Zelensky anaonya Trump akishinda urais ataachana na Ukraine - The Guardian
Trump aliahidi mwaka jana kwamba ikiwa atamshinda Joe Biden, angekatiza msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kumaliza vita ndani ya saa 24.
Muhtasari
- Chelsea yamteua Maresca kama kocha mpya
- MrBeast aipiku T-Series kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi YouTube
- Nigeria yatumbukia gizani huku wafanyikazi wakigoma
- Kijana aliyenaswa kwenye video akimpiga polisi wa Kenya akamatwa
- Kocha wa Ujerumani alaani utafiti wa 'kibaguzi' uliofanywa na kituo cha televisheni
- Zelensky anaonya Trump akishinda urais ataachana na Ukraine - The Guardian
- 12 wauawa katika shambulio la bomu la Israel nchini Syria
- Yanga yatwaa ubingwa wa Shirikisho Tanzania ikiandikisha rekodi
- Wanandoa wavua kisanduku chenye $100,000 katika ziwa
- Vipimo vipya vya damu 'vyaweza kutabiri' kurejea tena kwa saratani ya matiti
- Rais wa Afrika Kusini akabiliwa na matokeo mabaya ya uchaguzi
- Sheinbaum achaguliwa rais wa kwanza mwanamke wa Mexico
- Marekani yatarajia Israel kukubali mpango wa kusitisha mapigano Gaza ikiwa Hamas itakubali
Moja kwa moja
Asha Juma & Ambia Hirsi
Lavrov yuko Guinea katika mkondo wa kwanza wa ziara barani Afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov yuko nchini Guinea, mkondo wa kwanza wa ziara yake mpya barani Afrika.
Guinea ni mojawapo ya mataifa ya Afrika Magharibi chini ya utawala wa kijeshi na mojawapo ya mataifa maskini zaidi, licha ya kuwa na madini na maliasili nyingi.
Mwanadiplomasia huyowa Urusi atakutana na kiongozi wa kijeshi, Jenerali Mamadi Doumbouya.
Bado hakuna maelezo zaidi, lakini vyanzo kutoka mji mkuu, Conakry, vinasema kuimarisha uhusiano wa Conakry-Moscow kutaongoza ajenda ya mkutano huo.
Ni safari ya kwanza ya Sergei Lavrov katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi tangu 2013 na ziara yake ya sita barani Afrika katika kipindi cha miaka miwili.
Wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilitangaza ziara hiyo kwenye programu ya mtandao wa kijamii ya Telegram ikiwa na picha ya Lavrov kwenye uwanja wa ndege wa Conakry lakini haikutoa maelezo kuhusu safari hiyo.
Watu wengi nchini Guinea na kambi ya kanda ya Afrika Magharibi watakuwa wakitazamia kuona matokeo ya ziara hii.
Wataalamu wa mambo wanaulizana kama Urusi inajaribu kujumuisha Guinea katika kundi la nchi tatu za Sahel—Burkina Faso, Mali, na Niger.
Lakini tofauti na nchi hizo tatu, Guinea haijakatiza ushirikiano wake na mkoloni wa zamani, Ufaransa.
Pia haijajiondoa katika jumuiya ya kikanda, ECOWAS.
Kwa zaidi ya miaka 40, Urusi imekuwa ikichimba madini ya bauxite nchini Guinea.
Inaendesha kampuni ya uchimbaji madini huko Kindia, kilomita 135 kutoka mji mkuu,Conakry.
Operesheni yake ya pili ya uchimbaji madini iko katika Fria, mji wa Guinea ya Chini, ulio kaskazini mwa Conakry karibu na Bwawa la Amaria kwenye Mto Konkouré.
Wakosoaji wanasema uhusiano wa Urusi na Guinea haujaleta maendeleo au manufaa yoyote kwa nchi hiyo.
Urusi imekuwa ikivutia nchi nyingi chini ya utawala wa kijeshi barani Afrika. Imepanua mkondo wake katika bara baada ya uhusiano na nchi za Magharibi kuporomoka kufuatia uvamizi wake nchini Ukraini mwaka wa 2022.
Sasa imetaka kuongeza ushawishi wake barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni.
Kuna uwezekano wa Bw. Lavrov kuzuru Chad na Burkina Faso, lakini hakuna maelezo wala tarehe ambayo imetolewa.
Tanzania: Mtoto mwenye ualbino aibwa, Polisi yafanya msako,

