Na Dinah Gahamanyi, Martha Saranga & Rashid Abdallah
Afrika Mashariki kukumbwa na ukame katika miezi ijayo
Chanzo cha picha, EARTH.ORG
Maelezo ya picha, Ethiopia, Uganda, Rwanda, Kenya, Burundi, na Tanzania zitaathiriwa na hali ya ukame.
Kituo
cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha Nchi za Jumuiya ya IGAD, kinasema kuwa eneo la
Afrika Mashariki litapata hali ya ukame kuliko kawaida kati mwezi wa Januari na
Machi 2025.
Katika
utabiri wake uliotolewa Jumatatu, kinasema Ethiopia, Uganda, Rwanda, Kenya,
Burundi, na Tanzania zitaathiriwa na hali ya ukame.
Kanda
hiyo pia itarekodi joto zaidi kuliko kawaida wakati wa msimu wa Januari hadi
Machi 2025. "Joto la kawaida huenda likarekodiwa katika maeneo machache ya
kaskazini mwa Uganda na magharibi mwa Sudan," imesema ripoti.
Kwa
mujibu wa kituo hicho, katika kanda nzima, kusini magharibi mwa Tanzania na
kusini magharibi mwa Uganda pekee ndizo zitakumbwa na hali ya mvua kuliko
kawaida katika kipindi hicho, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia
nchi katika ukanda huo.
Mataifa
ya Pembe ya Afrika ni miongoni mwa yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia
nchi kwani ukame, mafuriko, na wadudu waharibifu huwa jambo la kawaida huku
kukiwa na joto la juu la nyuzi joto 32, kulingana na kituo hicho.
Zaidi
ya watu milioni 64 walihitaji msaada wa kibinadamu katika Pembe ya Afrika
mwishoni mwa Novemba kutokana na migogoro na majanga ya hali ya hewa, Shirika
la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na IGAD walibainisha katika ripoti ya
hivi karibuni.
Timu za Afrika Mashariki kukutana kisiwani Pemba katika Kombe la Mapinduzi
Chanzo cha picha, TFF
Maelezo ya picha, Kikosi cha Zanzibar Heroes kikiwa katika mazoezi ya kujiandaa na kombe la Mapinduzi
Michuano
ya Kombe la Mapinduzi, inafungua pazia leo visiwani Zanzibar, ambapo
Kilimanjaro Stars kutoka Tanzania bara itakutana na timu ya taifa ya Zanzibar Heroes
usiku wa leo, katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
Timu
nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo ni Burkina Faso kutokea Afrika Magharibi
na Harambe Stars kutoka Kenya, ambao watacheza kesho katika uwanja huo huo.
Timu
ya taifa ya Burundi na Uganda The Cranes zilijitoa katika mashindano hayo dakika
za mwisho na kuifanya michuano hiyo kubaki na timu nne pekee.
Kombo
la Mapinduzi hufanyika kama sehemu ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea
Januari 12 mwaka 1964, yaliyoondoa utawala w Kisultani katika visiwa hivyo
ambavyo kwa sasa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Elon Musk akosolewa kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu magenge ya wabakaji
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Elon Musk
Ukosoaji
wa Elon Musk dhidi ya serikali ya Uingereza namna inavyoshughulikia magenge ya wabakaji
“sio sahihi na ni upotoshaji," amesema Katibu wa masuala ya Afya, Wes
Streeting.
Bilionea
Musk amechapisha msururu wa taarifa kwenye tovuti yake ya kijamii ya X,
akimshutumu Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer kwa kushindwa kushughulikia
magenge ambayo yaliwabaka wasichana wadogo, na kutaka waziri wa ulinzi Jess
Phillips afungwe jela.
Alipoulizwa
kuhusu maoni hayo, Streeting alisema "serikali hii inachukulia suala la
unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto kwa umakini mkubwa."
Amemwalika
Musk "kujitayarisha na kufanya kazi nasi" dhidi ya magenge ya
ubakaji.
Kiongozi
wa Conservative, Kemi Badenoch ametoa wito wa uchunguzi kamili kuhusu kile
alichokiita "kashfa ya magenge ya ubakaji" Uingereza.
Lakini
chama hicho pia kimemkosoa Musk kwa "kuchapisha taarifa ambazo sio sio
sahihi" na kujitenga na wito wake wa kutaka Phillips afungwe.
Israel imethibitisha kuwa inamshikilia mkuu wa hospitali ya Gaza Abu Safiya
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Mkurugenzi wa hospitali hiyo alizuiliwa wakati wa uvamizi wa Israel Ijumaa iliyopita
Israel imethibitisha kuwa inamshikilia mkurugenzi wa
hospitali ya Gaza Dr Hussam Abu Safiya baada ya hapo awali kuliambia shirika
lisilo la kiserikali la eneo hilo kuwa halina taarifa zake, na hivyo kuzua
wasiwasi kuhusu afya yake.
Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) ilisema "kwa
sasa anachunguzwa na vikosi vya usalama vya Israel" ana kwa ana.
Taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi kuhusu mkanganyiko huo
lakini ilisisitiza kwamba anashukiwa kuwa "gaidi" anayeshikilia
cheo" katika kundi la Hamas, Wapalestina wenye silaha wanalopigana na
Israel huko Gaza.
Dk Abu Safiya alikamatwa wakati jeshi la Israeli
likiwalazimisha wagonjwa na wafanyikazi wa afya kuondoka katika hospitali ya
Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza Ijumaa iliyopita, kwa madai kuwa kituo hicho ni
"ngome ya magaidi wa Hamas".
Siku ya Alhamisi IDF iliwaambia Madaktari wa shirika la
kutetea Haki za Kibinadamu Israel (PHRI) kwamba "haijamkamata wala kumshikilia
mtu huyo".
PHRI iliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Israel siku ya
Alhamisi, ikitaka kufahamishwa mahali alipo Dkt Abu Safiya kufichuliwa. Ilisema
mahakama iliipa IDF wiki moja kutekeleza.
Wakati huo huo mkuu wa Amnesty Agnès Callamard alisema
mamlaka ya Israel lazima "ifichue haraka aliko".
Alisema Israel imewazuilia "mamia ya wahudumu wa afya
wa Kipalestina kutoka Gaza bila kufunguliwa mashitaka" na kusema
"wameteswa na kutendewa vibaya na kuzuiliwa bila mawasiliano".
Hata hivyo Israel inakanusha kuwatesa wafungwa.
Awali familia ya Dkt Abu Safiya iliambia Idhaa ya Kiarabu ya
BBC kwamba wanaamini anazuiliwa katika kambi ya kijeshi ya Sde Teiman kusini
mwa Israel, ambapo majeshi ya Israel yamewachukua wafungwa wengi kutoka Gaza
kwa mahojiano.
Hapo awali wafichuaji waliambia BBC na vyombo vingine vya
habari vya kimataifa kuhusu hali ngumu sana inayowakabili wafungwa walioko.
Israel imesema wafungwa wote huko wanahifadhiwa "kwa
uangalifu na ipasavyo".
IDF iliamuru kila mtu ndani ya hospitali ya Kamal Adwan
kuondoka Ijumaa iliyopita asubuhi, na kutoa muda wa takribani dakika 15 kwa
hospitali hiyo kuwahamisha wagonjwa na wafanyikazi ndani ya eneo hilo, wahudumu
wa afya waliambia BBC.
Mji wa Beit Lahia, iliko hospitali hiyo umekuwa chini ya
vizuizi vikali vya Israel vilivyowekwa kwenye maeneo ya kaskazini mwa Gaza
tangu Oktoba.
Umoja wa Mataifa umesema eneo hilo limezingirwa kwa karibu
huku jeshi la Israel likizuia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa misaada katika
eneo hilo ambalo wastani wa watu 10,000 hadi 15,000 wamesalia.
