Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kuchunguza maandamano ya uchaguzi
Ingawa Tume hiyo inasema kuwa bado haifahamu ukubwa wa tatizo, lakini inaisitiza kwamba matokeo ya uchunguzi huo yanaweza kukamilika chini ya miezi miwili.
Muhtasari
- "Heche akabiliwa na mashtaka mawili ya ugaidi" – Wakili wake
- Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) chalaani mauaji ya raia Tanzania
- Dereva awagonga watembea kwa miguu Ufaransa, tisa wajeruhiwa
- Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kuchunguza maandamano ya uchaguzi
- Urusi inasema inawaondoa wanajeshi wa Ukraine huko Pokrovsk
- Israel yakabidhi miili ya Wapalestina 15
- Kenya: Mvua nchini kote itaendelea kunyesha mwezi Novemba
- Tarehe ya kikao cha kwanza cha wabunge wateule wa Tanzania yatangazwa rasmi
- Takriban watu saba wafariki baada ya ndege ya mizigo kuanguka Kentucky
- Mwanasheria mkuu wa serikali ya Tanzania aapishwa rasmi
- Vikosi vya usalama vyaendelea kushika doria, huku shughuli za kawaida zikianza kurejea Tanzania
- 60 wafariki dunia baada ya tufani kuharibu maeneo nchini Ufilipino
- Israel yatangaza mwili uliorudishwa na Hamas ni mmoja wa mateka wao
- Zohran Mamdani ashinda kinyang'anyiro cha umeya wa New York
- ECOWAS na EU wakemea tishio la Trump kuhusu madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wakristo nchini Nigeria
- ICC yaonya ukatili unaoshuhudiwa El Fasher unaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu
- Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) yatangaza wajumbe wa viti maalum vya wanawake
- Maandamano Tanzania: Upinzani 'watangaza siku saba ya maombolezo' Tanzania
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Asha Juma
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) chalaani mauaji ya raia Tanzania
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelaani matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2025.
THRC na TLS wametaja matukio kama mauaji, mateso, ukamataji holela wa raia yanaashiria ukiukaji wa haki za binadamu.
Katika taarifa yao ya pamoja waliyoitoa leo Novemba 4, 2025, na kusainiwa na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, na Rais wa TLS Boniface Mwabukusi inasikitishwa na mauaji ya vijana wengi wakati wa maandamano ya amani hasa katika maeneo yasiyo ya maandamano.
Taasisi hizo zimeacha alama mbaya katika historia ya haki, demokrasia, na utawala wa sheria nchini, na kutaka uchunguzi huru na kuwawajibisha wote waliohusika. Tayari Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni idara huru ya Serikali, imesema inaanza uchunguzi wa kina, na kutoa majibu ndani ya miezi miwili.
“Wazazi wengine ambao hawakuona miili ya watoto wao wameanza kuulizia watapataje miili hiyo ili wakawazike. Ni muhimu sana wazazi wakapewa miili ya vijana wao walioumia au kufariki,” Inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Taasisi hizo za THRDC na TLS zimekemea kuhusu uharibifu wa mali za umma na binafsi na kusisitiza mazungumzo zaidi kuliko matumizi ya nguvu.
Imetaja pia kuzimwa kwa mitandao kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 3 ni ukiukaji mwingine wa haki ya kupata taarifa na mawasiliano.
Akizungumza baada ya kuapishwa mwishoni mwa wiki, Rais Samia Suluhu alitoa onyo kwa waliohamasisha maandamano na kufanya uvunjivu wa amani, ikiwmeo pia kuharibu mali za umma na binafsi.
Maandamano hayo yalianza siku ya uchaguzi Jumatano iliyopita, ambapo baadhi ya waandamanaji walichana mabango ya Rais Samia na kuchoma majengo ya serikali. Polisi na vyombo vingine vya dola vilitumika kukabiliana na waandamanaji. Wengi wa waandamanaji walikuwa wakilalamikia kutoshiriki kwa wagombea wawili wakuu wa upinzani, Tundu Lissu na Luhaga Mpina.
Lissu na chama chake cha CHADEMA, chama kikuu cha upinzani kilijiondoa katika kinyang'anyiro hicho, kikidai kufanyika kwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi mwingine wowote, huku Mpina wa ACT Wazalendo aliondolewa na INEC kwa madai ya kutokidhi vigezo vya kisheria.
