Je Rais Ndayishimiye anaashiria kurejea kwa uhusiano mwema kati ya Rwanda na Burundi?

Chanzo cha picha, CNDD/FDD
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
Katika kile kinachoonekana kama 'ishara njema' katika kutatua mzozo wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Burundi, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema kuwa anaamini nchi hizo mbili zitakuwa tena na uhusiano mwema hivi karibuni.
Uhusiano wa Burundi na Rwanda uliingia dosari tangu mwaka 2015, baada ya kila upande kuushutumu mwingine kuunga mkono mashambulio dhidi ya mwingine.
Akizungumza mwishoni mwa Juma, Rais Ndayishimiye alisema kuwa: ''Nina imani kubwa kuwa kesho tutapendana''
Alisisitiza kuwa "utashi wa viongozi wa nchi mbili unaonekana", na pia "sababu ya mzozo inafahamika".
Bw Ndayishimiye anasema kuwa sababu ya mzozo baina yao hata Rwanda inaifahamu, na "[watakapoiondoa], mnafahamu fika kuwa ni ndugu zetu, haifai kuendelea kuwa na malumbano ", alisema.

Chanzo cha picha, CNDD/ FDD
Viongozi wa Burundi wanawashutumu viongozi wa Rwanda kwa kuwapa hifadhi baadhi ya watu waliojaribu kuupindua utawala wa Burundi mwaka 2015, shutuma ambazo Rwanda inazikanusha.
Wakati huo huo watawala wa Rwanda wanawashutumu viongozi wa Burundi kwa kuyasaidia makundi yanayopinga utawala wa Kigali yaliyopo mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, tuhuma ambazo upande wa Burundu unazipinga.
Kauli hizi za Rais Ndayizeye zimekuja kufuatia juhudi za hivi karibuni za kujaribu kuutanzua mzozo huo.
Katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa pande mbili wakiwemo mawaziri wa mambo ya nje wamekuwa wakifanya mazungumzo kujaribu kuutatua mzozo wa nchi uliozorotesha biashara kati ya nchi hizo mbili.
Kubadili kauli
'Nchi inayotumia unafiki'
Katika hotuba yake aliyoitoa katika eneo la Busoni mkoni Kirundo Mwezi Agosti 2020, Rais Evariste Ndayishimiye alisema kuwa nchi yake haitakuwa na uhusiano na nchi ambayo ''inatumia unafiki''.
Bw Ndayishimiye alikuwa akizungumzia kuhusu wakimbizi wa Burundi waliokuwa nchini Rwanda ambao alisema ''walitekwa nyara'' na nchi waliyokimbilia.
"Tunafahamu kuwa wamewateka nyara kwasababu hakuna mtu anayetaka kurejea nchini mwake huku kukiwa na nchi inayomkataza kurudi kwao...ina maanisha kuwa wamewashikilia kama wafungwa'', alisema rais Ndayishimiye.
"Tunafahamu fika ni kwanini wale wakimbizi wametekwa nyara!
Waliwateka ili waendelee kuwalinda waliofanya maasi nchini mwetu. Tunafahamu, kwani hao waliofanya maasi wanawasaidia nini kwa kuwapatia hifadhi?"

Chanzo cha picha, UNHCR
Kulingana na Ndayishimiye, waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda aliwambia waandishi wa habari kuwa waliona kuwa kwa upande wa Burundi "utashi wa kuishi vyema " na Rwanda "huenda haupo".
Hakikupita kipindi kirefu, viongozi kijeshi na kisiasa kutoka nchi mbili walikutana kufanya mazungumzo katika hatua ya kufufua uhusiano mwema baina ya nchi mbili.
Athari za mzozo
Wanyarwanda na Warundi wengi wangependa kurejea kwa uhusiano mwema, kwa maslahi ya mwananchi wa kawaida.

Chanzo cha picha, LIVE EVENT
Mzozo huu ulikatiza shughuli za kibiashara na kijamii baina ya nchi mbili baada ya safari kati ya nchi hizo kufungwa.
Akizungumzia kuhusu matumaini ya kupata suluhu ya mvutano huo wa kidiplomasia, Bw Ndayishimiye alisema:
"Huwa wanasema kuwa 'ukiwaona ndugu wamekosana, usiwaingilie. Kwasababu wao ndio huwa wanaojua wanachopigania kwani huwa wanapatana wenyewe ''.
Aliongeza kuwa : " Kuna msemo usemao 'ndugu yako hata akija akiwa na nia ya kukugonga na jembe huwa anabadili nia na kukupiga na mpini wa jembe ".
Kauli hii iliyotolewa na Rais Evariste Ndayizeye inaangaliwa na wengi kama ishara ambayo huenda inaashiria kurejesha uhusiano mwema baina ya nchi mbilio, na kauli zake za hivi karibuni zinatofautiana na zile alizozitoa Agosti mwaka 2020 ambazo zilizokatiza matumaini ya kurejea kwa uhusiano.












