Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ireland, Norway, na Uhispania kulitambua taifa la Palestina

Mataifa ya Ulaya Ireland, Norway, na Uhispania yametangaza hivi punde kulitambua taifa la Palestina

Muhtasari

  • Urusi ilirusha silaha ya kushambulia satelaiti - Marekani:
  • UN yasitisha usambazaji wa chakula Rafah
  • Moshi wa jenereta wawaua wanafunzi Nigeria - ripoti
  • Kiongozi mkuu wa Iran aongoza ibada ya mazishi ya Raisi
  • Ni nchi ngapi zimetambua taifa la Palestina?
  • Ireland, Norway, na Uhispania kulitambua taifa la Palestina
  • Umati wa watu wakusanyika kabla ya mazishi ya rais wa Iran
  • Ukraine yapata mafanikio katika vita vingine - kupambana na ufisadi
  • Israel yabatilisha uamuzi wa kufunga matangazo ya moja kwa moja ya shirika la habari la Associated Press Gaza
  • Kamanda wa zamani wa jeshi la Urusi ashikiliwa kwa tuhuma za ulaghai
  • Kenya yatetea gharama ya ndege kwa safari ya Rais Ruto Marekani
  • Marekani yaashiria uwezekano wa vikwazo dhidi ya ICC juu ya vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa Israel

Moja kwa moja

Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Mpango wa Urusi wa kuhamisha mipaka ya bahari wazua hofu katika mataifa ya Baltic

    Kumekuwa na wito wa utulivu nchini Finland na mataifa ya Baltic baada ya rasimu ya amri ya Urusi iliyopendekeza kurekebisha mipaka yake katika Bahari ya Baltic.

    Latvia ilisema inajaribu kufafanua hali hiyo, lakini Lithuania ilionya kwamba Kremlin ilikuwa na lengo la kuwatisha majirani zake na "uchochezi wa makusudi, unaolenga kuongezeka".

    Rais wa Finland Alexander Stubb alisema viongozi wa kisiasa wanafuatilia hali hiyo kwa karibu na "kuchukua hatua kama kawaida: kwa utulivu na kwa kuzingatia ukweli".

    Rasimu ya amri ya wizara ya ulinzi ya Urusi inapendekeza kuhamishwa kwa mipaka ya bahari inayozunguka visiwa vya Urusi katika Ghuba ya Finland na kuzunguka eneo la Kaliningrad.

    Amri hiyo iliangaziwa kwa mara ya kwanza Jumanne, wakati shirika la habari la Tass la Urusi na vyombo vingine vya habari viliripoti juu ya pendekezo lake la kuchora upya mipaka ya zamani ya enzi ya Sovietimnamo Januari 1985.

    Haijabainika ikiwa rasimu ilipendekeza kupanua mipaka yake katika maji ya Finland katika maji ya Baltic au Luthuania karibu na Kaliningrad.

    Lakini, ingejumuisha eneo la Ghuba ya mashariki ya Ufini, visiwa kadhaa karibu na pwani ya Finland na maeneo karibu na miji miwili ya Baltiysk na Zelenogradsk huko Kaliningrad.

    Finland na nchi za Baltic zote ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, EU na Nato na muungano huo wa kijeshi umejitolea kulinda mipaka yao.

  3. Urusi ilirusha silaha ya kushambulia satelaiti - Marekani

    Marekani inasema Urusi wiki iliyopita ilirusha silaha ambayo inaamini inaweza kuwa na uwezo wa kushambulia setilaiti.

    "Urusi ilirusha setilaiti kwenye mzunguko wa chini ya sayari ya Dunia ambayo tunatathmini uwezekano kuwa silaha ya anga ya juu," alisema msemaji wa Pentagon Brig General Pat Ryder Jumanne jioni.

    Ilikuwa kwenye "mzunguko sawa" na satelaiti ya serikali ya Marekani, alisema, akiongeza kuwa Washington itaendelea kufuatilia hali hiyo na inapaswa kuwa tayari kulinda maslahi yake.