Chanzo cha picha, N
Chama cha watu wenye Ualbino nchini Tanzania kinasema kimeshtushwa na tukio la kuibwa kwa mtoto mwenye ualbino, Asiimwe Novath wa umri wa miaka miwili na nusu. Asiimwe alichukuliwa nyumbani kwao kaskazini magharibi mwa nchi hiyo katika kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera Mei 30 majira ya saa mbili usiku.
Kwa takriban miaka kumi sasa, matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino yalipungua kwa kiasi kikubwa. Sasa kutekwa kwa mtoto Asiimwe kumeishtua jamii.
Mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania, Godson Solomon Mollel anasema wameshtushwa na kusikitishwa na tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Blacius Chatanda aliiambia BBC kuwa bado wanamtafuta mtoto huyo huku uchunguzi ukiwa bado unaendelea.
Alisema wanawashikilia watu watatu kuhusiana na kuibwa kwa mtoto Asiimwe. Amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni baba wa mtoto na watu wengine wawili ambao hawana uhusiano na mtoto, japo hakuwataja majina yao. Pia aliznguzmzia matuko ya aiana hiyo mkaoni Kagera.
”Matukio haya kwa mkoa wa Kagera hayajazoeleka lakini pia mikoa mingine ambayo matukio kama haya yalikuwa yanatokea kwa kipindi kirefu yalikuwa yamepotea. Kimsingi tukio hili kwa Kagera limevuta hisia za wananachi wengi hasa wananchi wema wamechukizwa na tukio la namna hiyo, kimsingi hakuna mtu ambaye anaweza kufurahia tukio la namna hii’
Kanda ya ziwa Victoria bado imeendelea kuwa eneo ambalo kuna matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino. Mollel anasema ni ndani ya mwezi mmoja tu uliopita tukio la kikatili dhidi ya mtoto mwenye ualbino lilitokea mkoani Geita.
‘Kwa kuchukuliwa mtu hadharani, tukio la Geita ndilo tungelifananisha na hilo ambalo mtoto Kazungu Julius alikatwa mkono wake na kichwa na bega’.
Baada ya tukio hili la mtoto Asiimwe, polisi mkoani Kagera wanasema wameimarisha ushirikiano na wananchi kupata taarifa za wahalifu kwa haraka na kuimarisha ulinzi kwa watu wenye ualbino.
‘Kwa Kagera hili ndiyo limetokea, lakini sidhani kama yanaweza kutokea matukio mengine ya namna hiyo kwa mkoa huu kwa sababu polisi ipo karibu sana na wananchi na imejikita sana kwa polisi jamii na ile miradi yake lakini, kata zote zina wagakuzi kata na askari kata na vikundi shirikishi, kwa ujumla wananchi wamaeneo haya wamejipanga vizuri kwa sasa’
Miaka kumi iliyopita, juhudi kubwa zilifanywa kukamata wahalifu na kutoa elimu kwa umma kukabiliana na mauaji haya ya kikatili. Mathalani mwanzoni mwa mwaka 2015, zaidi ya waganga wa jadi 200 walikamatwa, wakihusishwa na mauaji haya ya kinyama. Kuibuka kwa matukio haya mapya kunaashiria uhitaji tena kwa jamii na vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino Tanzania.
Matukio ya namna hiyo pia yamekuwa yakiripotiwa katika nchi Jirani ya Malawi.
Chelsea yamteua Maresca kama kocha mpya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Maresca amechukua mikoba ya kuinoa Chelsea iliyoshika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya England msimu uliopita Chelsea wamemteua mkufunzi wa Leicester Enzo Maresca kama kocha wao mpya kwa kandarasi ya miaka mitano na chaguo la nyongeza ya mwaka.
Muitaliano huyo anachukua nafasi ya Mauricio Pochettino, ambaye aliondoka kwa makubaliano tarehe 21 Mei baada ya msimu mmoja tu Stamford Bridge.
Maresca, 44, alichukua jukumu la kuinoa Foxes mnamo Juni 2023 na kuwaongoza kuchukua ubingwa msimu uliopita
"Kujiunga na Chelsea, moja ya klabu kubwa duniani, ni ndoto kwa kocha yeyote," alisema. "Ndio maana nimefurahishwa sana na fursa hii.
"Ninatarajia kufanya kazi na kundi la wachezaji na wafanyikazi wenye vipaji ili kukuza timu ambayo inaendeleza utamaduni wa mafanikio wa klabu na kuwafanya mashabiki wetu wajivunie."
Maresca, ambaye ataanza kazi yake mpya Julai 1, ni kocha wa Chelsea katika kipindi cha miaka mitano na wa nne tangu mwekezaji Mmarekani Todd Boehly na kampuni ya hisa ya Clearlake Capital kuinunua klabu hiyo Mei 2022.
MrBeast aipiku T-Series kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi YouTube

Chanzo cha picha, MrBeast
MrBeast imeipiku T-Series kama chaneli kubwa zaidi ya YouTube katika mashindano ya muda mrefu ya ubabe wa wafuasi katika mtandao huo.
Lebo ya muziki ya India ya T-Series, ambayo hupakia vionjo vya filamu na video za muziki, ilishikilia rekodi ya chaneli kubwa zaidi ya YouTube kwa miaka mitano, kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo siku ya Jumapili.
MrBeast, jina halisi Jimmy Donaldson, alikuwa tayari mtu binafsi na wafuasi wengi zaidi.
Lakini kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa ameweka historia kwenye jukwaa hilo akiwa na wafuasi milioni 269 wanaoonekana kutoweza kufikiwa, akiiondoa T-Series.
Akiwa na takriban video 800 MrBeast amejitengenezea jina kwa kwa kufanya matukio makubwa - ikiwa ni pamoja na kutoa visiwa vya kibinafsi, kuzikwa hai, na kuandaa toleo la maisha halisi ya filamu maarufu ya Netflix, Squid Game.
Katika chapisho kwenye X, MrBeast alisema hatimaye "amelipiza kisasi" nyota wa YouTube Felix Kjellberg, anayejulikana kama PewDiePie, kwa kuvuka idadi ya wafuasi 266m wa T-Series.
Nigeria yatumbukia gizani huku wafanyikazi wakigoma

Chanzo cha picha, Gift Ufeoma/BBC
Maelezo ya picha, Huu ni mgomo wa nne wa kitaifa tangu Rais Bola Tinubu kuchukuwa hatamu ya uongozi mwaka jana Mamilioni ya Wanigeria hawana umeme baada ya gridi ya taifa kuzimwa kama sehemu ya mgomo wa taifa kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha.
Nchi ilitumbukia gizani muda mfupi baada ya saa 02:00 kwa saa za ndani (01:00 GMT) wakati wanachama wa vyama vya wafanyakazi walipozuia wahudumu katika vyumba vya kudhibiti umeme nchini kufanya kazi na kuzima vituo vidogo vya umeme.
Safari nyingi za ndege pia zimesitishwa katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi nchini humo mjini Lagos, na katika mji mkuu, Abuja, huku abiria wakiwa wamekwama.
Vyama vya wafanyakazi vinadai nyongeza kubwa ya kima cha chini cha mshahara, vikisema wafanyakazi hawawezi kuishi kwa kiwango cha sasa cha naira 30,000 sawa na dola 22 za kimarekani kwa mwezi.
Serikali inajitolea kuongeza hili maradufu lakini mlinzi Mallam Magaji Garba anaambia BBC kwamba hii haitatosha hata kununua gunia la kilo 50 la mchele, ambalo anahitaji kulisha familia yake kila mwezi.
Mfuko wa mchele hugharimu $56 - zaidi ya pendekezo la serikali, hata kabla ya kuzingatia matumizi mengine.
"Ninatoa wito kwa serikali itufikirie na kuongeza kima cha chini cha mshahara ili tuweze kuishi na kula chakula kizuri," asema Bw Magaji, ambaye anafanya kazi katika wizara ya elimu katika jiji la kaskazini la Kano.
"Sio haki kwamba tuna maafisa wakuu wa serikali wanaopata mamilioni kila mwezi na wafanyikazi wadogo wanalipwa mshahara ambao hauwezi kukidhi mahitaji yao."
Mzee huyo wa miaka 59 alisema wakati mwingine hulazimika kutembea kwa miguu kwenda kazini kwani hana uwezo wa kulipia usafiri.
Kijana aliyenaswa kwenye video akimpiga polisi wa Kenya akamatwa

Chanzo cha picha, AFP
Polisi nchini Kenya wamemkamata dereva wa gari mwenye umri wa miaka 19 ambaye alirekodiwa akimpiga polisi wa trafiki akiwa kazini mjini Nairobi.
Katika video ambayo imekuwa ikisambazwa sana, kijana huyo anaonekana akimshambulia polisi huyo kwa makonde na mateke ya kichwa hata baada ya afisa huyo kuanguka chini.
Dereva huyo alitoroka baada ya watu wengine kuingilia kati kumsaidia afisa huyo.
Shambulio hilo la kushtukiza limezua hisia nadra ya huruma kwa polisi, ambao wana sifa ya ukatili na ulaji riushwa.
Ripoti ya polisi ilisema mtu huyo alisimamishwa awali baada ya kugeuza gari kwenye barabara yenye mshughuli nyingi, na kuwazuia madereva wengine kuendelea na safari zao.
Ilisema kuwa afisa wa trafiki, Patrick Ogendo, aliingia ndani ya gari hilo na kumwagiza aendeshe hadi kituo cha polisi kilicho karibu.
Wakiwa njiani, "dereva alisimama ghafla na kuchomoa upanga chini ya kiti".
"Afisa huyo aliruka nje ya gari kwa usalama wake ndipo dereva akaanza kumpiga makonde na mateke," taarifa hiyo iliongeza.
Polisi huyo alipata huduma ya kwanza katika kituo cha afya kilicho karibu na kisha kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Mtu anayedaiwa kuwa mshirika wa mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la tukio na maafisa wa polisi waliokuwa wakifanya msako wa kumtafuta mtu aliyefanya shambulizi hilo, ilisema taarifa hiyo.
Shambulio hilo limelaaniwa vikali, huku wengine wakielezea shambulio hilo kuwa halikubaliki.
“Unamshambulia vipi afisa wa polisi aliyevalia sare kwa njia hii?” akauliza Robert Alai, mjumbe wa bunge la kaunti ya Nairobi.“Hili halikubaliki kabisa.
Hatufai kuruhusu maafisa wetu wa polisi waliovalia sare kudhalilishwa hadi kiwango hiki,” akasema Mike Sonko, gavana wa zamani wa Nairobi.
Mshukiwa aliripotiwa kukamatwa katika makazi yake viungani mwa mkuu baadaye Jumapili jioni.
Mkuu wa trafiki wa Nairobi Vitalis Otieno aliambia vyombo vya habari kuwa atashtakiwa kwa makosa kadhaa ikiwemo jaribio la mauaji.
Kocha wa Ujerumani alaani utafiti wa 'kibaguzi' uliofanywa na kituo cha televisheni

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Maelezo ya picha, Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Julian Nagelsmann Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Julian Nagelsmann amelaani utafiti wa hivi majuzi wa "ubaguzi wa rangi" ambao uliwauliza washiriki ikiwa wanataka kuona wachezaji wengi weupe kwenye timu ya taifa ya kandanda.
Kura ya maoni ya shirika la utangazaji la ARD ilisema 21% ya waliohojiwa walikubaliana na pendekezo hilo.
"Ni ubaguzi wa rangi. Ninahisi tunahitaji kuamka. Watu wengi barani Ulaya walilazimika kukimbia.. kutafuta nchi salama," Nagelsmann alisema Jumapili.
Kicha huyo mwenye umri wa miaka 36 alisema alikubaliana na kiungo wa kati wa Ujerumani Joshua Kimmich, ambaye alielezea utafiti huo kama "ubaguzi wa rangi" siku moja kabla.
"Josh [Kimmich] alijibu vizuri sana, kwa maelezo ya wazi na ya kufikiria," Nagelsmann alisema katika mkutano mfupi kwenye uwanja wa mazoezi wa timu yake.
"Nakubaliana naye kabisa. Swali hili ni la kichaa. "Kuna watu huko Uropa ambao wamelazimika kukimbia kwa sababu ya vita, sababu za kiuchumi, majanga ya mazingira, watu ambao wanataka tu kuchukuliwa
"Tunapaswa kuuliza tunafanya nini kwa sasa? Sisi nchini Ujerumani tunafanya vizuri sana, na tunaposema kitu kama hicho, nadhani ni wazimu jinsi tunavyofumbia macho na kuzuia mambo kama hayo."
ARD - shirika la utangazaji la Ujerumani - lilisema limeagiza utafiti huo kuwa na data zinazoweza kupimika, baada ya mwandishi wa habari anayefanya kazi kwenye filamu ya kandanda kuulizwa mara kwa mara kuhusu muundo wa timu ya taifa.
Utafiti huo ulijumuisha washiriki 1,304 waliochaguliwa bila mpangilio.
Zelensky anaonya Trump akishinda urais ataachana na Ukraine - The Guardian

