Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Papa atoa kipaumbele kwa Afrika ambako Ukatoliki unakuwa kwa kasi zaidi
- Author, Lebo Diseko
- Nafasi, Global religion correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Papa Leo XIV anataka kuweka ''Afrika machoni pa ulimwengu'' kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Vatican kupitia ziara yake kubwa barani humo, akilenga kuangazia masuala ya amani, uhamiaji na mazungumzo kati ya dini mbalimbali.
Anapoanza ziara yake ya siku 11, leo Jumatatu, Hii ni safari yake ya pili kubwa nje ya nchi tangu alipotawazwa kuwa Papa mwezi Mei mwaka jana, na inaakisi nafasi inayozidi kuimarika ya Afrika ndani ya Ukatoliki wa kimataifa.
Zaidi ya theluthi moja ya Wakatoliki duniani, takribani watu milioni 288 kufikia mwaka 2024, wanaishi barani Afrika, hali inayoifanya kuwa moja ya maeneo yanayokua kwa kasi zaidi kwa Kanisa.
Takwimu za hivi karibuni za Vatican zinaonyesha ongezeko kubwa la waumini waliobatizwa katika bara hili.
Ziara hiyo, inayochukuliwa kuwa ya kipaumbele binafsi kwa Papa Leo, itamfikisha katika miji 11 ndani ya nchi nne: Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea. Kwa jumla, atasafiri takribani kilomita 18,000, akitumia safari 18 za ndege.
Ingawa karibu nchi zote katika ziara hiyo zina idadi kubwa ya Wakatoliki, Papa amechagua kuanza safari yake nchini Algeria, nchi isiyo ya Kikatoliki kwa wingi, kwa sababu ya umuhimu wake wa kipekee wa kihistoria na kiimani.
Algeria ni mahali alipozaliwa Mtakatifu Augustino, mwanafalsafa na mwanateolojia wa karne ya nne ambaye mafundisho yake kuhusu unyenyekevu na maisha ya kijamii yameacha alama kubwa katika Kanisa. Papa Leo XIV ndiye Papa wa kwanza kutoka katika shirika linalofuata mafundisho yake.
Akiwa huko, Papa anatarajiwa kutembelea eneo lililojulikana zamani kama Hippo - sasa Annaba - ambako Mtakatifu Augustino aliwahi kuwa askofu, na kuongoza ibada ya Misa.
Ziara hii itakuwa ya kwanza kwa Papa yeyote kufika nchini Algeria, na mazungumzo na ulimwengu wa Kiislamu yanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya ratiba yake.
Miongoni mwa matukio muhimu ni ziara katika Great Mosque of Algiers, pamoja na kutembelea Basilica of Our Lady of Africa - eneo la hija na sala linaloheshimiwa na Wakristo na Waislamu kwa pamoja.
Nyuma ya sanamu ya Bikira Maria mwenye asili ya Kiafrika kuna maandishi yasemayo: "Tuombee, na uwaombee Waislamu."
End of Pia unaweza kusoma:
Padri Peter Claver Kogh, msimamizi wa basilika hiyo, aliiambia BBC kuwa "Papa Leo atatuhimiza kuimarisha imani yetu na kujenga dunia mpya.
''Dunia yenye amani ambako watu wanaishi kwa maelewano."
Hata hivyo, ziara hiyo inajiri wakati ambapo makundi ya haki za binadamu yanaeleza wasiwasi wao kuhusu namna Algeria inavyowatendea walio wachache wa kidini.
Algeria ina idadi kubwa ya waislamu wa dhehebu la Sunni.
Katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya Wakristo na Waislamu wa madhehebu ya Ahmadi wamekumbwa na vifungo kwa tuhuma za "ibada zisizoidhinishwa" au kuikosea dini ya Kiislamu.
Baada ya Algeria, Papa ataelekea Cameroon, ambako mzozo katika maeneo mawili yanayotumia Kiingereza unatoa taswira nzito ya changamoto zinazolikabili taifa hilo.
End of Pia unaweza kusoma:
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 6,000 wamepoteza maisha na zaidi ya nusu milioni wameyakimbia makazi yao kutokana na ghasia zilizoanza karibu muongo mmoja uliopita, zikichochewa na mvutano kati ya watu wanaotaka kujitenga wanaozungumza Kiingereza na serikali inayotawaliwa na kifaransa.
Katika mji wa Bamenda, kitovu cha mzozo huo, Papa ataongoza Misa ya kuombea amani na haki. Wakazi wengi wana matumaini kuwa ziara hiyo itachochea maridhiano.
Ernestine Afanwi, mama mwenye umri wa miaka 45 aliyelazimika kukimbia makazi yake baada ya nyumba na biashara yake kuharibiwa, alisema:
"Mungu anakuja - kwa sababu yeye ni Mungu duniani - najua kwamba kila kitu kitatatuliwa,"anasema Ernestine.
Kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, yeye na watoto wake sita wamekuwa wakiishi na wakimbizi wengine wa ndani kwenye kiwanda cha kusindika chakula cha zamani cha ramshackle katika mji mkuu, Yaoundé.
"Ikiwa ningekutana ana kwa ana na Papa, ningemwambia matatizo yangu yote [na kumwomba] kuiombea ardhi,"aliiambia BBC.
Ziara hiyo pia itamfikisha Papa nchini Angola, taifa lililowahi kushuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miongo kadhaa hadi mwaka 2002.
Hapa, ujumbe wa amani na ujenzi upya utapewa kipaumbele.
Papa anatarajiwa kuongoza ibada kubwa itakayowakutanisha waumini wapatao 200,000 katika nchi ambayo kati ya asilimia 40 hadi 55 ya watu wake ni Wakatoliki.
Uwepo wa Kanisa Katoliki nchini Angola ulianza mwishoni mwa Karne ya 15, wakati wavumbuzi wa Kireno na wamisionari walifika kwenye pwani ya Angola.
Kituo cha mwisho kitakuwa Equatorial Guinea, ambako zaidi ya asilimia 70 ya wananchi ni Wakatoliki.
Masuala ya haki za kijamii yanatarajiwa kujitokeza, hasa ikizingatiwa kuwa rais wa nchi hiyo, Teodoro Obiang Nguema, amekuwa madarakani kwa karibu miaka 50, akiwa mmoja wa viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani.
Wakosoaji wamekuwa wakiishutumu serikali yake kwa ukiukaji wa haki za binadamu, madai ambayo serikali imekuwa ikiyakanusha.
Mbali na kukutana na viongozi wa serikali, Papa atatembelea hospitali ya wagonjwa wa akili, gereza, na pia kukutana na vijana, ikiashiria dhamira yake ya kugusa maisha ya watu wa kawaida.
Ingawa hii ni ziara yake ya kwanza ya kichungaji barani Afrika tangu awe Papa, si mgeni katika bara hili. Akiwa Kardinali Robert Prevost, aliwahi kutembelea nchi kadhaa zikiwemo Kenya na Tanzania.
Katika umri wa miaka 70, Papa Leo anatarajiwa kutoa takribani hotuba 25, kukutana na viongozi wa kisiasa, jamii za Kikatoliki na kushiriki katika majadiliano ya kidini.
Kwa ujumla, ukubwa na uzito wa ziara hii vinaonyesha wazi mkakati wa Vatican kuipa Afrika nafasi ya mbele katika maisha ya Kanisa la Katoliki duniani.
Kwa kuichagua Afrika kama kitovu cha ziara hii pana, Papa Leo anathibitisha kuwa bara hili si tu mahali pa imani, bali pia ni chemchemi ya matumaini, uthabiti na ukuaji wa baadaye wa Kanisa.
Ripoti ya ziada ya Nomsa Maseko, Paul Njie huko Yaoundé na Ager Oueslati huko Algiers
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid