Treni ya umeme Tanzania ni mwanzo mpya kwa Afrika Mashariki

Chanzo cha picha, Tanzania Railways Corporation
- Author, Basillioh Rukanga & Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Jengo lenye rangi kama madini adimu ya tanzanite, ni jengo la reli mpya jijini Dar es Salaam – ambayo ni ishara ya hamu ya mafanikio katika usafiri Tanzania.
Treni zinazotumia umeme nchini Tanzania, ambazo ni za kwanza katika eneo hili - hubeba abiria kutoka mji wa kibiashara Dar es Salaam hadi mji mkuu, Dodoma, kwa safari ya chini ya saa nne, nusu ya muda ukisafi kwa barabara.
Ni alama ya kuazishwa moja ya miradi ya kimkakati nchini - ujenzi wa Reli ya Standard Gauge (SGR) yenye urefu wa kilomita 2,560 (maili 1,590) inayotarajiwa kuunganisha miji muhimu na kuunganisha nchi jirani Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Safari za kilomita 460 (maili 285) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma zimefunguliwa tangu Agosti, na Rais Samia Suluhu alielezea reli hiyo kama "njia ya maisha yetu ya baadaye" ambayo "itaboresha nafasi yetu katika eneo hili.”
Huko Dodoma, kituo cha treni hiyo ni jengo jingine kubwa, linalofanana na vilima vyenye mawe katika jiji hilo - juhudi za kuchanganya urithi wa asili wa nchi na usasa.
Mji Mkuu ulio katikati ya nchi, uliteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa kitovu cha madaraka miaka 50 iliyopita, lakini ilimchukua Rais John Magufuli kuvilazimisha vyombo vya serikali kuhamia huko.
Wakati shughuli nyingi za kibiashara, na hata baadhi ya kazi za serikali, zikiendelea jijini Dar es Salaam, uhusiano wa haraka na bora wa usafiri kati ya miji hiyo umeonekana kuwa muhimu.

Chanzo cha picha, Basillioh Rukanga / BBC
Treni ya umeme pia zimeyafanya mambo kuwa mepesi na rahisi kwa Mtanzania wa kawaida. Ni mbadala wa safari za barabarani au treni ya zamani ya mwendo wa polepole.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ndani ya treni, mazingira ni safi na kuburudisha. Kuna meza ya kukunja katika kila kiti. Wafanyakazi wa treni wako tayari kuuza vinywaji vya moto na baridi pamoja na vitafunio.
"Tunashukuru, hatuchoki," Gloria Sebastian anayeishi Dar es Salaam, aliambia BBC wakati wa safari ya kutembelea familia yake Dodoma.
Na hayuko peke yake.
Mtu ambaye anasimamia ujenzi na uendeshaji wa huduma ya SGR anasema abiria 7,000 husafiri kwa safari nane za kila siku.
Machibya Masanja anaiambia BBC mahitaji yamekuwa makubwa kiasi kwamba "hatuwezi kukidhi mahitaji kwa safari hizo tunazofanya kwa siku. Tunatarajia idadi [ya abiria] itaongezeka mara mbili au tatu." Kuna mipango inaendelea ya kuongeza safari zaidi.
Hilo linamaanisha kupanga safari mapema ni muhimu. Malipo lazima yafanywe ndani ya saa moja ili kupata kiti. Bei ya chini (economy class) kwenda Dodoma inagharimu shilingi 40,000 za Kitanzania ($15; £11), bei ya juu (business class) ni shilingi 70,000 ($26).
Treni ya asubuhi inaondoka Dar es Salaam saa 12:00, lakini watu wanatakiwa kufika saa mbili mapema kwa ajili ya ukaguzi wa usalama.
Ndani ya jengo hilo lenye umbo la tanzanite - linafanana na eneo la uwanja wa ndege. Abiria hupanga foleni na kupitia ukaguzi kama tu kwenye uwanja wa ndege. Mizigo huskaniwa na wakati mwingine watu hukaguliwa kabla ya kuingia kwenye treni.
Mtu mmoja aliiambia BBC, anahisi ukaguzi huo mkali sio wa lazima, kwa vile hakuonekani kuwa kuna tishio lolote la moja kwa moja la usalama.
Hata hivyo, kuna wasiwasi kutoka kwa maafisa - uliothibitishwa na tukio la afisa wa polisi kuihoji timu ya BBC iliyokuwa ikipiga picha kwenye kituo hicho - lakini waliendelea na kazi baada ya ukaguzi fulani.