Chanzo cha picha, Reuters
Siku ya Jumamosi, IDF ilisema iliwakamata wapiganaji 240 huko Kamal Adwan na kusema Dk Abu Safiya alikuwa miongoni mwa wafanyikazi wa afya waliochukuliwa kuhojiwa.
Picha za video zilimuonyesha akitembea kuelekea kwenye gari la kivita la Israel kabla ya kupelekwa kuhojiwa. Msemaji wa jeshi la Israel alithibitisha kukamatwa siku hiyo hiyo, akisema daktari huyo alikuwa amehamishwa kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano.
Dk Abu Safiya hapo alikamatwa na vikosi vya Israel wakati wa uvamizi wa awali katika hospitali hiyo mwezi Oktoba, lakini aliachiliwa muda mfupi baadaye. Wakati wa operesheni hiyo ya Israel mtoto wa kiume wa Dkt Abu Safiya mwenye umri wa miaka 15 aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani. Picha za baadaye siku hiyo zilimuonyesha akiongoza dua ya mazishi ya mwanawe katika eneo la hospitali.
Mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya afya vya Gaza yamesababisha kulaaniwa zaidi.
Siku ya Jumanne Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema mashambulizi ya Israel katika hospitali na kandokando ya hospitali yamechangia kuharibu mfumo wa afya wa Gaza kabisa" na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Ujumbe wa Israel mjini Geneva ulisema vikosi vya Israel vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na "kamwe havitalenga raia wasio na hatia".
Israel ilianzisha kampeni ya kuiangamiza Hamas kujibu mashambulizi ya kundi hilo,mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 45,580 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.
Venezuela yatoa donge nono kwa atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa mgombea wa urais
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Edmundo González (kulia), mgombea urais aliye uhamishoni, pamoja na kiongozi wa upinzani María Corina Machado (kushoto) Julai 2024.
Serikali ya Venezuela imetangaza zawadi ya dola za kimarekani 100,000
(£81,000) kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa mgombea
urais wa upnde wa upinzani Edmundo González aliye uhamishoni.
Alitoroka nchini Venezuela mwezi Septemba na akapewa hifadhi
ya kisiasa nchini Uhispania baada ya Venezuela kuamuru akamatwe,
wakimtuhumu González kwa njama na kughushi nyaraka.
González ameapa atarejea Venezuela kabla ya kuapishwa
kwa Rais Nicolas Maduro Ijumaa ijayo, akiishutumu serikali kwa kuiba kura.
Muda mfupi baada ya kitita hicho kutangazwa, González
alisema anasafiri kwenda Argentina kuanza ziara yake Amerika Kusini, ambapo
atakutana na Rais mkosoaji mkali wa Maduro, Javier Milei siku ya Jumamosi.
Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeiamuru
Venezuela "kujizuia kuharibu" hesabu za kura za uchaguzi wa rais wa
Julai 2024.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CNE) inayoungwa mkono na serikali
ilimtangaza Maduro, kuwa mshindi lakini ilishindwa
kutoa hesabu za kura ili kuunga mkono ushindi huo.
Upinzani, kwa msaada wa mashahidi walioidhinishwa ulikusanya
na kuchapisha zaidi ya 80% ya hesabu za kura, unasema hizo zinathibitisha kuwa mgombea wake, González, alikuwa mshindi kwa kupata wingi wa
kura.
González hakuwa maarufu sana nchini Venezuela alipojiandikisha
kama mgombeaji wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo mwezi Machi. Hakuwahi kugombea nyadhifa za umma hapo awali na hata hakujulikana
sana katika duru za upinzani.
Lakini miezi kadhaa baada ya kuamua kugombea wadhifa wa juu,
mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya chini wa zamani alimshinda Maduro katika kura za maoni.
Venezuela imeshuhudia mgawanyiko kati ya serikali na wafuasi
wa upinzani ukizidi kuwa mkubwa katika muongo mmoja uliopita.