Soma zaidi:
Dereva awagonga watembea kwa miguu Ufaransa, tisa wajeruhiwa
Dereva amewavamia watembea kwa miguu na waendesha baiskeli katika kisiwa cha Oleron cha Ufaransa karibu na pwani ya Atlantiki siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani Laurent Nunez alisema, na takriban watu tisa walijeruhiwa kabla ya dereva huyo kukamatwa, kulingana na maafisa wa eneo hilo.
Mshukiwa mwenye umri wa miaka 35 alipaza sauti akisema "Allahu Akbar" ikimaanisha ("Mungu ni Mkuu") alipokamatwa na polisi, mwendesha mashtaka wa eneo hilo, Arnaud Laraize, aliliambia gazeti la Sud Ouest.
Mbunge wa eneo hilo Olivier Falorni, hata hivyo, alisema sababu ya shambulio hilo kwenye kisiwa tulivu kinachopendwa na watalii wakati wa kiangazi bado haijajulikana, akisema mshukiwa hakuwa kwenye orodha ya Ufaransa ya watu wenye itikadi kali.
Vyombo vya habari vya Ufaransa vilisema ofisi ya mwendesha mashitaka wa kupambana na ugaidi haikuwa inasimamia uchunguzi huo katika hatua hii, na kwamba uchunguzi wa jaribio la mauaji kwa sasa unashughulikiwa na ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo la La Rochelle.
Ofisi ya mwendesha mashtaka dhidi ya ugaidi haikuweza kupatikana mara moja ili kutoa maoni yake.
Takriban watu tisa walijeruhiwa wakati gari la mshukiwa lilipowagonga katika maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Oleron, meya wa Dolus-d'Oleron, Thibault Brechkoff, aliiambia BFM TV.
Nunez alisema wawili kati ya waliojeruhiwa walikuwa katika uangalizi maalum - baadhi ya vyombo vya habari vya Ufaransa baadaye vilisema hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa wanne kati yao.
Gazeti la Le Parisien lilisema wachunguzi wanaangalia uwezekano kwamba mshukiwa anaweza kuwa na matatizo ya kiakili.
Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kuchunguza maandamano ya uchaguzi
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Nchini Tanzania (THBUB) imesema itaanzisha uchunguzi wa kina kufuatia maandamano yalioshuhudiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, na kusababisha uharibifu wa mali na vifo vya raia.
Ingawa Tume hiyo inasema kuwa bado haifahamu ukubwa wa tatizo, lakini inaisitiza kwamba matokeo ya uchunguzi huo yanaweza kukamilika chini ya miezi miwili.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni idara huru ya Serikali, iliyoanzishwa kama taasisi ya Kitaifa iliyo kitovu cha kukuza na kulinda haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Novemba 5, 2025 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, anasema matokeo ya uchunguzi huo ndio itaamua namna ya kuishauri Serikali ili kuepuka vurugu katika chaguzi zingine zijazo.
“Matukio ya aina hiyo hayawezi kuvumiliwa katika jamii inayothamini amani na utawala wa sheria” Alisema na kuongeza "kwa namna yoyote ile, matukio ya aina hii yaliyotokea hayapaswi kuungwa mkono, kwa sababu yanavunja amani ya nchi na kuhatarisha usalama wa wananchi,”.
“Sisi kama Tume, kutokana na matukio hayo, tumeamua kufanya uchunguzi wa kina na tayari tumejipanga vizuri kuhakikisha jambo hili linashughulikiwa ipasavyo”, anasema Mwaimu.
Maandamano hayo yalianza siku ya uchaguzi Jumatano iliyopita, ambapo baadhi ya waandamanaji walichana mabango ya Rais Samia na kuchoma majengo ya serikali.
Polisi na vyombo vingine vya dola vilitumika kukabiliana na waandamanaji.
Soma zaidi:
Urusi inasema inawaondoa wanajeshi wa Ukraine huko Pokrovsk
Urusi imesema Jumatano kwamba vikosi vyake vilikuwa vinasonga mbele kaskazini ndani ya mji wa Pokrovsk wa Ukraine na kuwaondoa wanajeshi wa Kyiv katika harakati za kuchukua udhibiti kamili wa kile ambacho kimekuwa kitovu muhimu cha usafirishaji kwa jeshi la Ukraine.
Ukraine imekiri kuwa wanajeshi wake wanakabiliwa na wakati mgumu katika mji huo wa kimkakati wa mashariki, ambao Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka kwa zaidi ya mwaka mmoja, lakini inakanusha kuwa wamezingirwa na kusema kwamba wanaendelea kuijiimarisha.
Urusi inachukulia mji huo kama fursa ya kuweza kuteka asilimia 10 iliyosalia, au kilomita za mraba 5,000 (maili za mraba 1,930) za eneo la mashariki la viwanda la Donbas la Ukraine, mojawapo ya malengo yake kuu katika vita vilivyodumu kwa takriban miaka minne.
"Vikundi vya shambulio vya jeshi la 2 na la 51 viliendelea kuharibu vitengo vya Vikosi vya Wanajeshi vya Ukraine vilivyozunguka katika eneo la makazi la wilaya ndogo ya Prigorodny, katika sehemu ya mashariki ya Wilaya ya Kati na katika sekta ya kibinafsi (ambapo kuna nyumba za makazi)," Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema katika taarifa.
"Mashambulio ya upande wa kaskazini yanaendelea," iliongeza, ikisema kwamba vikosi vyake pia vilikuwa vikiwaondoa wanajeshi wa Ukraine kutoka kwa makazi kwenye ubavu wa kusini-mashariki mwa Pokrovsk na kuzima majaribio mengi ya Ukraine ya kujinasua kutokana na kuzingirwa.
Soma zaidi:
Israel yakabidhi miili ya Wapalestina 15
Nasser Medical Complex iliyoko Khan Younis katika Ukanda wa Gaza imethibitisha kuwasili kwa miili 15 ya Wapalestina waliouawa katika Ukanda huo, ambao miili yao ilikuwa ikishikiliwa na Israel, na kukabidhiwa kupitia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ikiwa ni utekelezaji wa masharti ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hii inafanya idadi ya miili iliyokabidhiwa jeshi la Israel kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kufikia 285.
Makabidhiano hayo yalifanyika baada ya Hamas kukabidhi mwili wa mmoja wa wanajeshi wa Israel uliokuwa wanaushikilia usiku wa Jumanne.
Katika muktadha unaohusiana na hayo, mashahidi wa tukio hilo walithibitisha kwamba wawakilishi wa Shirika la Msalaba Mwekundu na Brigedi za Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, walielekea eneo la Shuja'iyya mashariki mwa Mmi wa Gaza, kwa ajili ya kukamilisha operesheni ya kutafuta miili ya mateka zaidi wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Soma zaidi:
Kenya: Mvua nchini kote itaendelea kunyesha mwezi Novemba
Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya (KMD) imetangaza kuwa mvua zitaendelea kunyesha nchini kote mwezi huu wa Novemba.
Katika mtazamo wake wa hali ya hewa, shirika hilo lilisema kuwa mvua zaidi ya wastani inatarajiwa kuendelea katika kaunti za Bonde la Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, na Kati na Kusini mwa Bonde la Ufa.
Vile vile, mvu ya chini ya wastani au kawaida inatarajiwa katika kaunti za Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa (pamoja na Nairobi), nyanda za juu Kusini-mashariki, Pwani na sehemu kubwa ya Kaskazini-mashariki.
"Mvua itakayonyesha haitakuwa ya kiwango sawa, na vipindi vya ukame vya hapa na pale katika maeneo kadhaa ya nchi," mtaalamu wa hali ya hewa alibainisha.
Hata hivyo, halijoto inatarajiwa kusalia joto zaidi kuliko kawaida nchini kote huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa mafuriko katika eneo la magharibi na vipindi virefu vya kiangazi katika maeneo ya mashariki mwa nchi.
Maeneo ya Nyanda za Juu Magharibi, Mashariki mwa Bonde la Ufa na Bonde la Ziwa yamebainishwa haswa kuwa yana uwezekano wa kupata mvua za wastani, hivyo kuhitaji tahadhari kutokana na udongo ambao tayari umejaa maji.
Tarehe ya kikao cha kwanza cha wabunge wateule wa Tanzania yatangazwa rasmi
Shughuli za Bunge jipya la Kumi na tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 11 Novemba 2025 mjini Dodoma, kufuatia tangazo lililotolewa na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kitafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Novemba 2025.
