Matokeo rasmi ya uchaguzi Afrika kusini kutangazwa Jumapili

Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu Afrika kusini yanatarajiwa kutangazwa Jumapili jioni, afisa mmoja wa tume anasema.

Muhtasari

  • Viongozi wa ANC wajadili njia ya kusonga mbele
  • Hakuna usitishaji vita Gaza hadi malengo ya vita vya Israel yatimie - Netanyahu
  • Matokeo rasmi ya uchaguzi Afrika kusini kutangazwa Jumapili
  • Jennifer Lopez afuta ziara yake ya Marekani
  • Uchaguzi Afrika Kusini: Chama cha EFF cha Julius Malema chapata pigo kubwa
  • Chama cha Zuma chadai kuhesabiwa upya kwa kura
  • Balozi wa Uingereza aondoka baada ya 'kuwanyooshea bunduki wafanyakazi'
  • Mwandamanaji ajifunga minyororo kwenye nguzo ya kufungia magoli kupinga uvamizi wa Israel, Gaza
  • Matokeo ya uchaguzi Afrika kusini: Hatma ya ANC
  • Champions League: Uzito wa fainali kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund huko Wembley
  • Mamake Michell Obama, Marian Robinson afariki dunia
  • Mama aliyemuua binti yake baada ya kukataa ndoa iliyopangwa akamatwa Pakistan
  • Ufilipino yaionya China dhidi ya 'vitendo vya vita'
  • Biden: Ni 'Uzembe' kwa Trump kusema kesi yake ilipangwa

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Viongozi wa ANC wajadili njia ya kusonga mbele

    Chanzo cha ANC chasema kuwa maafisa saba wakuu wa ANC, akiwemo Rais Cyril Ramaphosa wanakutana kujadili njia ya kusonga mbele baada ya matokeo ya uchaguzi.

    Kama ilivyo kwa nchi nzima, jimbo tajiri zaidi la Afrika Kusini la Gauteng linatazamiwa kuwa na serikali ya mseto baada ya chama cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake.

    Kwa 97% ya kura kukamilika kuhesabiwa, ANC imepata 35% tu ya kura – kupoteza kwa kiasi kikubwa tangu uchaguzi wa 2019 ilipopata 50%.

    Bado ni chama kikubwa zaidi katika jimbo hilo, ambacho kinajumuisha jiji kubwa zaidi la Johannesburg na mji mkuu, Pretoria, lakini kitahitaji kuunda muungano.

    Chama cha Democratic Alliance (DA) kiko katika nafasi ya pili, kwa asilimia 28 ya kura, kikifuatiwa na Economic Freedom Fighters (EFF) kwa asilimia 13%.

    ANC imekuwa na wengi katika jimbo hilo tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

  3. Hakuna usitishaji vita Gaza hadi malengo ya vita vya Israel yatimie - Netanyahu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesisitiza kuwa hakutakuwa na usitishaji vita wa kudumu huko Gaza hadi pale uwezo wa kijeshi na uongozi wa Hamas utakapoangamizwa na mateka wote waachiliwe.

    Kauli yake inawadia baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kutangaza kuwa Israel imependekeza mpango wa hatua tatu kwa Hamas unaolenga kufikia usitishaji vita wa kudumu.

    Mwanasiasa mkuu wa Hamas ameiambia BBC kuwa "itakubali makubaliano haya" ikiwa Israel itafanya hivyo.

    Mazungumzo hayo yanawadia huku mapigano yakiendelea huko Rafah, kukiwa na ripoti za mashambulizi ya anga ya Israel siku ya Jumamosi katika mji huo ulio kwenye mpaka wa Misri na Gaza.

    Hakuna hakikisho kwamba shinikizo la umma la Bw Biden kwa Israel na Hamas kuukubali mpango huo litachochea makubaliano.

    Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, ofisi ya Bw Netanyahu ilisema kuwa "masharti ya Israel ya kumaliza vita hayajabadilika".

    Imeorodhesha haya kama "kuharibiwa kwa uwezo wa kijeshi na kiutawala wa Hamas, kuachiliwa kwa mateka wote na kuhakikisha kuwa Gaza haileti tishio tena kwa Israel".

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa Israel "itaendelea kusisitiza masharti haya yatimizwe" kabla ya kukubaliana na usitishaji wa kudumu wa mapigano, na kusisitiza kwamba hakuna makubaliano yanayoweza kusainiwa kabla ya kufikiwa kwa hayo kwanza.