Sauti ya maridhiano ya González wakati wa kampeni ya urais
ilikuwa tofauti kabisa na ile ya Maduro, ambaye alionya kuhusu "umwagaji
wa damu" iwapo González atashinda.
Uchaguzi wa
marudio wa 2018 uliomuweka Maduro madarakani ulipuuzwa na wengi kuwa haukuwa huru na wa haki.
Polisi
nchini Mauritius imemkamata gavana wa zamani wa benki kuu ya nchi hiyo siku ya
Ijumaa kuhusiana na uchunguzi wa kesi ya utapeli, vimeripoti vyombo vya habari
vya ndani katika taifa la kisiwa cha Bahari ya Hindi.
Mwezi
uliopita, kitengo cha polisi cha Mauritius cha kupambana na utakatishaji fedha
kilitoa amri ya kukamatwa kwa Harvesh Kumar Seegolam kutokana na kesi hiyo,
bila kutoa maelezo zaidi. Seegolam alikuwa nje ya nchi wakati agizo hilo
lilipotolewa.
"Gavana
wa zamani wa Benki ya Mauritius, Harvesh Seegolam, alikamatwa alipowasili
katika uwanja wa ndege wa Plaisance Ijumaa ya Januari 3," imeripoti Le
Défi Media Group.
Msemaji
wa polisi amethibitisha kukamatwa kwake lakini alikataa kutoa maelezo yoyote.
Na pia wakili wa Seegolam, hajaeleza chochote.
Kukamatwa
huko pia kuliripotiwa na vyombo vingine likiwemo gazeti la kila siku la
l'Express.
Kukamatwa
kwa gavana huyo wa zamani ni hatua ya kwanza kubwa ya serikali ya Waziri Mku,
Navin Ramgoolam, ambaye amesema serikali iliyopita ilighushi pato la taifa,
nakisi ya bajeti na takwimu za deni la umma kwa miaka mingi.
Ukungu watatiza shughuli za maisha na usafari India
Chanzo cha picha, ANI
Ukungu mzito umetanda
Delhi na maeneo ya kaskazini mwa India, na kusababisha changamoto za ucheleweshaji
wa safari na taharuki.
Zaidi ya safari
100 za ndege zilicheleweshwa katika uwanja wa ndege wa Delhi siku ya Ijumaa
asubuhi, kwa mujibu wa shirika la habari la PTI. Mamia ya safari za garimoshi
pia zimepangwa upya, au kuchelewa.
Mamlaka ya hali
ya hewa nchini India imesema kuwa hali ya ukungu huenda ikaendelea kwa siku
chache zijazo.
Ukungu mzito ni
kawaida katika kipindi hiki cha mwaka huko Delhi na maeneo mengine ya kaskazini
mwa India, wakati eneo hilo likikabiliwa na wimbi la baridi kali.
Picha na video
zilionyesha miji kadhaa iliyogubikwa na ukungu mzito.
Takriban viwanja
vya ndege tisa kikiwemo kile cha Delhi vimeripotiwa kutoonekana vizuri Ijumaa
asubuhi, Idara ya Hali ya Hewa ya India (IMD) ilisema.
Uwanja wa ndege
wa Delhi umetoa ushauri kwa abiria, na kuwataka kuchukua tahadhari kutokana na kuahirishwa kwa safari.
"Wakati
kutua na kupaa kukiendelea kwenye uwanja wa ndege wa Delhi, safari za ndege
ambazo hazifuati mfumo wa CAT III zinaweza kuathiriwa," taarifa ya uwanja
wa ndege ilieleza ikirejelea mfumo wa rada ambao huwezesha kutua wakati kuna muonekano
hafifu sana.
Mashirika kadhaa
ya ndege pia yametoa taarifa kuwataka wasafiri kuangalia ratiba za ndege kabla
ya kupanga safari zao.
