"Najiona kama Mrusi": Waukraine waliochukua silaha dhidi ya nchi yao

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Magharibi mwa Ukraine, nyuma ya kuta ndefu na safu za malango yaliyofungwa, kuna kambi iliyojaa wanaume waliotekwa wakiipigania Urusi.

Wengi wa wale waliokaa chini kwa kujikunyata kivulini pembezoni mwa uwanja wa gereza walitoka katika miji mikubwa kama vile St. Petersburg na Yekaterinburg, badala ya kutoka maeneo ya mbali na maskini kama ilivyokuwa mwanzoni mwa uvamizi huo mkubwa.

Lakini si wafungwa wote ni Warusi.

Miongoni mwao kuna askari kutoka Ukraine yenyewe: wanaume walioenda kupigana dhidi ya nchi yao wenyewe.

Kufanya mahojiano na wafungwa wa vita si jambo rahisi: kwanza kabisa, ni lazima kuhakikisha hawashinikizwi, na kisha kutathmini jinsi wanavyozungumza kwa uwazi katika mazingira hayo.

Hata hivyo, kwa kuwa hakuna fursa ya kuwafikia wanajeshi walio ndani ya Urusi, hii ni nafasi ya kutathmini mwenendo wa vita hivi na kuchunguza nini kinaweza kuwachochea wanajeshi wanaopigana.

Hii inajumuisha pia askari waliozaliwa Ukraine lakini wanaopigana upande wa Urusi.

Tulimpa kila mmoja haki ya kukataa mahojiano, na tukazungumza na wale waliokubali tukiwa mbali na walinzi na bila kamera.

Mbali na mahojiano rasmi, nilipata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wafungwa, kwa lugha ya Kirusi, katika maeneo kadhaa.

Anton alikuwa na umri wa miaka 10 wakati eneo lake la Donbas, mashariki mwa Ukraine, lilipochukuliwa na vikosi vinavyoiunga mkono Moscow.

Mnamo mwaka wa 2022, wakati Vladimir Putin alipochochea vita kamili, Anton alitimiza umri wa miaka 18 na kujiunga mara moja na mapigano, kwa upande wa Urusi.

"Sijutii uamuzi wangu. Nilienda kutetea ardhi yangu," Anton anasisitiza na kuniambia kuwa marafiki zake pia walijitolea. "Kisha unapokea ujumbe mfupi wa simu (SMS). Amekufa, amekufa, amekufa."

Wafungwa wengine wanasema vivyo hivyo: kwamba watu wote walioenda nao vitani wameuawa.

Pia wanasema kuwa watu wachache wanajitolea kuchukua nafasi zao, licha ya malipo makubwa ya kujiunga, jambo linaloashiria kuwa nia ya Putin ya kuepuka uhamasishaji wa watu wengi inaweza kukabiliwa na changamoto hivi karibuni.

Wakati Ukraine inapowakamata raia wake yenyewe kwenye uwanja wa vita, huwafungulia mashtaka ya uhaini.

Hata hivyo, wanaume hao baadaye hupelekwa kwenye kambi za wafungwa wa vita pamoja na Warusi.

Rasmi, Kyiv bado inawaona kama raia wa Ukraine na kuchukulia udhibiti wa Urusi katika maeneo yao kuwa wa muda mfupi. Lakini hali halisi ni ngumu zaidi.

"Najiona kama Mrusi. Nchi haina maana, yote ni kuhusu utaifa. Familia yangu yote inatoka Urusi. Mizizi yangu yote inatoka huko," anasema.

Tunapojiuliza kuhusu jina lake la ukoo la Kiukreni, anapuuza hilo kama lisilo na maana.

Kizazi kizima kilichozaliwa Ukraine sasa kimekua chini ya uvamizi, huku elimu na vyombo vya habari vya Urusi vikidhibitiwa kikamilifu na Kremlin.

Vyote vimeonyesha mamlaka huko Kyiv kama "Wanazi" na haramu kwa miaka mingi.

