Boris Johnson akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu kwa kuhudhuria karamu wakati wa Lockdown

Maelezo ya video, "Ninaomba msamaha kutoka moyoni": Tazama Boris Johnson akikubali kuhudhuria karamu mnamo Mei 2020

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameomba msamaha kwa kuhudhuria karamu ya "njoo na pombe yako" wakati wa amri ya kutotoka nje ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Kiongozi wa chama cha Labour Sir Keir Starmer amesema Waziri Mkuu sasa lazima aache visingizio vyake "vya kusikitisha" na uwongo "wa kipuuzi".

Wakati Waziri Mkuu akipambana kuokoa wadhifa wake, alikiri bungeni "hasira" ya umma juu ya hafla ya Mei 2020 kwenye bustani ya Downing Street.

Alisema anajutia kitendo chake, na anaamini tukio hilo lilihusiana na kazi.

Alisema alitumia takriban dakika 25 kwenye hafla hiyo, ili aweze "kushukuru vikundi vya wafanyikazi" kwa bidii yao.

Lakini aliongeza: "Kwa kuzingatia athari ya tukio lenyewe bila shaka ningemrudisha kila mtu ndani.

"Ningepata njia nyingine ya kuwashukuru, na nilipaswa kutambua kwamba - hata kama ingesemwa kitaalamu ingekiuka mwongozo - kungekuwa na mamilioni na mamilioni ya watu ambao hawangeona hivyo. "

Wabunge wa upinzani walijitokeza kumtaka waziri mkuu ajiuzulu - au wabunge wake wamtoe kwa lazima - katika Maswali ya Waziri Mkuu yenye dhoruba.

Sir Keir Starmer alisema: "Hali ndio hiyo. Baada ya miezi kadhaa ya udanganyifu na udanganyifu, tamasha la kusikitisha la mtu ambaye ameishiwa njiani limefika ukingoni.

"Utetezi wake...kwamba hakutambua kuwa alikuwa kwenye tafrija ni ujinga kiasi kwamba unakera umma wa Uingereza.

"Hatimaye amelazimika kukiri kile ambacho kila mtu alijua, kwamba wakati nchi nzima ilikuwa imefungwa alikuwa akiandaa karamu za pombe Downing Street. Je, sasa atafanya jambo la heshima na kujiuzulu?"