    Siku ya Ijumaa, Bw Biden alielezea mpango huo kama pendekezo la kina la Israel ambalo lilifungua njia ya usitishaji wa kudumu wa mapigano.

    Awamu ya kwanza itajumuisha usitishaji vita kamili, kuondolewa kwa vikosi vya Israel kutoka maeneo yenye watu wengi na kubadilishana baadhi ya mateka kwa wafungwa wa Kipalestina.

    Soma zaidi:

  4. Matokeo rasmi ya uchaguzi Afrika kusini kutangazwa Jumapili

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu Afrika kusini yanatarajiwa kutangazwa Jumapili jioni, afisa mmoja wa tume anasema.

    Zoezi la kuhesabu kura linaingia katika hatua ya mwisho huku 98% ya matokeo yakiwa yamepokewa tayari.

    Naibu mkurugenzi mtendaji wa tume ya uchaguzi nchini Mawethu Mosery, ameiambia televisheni ya eNCA kwamba tume itakesha usiku kucha Jumamosi kukabiliana na pingamizi na maombi.

    Chama tawala ANC kinatarajiwa kupoteza nguvu kilichoshikilia katika miongo mitatu ya siasa baada ya kupungua kwa wafuasi wake kwa kiwango kikubwa.

  5. Jennifer Lopez afuta ziara yake ya Marekani

    .

    Jennifer Lopez amesema "amesikitika" sana baada ya kufuta tamasha lake la moja kwa moja nchini Marekani.

    Kampuni ya utoaji tikiti ya Live Nation ilitangaza Ijumaa kuwa ziara ya majira ya joto ya 2024 imefutwa, ikisema mwimbaji huyo "anachukua likizo kuwa na mtoto wake, familia na marafiki wa karibu".

    Akiwahutubia mashabiki kupitia jarida lake, mwimbaji huyo aliandika: "Nimehuzunika sana na kukukatishwa tamaa."

    Live Nation iliwahakikishia mashabiki katika taarifa kwamba watarejeshewa pesa zao.

    Ziara hiyo ilikuwa imepangwa baada ya albamu ya tisa ya Lopez, ‘This Is Me... Now’, ambayo ilitolewa miaka 20 baada ya albamu yake maarufu, This Is Me... Then. Ni albamu ya kwanza ya mwimbaji huyo kwa miaka mitano.

    Akiwaandikia mashabiki, Lopez alisema: "Singefanya hivi ikiwa singehisi kuwa ni muhimu.

    "Nawaahidi nitawafanyia kitu kizuri na tutakuwa pamoja tena. Nawapenda sana. Mpaka wakati mwingine."

  6. Uchaguzi Afrika Kusini: Chama cha EFF cha Julius Malema chapata pigo kubwa

    ,

    Chanzo cha picha, Reuters

    Baada ya chama tawala cha African National Congress (ANC), aliyeshindwa zaidi katika uchaguzi huu ni chama chenye msimamo mkali cha Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na Julius Malema.

    EFF imepoteza hadhi yake kama chama cha pili kwa ukubwa nchini Afrika Kusini kwa mshiriki wa mara ya kwanza - chama kipya cha Rais wa zamani Jacob Zuma, Umkhonto weSizwe (MK).

    Huku takriban matokeo yote yakitangazwa, EFF imesimama kwa asilimia 9, chini kutoka 11 iliyopata katika uchaguzi uliopita.

    Kura za MK zimesimama kwa asilimia 15, huku chama hicho kikipata kura kutoka kwa ANC na EFF.

    Hili ni pigo kubwa kwa Malema na EFF.

    Ana matarajio ya siku moja kuwa rais wa Afrika Kusini, na alikuwa na matumaini kwamba EFF itachukua nafasi ya pili katika uchaguzi huu, na kumfanya kuwa kiongozi wa chama kikubwa zaidi cha upinzani.

    Hata hivyo, ndoto hiyo ilikatizwa na wapiga kura.

  7. Chama cha Zuma chadai kuhesabiwa upya kwa kura

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chama cha Umkhonto we Sizwe (MK) cha Rais wa zamani Jacob Zuma kimewasilisha malalamishi kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Afrika Kusini (IEC)

    Huku 98% ya kura zikiwa zimejumlishwa hadi sasa, MK inashindwa kupata wingi wa kura katika ngazi ya mkoa huko KwaZulu-Natal.

    Msemaji wa chama Nhlamulo Ndhlela amesema idadi ya IEC hazilingani na walizokusanya mashinani na hivyo wanataka kuhesabiwa upya kwa kura.

    Ndhlela ametoa wito kwa wafuasi wa MK kutofanya vurugu.

