Majina 11 yaliyotikisa usajili wa Januari 2026

Chanzo cha picha, BBC/Getty
Dirisha la usajili wa Januari 2026 limefungwa rasmi nchini England na katika ligi nyingine kubwa duniani, likiacha nyuma yake mchanganyiko wa dili za kushangaza, maamuzi ya kimkakati na uhamisho uliotikisa mashabiki.
Tofauti na Januari nyingi zilizopita ambazo mara nyingi huonekana tetesi nyingi, safari hii vilabu kadhaa hasa vya Ligi Kuu ya England vilichukua hatua kubwa kifedha, vikihusika katika uhamisho wa wachezaji waliogharimu mamilioni ya pauni.
Kwa mujibu wa takwimu za soko la usajili, vilabu vya ligi kuu England vilihusika katika uhamisho saba kati ya kumi ghali zaidi duniani kwa mwezi Januari, ishara nyingine ya nguvu yao ya kifedha katika soka la kisasa.
Hawa hapa ni wachezaji 10 waliotikisa zaidi dirisha la usajili wa Januari 2026, si kwa thamani pekee, bali pia kwa uwezo wao ndani na nje ya uwanja.
1. Antoine Semenyo: Bournemouth kwenda Manchester City (£65m)

Chanzo cha picha, Getty Images
Huu ndio ulikuwa uhamisho uliokuwa ukisubiriwa zaidi tangu dirisha lifunguliwe. Kila klabu kubwa ilifahamu uwepo wa kipengele cha kuvunja mkataba cha pauni milioni 65 kwa Semenyo, lakini Manchester City ndiyo iliyokuwa ya haraka na yenye maamuzi. Ikachukua hatua.
Katika mbio zilizowahusisha Liverpool, Manchester United na Tottenham, City ilionyesha tena kwa nini mara nyingi hushinda vita vya usajili.
Semenyo anawasili Etihad kama mchezaji aliyekomaa, tayari kwa kucheza soka la kiwango cha juu, na tarari ameanza kuonyesha uwezo wake wa kufunga katika michuano mbalimbali aliyoanza kuichezea Man city.
2. Jeremy Jacquet: Rennes kwenda Liverpool (£60m)

Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool wamekamilisha dili la pauni milioni 60 kumsajili beki wa kati wa Rennes, Jeremy Jacquet, katika uhamisho wa dakika za mwisho uliowashangaza wengi kutokana na umri wake mdogo wa miaka 20.
Ingawa makubaliano yamekamilika sasa, Jacquet atasalia Rennes hadi mwisho wa msimu kabla ya kujiunga rasmi na Liverpool majira ya kiangazi.
Uamuzi wa Liverpool kuwekeza kiasi kikubwa kwa beki kijana unaeleweka katika muktadha wa matatizo ya kikosi chao hasa eneo la ulinzi wa kati. Mabingwa hao wa England wamekuwa wakikabiliwa na ufinyu wa wachezaji katika nafasi hiyo, huku hatma ya Ibrahima Konaté ikiwa mashakani kutokana na uwezekano wa kuondoka bure mwishoni mwa msimu.
Jacquet ameonekana kama mradi wa muda mrefu wa Anfield, beki mwenye uwezo wa kimwili, utulivu katika umiliki wa mpira, na uelewa wa kisasa wa nafasi ya beki wa kati.
3. Jørgen Strand Larsen: Wolves kwenda Crystal Palace (£43m)
Kwa Wolves, huu ulikuwa uamuzi mgumu sana kwao kuuza nyota na tegemeo lake lakini ulikuwa uamuzi wa lazima. Kuuza mshambuliaji wao kwa fedha kubwa katikati ya msimu kulizua maswali, lakini pauni milioni 43 ni dau ambalo halikuwa rahisi kulikataa.
Crystal Palace, kwa upande wao, waliona nafasi ya kumjengea kocha wao kikosi chenye ushindani zaidi. Strand Larsen anawasili Selhurst Park akiwa na jukumu la kubeba matumaini ya mabao, huku Wolves wakipata nafasi ya kupanga upya mipango yao ya muda mrefu.
Alitarajiwa kwenda kuziba nafasi ya Jean-Philippe Mateta ambaye mpango wake wa kwenda AC Milan ulikwama baada ya vipimo vya afya kuonyesha ana matatizo yanayoweza kumuweka nchi kwa muda.
4. Brennan Johnson: Tottenham kwenda Crystal Palace (£35m)

Chanzo cha picha, Getty Images
Palace hawakupoteza muda baada ya kumpoteza Semenyo. Kabla hata dirisha halijafunguliwa rasmi, walivunja rekodi yao ya uhamisho kwa kumsajili Brennan Johnson, shujaa wa Tottenham katika michuano ya Ulaya.
Uamuzi wa Spurs kumuachia Johnson haukupokelewa vyema ndani ya kikosi, huku baadhi ya wachezaji wakishangazwa kuuzwa kwa mchezaji muhimu hasa katika mechi kubwa.
Kwa Palace, huu ulikuwa ushindi wa mapema katika dirisha la usajili.
5. Lucas Paquetá: West Ham kwenda Flamengo (£35.8m)
Huu ulikuwa zaidi ya uhamisho wa kawaida ulikuwa kurudi nyumbani. Flamengo walipokea kwa shangwe kurejea kwa Paquetá, wakiuona kama usajili wa kihistoria katika soko la soka la Brazil.
West Ham walijaribu kila walichoweza kumbakiza kiungo huyo mbunifu, lakini dhamira ya mchezaji kurejea nyumbani ilizidi nguvu za hoja za kifedha.
Uhamisho huu umeacha pengo kubwa la ubunifu kwa The Hammers.
6. Conor Gallagher: Atlético Madrid kwenda Tottenham (£34.6m)
Fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya Brennan Johnson zilitumika moja kwa moja kumsajili Conor Gallagher. Tottenham walikuwa wanahitaji nguvu, kasi na nidhamu katikati ya uwanja na Gallagher alionekana kuwa jibu la hilo.
Ingawa swali linaendelea kubaki kama uhamisho huu utalipa kwa kiwango cha fedha kilicholipwa, hakuna shaka kuwa Gallagher analeta nguvu na ari ambayo Spurs walikuwa wanakosa. Ni nyota mkubwa.
7. Ademola Lookman: Atalanta kwenda Atlético Madrid (£30.2m)

Chanzo cha picha, Getty Images
Atlético Madrid waliwekeza kwa busara fedha walizopata, wakimsajili Ademola Lookman, mmoja wa wachezaji waliokuwa na takwimu nzuri katika ligi kuu ya itali (Serie A).
Mabao 55 na pasi za mwisho 27 katika mechi 137 akiwa na Atalanta zilizungumza zenyewe.
Lookman anatarajiwa kuongeza makali ya ushambuliaji kwa kikosi cha Diego Simeone, huku akileta kasi na uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za mbele.
8. Oscar Bobb: Manchester City kwenda Fulham (£27m)
Kwa wengi, pauni milioni 27 kwa mchezaji aliyeanza kikosi cha kwanza katika mechi 13 tu za ligi ilionekana bei kubwa. Hata hivyo, Fulham waliamini wanamchukua mchezaji mzuri kabla thamani yake haijapaa zaidi.
Manchester City huenda wakaja kujuta uamuzi huu baadaye, hasa kama Bobb ataendelea kukua na kuonyesha kipaji chake kikamilifu.

Chanzo cha picha, Getty Images
9. Mohamed Kader Meïté: Rennes kwenda Al Hilal (£26m)
Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 18 alihusishwa na vilabu vikubwa barani Ulaya, lakini hatimaye akaelekea Saudi Arabia.
Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa kuhusu mwelekeo wa wachezaji vijana kuchagua fedha mapema katika taaluma zao.
Kwa Al Hilal, huu ni uwekezaji wa baadaye huku kwa upande wa Meïté, ni mwanzo wa safari yenye maswali mengi.
10. Taty Castellanos: Lazio kwenda West Ham (£26m)

Chanzo cha picha, Getty Images
West Ham walijua hawakuwa na muda wa kupoteza. Katika mapambano ya kubaki Pligi kuu, walihitaji mshambuliaji mpya haraka. Castellanos, licha ya msimu usio bora Lazio, aliwasili na kuanza vyema, akifunga bao muhimu katika Kombe la FA.
Bao hilo liliwapa mashabiki matumaini mapyaangalau kwa muda.
Huenda akawasaidia West Ham kukwepa kushuka daraja.
11. Rayan: Vasco da Gama kwenda Bournemouth (£24.7m)
Bournemouth waliwekeza kwa kijana mwenye kipaji kikubwa, wakimchukua Rayan mwenye umri wa miaka 19.
Mabao 20 katika mechi 57 mwaka 2025 yalitosha kuwashawishi The Cherries, ambao pia wanaweza kulipa nyongeza endapo malengo fulani yatatimia, kulingana na mkataba waliosaini na klabu hiyo ya Brazil
Makala hii ni kwa msaada wa vyanzo mbalimbali ikiwemo football365 na Skysport