    Urusi haijatoa maoni hadharani kuhusiana na suala hilo.

    Moscow na Washington - wapinzani wawili wa kimataifa - wametofautiana mara kwa mara juu ya suala la silaha za anga za juu katika Umoja wa Mataifa katika wiki za hivi karibuni, huku pande zote mbili zikituhumiana kutafuta uwezo zaidi wa kijeshi.

    Mapema Jumanne msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova alidai kuwa Marekani ilikuwa inatataka kubadilisha anaga za juu kuwa "uwanja wa makabiliano ya kijeshi".

    Wataalam wa kijeshi wameonya kwa muda mrefu kwamba anaga za juu inaweza kuwa ngome ya pili ya vita katika ulimwengu unaozidi kutegemea teknolojia.

    Tangu ilipoanzisha uvamizi kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, Urusi imeonya kwamba satelaiti za Marekani zinazosaidia jeshi la Ukraine zinaweza kuwa shabaha halali.

    Mnamo Februari, Ikulu ya White House ilikiri kwamba Urusi ilikuwa ikitengeneza silaha mpya "ya kusumbua" ya anga, lakini ikasisitiza kwamba ilikuwa bado haijaitumia.

    Ilikuja baada ya mbunge mkuu wa chama cha Republican kutoa onyo la siri kuhusu tishio kubwa la usalama wa taifa, na kuzua uvumi mkali Washington DC.

    Maelezo zaidi:

  4. Vita vya Gaza: UN yasitisha usambazaji wa chakula Rafah

    Usambazaji wa chakula katika mji Rafah kusini mwa Gaza umesitishwa kutokana na ukosefu wa vifaa na ukosefu wa usalama, Umoja wa Mataifa unasema.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, Unrwa, lilionya kituo chake cha usambazaji na ghala la Mpango wa Chakula Duniani sasa haziwezi kufikiwa kwa sababu ya hatua zinazoendelea za kijeshi za Israel dhidi ya Hamas mashariki mwa Rafah.

    Takriban watu 810,000 kati ya zaidi ya milioni moja wanaokimbilia Rafah wamekimbia tangu operesheni ya Israel ilipoanza tarehe 6 Mei.

    Unrwa pia alisema vituo vyake vya afya havijapokea vifaa vya matibabu katika siku 10 zilizopita.

    Hayo yanajiri huku Marekani ikisema haiamini kuwa tani 569 za chakula na misaada mingine iliyoingia Gaza kupitia bandari ya kuelea iliyokamilika hivi karibuni imesambazwa kwa Wapalestina na mashirika ya misaada.

    Siku ya Jumamosi, umati wa Wapalestina waliokuwa wakihitaji chakula walikamata malori kadhaa ya WFP yaliyokuwa yakisafirisha misaada kutoka bandari hiyo ya muda kuelekea kwenye ghala katikati mwa mji wa Deir al-Balah, jambo ambalo lilisababisha shirika hilo kusimamisha shughuli ya usafirishaji.

    WFP ilisema usambazaji umesitishwa huku Umoja wa Mataifa ukipanga njia mpya ili kuepusha msongamano wa watu.

    Wakati huo huo, mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni alionya kwamba hospitali kubwa zaidi ambayo haifanyi kazi kwa sehemu kaskazini mwa Gaza iliripotiwa kupigwa mara nne siku ya Jumanne, wakati mapigano yakipamba moto kati ya vikosi vya Israeli na vikundi vyenye silaha vya Palestina katika eneo la karibu la Jabalia.

    Jeshi la Israel limesema linakagua ripoti kutoka kwa matabibu katika hospitali ya Kamal Adwan huko Beit Lahia kwamba idara yake ya dharura ilishambuliwa na makombora ya Israeli, na kuwalazimisha kuwakimbiza wagonjwa kwenye vitanda vya hospitali hadi mitaani nje.