Chanzo cha picha, EPA
Gazeti la The Guardian limechapisha mahojiano ya kipekee iliyofanya na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambapo anaonya dhidi ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani na kutupilia mbali uungaji mkono wa kijeshi kwa Ukraine.
Trump aliahidi mwaka jana kwamba ikiwa atamshinda Joe Biden, angekatiza msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kumaliza vita ndani ya saa 24.
Wale walio karibu na Trump pia walidokeza mpango anaopendekeza kupeana mikoa ya mashariki ya Ukraine kwa Urusi, pamoja na Rasi ya Crimea, kumaliza mapigano.
Lakini Rais Zelensky alisisitiza kuwa nchi yake haitakubali mpango huo, wala haiko chini ya shinikizo la Urusi ambayo inajaribu kuilazimisha kuachana na wazo la kujumuika na Ulaya na kujiunga na NATO katika siku zijazo.
Rais wa Ukraine alikiri kwamba kurejea kwa Trump katika Ikulu ya White House kunaweza kuhusisha kukatisha msaada wa kijeshi na kifedha kwa nchi yake, na kwamba Ukraine haiwezi kukabiliana na jeshi la Urusi lenye uwezo mkubwa bila silaha.
Alisema jambo hilo haliwezekani kutendeka, lakini likitokea athari zake zitakuwa hatari kwa msimamo wa Marekani katika ngazi ya kimataifa, na kwa sifa ya Trump binafsi, kwani atatajwa kuwa rais aliyeshindwa na ambaye amepunguza makali ya msimamo wa Marekani.
12 wauawa katika shambulio la bomu la Israel nchini Syria

Chanzo cha picha, EPA
Shambulio la makombora la Israel katika maeneo ya vijijini ya Aleppo nchini Syria alfajiri ya Jumatatu yamesababisha vifo vya takriban watu 12 na wengine kujeruhiwa, kulingana na Agence France-Presse
Shirika la Agence France-Presse limenukuu Shirika la Kufuatilia Haki za Binadamu la Syria likisema kwamba shambulio hilo la bomu lililenga mji wa Hayyan ulioko magharibi mwa Aleppo
Shirika hilo liliripoti kwamba kulikuwa na "shambulio la anga la Israel kwenye eneo la mji wa Hayyan katika vijiji vya kaskazini mwa Aleppo, ambapo shabaha hiyo ilisababisha milipuko ya mfululizo katika kiwanda cha shaba eneo hilo," ambacho kinadhibitiwa na vikundi vya Iran, na kusababisha kuuawa kwa watu 12 wa vikundi vinavyounga mkono Iran
Israel haijatoi maoni yoyote juu ya shambulio hilo.
Vyombo vya habari rasmi vya Syria vilinukuu chanzo cha kijeshi na kusema kuwa watu kadhaa waliuawa katika shambulio la anga la Israel lililolenga maeneo karibu na mji wa Aleppo nchini Syria siku ya Jumatatu.
Shirika la habari la Reuters linasema hili ni shambulio la pili kuripotiwa nchini humo katika kipindi cha chini ya wiki moja.
Yanga yatwaa ubingwa wa Shirikisho Tanzania ikiandikisha rekodi

Chanzo cha picha, Yanga
Mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara Yanga wamefanikiwa kuchukua taji lao la pili kwa msimu wa 2023/24 baada ya kuwalaza Azam FC kwenye fainali ya kombe la shirikisho usiku wa kuamkia leo huko visiwani Zanzibar.
Yanga ambao wamechukua taji lao la nane la shirikisho tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo iliwalazimu kupata ushindi huo kwa chagamoto ya mikwaju ya penati 5-6 baada ya dakika 120 kuisha 0-0
Licha ya kukosa penati mbili za kwanza Yanga walifanikiwa kutwaa ubingwa huo baada ya winga wa Azam, Iddy Suleiman kupaisha juu ya lango penati yake.
Ikiwa hii ni mara ya nane kuchukua taji hilo lakini Yanga imejiandikia historia yake baada ya kuchukua kombe hilo mara tatu mfululizo mwaka 2022,2023 na 2024.

Chanzo cha picha, Yanga
Miaka mingine ambayo Yanga walichukua ubingwa wa kombe la FA ni 1967, 1974, 1999, 2001 na 2016.
Joto laua zaidi ya watu 50 nchini India kwa siku tatu

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya watu 50 wamefariki dunia nchini India katika muda wa siku tatu zilizopita huku hali ya joto kali ikiendelea kukumba sehemu za nchi hiyo.
Takriban watu 33 walikufa katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh mwishoni mwa juma kutokana na joto.
Katika jimbo la Odisha (Orissa), takriban watu 20 walikufa kutokanana wimbi kali la joto, afisa aliliambia shirika la habari la ANI.
Vingi vya vifo hivi viliripotiwa tarehe 1 Juni wakati India ilipopiga kura katika awamu ya mwisho ya upigaji kura kwa uchaguzi wake mkuu.
Matokeo ya uchaguzi huo yamepangwa kutangazwa tarehe 4 Juni.
Kila baada ya miaka mitano, India hufanya uchaguzi wake mkuu katika miezi ya kiangazi ya Aprili na Mei.
Lakini mwaka huu, hali ya joto imekuwa ikivunja rekodi, huku nchi ikikumbwa na mawimbi ya joto ya mara kwa mara, makali zaidi na marefu zaidi.
Wizara ya afya ya serikali kuu inasema kwamba kumekuwa na vifo 56 vilivyothibitishwa vya mawimbi ya joto kutoka 1 Machi hadi 30 Mei. Karibu visa 24,849 mawimbi ya joto viliripotiwa katika kipindi hicho.
Uchina yaishutumu MI6 kwa kuajiri wafanyikazi wa serikali yake

Chanzo cha picha, Getty Images
China imelishutumu Shirika la Ujasusi la Uingereza MI6 kwa kuajiri wafanyikazi wa serikali ya China kama majasusi.
Katika chapisho kwenye idhaa yake rasmi ya WeChat, Wizara ya Usalama ya Nchi ya China ilisema watendaji wa MI6 walimgeuza Mchina aliyetambuliwa kwa jina lake la ukoo tu kama Wang na mkewe aliyeitwa Zhou dhidi ya Beijing.
Wote wawili walifanya kazi katika idara za "siri kuu" katika serikali ya Uchina.
Wizara hiyo ilidai kuwa MI6 ilianza kumtumia Bw Wang alipoenda Uingereza kwa masomo yake mwaka wa 2015, chini ya mpango wa kubadilishana wa China na Uingereza.
Wahudumu hao walimchukulia kwa "uangalifu maalum" nchini Uingereza, kama vile kumwalika kwa chakula cha jioni na ziara ili "kuelewa vyema maslahi na udhaifu wake" wizara ilidai.
BBC imeiomba mamlaka ya Uingereza kutoa majibu.
Haya yanajiri muda wa mwezi mmoja tu baada ya Uingereza kuwafungulia mashtaka wanaume wawili kwa kuwa majasusi wa China. Polisi wa Uingereza wamewashutumu kwa kutoa "makala, maelezo, nyaraka au taarifa" kwa taifa la kigeni, huku China ikitaja madai hayo kuwa ni "kashfa mbaya".
Mapema mwezi huu,askari wa zamani wa Wanamaji wa Kifalme aliyeshtakiwa kwa kusaidia huduma ya ujasusi ya Hong Kong alipatikana amekufa, polisi walisema.
Beijing na nchi kadhaa za Magharibi zimezidi kuwa na tuhuma za ujasusi.
Kwa upande wa Bw Wang, mamlaka ya Uchina ilisema wahudumu wa MI6 walichukua fursa ya "tamaa yake kubwa ya pesa" na walifanya urafiki naye chuoni kwa kisingizio kwamba walikuwa wanachuo, na kumfanya atoe "huduma za malipo ya ushauri".
Baada ya muda, na chini ya tathmini yao kwamba "hali zilikuwa zimeiva", watendaji hao walimwomba aitumikie serikali ya Uingerezakwa malipo bora na matoleo ya usalama, Wizara ya Usalama ya Nchi ya China ilidai.
Wanandoa wavua kisanduku chenye $100,000 katika ziwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanandoa "wanaovua kwa sumaku" wanasema wamevuta kijisanduku kilichokuwa na wastani wa $100,000 (£78,000) kutoka ziwa la New York.
James Kane na Barbie Agostini walirusha kamba ya kuvua yenye sumaku kwenye ziwa eneo la Queens siku ya Ijumaa na kuvuta kijisanduku.
Walipofungua ndani ya sanduku hilo walikuta limejaa noti za $100 zilizoharibiwa na maji.
Walisema polisi imewaambia kuwa kisanduku hicho hakikuhusishwa na uhalifu wowote na kwamba wanaruhusiwa kuweka pesa hizo. BBC imeenda katika Idara ya Polisi ya New York (NYPD) ili itoe maoni.
"Tumepata visanduku vingi hapo awali," Bw Kane alisema. "Na kisha nikaona idadi ya noti na kufikiria: 'Hii haiwezekani.'
"Tulilitoa nje na ilikuwa ni rundo kubwa la mamia," aliongeza. "Hili ni rundo nene - zimelowa, zimeharibiwa sana."
"Hakukuwa na vitambulisho katika kijisanduku, wala namna ya kumpata mmiliki halisi,," Bi Agostini alisema. "[Polisi] walisema: 'Hongereni!'"
Uvuvi wa sumaku unahusisha kuvuta kamba yenye sumaku kali kupitia maziwa na mito na kuona kile kinachovutwa juu.
Wanandoa hao walisema walianza uvuvi wa sumaku wakati wa janga la Covid-19 na kuongeza kuwa siku za nyuma, wamewahi kupata maguruneti ya zama za Vita vya Pili vya Dunia, bunduki za karne ya kumi na tisa na pikipiki ya kubwa.
Vipimo vipya vya damu 'vyaweza kutabiri' kurejea tena kwa saratani ya matiti