IMD inachukulia hali
ya ukungu kuwa "mzito" ikiwa mwonekano unapungua chini ya 200m na
"mzito sana" ikiwa utashuka chini ya 50m.
Idara ya hali ya
hewa imesema kuwa Delhi inaweza kupata mvua nyepesi hadi wastani mnamo 6
Januari, ambayo huenda ikapunguza zaidi joto.
Watu wawili wafariki baada ya ndege ndogo kuanguka katika jengo la California
Maelezo ya picha, Wawili wafariki baada ya ndege ndogo kugonga paa la kiwanda huko California
Watu wawili wamefariki na wengine 18 kujeruhiwa baada ya
ndege ndogo kuanguka katika jengo la kibiashara kusini mwa California, maafisa
wanasema.
Watu kumi walipelekwa hospitalini wakiwa na majeraha,
Idara ya Polisi ya Fullerton ilisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii X
Alhamisi, huku wengine nane wakitibiwa majeraha na kuruhusiwa kuondoka eneo la
tukio.
Ndege hiyo yenye injini moja aina RV-10 ilianguka saa
14:15PST (20:15GMT), kwa mujibu wa mamlaka ya Usafiri wa Anga.
Maafisa hawajatoa maelezo zaidi kuhusu namna ajali hiyo
ilivyotokea.
Haijabainika iwapo watu wawili waliofariki walikuwa
wafanyakazi au abiria ndani ya ndege hiyo.
Polisi wanasema wanahamisha majengo katika eneo hilo, na
kuutaka umma kukaa mbali na eneo la ajali.
Mbunge Lou Correa, ambaye anawakilisha eneo la Kaunti ya
Orange, lenye umbali wa maili 25 (40km) kusini mwa Los Angeles, alisema kuwa
jengo lililoangukiwa na ndege hutumika kwa biashara ya kutengeneza samani.
Picha za angani za eneo la tukio zinaonyesha baadhi ya
mabaki ya ndege ndani ya jengo hilo.
Ajali hiyo pia ilizua moto ambao ulizimwa na maafisa wa
zima moto.
Picha za usalama zilizorekodiwa kutoka kwenye jengo
hilo, kando ya barabara zinaonyesha mlipuko mkali, vimeeleza vyombo vya habari
vya eneo hilo.
"Watu wanatetemeka kutokana na
hali hiyo," shahidi Mark Anderson aliambia KRCA-TV.
"Ilikuwa ni kishindo kikubwa
tu, na kisha mmoja wa watu akatoka nje na kusema, 'Ee Mungu wangu, jengo
linawaka moto.'
Mahali ambapo ndege ilianguka ni
karibu na Uwanja wa Ndege wa Manispaa wa Fullerton, takriban maili 6 (kilomita
10) kutoka Disneyland.
Ndege hiyo inaonekana kurejea
katika uwanja wa ndege muda mfupi baada ya kupaa, kulingana na KRCA-TV.
Takriban watu 100 hatimaye
walihamishwa kutoka kiwanda cha samani cha Michael Nicholas Designs, kwa mujibu
wa gazeti la Orange County Register.
Juanita Ramirez, mfanyakazi,
aliambia gazeti hilo kwamba alisikia kishindo kikubwa kabla ya kuona mlipuko mkubwa
wa moto ukiruka kuelekea kwake.
Hii ni ndege ya pili kuanguka
katika eneo hilo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kwa mujibu wa CBS,
mshirika wa BBC nchini Marekani.
Mnamo tarehe 25
Novemba, ndege nyingine ilianguka kwenye mti karibu na eneo la ajali hii.
Mashirika ya kiraia Kenya yataka kesi za utekaji nyara zipelekwe ICC
Mashirika
mawili ya kiraia nchini Kenya yameiomba mahakama kuu ya nchi hiyo kumshurutisha
Mwanasheria Mkuu, Dorcas Oduor kupeleka kesi za utekaji nyara na kupotea kwa watu katika taifa hilo la Afrika Mashariki,
katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uchunguzi na hatua zaidi, limeripoti
gazeti la The Standard.
