Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Prof. Janabi achaguliwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika

Duru mpya ya mazungumzo imefanyika huko Doha baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga yaliouwa mamia ya watu.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Prof. Janabi achaguliwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika

    Humphrey Mgonja

    Mshauri wa Rais wa Masuala ya Tiba nchini Tanzania na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika katika uchaguzi uliofanyika leo, Mei 18, 2025, jijini Geneva, Uswisi.

    Prof. Janabi alikuwa mgombea pekee kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, akiwania nafasi hiyo dhidi ya wagombea wanne kutoka Afrika Magharibi. Wagombea hao ni Dkt. N’da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, Dkt. Dramé Mohammed Lamine (Guinea), Dkt. Boureima Hama Sambo (Niger), na Prof. Mijiyawa Moustafa kutoka Togo.

    Katika kampeni yake ya kuwania nafasi hiyo, Prof. Janabi aliwasilisha vipaumbele saba mbele ya Mawaziri wa Afya wa nchi wanachama wa WHO barani Afrika, akisisitiza umuhimu wa maboresho ya huduma za afya, upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya kugharamia huduma bora, na maandalizi ya kukabiliana na majanga na dharura za kiafya.

    Uchaguzi huo umefanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule, Dkt. Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.

    Soma zaidi:

  3. Hospitali zote kaskazini mwa Gaza zimefungwa - wizara ya afya

    Hospitali zote tatu za umma kaskazini mwa Gaza "zimefungwa", wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas imesema, huku Israel ikiendelea na mashambulizi yake ya kunyakua maeneo ya eneo hilo.

    Wizara hiyo ilisema Jumapili kwamba vikosi vya Israel vilizingira hospitali ya Indonesia huko Beit Lahia, "kwa silaha nzito... na kuzuia kuwasili kwa wagonjwa, wafanyikazi wa matibabu, na vifaa".

    Hospitali hiyo ilikuwa ya mwisho kaskazini kufanya kazi, ilisema.

    Jeshi la Israel siku ya Jumamosi lilitangaza kuzindua "Operesheni ya Gideon's Chariot", huku kukiwa na wimbi baya zaidi la mashambulizi huko Gaza katika kipindi cha miezi kadhaa.

    Hamas ilijitolea kuwaachilia mateka tisa kwa kubadilishana na mapatano ya siku 60 ya kusitisha vita na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina, afisa wa Palestina aliiambia BBC baada ya mazungumzo mapya kufanyika Jumamosi.

    Wizara ya afya ilisema Jumapili: "Baada ya kuharibiwa kwa Hospitali ya Beit Hanoun na Hospitali ya Kamal Adwan, na Hospitali ya Indonesia kusitisha huduma, hospitali zote za umma kaskazini mwa Ukanda wa Gaza sasa zimefungwa."

    Soma zaidi:

  4. Papa akemea unyanyasaji wa maskini na utawala wa kibabe katika Misa ya kutawazwa

    Papa Leo XIV ametawazwa na kuchukua rasmi majukumu yake ya upapa.

    Akitoa hotuba yake, Papa aliweka vipaumbele vyake kwa upapa siku ya Jumapili, akikosoa unyanyasaji wa maskini na utawala wa kibabe wakati wa mahubiri kwa umati wa maelfu wakiwemo watu mashuhuri duniani.

    Akizungumza katika uwanja wa St Peter's Square, Papa alitumia Misa yake kuangazia vipaumbele vya mtangulizi wake, Francis.

    Alikosoa "chuki, vurugu, hofu ya utofauti na mtazamo wa kiuchumi ambao unatumia rasilimali za Dunia na kuwatenga maskini zaidi," alisema.

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walikuwa miongoni mwa waliohudhuria.

    Vatican ilisema baadaye Papa atakutana na Zelensky kwa faragha ili kujadili vita nchini Ukraine.

