Wanaume wawili
wa Kipalestina, waliojeruhiwa wakati wa operesheni ya kijeshi katika Ukingo wa
Magharibi unaokaliwa wiki jana, wameiambia BBC kwamba wanajeshi wa Israel
waliwalazimisha kuingia kwenye boneti ya jeep ya jeshi na kuwaendesha - wakati
mwingine kwa kasi - kwenye barabara za vijijini.
Maelezo hayo
yanawadia siku chache baada ya video ya Mujahid Abadi Balas mwenye umri wa
miaka 23 akining’inia kwenye boneti ya jeep hiyo hiyo ya jeshi la Israel
kuzusha hasira kimataifa.
BBC sasa
imezungumza na wanaume wawili wanaodai kutendewa kama hivyo wakati wa
operesheni huko Jabariyat, viungani mwa Jenin, Jumamosi iliyopita.
Samir Dabaya
mwenye umri wa miaka 25, ambaye sasa yuko hospitalini huko Jenin, anasema
alipigwa risasi mgongoni na wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni ya
Jabariyat, na alilala kifudifudi na kuvuja damu kwa saa nyingi, hadi wanajeshi
walipokuja kumtathmini hali yake.
Walipomgeuza
na kukuta yu hai, alipigwa na bunduki, anasema kabla ya kuokotwa, akabebwa hadi
kwenye gari aina ya jeep na kutupwa juu yake.
“Walinivua
[suruali]. Nilitaka kushikilia gari, lakini [mwanajeshi mmoja] alinigonga usoni
na kuniambia nisifanye hivyo. Kisha akaanza kuendesha gari,” alisema.
"Nilikuwa nikingojea kifo tu."
Samir
alituonyesha picha za video kutoka kwa kamera ya ulinzi ambayo inaonekana
ikimuonyesha akiwa nusu uchi, akiwa amelala kwenye jeep ya mwendo kasi, ikiwa
na alama ya namba 1 ubavuni.
Mahali
panaonekana kuendana na mahali ambapo operesheni hiyo ilifanyika, lakini hakuna
tarehe au saa inayoonekana kwenye rekodi.
Mwanaume
mwingine wa Palestina, Hesham Isleit, pia aliiambia BBC kwamba alipigwa risasi
mara mbili wakati wa operesheni huko Jabariyat na kulazimishwa kupanda kwenye
jeep hiyo hiyo ya kijeshi, iliyokuwa na nambari 1.
Alielezea
"kupigwa risasi kutoka pande zote" na kusema alijaribu kukimbia
lakini alipigwa risasi ya mguu, na kisha kikosi cha jeshi kilifika kumchukua
yeye na mtu mwingine.
"Walituamuru
tusimame, na wakatuvua nguo," alisema, "kisha wakalazimisha tupande
mbele ya jeep."
Gari lilikuwa moto sana, lilihisi "kama moto",
anasema.
“Nilikuwa peku na bila nguo. Nilijaribu kuweka mkono
wangu kwenye jeep lakini sikuweza, ilikuwa inawaka moto. Nilikuwa nikiwaambia liko
moto sana, na lakini wakinilazimisha kupanda - wakiniambia kwamba ikiwa sitaki
kufa, nifanye hivyo."
Tulitoa madai haya kwa jeshi la Israel; likasema kesi
hizo zinaendelea kuchunguzwa.