Tangazo hilo limefuatia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliotolewa kupitia Gazeti la Serikali, toleo maalum namba
11, la tarehe 4 Novemba 2025.
Kikao hicho cha kwanza kinatarajiwa kushuhudia shughuli muhimu kadhaa, zikiwemo: Kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika na Naibu Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitishwa kwa uteuzi wa Waziri Mkuu, na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ufunguzi wa Bunge jipya utakuwa ni tukio muhimu litakaloweka msingi wa kazi za Bunge la kumi na tatu, likihusisha wabunge wapya na wale waliorejea, huku macho ya Watanzania yakielekezwa Dodoma kuona sura mpya za uongozi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Chama cha mapinduzi,CCM kimeendelea kutawala bunge kikipata ushindi wa zaidi ya 90% ya wabunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Soma pia:
Takriban watu saba wafariki baada ya ndege ya mizigo kuanguka huko Kentucky
Takriban watu saba wameuawa wakati ndege ya mizigo ya UPS ilipoanguka ilipokuwa ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa Louisville, Kentucky Jumanne jioni, gavana wa jimbo hilo alisema.
Andy Beshear alisema wafanyakazi watatu wa ndege hiyo huenda wakawa miongoni mwa waliofariki baada ya ndege hiyo ya mizigo kulipuka ilipokuwa ikiondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Louisville Muhammad Ali mwendo wa saa 17:15 kwa saa za eneo (22:15 GMT).
Takriban watu wengine 11 wamejeruhiwa wakati ndege hiyo ilipoanguka na kusababisha moshi mwingi angani.
Maafisa wameonya kuwa watu wamepata majeraha "makubwa" katika tukio hilo na kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Pia unaweza kusoma:
Mwanasheria mkuu wa serikali ya Tanzania aapishwa rasmi
Mwanasheria mkuu wa Tanzania Hamza Johari amekula kiapo cha kazi Jumatano ya tarehe 05/11/2025 katika ikulu ya Chamwino Dodoma.
Hamza Said Johari aliteuliwa siku ya Jumatatu na Rais Samia Suluhu baada ya kuingia ikulu kwa muhula wa pili utakaokamilika 2030.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria hafla hiyo ya uapisho wa mwanasheria mkuu wakiongozwa na Rais Samia Suluhu.
Aliyeongoza uapisho huo ni Jaji mkuu George Mcheche Masaju.
Mwanasheria mkuu huyu pia alikuwa katika wadhifa huo muhula uliopita wa Rais Samia.
Kabla ya kuwa Mwanasheria mkuu wa serikali ya muungano wa Jamhuri ya Tanzania alikuwa mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania.
Kwa mujibu wa Ibara ya 112(1)(b), Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kati ya Wajumbe Sita.
Vikosi vya usalama vyaendelea kushika doria, huku shughuli za kawaida zikianza kurejea Tanzania
Kufuatia siku kadhaa za machafuko katika miji mbalimbali nchini Tanzania, maisha yameonekana kurudi kawaida lakini vikosi vya usalama vimeonekana vikishika doria katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
BBC imeshuhudia maafisa wa polisi na wanajeshi wakiwa katika vituo vya mwendekasi, ofisi ya serikali na maeneo ya biashara kama vituo vya kujaza mafuta wakiwa na silaha pamoja na magari.
Hali hii inafuatia vurugu zilizotokea kuanzia Jumatano ya tarehe 29, siku ambayo Tanzania iliingia kufanya uchaguzi mkuu wa kumchagua rais, wabunge na madiwani.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu yanaeleza kuwa mamia ya watu wameuwawa katika vurugu hizo, huku serikali ya Tanzania ikikiri kutokea kwa vurugu lakini bado haijatoa idadi kamili ya waliouwawa.
Pia unaweza kusoma:
60 wafariki dunia baada ya tufani kuharibu maeneo nchini Ufilipino
Angalau watu 66 wamefariki dunia, huku mamia ya maelfu wakikimbia makazi yao, baada ya moja ya tufani zenye nguvu zaidi mwaka huu kupita katikati ya Ufilipino, kwa mujibu wa mamlaka.
Tufani Kalmaegi imeathiri miji yote kwenye kisiwa cha kati chenye idadi kubwa ya watu, Cebu, ambapo watu 49 walifariki.