    Papa alisema alitaka kuona kanisa lenye umoja zaidi, na kwamba watu hawapaswi kujifungia katika vikundi vidogo na au kujiona bora zaidi ulimwenguni.

    "Ninakuja kwenu kama kaka," alisema.

    Katika mahubiri yake, papa wa 267 papa alisema atatafuta kutawala "bila kuingia katika majaribu ya kuwa mbabe".

    Maelfu ya mahujaji walijaa uwanjani hapo na kusimama kwa heshima huku papa akipokea ishara za ofisi, kuwabariki watu na kutoa mwito mkali wa umoja.

    Papa alipewa pete ya mvuvi na kadinali. Pete hii maalum ni ishara ya jukumu lake, na ni utamaduni wa tangu enzi za Mtakatifu Petro, ambaye alikuwa mvuvi.

    Soma zaidi:

  5. Wakili Martha Karua na wenzake wazuiwa kuingia Tanzania

    Na Humphrey Mgonja,

    Kupitia mitandao ya kijamii, wakili na kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party nchini Kenya, Martha Karua, mapema leo alichapisha kipande cha video akieleza kuwa yeye pamoja na wanaharakati wawili wa haki za binadamu — Gloria Kimani na Lynn Ngugi — walizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuwasili wakitokea Kenya.

    Wanaharakati hao walikuwa wamealikwa nchini Tanzania na Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki, ambapo walitarajiwa kuhudhuria kesi itakayosikilizwa kesho dhidi ya mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

    Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kupitia ujumbe aliouandika, amelaani kitendo cha wanaharakati hao kuzuiwa, akidai kuwa ni juhudi za kuficha aibu ya kesi ya uongo inayomkabili kiongozi wao, ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi ya uhaini, kufuatia mahakama kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa kwa mfumo wa mahakama ya wazi.

    Aidha, taarifa iliyotolewa na Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) imesema kuwa tayari wameshatuma wakili wao kutoa msaada wa kisheria, huku wakisisitiza kuwa waliokamatwa waachiwe mara moja.

    Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote rasmi kueleza sababu za kuwazuia wanaharakati hao.

  6. Mlipuko mbaya karibu na kliniki ya uzazi ni 'kitendo cha ugaidi' - FBI

    Mlipuko wa bomu nje ya kliniki ya uzazi ya California imeua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wanne katika "kitendo cha kukusudia cha kigaidi", maafisa wa FBI wamesema.

    Mlipuko huo ulitokea kabla ya 11:00 saa za eneo chini ya maili moja kutoka katikati mwa jiji la Palm Springs, karibu na biashara kadhaa ikiwa ni pamoja na Vituo vya Uzazi vya Marekani (ARC). Kliniki hiyo ilisema hakuna mtu kutoka kituo hicho aliyejeruhiwa.

    FBI baadaye ilisema ilikuwa na "mtu mmoja" anayefuatiliwa katika uchunguzi wake, lakini maafisa "hawakuwa wakimsaka" mshukiwa.

    Michael Beaumier, shahidi, alisema aliangushwa na baiskeli yake na mlipuko huo. "Ulikuwa ni mlipuko mkubwa na nilisikia madirisha yakivunjika pande zote," alisema.

    Rhino Williams, ambaye alikuwa katika mgahawa wake karibu, aliambia BBC awali alidhani mlipuko huo ulikuwa wa ndege au helikopta iliyoanguka.

    FBI ilisema katika kikao kifupi cha Jumamosi kwamba lilikuwa shambulio la makusudi.

    "Hiki kilikuwa kitendo cha kukusudia cha ugaidi. Uchunguzi wetu utakapoendelea tutabaini kama ni ugaidi wa kimataifa au ugaidi wa ndani," alisema Akil Davis, mkuu wa ofisi ya FBI ya Los Angeles.

    Mkuu wa polisi wa Palm Springs Andy Mills alisema mlipuko huo uliharibu majengo kadhaa, mengine vibaya.

    Aliongeza kuwa mtu aliyeuawa haijafahamika ni nani.

  7. Watu wawili wamefariki wakati meli ya jeshi la wanamaji la Mexico ilipogonga Daraja

    Watu wawili wamefariki na wengine 19 kujeruhiwa baada ya meli ndefu ya mafunzo ya Wanamaji wa Mexico kugonga Daraja la Brooklyn la New York City.

    Polisi walisema Cuauhtémoc, ikiwa na watu 277, ilipoteza nguvu za umeme siku ya Jumamosi wakati nahodha alipokuwa akiendesha meli hiyo, na kuielekeza kwenye kingo za daraja upande wa Brooklyn.

    Kanda za video zinaonyesha milingoti mirefu ya meli inakata daraja ilipokuwa ikipita chini ya muundo huo. Wafanyakazi walikuwa wamesimama kwenye nguzo huku wakiruka na kuanguka kwenye sitaha, mamlaka ilisema.

    Mkazi wa Brooklyn, Nick Corso, aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema ilisababisha hofu. Kulikuwa na "mayowe mengi, baadhi ya mabaharia wakining'inia kutoka kwenye milingoti," aliiambia AFP.

    Meya wa jiji la New York Eric Adams alithibitisha kwenye mtandao wa X kwamba watu wawili walikufa na wawili kati ya 19 waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya.

    Daraja la Brooklyn halikupata uharibifu wowote na lilifunguliwa tena baada ya ukaguzi wa awali.

    Polisi walisema wanaamini kuwa "maswala ya kiufundi" na kukatika kwa umeme ndiko kulikosababisha mgongano huo.

    Soma zaidi:

  8. Hamas kuwaachilia baadhi ya mateka katika mazungumzo mapya

    Hamas imependekeza kuwaachilia mateka zaidi chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, baada ya mazungumzo mapya kufanyika siku ya Jumamosi.

    Mazungumzo hayo yalianza saa chache baada ya jeshi la Israel kuanzisha mashambulizi mapya katika Ukanda wa Gaza.

    Hamas imekubali kuwaachilia mateka tisa kwa mabadilishano ya usitishaji mapigano ya siku 60 na Israel iwaachilie wafungwa wa Kipalestina, afisa wa Palestina aliambia BBC.

    Afisa huyo alisema mpango huo mpya uliopendekezwa pia utaruhusu kuingia kwa malori 400 ya misaada kwa siku, na kuwaondoa wagonjwa kutoka Gaza.

    Israel, kwa upande wake, imedai ithibitishiwe mateka walio hai na taarifa za kina juu ya wale waliosalia.

    Duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano imefanywa kupitia wapatanishi wa Qatar na Marekani mjini Doha, na ilianza Jumamosi alasiri kwa saa za huko.

    Israel bado haijajibu hadharani kuhusu mpango huo uliopendekezwa, lakini ilisema kabla ya mazungumzo hayo kwamba haitaondoa wanajeshi wake huko Gaza au kuhakikisha kuwa itakomesha vita.

    BBC inafahamu kuwa pendekezo hilo halitajumuisha vipengele hivi.

    Jeshi la Israel lilitangaza kuanzisha mashambulizi mapya yaliyopewa jina la "Operation Gideon's Chariots" mapema Jumamosi, huku kukiwa na wimbi baya zaidi la mashambulizi huko Gaza katika kipindi cha miezi kadhaa.

    Takriban watu 300 wameuawa tangu Alhamisi, waokoaji wanasema, ikiwa ni pamoja na katika hospitali na kambi za wakimbizi kaskazini na kusini mwa Ukanda huo.

    Maelfu wamekufa tangu Israel ianze tena mashambulizi tarehe 18 Machi, kufuatia kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji mapigano uliodumu kwa miezi miwili.

    Soma zaidi:

  9. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 18/05/2025.Karibu.