Wakati wasichana wawili wa Kibrazili waliporipotiwa
kutoweka mnamo Septemba 2022, familia zao na Shirika la Upelelezi la Marekani
– FBI, walianzisha msako mkali kote Marekani ili kuwapata. Walichojua
ni kwamba walikuwa wakiishi na mshawishi wa Instagram Kat Torres.
Torres sasa amehukumiwa kifungo cha miaka minane jela kwa
ulanguzi wa binadamu na utumwa wa mmoja wa wanawake hao.
BBC pia imeambiwa kuwa mashtaka yamewasilishwa dhidi yake
kuhusiana na mwanamke wa pili.
Je, mwanamitindo huyo wa zamani ambaye aliwekwa kwenye jalada
la magazeti ya kimataifa alianzaje kuwahadaa wafuasi wake na kuwarubuni katika ulanguzi
wa kingono?
"Alikuwa kama mwenye kunipa tumaini," anasema
Ana, akielezea hisia zake baada ya kuona ukurasa wa Instagram wa Torres mnamo
2017.
Ana hakuwa
mmoja wa wanawake waliopotea waliolengwa katika msako wa FBI - lakini yeye pia
alikuwa mwathirika wa kulazimishwa na Torres na angekuwa muhimu kwa uokoaji
wao.
Anasema
alivutiwa na historia ya Torres kutoka kuwa mtu masikini wa Kibrazili hadi mwanamitindo
wa kimataifa, akishirikiana na waigizaji mashuhuri wa Hollywood.
"Alionekana
kama alikuwa ameshinda ghasia katika utoto wake, unyanyasaji, matukio yote ya
kutisha," Ana aliambia Uchunguzi wa BBC Eye na BBC News Brasil.
Ana mwenyewe
alikuwa katika mazingira magumu. Anasema aliteseka utotoni kwa vurugu, alihamia
Marekani peke yake kutoka kusini mwa Brazili, na awali alikuwa katika uhusiano
wa unyanyasaji.
Torres
alikuwa amechapisha hivi majuzi wasifu wake uitwao A Voz [The Voice], ambamo
alidai kuwa angeweza kutabiri kutokana na nguvu zake za kiroho, na alikuwa
amehojiwa kwenye vyombo vya habari maarufu vya Brazili.
“Alikuwa kwenye jalada la magazeti. Alionekana na watu
maarufu kama vile Leonardo DiCaprio. Kila kitu nilichoona kilionekana kuwa cha
kuaminika, "anasema.
Ana anasema alivutiwa hasa na mtazamo wa Torres wa
kiroho.
Kitu ambacho Ana hakujua ni kwamba simulizi ya kutia moyo
aliyosimulia Torres ilitokana na nusu ukweli na uwongo.