  8. Balozi wa Uingereza aondoka baada ya 'kuwanyooshea bunduki wafanyakazi'

    .

    Chanzo cha picha, X/@subdiplomasia

    Balozi wa Uingereza nchini Mexico ameripotiwa kuacha wadhifa wake mapema mwaka huu baada ya kumuoteshea bunduki mfanyikazi wa ubalozi wa eneo hilo.

    Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, iliyoripotiwa awali na Financial Times, inamuonyesha Jon Benjamin akimwotesha mtu mwingine kwa bunduki huku akitazama chini kwenye silaha hiyo.

    Iliandikwa: "Katika muktadha wa mauaji ya kila siku huko Mexico na wafanyabiashara wa dawa za kulevya, anathubutu kutania."

    Bw Benjamin bado hajatoa maoni yake kuhusu kile kinachoonekana kuwa mzaha mbaya.

    Hakuna tangazo rasmi kuhusu nafasi ya Bw Benjamin ambalo limetolewa na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO).

    Lakini hajaorodheshwa tena kama balozi wa Mexico kwenye tovuti rasmi ya serikali, ambayo inasema alikuwa katika wadhifa huo "kati ya 2021 na 2024".

    Katika video hiyo, mwanamume anayefanana na Bw Benjamin anaonekana akisongeza silaha karibu na gari hilo, akiwalenga watu tofauti. Kicheko kinaweza kusikika kwa nyuma. Mwanaume mmoja anaonekana akionyesha ishara ya kuwa na wasiwasi kwani silaha hiyo inamlenga yeye.

    BBC imewasiliana na Bw Benjamin kutafuta maoni yake.

  9. Mwandamanaji ajifunga minyororo kwenye nguzo ya kufungia magoli kupinga uvamizi wa Israel, Gaza

    .

    Chanzo cha picha, SNS

    Mwandamanaji amejifunga minyororo kwenye nguzo ya kufunga magoli kabla ya mchezo wa kufuzu kwa mashindano ya Euro 2025 kwa Wanawake wa Scotland dhidi ya Israel kwenye uwanja wa Glasgow's Hampden.

    Mechi hiyo ilicheleweshwa kwa takriban dakika 45 baada ya mwanamume huyo kutumia kufuli nzito kujifunga kwenye eneo la kufunga magoli akipinga operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza.

    Pande hizo mbili ziliporejea uwanjani, timu ya Israel ilinyanyua fulana iliyokuwa na ujumbe "Walete Nyumbani" wakimaanisha mateka waliochukuliwa na kundi la Hamas kwenye picha rasmi ya timu.

    Mchezo huo hatimaye ulianza dakika 45 baadaye kuliko ilivyopangwa, huku Scotland ikishinda mabao 4-1.

    Mamia ya watu, wengine wakiwa wamebeba majeneza madogo na bendera za Palestina, walikuwa wamekusanyika nje ya lango kuu.

    Mwandamanaji huyo aliyeingia kwenye uwanja wa taifa hapo awali alikuwa amevalia vazi ambalo huenda lilimfanya kudhaniwa kuwa msimamizi.

    Aliondolewa kwenye nguzo ya kufungia magoli na kuongozwa kutoka uwanjani na polisi.

  10. Matokeo ya uchaguzi Afrika kusini: Hatma ya ANC

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chama tawala Afrika kusini kimefanikiwa kujikusanyia 40% ya kura katika uchaguzi mkuu nchini wakati zoezi la kuhesabu kura likielekea kukamilika.

    Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa chama ambacho Nelson Mandela alikiongoza kupata ushindi wa kishindo baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi mnamo 1994.

    Kimepoteza uwingi bungeni kwa mara ya kwanza, lakini matokeo haya yanakuja kwa mshtuko kwa rais Cyril Ramaphosa na chama chake.

    Wachambuzi wengi walitabiri kuwa chama hicho kitafikia 50% na katika hali mbaya sanakitakaribiakujizolea 45% ya kura.

    Kwa sasa ANC kimefanikiwa kujizolea 40% baada ya 97% ya matokeo kutoka maeneo ya kupiga kura kutangazwa na tume ya uchaguzi.

    Chama hicho sasa kitalazimika kuingia katika muungano, hatua inaidhinisha mwanzo mpya katika siasa za Afrika kusini.

    Uchaguzi ulifanyika Mei 29.

  11. Champions League: Uzito wa fainali kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund huko Wembley

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Meneja wa Real Madrid Carlo Ancelotti anasema wachezaji wake watahisi msisimko wa fainali ya ligi ya mabingwawatakapokutana na Borussia Dortmund huko Wembley.