Wengine 26 bado hawajulikani walipo, alisema afisa wa ulinzi wa kiraia katika mahojiano ya redio Jumatano.
Video zinaonyesha watu wakiokolewa kwenye paa za majengo, huku magari na kontena za mizigo zikisogea barabarani kwa nguvu za tufani.
Idadi rasmi ya vifo inajumuisha wanajeshi sita wa helikopta ya kijeshi iliyoanguka kwenye kisiwa cha Mindanao, kusini mwa Cebu, baada ya kutumwa kusaidia jitihada za msaada.
Helikopta hiyo ilianguka Jumanne karibu na Agusan del Sur, ikiwa moja kati ya nne zilizotumwa kusaidia.
“Mawasiliano na helikopta yalipotea, jambo ambalo lilisababisha mara moja kuanzishwa kwa operesheni ya uokoaji,” alisema Jeshi la Anga la Ufilipino.
Baadaye, msemaji alisema miili sita ilipatikana, ikidhaniwa kuwa ni ya rubani na wafanyakazi wake.
Tufani, inayojulikana hapa kama Tino, imepungua nguvu tangu ilipopiga kisiwa mapema Jumanne, lakini bado inapeleka upepo wenye kasi ya zaidi ya 80 mph (130 km/h).
Inakadiriwa itapita katika kisiwa cha Visayas na kuingia kwenye Bahari ya China Kusini ifikapo Jumatano.
Rafaelito Alejandro, naibu msimamizi wa Ofisi ya Ulinzi wa Kiraia, alitoa idadi iliyosasishwa ya vifo katika mahojiano na kituo cha redio cha DZMM Jumatano.
Waokoaji wanasubiri anga kutulia kabla ya kusambaza msaada.
Alisema: “Changamoto ni mabaki na magari barabarani. Kuna mengi ya kusafisha.” Carlos Jose Lañas, muokoaji wa hiari, aliambia BBC kwamba licha ya kujiandaa kwa hali mbaya zaidi, walishangazwa na ukubwa wa mafuriko.
“Hii ndiyo mafuriko mabaya zaidi niliyowahi kuyapata,” alisema kijana huyo wa miaka 19.
“Karibu mito yote hapa Cebu imevunja kingo. Hata wahudumu wa dharura hawakutarajia hali kama hii.”
Soma pia:
Israel yathibitisha mwili uliorudishwa na Hamas ni wa mmoja wa mateka wao
Israel imethibitisha Jumatano ya 05/11/2025 kuwa mwili uliokabidhwa na Hamas Jumanne ni wa Sajenti Itai Chen, mateka Muisraeli-Mmarekani aliyotekwa Oktoba 7, 2023.
Hamas iliukabidhi mwili kwa shirika la msalaba mwekundu baada ya operesheni ya utafutaji katika mtaa wa Shuja’iyya.
Al-Qassam alisema mwili ulipatikana ndani ya mstari njano, maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Israeli.
Chanzo cha Hamas kiliambia AFP kuwa miili mingine ya mashahidi wa Palestina pia ilipatikana chini ya mabaki ya majengo.
Hadi sasa, miili 21 imekabidhiwa huku 7 ya askari bado yapo katika eneo hilo.
BBC imefahamu kuwa Marekani ilisambaza, siku ya Jumatatu, kwa idadi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, rasimu ya azimio linalotaka kuanzishwa kwa kikosi cha kimataifa katika Ukanda wa Gaza, na mamlaka ya kuongezwa kwa muda usiopungua miaka miwili.
Mradi huo, ambao wanadiplomasia waliozungumza na BBC waliuelezea kuwa "nyeti lakini sio siri," unafungua mlango kwa majadiliano muhimu kuhusu usimamizi na usalama wa siku zijazo wa sekta hiyo baada ya vita.
Rasimu hiyo inaonesha kuwa Marekani itaongoza katika awamu ya kwanza kikosi hicho kitakachojulikana kama ISF ("International Security Force") , ambapo shughuli zitasimamiwa kwa ushirikiano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa.
Kikosi hicho kinalenga kulinda mipaka ya Gaza na Israel na Misri, kulinda raia na korido za kibinadamu, kutoa mafunzo kwa kikosi kipya cha polisi cha Palestina, pamoja na kuwapokonya silaha makundi yenye silaha na kuzuia kujengwa upya kwa miundombinu yao ya kijeshi.
Katika maendeleo mengine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliomba kumalizika mapema kwa kesi yake ya ufisadi kutokana na mkutano wa dharura wa kidiplomasia na Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani, Tulsi Gabbard, anayemtembelea Israel.
Netanyahu amelalamika kuwa kesi hiyo inayodumu tangu 2020 inamkosesha uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama waziri mkuu.
Zohran Mamdani ashinda kinyang'anyiro cha umeya wa New York
Zohran Mamdani, mwenye umri wa miaka 34, sasa ndiye Meya mpya wa Jiji la New York na Meya wa kwanza Muislamu wa jiji kubwa zaidi nchini Marekani.
Hii ni baada ya uchaguzi kukamilika.
Mamdani, anayejitambulisha kama msoshalisti wa kidemokrasia, alikuwa hajulikani sana miezi michache iliyopita.
Hata hivyo, amepata ushindi mkubwa kupitia kampeni zilizoahidi kutoza kodi zaidi kwa mamilionea ili kufadhili mipango mipya ya kijamii.
Meya mteule wa New York, Zohran Mamdani, ameibuka jukwaani akipunga mkono na kutabasamu huku umati mkubwa ukishangilia kwa sauti na kupaza jina lake, “Zohran! Zohran!”
Akiwahutubia wafuasi wake waliokuwa wamefurika kusherehekea ushindi huo, Mamdani alisema kuwa leo inaashiria mwanzo wa siku mpya yenye matumaini kwa binadamu wote.
“Kwa muda mrefu, wafanyakazi wa New York wameambiwa na matajiri na wenye ushawishi kwamba madaraka si yao,” alisema Mamdani.
“Lakini katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita, mmeonyesha ujasiri wa kutafuta kitu kikubwa zaidi. Usiku huu, kinyume na matarajio yote, tumekipata.”
Akaongeza kwa kusema, “Mustakabali uko mikononi mwetu,” huku umati ukishangilia kwa nguvu.
Ingawa hotuba yake ilijikita zaidi katika kuelezea maono yake kwa jiji la New York, haikuchukua muda kabla ya kumjibu mkosoaji wake mkubwa, Rais wa Marekani Donald Trump.
“Donald Trump, najua unatazama,” alisema kwa ucheshi. “Nina maneno manne kwako: ongeza sauti.”
Kwa ishara hiyo, umati ulilipuka kwa kelele kubwa zaidi. Mamdani aliendelea kumkabili moja kwa moja Trump kwa kusema: “Ili umfikie yeyote kati yetu, italazimu upitie kwetu sote.”
Wakati Mamdani akiendelea na hotuba yake, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Truth Social: “… NA HIVYO NDIVYO INAVYOANZA!”
Rais wa Marekani Trump alikuwa ametishia kukata ufadhili wa serikali kuu kwa Jiji la New York iwapo Mamdani angeshinda dhidi ya Andrew Cuomo (mwaniaji huru) na Curtis Sliwa (Mrepublican).
Wakati huo huo, chama cha Democrat kinatarajiwa pia kushinda uchaguzi wa ugavana katika majimbo ya Virginia na New Jersey.
Aidha, wapiga kura wa California wamepitisha uamuzi wa kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi ili kuimarisha nafasi ya chama cha Democrat kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
ECOWAS na EU wakemea tishio la Trump kuhusu madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wakristo nchini Nigeria
Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imekanusha kama ya uongo na yenye hatari madai kwamba makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo yanawalenga watu wa dini fulani au yanafanya mauaji ya kimbari dhidi ya waumini wa wakristo.
Taarifa hii inatolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutishia kuchukua hatua za kijeshi nchini Nigeria kutokana na kile alichokiita “mauaji ya halaiki ya Wakristo.”
Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne, ECOWAS ilisema madai kama hayo yanaweza kuongeza hali ya kutokuwa na usalama na kudhoofisha mshikamano wa kijamii katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na vurugu za kigaidi.
“Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) inapenda kuwakumbusha washirika na jumuiya ya kimataifa kuhusu ongezeko la kiwango cha vurugu ambazo makundi ya kigaidi ya aina mbalimbali yamekuwa yakifanya katika baadhi ya nchi za eneo hili, zikiwemo Nigeria,” taarifa hiyo ilisema.
ECOWAS ilisisitiza kwamba mashambulizi ya kigaidi katika Afrika Magharibi yanalenga raia wasio na hatia bila kujali dini, kabila, au jinsia.
Iliitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono nchi wanachama katika mapambano dhidi ya ugaidi “unaolenga jamii zote.”
Umoja wa Ulaya (EU) pia ulitoa maoni kuhusu sakata hilo, ukisema umezingatia kauli zilizotolewa na serikali ya Marekani.
Msemaji wa mambo ya nje wa EU, Anouar El Anouni, alionesha mshikamano na waathirika wote wa vurugu nchini Nigeria, wakiwemo walioathirika na mashambulizi ya hivi karibuni katika maeneo ya kusini na kaskazini mashariki.
“Tunatambua kuna sababu nyingi zinazopelekea vurugu nchini Nigeria. Dini ni moja tu kati ya hizo na hata hivyo, ni katika baadhi ya matukio pekee,” alisema Bwana El Anouni.
Alisisitiza dhamira ya EU ya kuhakikisha umoja na kuishi kwa amani miongoni mwa wananchi wa Nigeria, “bila kujali tofauti za kijiografia, kikabila, kisiasa au kidini.”
Onyo la Rais Trump lililochapishwa katika jukwaa lake la kijamii Truth Social limezua mjadala mpana na hisia kali.
Wachambuzi wanasema kauli zake zinagusa nyufa nyeti za kidini na kisiasa nchini Nigeria.
Nigeria imegawanyika karibu sawa kati ya kaskazini yenye Waislamu wengi na kusini yenye Wakristo wengi.
Wakati makundi yenye misimamo mikali kama Boko Haram na ISWAP (Islamic State West Africa Province) yameshambulia makanisa na jamii za Kikristo, pia yamewaua mamia ya Waislamu wanaopinga itikadi zao.
Wachambuzi wanaonya kwamba kuelezea vurugu hizi kama “mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo” kunarahisisha kupita kiasi mchanganyiko wa sababu mbalimbali ikiwemo umasikini, migogoro ya ardhi, na mvutano wa kikabila vinavyochangia ukosefu wa usalama nchini Nigeria na eneo zima la Sahel.
Wito wa ECOWAS na EU huenda unalenga kuhimiza utulivu na kushirikiana kimataifa katika kushughulikia mizizi ya vurugu, hasa katika Afrika Magharibi na eneo la Sahel.
Soma zaidi:
ICC yaonya ukatili unaoshuhudiwa El Fasher unaweza kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeonya kwamba ukatili unaoripotiwa mjini El-Fasher unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo imesema ina wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa za mauaji ya halaiki, ubakaji, na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu nchini Sudan.
Wakati huo huo, serikali ya kijeshi ya Sudan inaendelea na mazungumzo kuhusu masuala ya usalama, kufuatia kutekwa kwa mji wa El-Fasher — ngome ya mwisho ya jeshi katika eneo la Darfur — na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).
Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, kiongozi wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, alikiri kwamba baadhi ya wanajeshi wake walihusika katika makosa na ameahidi kufanyia uchunguzi suala hilo.
Hemeti, ambaye alijipatia utajiri wake kupitia biashara ya ngamia na dhahabu, sasa ameibuka kama mtu mwenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa siasa za Sudan, huku wanamgambo wake wakidhibiti takriban nusu ya nchi.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva ameonya kwamba ukatili unaofanyika Al-Fasher unafikia kiwango cha mauaji ya kimbari, na amesema hali inayofanana na njaa kali inaendelea kutokana na hatua ya RSF kuzuilia misaada ya kibinadamu madai ambayo RSF wamekanusha.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kwamba “mji wa Fasher na maeneo yanayouzunguka huko Kaskazini mwa Darfur ndio kitovu cha mateso, njaa, ghasia, na uhamishaji wa watu.”
Amesisitiza pia kuwa kuna “taarifa endelevu za ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.”
Chanzo cha serikali ya Sudan kimeiambia shirika la habari la AFP kwamba mamlaka zinazingatia pendekezo la Marekani kuhusu kusitisha mapigano.
Washington, kupitia kundi la Quad, imekuwa ikisukuma juhudi za kusitisha vita na kuweka ramani ya amani ya kumaliza mzozo huo.