    WHO pia ilisema hospitali ya al-Awda huko Jabalia imezingirwa tangu Jumapili, huku makumi ya wafanyikazi, wagonjwa na watu walioandamana nao wamekwama ndani.

  5. Moshi wa jenereta wawaua wanafunzi Nigeria - ripoti

    Takriban wanafunzi saba wa chuo kikuu wamefariki baada ya kuvuta moshi kutoka kwa jenereta katika studio ya muziki katika jimbo la Bayelsa lenye utajiri wa mafuta nchini Nigeria.

    Vijana hao wanasemekana kufanya kazi hadi Jumatatu usiku na kulala kwenye studio iliyofungwa huku jenereta ikiendelea kufanya kazi.

    Wanashukiwa kupungukiwa na hewa ya kaboni lakini polisi wanasema uchunguzi unaendelea.

    Biashara na kaya nyingi nchini Nigeria zinategemea jenereta zinazotumia dizeli au petroli kwa sababu ya ugavi wa umeme usiotosheleza.

    Miili sita ilipatikanaJumanne asubuhi, huku mmoja wao, aliyepatikana akiwa amepoteza fahamu, akikimbizwa katika hospitali ya karibu lakini akafariki baadaye, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Wakazi wa eneo hilo walipiga kelele walipochungulia kupitia dirisha la studio na kuona miili hiyo ikiwa imetapakaa sakafuni.

    Polisi walifika na kuzingira eneo hilo baada ya kuhamisha miili katika eneo la Amarata la Yenagoa - mji mkuu wa jimbo la Bayelsa.

    "Uchunguzi unafanywa lakini kulingana na kile tumeona, sumu ya kaboni kutokana na moshi wa jenereta huenda imechangia vifo hivi," msemaji wa polisi Musa Mohammed aliambia BBC.

    Walioathiriwa walikuwa ni wahitimu wa shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Niger Delta (NDU) kinachomilikiwa na serikali huko Amassoma, ambao walijihusisha na biashara ya kurekodi muziki ili kujikimu kimaisha wanapoendelea na masomo yao.

    Hii si mara ya kwanza kwa moshi wa jenereta kuua watu nchini Nigeria, mzalishaji mkuu wa mafuta barani Afrika.

    Mnamo 2009, angalau wanafamilia 13, wakiwemo watoto wanne, walikufa baada ya kuvuta moshi yenye sumu kutoka kwa jenereta yao ya umeme walipokuwa wamelala katika kijiji cha kusini-mashariki mwa jimbo la Imo.

  6. Kiongozi mkuu wa Iran aongoza ibada ya mazishi ya Raisi

    Kiongozi mkuu wa Iran ameongoza mazishi ya marehemu rais wa nchi hiyo, waziri wa mambo ya nje na wengine waliofariki katika ajali ya helikopta siku ya Jumapili.

    Ayatullah Ali Khamenei aliongoza sala ya mazishi katika Chuo Kikuu cha Tehran.

    Rais Ebrahim Raisi alifariki dunia pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wengine sita katika ajali ya helikopta karibu na mpaka na Azerbaijan.

    Mamlaka ilikuwa imeonya maandamano dhidi ya mazishi na ujumbe wa matusi mtandaoni.

    "Ee Mwenyezi Mungu, hatukuona chochote isipokuwa kheri kutoka kwake," Ayatollah Khamenei alisema katika sala ya kawaida ya wafu kwa Kiarabu.

    Kaimu rais wa Iran, Mohammad Mokhber, alisimama karibu na kulia hadharani wakati wa ibada.

    Kisha watu walibeba jeneza kwenye mabega yao, huku kelele za "Kifo kwa Marekani" zikisikika nje.

    Walizipakia kwenye trela na kuendeshwa katikati ya jiji la Tehran hadi Azadi Square, ambapo hayati rais Rais alikuwa akitoa hotuba siku za nyuma.

    Waliohudhuria walikuwa viongozi wakuu wa Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi la Iran, moja ya asasi yenye nguvu nchini.