Chanzo cha picha, Institute of Cancer Research
Vipimo vipya vya damu vya "kina zaidi" vyaweza kutabiri ikiwa saratani ya matiti itarejea miaka kadhaa kabla ya ugonjwa huo kuonekana kwenye vipimo vya uchunguzi, watafiti wanasema.
Ilichukua sampuli za DNA ya uvimbe kabla ya kurudi tena na ilipatikana kuwa sahihi 100% katika kutabiri ni wagonjwa gani saratani yao itarejea.
Inatarajiwa kuwa kipimo kinaweza kuruhusu matibabu kuanza mapema na kuimarisha viwango vya kuishi.
Utafiti wa Uingereza umetajwa kuwa "wa kipekee" na wataalam lakini bado uko katika hatua zake za awali.
Saratani ya matiti ni aina ya kawaida ya ugonjwa huo ulimwenguni, ambapo wanawake milioni 2.26 waligunduliwa mnamo 2020 na vifo 685,000 vikatokea katika mwaka huo huo, kulingana na shirika la saratani ya matiti Uingereza.
Timu ya watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Saratani (ICR) London ilifanya majaribio kwa wagonjwa 78 wenye aina tofauti za saratani ya matiti katika hatua ya awali.
Kwa wastani, kipimo cha damu kiligundua saratani miezi 15 kabla ya dalili kuonekana au ugonjwa kuonyeshwa kwenye vipimo, kulingana na matokeo yaliyowasilishwa kwenye mkutano wa Jumuiya ya Kitabibu huko Chicago Jumapili.
Ugunduzi wa mapema zaidi ulikuwa miezi 41 kabla ya uchunguzi kuthibitisha utambuzi.
Mtafiti mkuu Dk Isaac Garcia-Murillas, kutoka ICR, alisema: "Seli za saratani ya matiti zinaweza kubaki mwilini baada ya upasuaji na matibabu mengine lakini kunaweza kuwa na seli chache sana ambazo hazionekani kwenye uchunguzi wa ufuatiliaji."
Aliongeza kuwa seli hizo zinaweza kusababisha mgonjwa kuanza kudhoofika tena miaka mingi baada ya matibabu yao ya awali.
Dk Garcia-Murillas alisema utafiti huo unaweka msingi wa ufuatiliaji bora wa baada ya matibabu na matibabu yanayoweza kuongeza siku za kuishi.
Watafiti walijaribu sampuli za damu wakati wa utambuzi, kisha ikafuatia upasuaji na matibabu ya kemikali yaani chemotherapy.
Soma zaidi:
Rais wa Afrika Kusini akabiliwa na matokeo mabaya ya uchaguzi

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amekiri kuwa chama chake cha African National Congress (ANC) kimepata changamoto katika matokeo ya uchaguzi, baada ya chama hicho kupoteza wingi wa kura kwa mara ya kwanza tangu utawala wa kibaguzi kumalizika miaka 30 iliyopita.
Chama cha ANC, ambacho kiliwahi kuongozwa na Nelson Mandela, kilishinda viti 159 katika bunge lenye viti 400 katika uchaguzi wa Jumatano, idadi ya chinikutoka 230 katika bunge lililopita.
Bw Ramaphosa bado alitaja matokeo kama ushindi kwa demokrasia, akitoa wito kwa vyama vinavyopingana kutafuta muafaka - inaonekana kujiandaa kwa mazungumzo ya muungano.
Chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimesema kiko tayari kwa mazungumzo ya muungano na Bw Ramaphosa, lakini kinapinga vipaumbele vingi vya serikali yake.
Pamoja na kura zote kuhesabiwa, ANC ilimaliza kwa kupata40% - chini kutoka 58% katika uchaguzi uliopita, tume ya uchaguzi ilitangaza Jumapili.
Hii ilikuwa chini kuliko hali ya chama inayohofiwa kuwa mbaya zaidi ya 45%, wachambuzi walisema. Chama cha ANC sasa lazima kiingie katika muungano ili kuunda serikali ijayo.
“Watu wetu wamezungumza, tupende tusitake, wamezungumza,” Bw Ramaphosa alisema.
"Kama viongozi wa vyama vya siasa, wote wanaochukua nafasi za uwajibikaji katika jamii, tumesikia sauti za watu wetu na lazima tuheshimu matakwa yao."
Aliongeza kuwa wapiga kura walitaka vyama kutafuta muafaka.
“Kupitia kura zao, wamedhihirisha wazi na wazi kwamba demokrasia yetu ni imara na inadumu,” alisema.
Soma zaidi:
Sheinbaum achaguliwa rais wa kwanza mwanamke wa Mexico