Kikundi cha Majadiliano ya Usalama cha Quadrilateral (Quad) ni jukwaa la kimkakati kati ya Marekani, India, Japani, na Australia, lililoanzishwa mwaka 2007.
Watu wasiopungua 40 nchini Sudan wameuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani lililolenga mazishi yaliyokuwa yakifanyika nje ya mji wa el-Obeid, ambao unashikiliwa na jeshi, katika jimbo la Kordofan Kaskazini, maafisa na wanaharakati wamesema.
Wamelilaumu jeshi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kwa shambulio hilo lililotokea Jumatatu katika kijiji cha al-Luweib, wakati waombolezaji walipokuwa wamekusanyika ndani ya hema. RSF bado haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.
Mwisho wa mwezi Oktoba, kikosi cha RSF, ambacho kimekuwa katika vita na jeshi la Sudan kwa zaidi ya miaka miwili, kiliteka mji wa kimkakati wa Fasher baada ya mzingiro wa miezi 18.
Soma pia:
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) yatangaza wajumbe wa viti maalum vya wanawake
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza majina ya wajumbe wa viti maalum vya wanawake watakaokuwemo katika Baraza la Wawakilishi, kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Thabit Aidarous, uteuzi huo umefanyika katika kikao maalum cha tume hiyo kilichofanyika tarehe 4 Novemba.
Jumla ya wajumbe 20 wa viti maalum wameteuliwa, wakiwemo wajumbe 16 kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na wajumbe 4 kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, kwa uwiano unaoakisi uwakilishi wa vyama hivyo katika Baraza la Wawakilishi.
Tume imesema uteuzi huo umefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 67(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, pamoja na kifungu cha 55(3) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 4 ya mwaka 2018.
Haya yanajiri, baada ya Chama cha upinzani, ACT-Wazalendo, kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais visiwani Zanzibar.
Mgombea wa urais wa chama hicho Outhman Masoud alieleza kutoridhishwa kwake.
“Wananchi wa wameibiwa sauti yao… suluhu pekee ya kupata haki ni uchaguzi mpya,”
Soma pia:
Maandamano Tanzania: Chadema 'yatangaza siku saba za maombolezo'
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza ''siku saba za maombolezo ya kitaifa,'' kuanzia leo tarehe 5 Novemba kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha katika ghasia zilizokumba uchaguzi mkuu.
''Tumechukua hatua hii kutokana na matukio ya kusikitisha yaliyosababisha vifo, majeruhi na baadhi ya wananchi kupotea,'' alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho Brenda Rupia.
Akitangaza uamuzi huo, katika mtandao wa kijamii wa Instagram , Bi. Brenda Rupia, amesema hatua hiyo ni njia ya kuonyesha heshima kwa wale waliopoteza maisha katika maandamano yaliyofanyika Tanzania tangu siku ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba.
Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa bendera zote za CHADEMA zitapeperushwa nusu mlingoti kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni, kwa siku zote saba za maombolezo.
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan bado haijatoa idadi kamili ya watu waliofariki dunia katika maandamano hayo yaliyokumbwa na ghasia.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia, idadi ya waliouawa inakadiriwa kufikia watu 500, ingawa CHADEMA imedai kuwa idadi hiyo huenda ni ya juu zaidi.
Kiongozi wa CHADEMA, Tundu Lissu, bado anazuiliwa tangu mwezi Aprili kwa tuhuma za uhaini.
Kabla ya kukamatwa kwake, aliwataka wafuasi wa chama hicho wasishiriki uchaguzi wa Oktoba 29 hadi pale mageuzi ya sheria ya uchaguzi yatakapofanyika.
Baada ya kuapishwa kwake, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaonya wale aliowaita “wanaoendeleza maandamano haramu”, akidai kuwa baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakizua ghasia katika maeneo kadhaa ya Tanzania ni raia wa nchi jirani, ingawa hakubainisha ni wa taifa gani.
Vile vile, Rais Samia alikemea vikali matendo hayo akisema "kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania.
"Sasa tuchague lenye manufaa kwetu kwani usalama wa taifa lolote hulindwa kwa wote, kwa nguvu zote na kwa gharama zozote."alisema Rais Samia.
Soma pia:
Hujambo na karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 05/11/25 ambayo tutaangazia matukio yanayochipuka nchini Tanzania na kimataifa.