    Washindi hao mara 14 ya ligi hiyo wanakutana Jumamosi usiku na timu hiyo ya Ujerumani walioibuka katika nafasi ya tano kwenye ligi ya Bundesliga msimu huu.

    Ancelotti – meneja aliyepata ufanisi mkubwa kwa mataji manne anafahamu kwamba hakuna uhakikisho wa ushindi.

    "Fainali ya ligi ya mabingwa ni mashindano muhimu na hatari mnoe," anasema Ancelotti.

    "Lazima uwe na bahati nzuri, ucheze vizuri na uwe muangalifu saa zote lakini unapofika kwenye fainali ushindi upo karibu kiasi cha kwamba unakuwa na wasiwasi".

    Tofauti na Dortmund, ambao wamekuwa na kibarua kigumu nyumbani lakini wakatamba Ulaya, mabingwa wa Uhispania wamekuwa na hali tofuati katika hatua za mbele za amshindano hayo.

    Real imewafunga Manchester City kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya timu nane za mwishona kufunga magoli mawili katika awamu ya pili ya nusu fainali na kusongea juu ya Bayern Munich.

    "Ni upanga wa pande mbili ni lazima tuishangilie vilivyo alafu wasiwasi unaanza tukihofia huenda kitu kikaharibika kwasababu tuko karibu sana kukifikia kitu muhimu sana katika soka." Ancelotti, alieleza siku ya Ijumaa.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Mamake Michell Obama, Marian Robinson afariki dunia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Michelle Obama na Marian Robinson wakipiga makofi kwenye hafla

    Marian Robinson, mamake Michelle Obama, mkewe rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amefariki dunia akiwana umri wa miaka 86.

    Katika taarifa rasmi, familia yake imesema kuwa Robinson alifariki Ijumaa asubuhi.

    Robinson alionekana sana katika ikulu ya Marekani katika miaka minane ya utawala wa Barack Obama kati ya mwaka 2009 hadi 2017.

    Kwa muda mwingi huo alishughulika kuwalea wajukuu zake wawili Malia na Sasha – binti zake Michelle na Barack Obama.

    Katika taarifa kwenye mtandao wa X uliofahamika kama twitter zamani, Michelle Obama alimueleza mamake kuwa kama mtu muhimu kwake – "jiwe la singi ambaye siku zote alinisaidia kwa chochote nilichokihitaji".

    " Alikuwa kiungo muhimu kwa familia yetu yote na tumesikitika kutangaza kuwa ameafiriki dunia leo," aliandika.

    Katika ujumbe tofuati kwenye mtandao huo wa X,Bwana Obama amesema kuwa“ Alikuwepo na atasalia kuwepo Marian Robinson mmoja pekee”.

    “Katika huzuni wetu tunapata nguvu kwa zawadi ya maisha yake,” aliongeza. “Na kwa maisha yetu yote tutajaribu kuishi kwa mfano wake.”

    Hakuna maelezo zaidi yaliotolewa kuhusu chanzo cha kifo chake.

  13. Mama aliyemuua binti yake baada ya kukataa ndoa iliyopangwa akamatwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke mmoja aliyepatikana na hatia ya kumuua bintiye nchini Italia ameripotiwa kukamatwa nchini Pakistan baada ya kutoroka kwa miaka mitatu.

    Mahakama ya Italia ilimhukumu Nazia Shaheen kifungo cha maisha bila kuwepo Desemba mwaka jana kwa mauaji ya 2021 ya Saman Abbas, 18.

    Shaheen na mumewe, Shabbar Abbas, walimuua binti yao baada ya kukataa ndoa iliyopangwa.

    Wawili hao kisha walitoroka nchini, na hatimaye Abbas alipatikana na kurejeshwa kutoka Pakistan mnamo Agosti 2023.

    Lakini Shaheen, 51, aliepuka kukamatwa hadi wiki hii, wakati aliripotiwa kufuatiliwa hadi kijijini kwenye mpaka wa Kashmir katika operesheni iliyohusisha Interpol na Polisi wa Shirikisho la Pakistan, vyanzo vililiambia shirika la habari la Italia Ansa.

    Alifikishwa mahakamani siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad, kwa taratibu za kumrejesha nyumbani, magazeti ya Italia yaliripoti.

    Kile kinachojulikana kama mauaji ya heshima ya Saman Abbas na familia yake mwishoni mwa Aprili 2021 yalishtua Italia.