Tangu uvamizi kamili, eneo kubwa zaidi limeathiriwa na hilo.

Anton ameyachukua yote na sasa anazungumza karibu kabisa katika kaulimbiu za Kirusi.

Anamtaja Putin kama "Rais wangu" na anaamini anapaswa kushinikiza kuteka eneo lililobaki la Donbas, licha ya mamia ya maelfu ya watu kupoteza maisha katika jaribio hilo.

"Inasikitisha kwamba watu walikufa, hasa wale wasio na hatia," anasema Anton. "Lakini vita ni vita. Ingeweza kumalizika. Lakini hakuna aliyeitaka hiyo."

Katika hospitali ya gereza, Artyom amelala kwenye kitanda kilicho pembeni, mwili wake ukiwa umejaa vipande vya chuma kutoka kwenye milipuko. Alikuwa amepigana kwa miezi miwili pekee.

Kama ilivyokuwa kwa Anton, yeye pia alikwenda vitani kwa hiari yake si kwa ajili ya pesa pekee.

"Tuna dukuduku zetu wenyewe," anasema Artyom, akikumbuka jinsi eneo lake lilivyoshambuliwa vikali mwaka 2014 wakati majeshi ya Ukraine yalipojaribu kuzuia eneo hilo kujitenga na Kyiv.

Lakini uzoefu wake wa kijeshi umemwacha na uchungu. Kamanda wake alikuwa "mbaya" na hakuwahi kupata hata senti moja ya malipo yake ya awali ya kujiunga ya ruble 400,000 (pauni 3,470; dola 5,000).

Kinachoongeza uchungu zaidi kwa majeraha mengi ya Artyom ni ukweli kwamba askari wa Urusi aliyejeruhiwa na kulala kwenye kitanda cha mkabala naye alilipwa kiasi mara tano zaidi ya hicho.

Wanajeshi wote wa Ukraine waliotekwa vitani tuliowahoji walitoka katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 2014, na karibu wote walijiunga na jeshi la Urusi kwa hiari yao wenyewe.

Hata hivyo, mwanamume mmoja kutoka eneo la Donetsk alituambia kuwa alilazimishwa kupigana.

Macho yake yalikuwa yakitazama huku na huko alipokuwa akizungumza, akiwa na wasiwasi kuhusu ni nani anayeweza kumwamini.

Takwimu rasmi moja, ikirejelea taarifa za kijasusi, inaonyesha kuwa zaidi ya raia 50,000 wa Ukraine wameandikishwa jeshini kwa nguvu katika maeneo hayo yaliyokaliwa kwa mabavu. Wengine wanakadiria idadi hiyo kuwa kubwa zaidi.

Mwanamume huyu alituambia kuwa wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi, familia yake ilibaki huko, si kwa sababu ya utiifu wa kisiasa au uzalendo, bali kwa sababu Donetsk ndiyo ilikuwa nyumbani kwao.

Sasa, lengo lake kuu lilikuwa kurudi kwa mkewe na watoto wake, kisha kuepuka kurejeshwa mstari wa mbele wa vita. "Nitajificha tu," alieleza kwa siri.

Mbele kidogo, harufu kali ya rangi ya 'varnish' kutoka kwenye choo cha nje inanuka.

Afisa mmoja anainua mpini wa plastiki wenye rangi ya dhahabu kutoka kwenye begi karibu na mlango. "Jaribuni kukisia hiki ni cha kazi gani?" anatuuliza huku akitabasamu.

Ndani, nashangazwa na ninachokiona: wanaume wanaofanya kazi humo wanatengeneza majeneza ya mbao kwa kuyagonganisha pamoja.

Ninaambiwa kuwa mkataba wa mwisho ambao gereza hilo lilipata ulikuwa wa kutengeneza vibanda vya bustani. Huu wa sasa unahisiwa kuwa wa kutisha na kuhuzunisha.

Upande wa pili wa uwanja, katika karakana nyingine, kundi dogo la wafungwa wa kivita linatengeneza miti bandia ya Krismasi, huku mapambo ya rangi angavu yakining'inia kutoka kwenye mashine zao.

Kama ilivyo kwa watengenezaji wa majeneza, wananiambia kuwa hutumia mishahara yao kununua chakula cha ziada na sigara.

Sergei alizaliwa katika mji wa Luhansk nchini Ukraine lakini anasema yeye ni Mrusi kama wazazi wake, ambao walihamia eneo la Donbas wakati nchi zote mbili zilipokuwa sehemu ya Umoja wa Kisovyeti.

Alijiunga na jeshi la Urusi muongo mmoja uliopita "ili kutetea nchi yangu," lakini anadai kuwa atastaafu atakaporejea, na hatarudi mstari wa mbele wa vita. "Nimeshatimiza wajibu wangu."

Wengi hawatakuwa na chaguo.

Anayepanga matawi ya plastiki karibu na Sergei ni muuzaji wa dawa za kulevya ambaye alijiunga na jeshi, kama wengine wengi, kwa sababu moja tu: ili kuepuka kifungo cha muda mrefu gerezani.

"Kwangu mimi, miaka 15 gerezani ilikuwa mingi mno," Konstantin anaeleza. "Najua labda hilo halinifanyi nisilaumiwe, lakini ndiyo uhalisia. Nina umri wa miaka 44 sasa; ningekuwa na miaka 60. Kwa hiyo, hapana."

Ninapouliza kuhusu kuwaua raia wenzao wa nchi hiyo kwenye uwanja wa vita, Sergei anaita swali hilo kuwa la "uchochezi" na hataki kulijibu.

"Sioni jema lolote katika vita vyovyote, na katika vita kama hivi hakuna jema lolote linaloweza kuwepo tangu awali," Konstantin anajibu kwa uangalifu. "Sisemi kwamba sisi ni sawa na Waukraine, lakini tuna uhusiano wa karibu. Sote tuna ndugu huko. Hali hii si nzuri hata kidogo."

Bado anaamini kuwa uamuzi wake wa kupigana ulikuwa sahihi.

Yeye na Sergei hawatarajii vita hivyo kumalizika hivi karibuni. Wote wanaamini kuwa Putin hataacha hadi atakapodhibiti eneo lote la Donbas.

"Lakini kila mtu ninayemfahamu huko amechoshwa na hali hii," anasema Konstantin. "Nataka tu haya yaishe, haraka iwezekanavyo."

Wakati wa chakula cha mchana, wafungwa waliovalia ovaroli za rangi ya bluu iliyokolea huingia ukumbini kwa mpangilio, wakiwa wameinamisha vichwa na kushikilia mikono yao nyuma ya migongo.

Wanapokula, supu na kitoweo, video yenye kichwa "Hadithi za Uongo kuhusu Crimea" huonyeshwa mara kwa mara; video hiyo inapinga madai ya Urusi ya umiliki wa kihistoria wa rasi hiyo ambayo iliichukua kutoka Ukraine mwaka 2014, lakini hakuna anayeijali hata kidogo.

Jitihada hizo za kuwabadilisha mitazamo zinaonekana kutofanywa kwa dhati. Kwa Kyiv, lengo kuu ni kuwatumia wafungwa hawa wa kivita kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana ili kuwarejesha nyumbani askari wake yenyewe.

Hata hivyo, inapokuja suala la kujadili orodha za kubadilishana, inaonekana kuwa wanaume hao kutoka eneo la Donbas hawapewi kipaumbele na Urusi.

"Ni watu wapatao kumi na wawili pekee ndio wamehamishwa mwaka huu," Konstantin analalamika. "Inaonekana hawana nia ya kutubadilisha. Nadhani sisi tutakuwa wa mwisho kuondoka."

Taarifa za ziada zimetolewa na Anastasia Levchenko.