    Pia alikuwepo Ismail Haniyeh wa Hamas, kundi la wanamgambo ambalo Iran imewapa silaha na kuwaunga mkono wakati wa vita vinavyoendelea vya Israel na Hamas.

    Haniyeh anachukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Hamas na amekuwa mwanachama mashuhuri wa kundi hilo tangu 1980.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimeliorodhesha kuwa gaidi mwaka wa 2018.

    Soma pia:

  7. Ni nchi ngapi zimetambua taifa la Palestina?

    Takriban nchi 140 zimelitambua taifa la Palestina, kulingana na barua ya hivi majuzi kwa Umoja wa Mataifa.

    nchi hizo zinajumuisha wanachama wa Kundi la nchi 22 za Kiarabu katika Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Nchi 57 za Ushirikiano wa Kiislamu na Harakati Zisizofungamana na Siasa zenye wanachama 120.

    Uingereza na Marekani ni miongoni mwa mataifa ambayo hayaitambui rasmi taifa la Palestina.

    Mapema mwezi huu waziri wa mambo ya nje Bwana Cameron alipendekeza kuwa serikali, pamoja na washirika wake, inaweza "kuangalia suala la kulitambua taifa la Palestina, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa".

    Israel haitambui utaifa wa Palestina na serikali ya sasa ya Israel inapinga kuundwa kwa taifa la Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza. Inasema kuwa hali kama hiyo itakuwa tishio kwa uwepo wa Israeli.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Habari za hivi punde, Ireland, Norway, na Uhispania kulitambua taifa la Palestina

    Mataifa matatu ya UlayaMataifa ya Ulaya, Ireland, Norway, na Uhispaniayametangaza hivi punde kulitambua taifa la Palestina

    Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ametangaza hivi punde kwamba nchi yake italitambua jimbo la Palestina tarehe 28 Mei.

    Akiwa mjini Madrid, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alipigiwa makofi bungeni alipotangaza uamuzi wa taifa hilo wa Azama ya kuiunga mkono Palestina kama taifa: "Tunaenda kuitambua Palestina kwa sababu nyingi na tunaweza kuhitimisha hilo kwa maneno matatu - amani, haki na uthabiti," anasema.

    "Tunapaswa kuhakikisha kuwa suluhisho la serikali mbili linaheshimiwa na lazima kuwe na dhamana ya usalama ya pande zote.

    "Ni muhimu kwa pande hizo mbili kujadiliana kwa ajili ya amani na ni kwa sababu hii kwamba tunaitambua Palestina."

    Huko Dublin, waziri mkuu wa Ireland anasema suluhisho la serikali mbili ndio "njia pekee inayoaminika" kwa amani.

    Simon Harris anaongeza: "Tuna miongo mitatu baada ya mchakato wa Oslo, na labda zaidi kuliko hapo awali kutoka kwa usuluhishi wa haki, endelevu na wa kina."

    Anasema uamuzi haupaswi kusubiri "kwa muda usiojulikana" wakati ni "jambo sahihi la kufanya".

    Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Norway Jonas Gahr Store anasema nchi hiyo itatambua taifa la Palestina - kuthibitisha ripoti za awali.

    Waziri wa mambo ya nje wa Norway amechapisha kwenye X kuhusu uamuzi wa nchi hiyo "kuitambua Palestina kama taifa".

    Espen Barth Eide anasema: "Suluhu ya mataifa mawili ndiyo njia pekee ya amani kwa Israeli na Palestina."

    Anaongeza: "Katika wakati huu muhimu, kutambuliwa kwetu kunakuja katika kuunga mkono kazi kuelekea mpango wa amani wa kikanda."

    Unaweza pia kusoma:

  9. Umati wa watu wakusanyika kabla ya mazishi ya rais wa Iran

    Umati mkubwa wa watu umeanza kukusanyika katika mji mkuu wa Iran Tehran kwa ajili ya mazishi ya marehemu Rais wa nchi hiyo Ebrahim Raisi.