Chanzo cha picha, Efe
Claudia Sheinbaum amechaguliwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Mexico katika ushindi wa kihistoria.
Mamlaka rasmi ya uchaguzi ya Mexico imesema matokeo ya awali yameonyesha meya wa zamani wa Mexico City mwenye umri wa miaka 61 akishinda kati ya 58% na 60% ya kura katika uchaguzi wa Jumapili.
Hiyo inampa uongozi wa zaidi ya asilimia 30 ya pointi zaidi ya mpinzani wake mkuu, mfanyabiashara Xóchitl Gálvez.
Bi Sheinbaum atachukua nafasi ya mshauri wake, Rais anayemaliza muda wake Andrés Manuel López Obrador, tarehe 1 Oktoba.
Wapiga kura pia walikuwa wakiwachagua wajumbe wote wa Bunge la Mexico na magavana katika majimbo manane, pamoja na mkuu wa serikali ya Mexico City, katika kampeni hiyo iliyokumbwa na mashambulizi makali.
Serikali inasema zaidi ya wagombea 20 wa eneo hilo wameuawa kote Mexico, ingawa tafiti za kibinafsi zinaweka jumla ya 37 waliuawa.
Watu wawili waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi mawili kwenye vituo vya kupigia kura katika jimbo la Puebla siku ya Jumapili, maafisa walisema.
Marekani yatarajia Israel kukubali mpango wa kusitisha mapigano Gaza ikiwa Hamas itakubali

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Marekani ina "kila matarajio" kwamba Israel itakubali pendekezo la kusitisha mapigano ambalo litaanza kwa kusitishwa kwa uhasama kwa wiki sita huko Gaza ikiwa Hamas itakubali makubaliano hayo, kwa mujibu wa msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa John Kirby.
Mpango huo wa sehemu tatu uliozinduliwa na Rais Joe Biden wiki iliyopita pia utajumuisha "kuongezeka" kwa misaada ya kibinadamu, pamoja na kubadilishana baadhi ya mateka kwa wafungwa wa Kipalestina kabla ya kumalizika kwa vita.
Pendekezo hilo hata hivyo limekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa serikali ya Israel.
Mazungumzo hayo yanawadia huku mapigano yakiendelea huko Rafah, ambayo ilikumbwa na mashambulizi makali ya anga ya Israel mwishoni mwa juma.
Kwa mujibu wa UNRWA, shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, makazi yake yote 36 katika eneo la Rafah hakuna watu baada ya wakaazi kulazimika kukimbia mapigano.
Watu wengine milioni 1.7 wanakadiriwa kuhama makazi yao huko Khan Younis na sehemu za katikati mwa Gaza.
Akizungumza na ABC News Jumapili asubuhi, Bw Kirby alisema kuwa Marekani ilikuwa na "kila matarajio" kwamba Israel "itakubali" makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopendekezwa ikiwa Hamas itakubali.
"Tunasubiri jibu rasmi kutoka kwa Hamas," alisema, akiongeza kuwa Marekani inatumai kuwa pande zote mbili zitakubali kuanza awamu ya kwanza ya mpango huo "haraka iwezekanavyo".
Wakati wa kusitishwa kwa vita katika awamu ya kwanza ya makubaliano, Bw Kirby alisema "pande mbili zingekaa chini na kujaribu kujadili jinsi awamu ya pili itakavyokuwa, na lini hilo linaweza kuanza".
Katika hotuba ya televisheni wiki jana, Bw Biden alisema kuwa awamu ya pili ya mpango huo mateka wote waliosalia watarudishwa nyumbani, wakiwemo wanajeshi wa kiume. Usitishaji wa kudumu wa mapigano basi ungefanyika".
Siku ya Jumamosi, hata hivyo, mawaziri wawili wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel walitishia kujiondoa na kusambaratisha muungano wa serikali ya nchi hiyo ikiwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu atakubali makubaliano hayo.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 3/6/2024