Kituo
cha Sheria na Kituo cha Haki za Kijamii cha Mathare vilisema hapo jana kwamba, ni
wazi kuwa Polisi inashindwa kutekeleza jukumu lake la kulinda watu katika
jamhuri hiyo.
"Inavyoonekana
ni kuwa Jeshi la Polisi halina uwezo wa kufanya upelelezi, mahakama hii ina
wajibu wa kuwalinda na kuwatetea watu wa Kenya kwa kupeleka suala la kupotea kwa
watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai."
Takribani
watu 82 ambao wanaelezwa kuwa ni wakosoaji wa serikali wametekwa nyara tangu
maandamano kuhusu mapendekezo ya nyongeza ya ushuru yalitikisa nchi hiyo Juni
2024, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya.
Polisi
wamekanusha kuhusika na kusema watachunguza kutoweka kwa watu hao.
Ndege 22 zisizo na rubani zimedunguliwa usiku kucha - Urusi
Chanzo cha picha, Reuters
Wizara ya Ulinzi ya Urusi inadai kuwa ndege zisizo na rubani 22 za
Ukraine zilidunguliwa katika maeneo sita ya Urusi usiku kucha, ikiwa ni pamoja
na yale yaliyo mbali na mipaka ya Ukraine.
Ujumbe mfupi kutoka kwenye mitandao ya kijamii ya wizara hiyo unasema kuwa ndege 10 zisizo na rubani
zilidunguliwa katika eneo la Bryansk, nne kila moja katika mikoa ya Oryol na
Rostov, mbili katika mkoa wa Belgorod, na droni moja kila moja katika mikoa ya
Volgograd na Lipetsk.
Huku hayo yakijiri, Katika
mji mkuu Kyiv, nyumba ya kibinafsi
iliwaka moto baada ya na kuangukiwa na uchafu kutoka kwa droni iliyoungua.
Kulingana na mkuu mpya
wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, Timur Tkachenko, moto huo uliozuka katika wilaya ya Darnitsky kusini
mashariki mwa mji mkuu, tayari umezimwa.
"Waokoaji walizima
moto, habari kuhusu waathiriwa wa tukio hilo bado hazijatolewa."
Ndege nyingine isiyo na
rubani ya kamikaze ya Urusi ilitunguliwa kwenye wilaya ya Goloseevsky kusini
mwa Kyiv, kulingana na meya wa Kyiv Vitaliy Klitschko.
Jaribio la kumkamata rais wa Korea Kusini Yoon lasitishwa baada ya mzozo mkali
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wachunguzi wanasema wataamua juu ya hatua zinazofuata baada ya kufanya upya tathmini
Wachunguzi
wa Korea Kusini wamesitisha jaribio la kumkamata rais aliyesimamishwa kazi Yoon
Suk Yeol baada ya mvutano mkali wa saa sita na timu ya usalama nje ya nyumba
yake.
"Tumebaini kwamba kukamatwa hakuwezekani," ilisema ofisi ya upelelezi wa ufisadi
(CIO), ambayo imekuwa ikichunguza tamko la amri ya sheria la kijeshi la muda
mfupi lililotolewa na Yoon.
"Hatua
zinazofuata zitaamuliwa baada ya kutathminiwa upya," CIO ilisema, na
kuongeza kuwa "kukataa kutekeleza mchakato wa kisheria" kwa Yoon
"kunasikitisha sana".
Wafuasi wa Yoon, ambao wamepiga
kambi mbele ya makao ya rais kwa siku kadhaa, walishangilia kwa wimbo na densi
huku hatua ya kusitisha kukamatwa kwake ikitangazwa. "Tumeshinda!"
waliimba.
CIO ilisema kuwa wasiwasi juu ya usalama
wa timu uwanjani ni sababu nyingine katika uamuzi wao wa kusitisha jaribio la
kukamatwa.