    Bw Raisi alifariki pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wengine sita katika ajali ya helikopta siku ya Jumapili karibu na mpaka na Azerbaijan.

    Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ataongoza sala katika mji mkuu, kabla ya majeneza yaliyofunikwa bendera ya Iran kupelekwa katika uwanja mkuu wa Azadi mjini humo.

    Mamlaka imeonya dhidi ya maandamano ya kupinga mazishi hayo na ujumbe wa matusi mtandaoni.

    Kote katika mji mkuu, mabango makubwa yamewekwa yenye ujumbe wa kumsifu Bw Raisi kama "mfia dini", huku mengine yakimuaga "mtumishi wa watu wasiojiweza".

    Runinga ya serikali ilionyesha mitaa iliyojaa waombolezaji, wengi wao wakiwa wamebeba picha za Bw Raisi au bendera ya Iran.

    Pia, viongozi wachache wa kigeni wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo.

    Soma zaidi:

  10. Ukraine yapata mafanikio katika vita vingine - kupambana na ufisadi

    Ukraine imepambana na ufisadi uliokithiri tangu siku za kwanza za uhuru wake mwaka 1991, na maafisa wa serikali na wanakampeni huru wanasema kuwa vita hivi ni muhimu katika kushinda vita vilivyopo na Urusi.

    Wamepata mafanikio fulani. Shirika la Kupambana na Ufisadi la Transparency International linaorodhesha Ukraine katika kiwango chake cha juu zaidi tangu 2006: kwa sasa ni ya 104 kati ya nchi 180 katika Fahirisi yake ya Mitazamo ya Ufisadi.

    "Taasisi nyingi za kupambana na rushwa za Ukraine zinaonyesha matokeo mazuri," Andriy Borovyk, mkurugenzi mtendaji wa Transparency International Ukraine, anaiambia BBC.

    Kulingana na yeye, moja ya matokeo kama hayo ni kukamatwa kwa mkuu wa Mahakama ya Juu Zaidi wakati huo, Vsevolod Knyazev, kwa mashtaka ya ufisadi mnamo mwezi Mei 2023.

    "Hii inaweza kuwa yenye kutoa matumaini kwasababu ukiona mtu amekamatwa, utafikiria mara mbili kabla ya kufanya ufisadi," alisema.

    Kumekuwa na watu wengine waliokamatwa wa ngazi ya juu pia, akiwemo waziri wa kilimo Mykola Solsky na afisa wa huduma ya ujasusi ya SBU, Artem Shylo.

    Wote watatu wanakana makosa yoyote na wameachiliwa kwa dhamana. Uchunguzi unaendelea.

    Soma zaidi:

  11. Israel yabatilisha uamuzi wa kufunga matangazo ya moja kwa moja ya shirika la habari la Associated Press Gaza

    Israel imerejesha vifaa vya kurushia matangazo vya shirika la habari la Associated Press, saa chache baada ya kuvichukua kusini mwa Israel na kuzima matangazo ya moja kwa moja ya shirika hilo la habari la Marekani huko Gaza.

    Waziri wa Mawasiliano Shlomo Karhi alibatilisha uamuzi huo, ambao umesababisha shinikizo la kimataifa kuongezeka.

    Ikulu ya White House ilionyesha wasiwasi wake, wakati shirika hilo la Kigeni liliposema linasikitishwa na "hatua za hivi punde za serikali ya Israel kukandamiza chombo hicho cha habari". Umoja wa Mataifa umeshutumu hatua hiyo na kuiita "ya kushtua".

    Makamu wa rais wa shirika la AP Lauren Easton alisema "inalaani kwa maneno makali hatua za serikali ya Israel".

    Bw Karhi alisema vifaa hivyo vilitwaliwa kwa sababu vilikiuka sheria mpya ya vyombo vya habari kwa kutoa picha za matangazo kwenye mtandao wa chombo cha Al Jazeera wenye makao yake nchini Qatar, ambacho imekipiga marufuku.

