Afrika wiki hii kwa picha: 20-26 Oktoba 2017
Mkusanyiko wa picha bora kutoka Afrika na kuwahusu Waafrika maeneo mengine duniani wiki hii.

Chanzo cha picha, AFP
Waumini hawa wa madhehebu ya Legio Maria wanaonekana wakiathiriwa na mabomu ya kutoa machozi wakitembea mtaani Mathare, Nairobi wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na polisi siku ya uchaguzi wa marudio Alhamisi.

Chanzo cha picha, AFP
Uwanja wa Mohamed VI mjini Casablanca nchini Morocco hali ilikuwa hivi mashabiki wa Wydad Casablanca walipokuwa wanatazama timu hiyo yao ikilaza USM Alger ya Algeria na kufika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

Chanzo cha picha, AFP
Wanamitindo hawa waliovalia mavazi ambayo ni ubunifu wa Amede kutoka Nairobi walishiriki katika maonesho ya Mitindo na Mavazi ya Lagos siku ya Jumatano. lengo la maonesho hayo ni kusaidia na kuvumisha tasnia ya mitindo ya mavazi Nigeria na Afrika kwa jumla.

Chanzo cha picha, Reuters
Na nchini Kenya, Wakenya hawa walikuwa na ujumbe wa amani taifa hilo lilipokuwa likijiandaa kwa uchaguzi wa marudio ambao ulisusiwa na upinzani. Walionekana wakijipiga selfie wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mashujaa ambayo huadhimishwa kila tarehe 20 Oktoba.

Chanzo cha picha, AFP
Lakini kulitokea makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa upinzani kabla ya uchaguzi huo kufanyika - hapa mfuasi wa upinzani anaonekana akiandamana katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi siku ya Jumatano kabla ya uchaguzi kufanyika Alhamisi...

Chanzo cha picha, Reuters
Kulitokea vurugu zaidi Alhamisi, siku ya uchaguzi yenyewe. Hapa, mwanamume anaonekana akitazama kwa mbali wafuasi wa upinzani wakikabiliana na polisi...

Chanzo cha picha, Reuters
Na wahamiaji hawa kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaonekana kando ya barabara Jumamosi katika mji wa Misrata nchini Libya wakisubiri kazi.

Chanzo cha picha, Reuters
Msichana mkimbizi kutoka Sudan Kusini naye anaonekana hapa akiwa kambi ya wakimbizi ya Nguenyyiel siku ya Jumanne, wakati wa ziara ya balozi wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Gambella, Ethiopia.

Chanzo cha picha, EPA
Na Matembezi ya Pamoja ya Mandela yalifanyika Westminster, London, siku ya Jumatatu na kuhudhuriwa na mjane wake Graca Machel na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan pamoja na watu wengine mashuhuri.

Chanzo cha picha, Reuters
Na mtali huyu kutoka Uingereza Tom Morgan anaonekana akipaa juu ya Afrika Kusini siku ya Ijumaa. Alisafiri 25km (maili 15.5 ) akiwa amefungwa kwenye kiti cha watalii na kuinuliwa juu na puto 100 za gesi aina ya helium.

Chanzo cha picha, EPA
Na mteleza kwenye mawimbi Mike Schlebach wa Afrika Kusini anaonekana akishiriki mashindano ya kuteleza kwenye mawimbi baharini pwani ya mji wa Cape Town siku ya Jumatatu. Baadhi ya mawimbi yalikuwa na urefu wa 5m (16ft).
Picha kwa hisani ya AFP, EPA, PA na Reuters












