrick Garland alishutumu shirika la utangazaji la RT, la Urusi, kwa kuilipa kampuni ya Tennessee $10m "kuunda na kusambaza maudhui kwa watazamaji wa Marekani kwa ujumbe fiche wa serikali ya Urusi".

    Mkuu wa RT Margarita Simonyan alikuwa mmoja wa watu 10 walioidhinishwa kwa madai ya kujaribu kuharibu "imani ya umma kwa taasisi zetu". RT ilikanusha kuhusika.

    Bw. Garland alisema kuwa Moscow ilitaka kupata "matokeo" katika kinyang'anyiro kati ya Donald Trump na Kamala Harris.

    Msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby alisema kuwa mpango huo wa Urusi unalenga "kupunguza uungwaji mkono wa kimataifa kwa Ukraine, kuimarisha sera na maslahi yanayoiunga mkono Urusi, na kuathiri wapiga kura hapa Marekani".

    Afisa wa Hazina wakati huo huo alisema kuwa RT na vyombo vingine vya habari vya serikali ya Urusi vilijihusisha na "kampeni mbaya ya kuajiri kwa siri washawishi wa Marekani bila kujua kuunga mkono shughuli zao mbaya".

    Unaweza kusoma;

  16. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu