Tetesi za soka Ulaya: Manchester United inafikiria kumsajili Rafael Leao

Muda wa kusoma: Dakika 2

Manchester United huenda ikamgeukia winga wa Ureno Rafael Leao, 26, msimu huu wa kiangazi, huku AC Milan ikiwa tayari kujadili dili la kubadilishana wachezaji litakalomhusisha Marcus Rashford, 28, Manuel Ugarte, 25, au mshambuliaji wa Uholanzi Joshua Zirkzee, 24. (La Gazzetta dello Sport).

Crystal Palace imeandaa orodha ya makocha sita wanaoweza kumrithi Oliver Glasner mwishoni mwa msimu, huku Frank Lampard wa Coventry na Kieran McKenna wa Ipswich wakitajwa miongoni mwa wanaopewa nafasi. (Independent).

Manchester United haitaki kuingia kwenye ushindani wa kifedha ili kumsajili kiungo wa Nottingham Forest na England Elliot Anderson, 23, ambaye pia anawindwa na Manchester City, na huenda ikageukia chaguo jingine kama Carlos Baleba wa Brighton.(ESPN).

Newcastle inapanga mabadiliko makubwa ya kikosi kiangazi hiki, huku kipa Robin Risser wa Lens na James Trafford wa Manchester City wakitajwa kuwania nafasi ya kipa namba moja.(i paper).

Nahodha wa Manchester United Bruno Fernandes, 31, ana kipengele cha kuondoka cha pauni milioni 57 katika mkataba wake, lakini klabu hiyo inaamini kufuzu Ligi ya Mabingwa kutatosha kumshawishi kubaki Old Trafford. (Mirror).

Barcelona inaendelea kusukuma mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Atletico Madrid na Argentina Julian Alvarez, 26, lakini Arsenal na Paris St Germain bado hazijaondoa nia yao ya kumuwania. (Teamtalk).

Leeds United imefufua nia ya kumsajili kiungo mkabaji wa Sporting, Hidemasa Morita, 30, huku nyota huyo wa Japan akielezwa kuwa tayari kujiunga iwapo klabu hiyo itasalia Ligi Kuu. (Mail).

Marseille huenda ikalazimika kumuuza mshambuliaji wa England Mason Greenwood, 24, kwa sababu za kifedha, huku Juventus ikitajwa kuwa tayari kuwasilisha ofa, ingawa Marseille inahitaji angalau euro milioni 50 kumsajili mchezaji huyo.( La Gazzetta dello Sport).

Benfica imemuweka kocha wa Fulham Marco Silva, 48, kwenye orodha ya wanaotajwa kuchukua nafasi ya Jose Mourinho, ambaye anahusishwa na uwezekano wa kurejea Real Madrid msimu ujao. (Record)

Everton tayari imewasilisha ofa kwa PSV kwa ajili ya mshambuliaji Esmir Bajraktarevic, 21, raia wa Bosnia na Herzegovina aliyezaliwa Marekani, kabla ya dirisha la usajili la kiangazi. (SportSport).

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid