Unayopaswa kuyajua kuhusu kuapishwa kwa Donald Trump

- Author, Ana Faguy
- Nafasi, BBC News, Washington
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais mteule Donald Trump atarejea tena katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu, punde tu atakapo apishwa rasmi kuwa rais wa 47 wa Marekani.
Siku ya kuapishwa itajumuisha sherehe rasmi ya kuapishwa pamoja na tumbuizo la muziki, gwaride la sherehe na kucheza.
JD Vance pia atakula kiapo siku ya Jumatatu, na kuungana na Trump jukwaani kuanza rasmi utawala wao mpya.
Sherehe ya utambulisho ni nini?
Utambulisho ni sherehe rasmi inayoashiria kumalizika kwa muda wa rais mmoja madarakani na kuanza kwa utawala wa rais mpya.
Sehemu muhimu ya sherehe hizo ni pamoja na rais mteule kukariri kiapo: "Naapa kwa dhati nitatekeleza kwa uaminifu majukumu ya Ofisi ya Rais wa Marekani, na nitafanya kwa uwezo wangu wote, kuhifadhi, kulinda na kutetea Katiba ya Marekani."
Ingawa alishinda uchaguzi mwezi Novemba, Trump atakuwa rasmi rais wa 47 mara tu atakaposema maneno hayo.
Naye Vance atakula kiapo ili awe makamu wa rais rasmi.
Tukio hilo pia linajumuisha maonyesho ya muziki, hotuba - wakati ambapo Trump atahutubia wapiga kura wake na kueleza malengo yake ya miaka minne ijayo – vilevile gwaride na kucheza.
Sherehe itakavyokuwa
Siku ya pili ya sherehe ya kuapishwa kwa Trump itaanza kwa ibada katika Kanisa la St. John's, Lafayette Square, kanisa la kihistoria la Washington DC, ikifuatiwa na chai katika Ikulu ya White House.
Maonyesho ya muziki na matamshi ya ufunguzi yanapangwa kufanyika kwenye jukwaa kuu la hafla hiyo - lililoko kwenye majengo ya bunge la Marekani.
Kisha itafuatiwa na kuapishwa kwa Trump na Vance pamoja na hotuba ya kuapishwa.
Kisha Trump ataingia ndani ya Chumba cha Rais - karibu na ukumbi wa Seneti - kutia saini hati muhimu za kuanza utawala wake mpya.
Kamati ya Pamoja ya Bunge la Congress kuhusu sherehe za kuapishwa rais itaandaa chakula cha mchana ambacho rais atahudhuria.
Kisha gwaride litaanza, kutoka majengo ya Bunge (Capitol) kupitia mtaa wa Pennsylvania hadi Ikulu ya White.
Baadaye jioni, Trump ataonekana kwenye sherehe tatu za kucheza – ya Amiri Jeshi Mkuu, ya uhuru na ya Starlight. Anatarajiwa kuzungumza katika dansi zote tatu.
Unawezaje kutazama sherehe hiyo?
Kwa kawaida kuna mahitaji makubwa ya watu kuhudhuria sherehe hizo. Wajumbe wa Congress hupokea idadi fulani ya tiketi za sherehe, ambazo wanaweza kuzisambaza kwa wapiga kura wao.
Tiketi hizi ni za bure, lakini mara nyingi ni ngumu kuzipata. Wamarekani wanaweza kuwasiliana na wawakilishi wao moja kwa moja kuomba tiketi.
Ikiwa huwezi kuhudhuria ana kwa ana, kuna njia nyingi za kutazama. Ikulu ya White House inaonyesha mubashara sherehe hiyo kupitia runinga.
Nani atahudhuria?
Maafisa wa serikali wapatao 200,000 wanatarajiwa kujitokeza huko Washington DC, na itajumuisha wafuasi wake na wakosoaji wake.
Maseneta wengi wa Marekani na wabunge pia watahudhuria, pamoja na wageni wa utawala unaokuja.
Mbali na Trump, Vance na familia zao, pia rais anayeondoka na makamu wa rais watakuwepo. Hii inamaanisha tutamuona Rais Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris - pamoja na wenza wao Jill Biden na Doug Emhoff.
Marais wa zamani na wake wa rais pia mara nyingi huhudhuria katika hafla hiyo. Mwaka huu unatarajiwa kujumuisha George na Laura Bush na Barack Obama, ingawa Michelle Obama hatahudhuria.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