    Kijana huyo aliondoka na familia yake kutoka Pakistan hadi mji wa kijijini wa Novellara mnamo 2016, kulingana na ripoti za Italia.

    Baada ya kujua Saman Abbas alikuwa na mchumba, familia ilimtaka asafiri kwenda Pakistani kwa ndoa iliyopangwa mnamo 2020, lakini alikataa.

    Kisha alikaa kwa miezi kadhaa akiishi chini ya ulinzi wa huduma za kijamii, lakini akarudi nyumbani kwa familia yake huko Novellara miezi saba baadaye, baada ya kuhadaiwa kurejea, ripoti za Italia zilisema.

    Waendesha mashtaka walisema ni wakati huu kijana huyo alitoweka.

    Mwili wa Saman Abbas hatimaye ulipatikana mnamo Novemba 2021, karibu na familia hiyo ilipoishi, baada ya mjomba wake kufichua alikozikwa.

    Uchunguzi wa maiti yake uligundua alikuwa amevunjika mfupa wa shingo, labda kutokana na kunyongwa.

  14. Ufilipino yaionya China dhidi ya 'vitendo vya vita'

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr ameionya China kutovuka mstari mwekundu katika suala la Bahari ya China Kusini, ambako mzozo kati ya nchi hizo mbili unaendelea kushika kasi.

    Iwapo mfilipino yeyote atafariki kutokana na hatua za makusudi za Uchina, alisema, Ufilipino ingeichukulia kuwa karibu na "kitendo cha vita" na kujibu ipasavyo.

    Bw. Marcos alikuwa akizungumza katika kongamano la usalama nchini Singapore lililohudhuriwa na wakuu wa ulinzi kutoka sehemu mbalimbali za dunia, zikiwemo Marekani na China.

    Kujibu, msemaji wa jeshi la Uchina aliishutumu Ufilipino kwa "kuelekeza lawama kwa Uchina" na "kuishambulia kwa maneno".

    Katika miezi ya hivi karibuni mzozo wa muda mrefu kati ya China na Ufilipino kuhusu eneo katika Bahari ya China Kusini umeongezeka.

    Ufilipino imelalamika vikali kuhusu meli za kushika doria za China kurusha maji ya kuwasha kwenye boti za Ufilipino na meli za upelekaji bidhaa nchini humo huku Beijing ikisema inatetea uhuru wake.

  15. Biden: Ni 'Uzembe' kwa Trump kusema kesi yake ilipangwa

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Joe Biden amesema ilikuwa "uzembe" kwa mtangulizi wake, Donald Trump, kuitaja kesi yake kuwa na udanganyifu, siku moja baada ya kupatikana na hatia na kuweka kihistoria nchini humo.

    Akizungumzia maoni ya kwanza kwa umma ya Trump kuhusu kupatikana na hatia kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara, Bw. Biden alitetea mfumo wa sheria wa Marekani.

    "Kanuni ya Marekani kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria ilithibitishwa tena," Bw Biden alisema kuhusu kilichotokea.

    Mapema siku ya Ijumaa, Trump alitoa maneno makali kwenye mkutano na wanahabari katika jengo la Trump Tower huko Manhattan, akimtaja jaji kuwa "mpotovu", kesi hiyo ni "uzushi" na "majambazi" wa Democrats.

    Maoni ya Bw Biden siku ya Ijumaa alasiri yanawadia mwanzoni mwa mkutano wa waandishi wa habari wa White House ambapo alijadili Mashariki ya Kati na pendekezo jipya la Israel kwa Gaza.

    Bw Biden alisema mpinzani wake wa chama cha Republican katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba alikuwa amepewa "kila fursa" ya kujitetea, na haikuwa sawa kulalamika kwamba mchakato huo haukuwa wa haki.

    "Ni uzembe. Ni hatari. Ni kutowajibika kwa mtu yeyote kusema kuwa hii ilipangwa kwa sababu tu hawapendi uamuzi huo," alisema na kuongeza kuwa Trump anakaribishwa kuwasilisha rufaa.

    Bw Biden, ambaye amezungumza mara chache sana hadharani kuhusu matatizo ya kisheria ya Trump, alisema mfumo wa sheria ndio "msingi wa Marekani".

    "Mfumo wa sheria unapaswa kuheshimiwa na kamwe tusiruhusu mtu yeyote kuubomoa. Ni rahisi tu namna hiyo. Hiyo ndio Marekani. Ndivyo tulivyo," alisema.

    Soma zaidi:

  16. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 01/06/2024