    Kauli yake ya hivi majuzi kwenye mtandao wa X ilisema: "Kwa kuwa Wizara ya Ulinzi inapenda kuchunguza suala la matangazo kutoka maeneo haya ya Sderot kwasababu ya hatari iliyopo kwa vikosi vyetu, sasa nimeamuru kufuta operesheni na kurudisha vifaa kwa shirika la AP, hadi uamuzi tofauti utakapotolewa na Wizara ya Ulinzi."

    Bw Karhi anadai picha zinazodaiwa kusambazwa zilikuwa zikionyesha "nafasi za vikosi vyetu kaskazini mwa Ukanda wa Gaza huku zikiwaweka hatarini kwa mujibu wa maoni ya usalama na uamuzi wa serikali".

    Mapema mwezi huu, wizara hiyo ilisitisha shughuli za chombo cha Habari cha Al Jazeera nchini Israel, ikiishutumu kuwa "msemaji wa Hamas" na kudhuru usalama wa taifa.

    Hata hivyo, Al Jazeera ilikanusha madai hayo na ikashutumu marufuku hiyo na kuiita "kitendo cha uhalifu" kinachokiuka haki za binadamu. Pia ilishutumiwa na mashirika ya wanahabari kama pigo kwa uhuru wa vyombo vya habari.

    Al Jazeera imeendeleza operesheni katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza unaokaliwa kwa mabavu, ambao waandishi wa habari wa kigeni wamepigwa marufuku kuingia tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas mwezi Oktoba.

    Soma zaidi:

  12. Kamanda wa zamani wa jeshi la Urusi ashikiliwa kwa tuhuma za ulaghai

    Kamanda wa zamani wa jeshi la Urusi ambaye aliibua wasiwasi kuhusu vifo vingi vya wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine amezuiliwa kwa tuhuma za ulaghai mkubwa.

    Meja Jenerali Ivan Popov, 49, atazuiliwa kwa miezi miwili, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi viliripoti.

    Wakili wake alinukuliwa na shirika la habari la Tass akisema jenerali huyo alikanusha madai yote.

    Jenerali Popov alifutwa kazi kama kamanda wa jeshi la 58 mwaka jana baada ya kudai hadharani vifo vya watu wengi na majeraha kati ya wanajeshi wa Urusi na ukosefu wa msaada wa mizinga.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi haijazungumzia suala hilo.

    Rais wa Urusi Vladimir Putin alizindua uvamizi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.

    Siku ya Jumanne, mashirika ya habari ya Tass na Ria Novosti ya Urusi yalitaja vyanzo vikisema kwamba Jenerali Popov alishukiwa kwa udanganyifu mkubwa, na kesi yake itasimamiwa na mahakama ya kijeshi ya 235.

    Soma zaidi:

  13. Kenya yatetea gharama ya ndege kwa safari ya Rais Ruto Marekani

    Serikali ya Kenya imetetea gharama ya safari ya Rais William Ruto nchini Marekani.

    Bei ya kukodisha ndege ya kibinafsi ya kifahari ambayo yeye na ujumbe wake walisafiria inakadiriwa kuwa $1.5m (£1.2m), kulingana na kituo cha kibinafsi cha runinga cha KTN nchini Kenya.

    "Faida za ziara hii ni kubwa kuliko mara milioni kama hizo," msemaji wa serikali Isaac Mwaura aliambia BBC, bila kuthibitisha gharama.

    Zaidi ya watu 30 akiwemo mcheshi maarufu wanaripotiwa kuandamana na rais huyo aliyetua Atlanta, Georgia siku ya Jumatatu.

    Bw Ruto yuko katika ziara ya siku nne kwa mwaliko wa mwenzake wa Marekani Joe Biden. Ni ziara ya kwanza ya kitaifa kwa rais wa Kenya nchini Marekani katika miongo miwili na ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Afrika katika kipindi cha miaka 16.

    Anatazamiwa kufanya mazungumzo na Bw Biden siku ya Alhamisi, yakiangazia ushirikiano wa kibiashara na usalama, ikiwa ni pamoja na ahadi ya Kenya kuongoza ujumbe wa mataifa mbalimbali kurejesha utulivu nchini Haiti.

    Lakini baadhi ya Wakenya wameeleza kughadhabishwa na kukodi ndege kutoka kampuni ya RoyalJet inayomilikiwa na Dubai kwa ajili ya safari hiyo badala ya kutumia ndege yake ya kawaida ya rais ikizingatiwa hatua za kubana matumizi ya serikali na kupanda kwa gharama ya maisha.

    Haijabainika ni kwa nini rais alichagua ndege hiyo ya kibinafsi lakini kumekuwa na wasiwasi wa usalama kuhusu ndege ya kawaida ya rais, inayojulikana kama Harambee One, ambayo ilinunuliwa takriban miaka 30 iliyopita.

    Serikali ya Marekani ilikanusha ripoti kwamba ililipia ndege iliyotumiwa na Bw Ruto na ujumbe wake.

    "Ili tu kuwa wazi: Marekani haikulipia ndege ya Rais Ruto kwenda Marekani," msemaji wa ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, aliwaambia waandishi wa habari.

    Haya yanajiri huku kukiwa na hasira kuhusu mipango ya serikali ya kutoza ushuru wa ziada, huku Bw Ruto akiwataka Wakenya kuishi kulingana na uwezo wao.

    Gharama ya mkate, uhamishaji wa pesa kwa njia ya simu, muda wa maongezi na data inatazamiwa kupanda huku serikali ikitafuta kuongeza ushuru wa ziada wa $2.4bn katika mwaka wa fedha unaoanza Julai.

    Wakosoaji wanasema ushuru huo unasaidia tu kufadhili ubadhirifu serikalini badala ya kuboresha huduma za umma.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Marekani yaashiria uwezekano wa vikwazo dhidi ya ICC juu ya vibali vya kukamatwa kwa viongozi wa Israel

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amependekeza kuwa atashirikiana na wabunge kuhusu vikwazo vinavyowezekana dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC), huku mwendesha mashtaka akitafuta kibali cha kukamatwa kwa maafisa wakuu wa Israel.

    Bw Blinken aliambia kikao cha bunge kuwa "amejitolea" kuchukua hatua dhidi ya "uamuzi huo wenye mwelekeo mbaya".

    Maoni yake yanawadia huku kukiwa na msukumo wa chama cha Republican kuwawekea vikwazo maafisa wa ICC, ambao huenda ukapiga kura wiki hii.

    Marekani si mwanachama wa mahakama hiyo lakini imeunga mkono mashtaka ya awali, ikiwa ni pamoja na hati ya ICC ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu vita vya Ukraine.

    Katika kikao cha Jumanne cha Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, James Risch, Mrepublican mwandamizi, aliuliza kama Bw Blinken angeunga mkono sheria ya kushughulikia ICC "kwa kuingilia masuala ya nchi zingine ambazo zina mfumo wa mahakama huru, halali na wa kidemokrasia".

    "Tunataka kufanya kazi nanyi kwa misingi ya pande mbili ili kupata mwelekeo unaofaa. Nimejitolea kufanya hivyo," waziri alisema.

    Bw Blinken alisema "hakuna swali inabidi tuangalie hatua zinazofaa za kuchukua ili kukabiliana na, tena, ni uamuzi gani wenye mwelekeo mbaya".

    Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Karim Khan alitangaza siku ya Jumatatu kuwa ametuma maombi ya hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant.

    Bw Khan pia anatafuta vibali vya kukamatwa kwa maafisa watatu wa Hamas - Yahya Sinwar, kiongozi wake huko Gaza, Mohammed Deif, kamanda wa tawi lake la kijeshi la Qassam Brigades, na Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi yake ya kisiasa.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 22/05/2024