Wachunguzi
wana hadi Januari 6 kumkamata Yoon kabla ya hati ya sasa kuisha. Wanaweza, hata
hivyo, kutuma maombi ya hati mpya na kujaribu kumweka kizuizini tena.
Tangu
asubuhi na mapema, makumi ya gari za polisi zilijipanga barabarani nje ya
makazi ya Yoon katikati mwa Seoul.
CIO ilisema kuwa wasiwasi juu ya usalama
wa timu uwanjani ni sababu nyingine katika uamuzi wao wa kusitisha jaribio la
kukamatwa.
Wachunguzi
wana hadi Januari 6 kumkamata Yoon kabla ya hati ya sasa kuisha. Wanaweza, hata
hivyo, kutumpa maombi ya hati mpya na kujaribu kumuweka kizuizini tena.
Tangu
asubuhi na mapema, makumi ya gari za polisi zilijipanga barabarani nje ya
makazi ya Yoon katikati mwa Seoul.
Mwanaume wa Marekani aliyewauwa watu 15 New Orleans alitekeleza shambulio peke yake, FBI yasema
Chanzo cha picha, FBI
Mwanajeshi wa zamani wa Jeshi la Marekani aliyewauwa watu 15 kwa
kugonga lori kwenye umati wa watu waliokuwa wakisherehekea sikukuu ya mwaka mpya
huko New Orleans alikuwa ameahidi utiifu kwa Islamic State na alionekana
kurekodi ambapo alilaani muziki, dawa za kulevya na pombe.
Aamsud -Din Jabbar, mzaliwa wa
Texas mwenye umri wa miaka 42 ambaye aliwahi kuhudumu nchini Afghanistan, alitekeleza
peke yake k shambulio hilo, FBI ilisema
Alhamisi, ikibadilisha tathmini ya awali kwamba anaweza kuwa na washirika.
Aliuawa katika makabiliano ya risasi na polisi baada ya shambulio hilo,
ambalo pia lilijeruhi makumi ya watu na limetajwa na FBI kama kitendo cha
kigaidi.
"Ilikusudiwa na ni kitendo
kiovu," Naibu mkurugenzi msaidizi wa FBI Christopher Raia aliuambia
mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, akithibitisha hitimisho la
ofisi hiyo kwamba Jabbar alihamasishwa na Islamic State, kundi la wanamgambo
lenye wapiganaji nchini Iraq na Syria.
Msomali anayesafiri kwa pikipiki hadi ncha ya kusini mwa Afrika alivyofurahishwa na kabila la Tanzania
Chanzo cha picha, Faisal
Faysal Abdullahi Abdi
ni kijana mdogo wa Kisomali ambaye yuko katika safari ya pikipiki kwenda nchi
za Kiafrika.
Safari hii ni safari
ya kujifunza na kupata uzoefum Faisal aliiambia BBC.
Faisal alianza safari
hii kutoka Nairobi, akapitia mikoa ya Somalia ya Kenya Kaskazini Mashariki,
Mombasa, kisha Tanzania, ambako alienda hadi Malawi alipo sasa.
"Ninajaribu
kukumbuka safari yangu na kuwanufaisha vijana wa Somalia. Ninatumia mitandao ya
kijamii na kutuma taarifa kuhusu safari yangu baadaye kwa maandishi na
matangazo," Faisal Abdullahi Ali alisema kwa BBC.
Faisal alisema kuwa
aliamua gharama ya safari hii na anaifadhili yeye mwenyewe.
Katika safari hii,
anataka kufikia ncha ya kusini kabisa ya bara la Afrika Kusini.
"Sehemu ya
kuvutia zaidi ya safari yangu ilikuwa Kabila la Hadzabi, kabila pekee duniani
ambalo liko mbali na ustaarabu na linaishi kwa kutegemea uwindaji ,"
alisema Faisal.
Safari ya kufurahisha
Chanzo cha picha, Fasal
Kabila hili linaishi
kaskazini mwa Tanzania na ni moja ya makabila ambayo bado yanaishi katika
misitu ya mbali ya nchi hiyo.
Faisal alisema kwamba
amependezwa na maisha ya watu hawa.
"Wanapoishi na
kile wanachovaa kinavutia, kwahivyo unajiuliza je tuliishi hivi zamani?"
Alisema Faisal.
Katika siku za hivi
karibuni, kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaosafiri kwa pikipiki katika
mabara na nchi zinazotaka kufikia malengo tofauti.
Baadhi ya watu hawa
wanataka kuweka rekodi mpya katika uwanja wa usafiri, wakati wengine
wanatengeneza habari ili kutangaza, wakati wengine wanataka kupata uzoefu.
Chanzo cha picha, Faisal
Maelezo ya picha, Faisal ni kijana MwanaYouTube aliyezaliwa na kukulia huko Garisa katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya.
Kizaazaa kikubwa mjini Seoul huku wachunguzi wakijaribu kumkamata rais wa Korea Kusini
Chanzo cha picha, AFP
Ofisi ya Juu ya upelelezi wa uhalifu wa viongozi wa Umma inayopeleleza makosa ya ufisadi ilitangaza
kwamba itaanza kutekeleza agizo la kukamatwa kwa Rais Yoon Seok-yeol saa 8:07
za asubuhi asubuhi Ijumaa tarehe 3,
lakini jaribio hilo limezuiwa.
Inaarifiwa kuwa
wachunguzi na maafisa wa polisi wapatao 80 kutoka Shirika la Uchunguzi wa
Ufisadi walioingia kwenye lango kuu la makazi ya Yongsan wako kwenye mtafaruku,
wameshindwa kuingia ndani ya jengo hilo kutokana na kizuizi cha ulinzi.
Magari yaliyokuwa
yamewabeba wachunguzi wa taasisi ya uchunguzi wa rushwa yaliondoka katika eneo
la Serikali ya Gwacheon mwendo wa saa 6:14 asubuhi na kufika karibu na makazi
ya Rais huko Hannam-dong mwendo wa saa 7:20 asubuhi.
Kwasababu lango
kuu lilikuwa limefungwa na magari, wachunguzi wapatao 80 kutoka Ttasisi ya uchunguzi wa rushwa na polisi waliingia ndani ya nyumba hiyo kwa miguu.
Majibizano mengine yalizuka na wafanyakazi wa usalama, lakini waliingia lango
kuu bila mzozo wowote mkubwa.
Ofisi ya Uchunguzi
wa Ufisadi, ilishindwa kuingia ndani ya jengo hilo kutokana na walinzi
kuwazuia.
Wachunguzi wana hadi
tarehe 6 Januari kumkamata Yoon, kabla ya hati hiyo kuisha muda wake.
Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Gari lililokuwa limebeba wachunguzi wa shirika la uchunguzi wa Ufisadi liliwasili karibu na Makazi ya Rais huko Yongsan mwendo wa saa 7:20 asubuhi.
Sio mara ya kwanza
kushindwa kumkamata Yoon
Mnamo tarehe 2,
polisi walikadiria kuwa maelfu hadi 10,000 walikusanyika karibu na makazi ya
rais huko Hannam-dong, Yongsan-gu, Seoul. Wawakilishi Yoon
Hapo awali, ofisi ya Upelelezi wa ufisadi
ilipokea hati ya kukamatwa na hati ya upekuzi kutoka kwa mahakama mnamo tarehe
31 mwezi uliopita baada ya Rais Yoon kushindwa kujibu agizo la kujisalimisha
mara tatu.
Ingawa hakukuwa na
ajali kubwa katika eneo la tukio, baadhi ya wafuasi walipambana na polisi na
washiriki wa maandamano ya kupinga mashtaka waliokuwa karibu, wakipaza sauti
zao, au kulala chini barabarani na kuchukuliwa na polisi, na kusababisha hali
ya migogoro.