Polisi wa Rwanda wawaua watu wawili katika mpaka wa nchi hiyo na Uganda

Chanzo cha picha, IKULU RWANDA
Nyakati za mapema siku ya Jumapili nchini Rwanda, polisi waliwaua raia wawili wa Uganda baada ya kuvuka mpaka kuingia Rwanda na kuwashambulia maafisa polisi karibu na mpaka wilaya ya Nyagatare.
Polisi wa Uganda wamesema wanafanya uchunguzi vifo vya wafanyabiashara Job Ebidishanga, 32 and Bosco Tuheirwe, 35 waliopigwa risasi na polisi huku wenzao wengine watatu walitoroka kurudi Uganda.
Polisi wamesema kuwa ''watu waliokuwa wakivuka kwa magendo walikua wakiwashambulia maafisa wa polisi nao walichukua hatua za kujihami kwa kuwafyatulia risasi na kuwaua.
Juma lililopita, Havugimana Peter w'imyaka 26, raia wa Rwanda, alipigwa risasi kwenye bega na mwenzake 'Muhirwa' alipigwa kifuani walipovuka mpaka kuingia Rwanda wakiwa na viazi vitamu kutoka Uganda.
Havigimana alifanikiwa kutoroka kurudi Uganda na kupatiwa matibabu huku mwenzie, akiwa amejeruhiwa vibaya alibaki Rwanda, msemaji wa polisi nchini Uganda aliiambia BBC.
Majuma mawili yaliyopita, wanawake wawili raia wa Rwanda waliuawa katika wilaya ya Nyagatare Kaskazini mwa Rwanda, kwa madai ya kukamatwa wakivusha bidhaa kwa magendo kutoka Uganda na kujaribu kuwakimbia polisi.
Tangu mwezi Februari, mvutano kati ya Rwanda na Uganda umesababisha mamlaka za Rwanda kuzuia raia wa nchi hiyo kuvuka mpaka kuingia nchini Uganda, eneo ambalo biashara ya mpakani kati ya nchi hizo mbili imeshamiri.
Tangu wakati huo, raia kadhaa wa Rwanda wameuawa, wakijaribu kuvusha bidhaa kwa njia ya magendo kutokea Uganda kinyume na marufuku iliyowekwa, polisi wanasema wanafikia hatua hiyo kwa kuwa watu hujaribu kupambana na polisi.

Chanzo cha picha, Reuters
Makubaliano ya kumaliza mzozo
Mwezi Agosti, Raisi wa Rwanda, Paul Kagame na Yoweri Museveni wa Uganda walikubaliana kumaliza mzozo wa kisiasa ambao umeathiri maelfu ya watu.
Raisi Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda walisaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo jirani.
Walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya maraisi wa Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo , Angola na rais wa Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.
Joto la kisiasa limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.
Maafisa nchini Rwanda wameishutumu Uganda kwa kuwafunga na kuwatesa kinyume cha sheria raia wake nchini Uganda, wakati Uganda nayo inaishutumu Rwanda kutekeleza ujasusi katika ardhi yake.
"Tutashughulikia matatizo haya yote". Raisi Kagame aliwaambia waandishi wa habari baada ya kusaini makubaliano hayo.
Makubaliano ya leo yamefikiwa baada ya "jitihada zilizoidhinishwa na Angola kwa usaidizi wa DR Congo" kwa mujibu wa ikulu ya Angola.
Viongozi hao wawili wamlikubaliana kutilia mkazo kutatua mzozo wowote baina ya mataifa yao kwa njia amani shirika la habari nchini Angola, Angop liliripoti.
Unaweza pia kusoma