Chanzo cha picha, Basilioh Rukanga / BBC
Upandaji ulikuwa wa utulivu na wa utaratibu na treni iliondoka kwa wakati.
Kwa sasa treni zinatembea kwa kasi ya juu ya kilomita 120 kwa saa (75mph) lakini zinaweza kwenda kasi zaidi. Kisha treni ikaanza kutembea katika vitongoji vya Dar es Salaam wakati jua la asubuhi lilipoanza kuchomoza.
Ilipita katika nyasi zilizochanganyika na mandhari ya mashamba yenye miti mirefu - mto unaotiririka, vilima na tambarare. Na kulikuwa pia na mahandaki.
"Unashauriwa kutafuna kitu, kupiga miayo au kubaki mdomo wazi," mtangazaji alisema, na kuwafurahisha abiria.
Bernice Augustine alikuwa na bintiye kwa likizo ya wikendi mjini Dodoma.
"Inapendeza," anasema. "Huwezi kulinganisha na treni ya zamani: hii ni nzuri, ni safi, ni rahisi."
Hilaly Mussa Maginga ana kumbukumbu mbaya za safari za zamani. Baada ya safari ya Kigoma aliapa kutopanda treni tena kwani alichoka sana na sehemu ya chini ya mgongo wake ilikuwa na maumivu.
“Unapozoea kusafiri umbali mrefu unakaa mpaka unaumia, hivyo unapokuwa na chaguo hili la kusafiri kwa muda mfupi, kuna mengi ya kufurahia, tumetoka mbali namshukuru Mungu,” anasema.
Kwa Bw Maginga safari ya SGR ni safari shwari, isiyo na wasiwasi.
Haikuwa rahisi laikini

Chanzo cha picha, Basilioh Rukanga / BBC
Safari ya mradi huu kufikia hatua hii haijawa rahisi kabisa.
Kuanzia mwanzoni mwa 2017, sehemu ya kwanza ilikuwa imeratibiwa kukamilika mwaka 2019. Lakini ilikabiliwa na ucheleweshaji wa muda mrefu ambao kampuni ya ujenzi ilihusisha na Covid na gharama za ujenzi pamoja na maswala ya wafanyakazi.
Pia kumekuwa na maswali kuhusu gharama yake kubwa ya ujenzi, inayokadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 10 (£8bn) baada ya kukamilika.
Kampuni ya Uturuki ya Yapi Merkezi ndiyo mkandarasi mkuu wa sehemu nne za kwanza za njia hiyo, ikiwa ni pamoja na sehemu ya Dar es Salaam hadi Dodoma, huku kampuni za China zikijenga sehemu nyingine mbili.
Pesa za ujenzi zimetoka serikali ya Tanzania na wakopeshaji ikiwemo Denmark na Sweden, benki ya Exim ya China na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Lakini Masanja anasema ni mapema sana kuwa na wasiwasi kuhusu faida, akisema hilo litafahamika mara tu mtandao mzima utakapokamilika.
Anaongeza kuwa huduma hiyo inazalisha mapato ya kutosha ili kukabiliana na gharama za uendeshaji, na kuanzia Januari wanapanga kuanzisha treni za mizigo.
Kwa sasa, anasema, "mchango wake wa kijamii una faida zaidi."
Huduma hiyo mara kwa mara imetatizwa na hitilafu ya umeme lakini Masanja anasema wanajenga njia maalumu ya kusambaza umeme, kwa kutumia uwezo mkubwa wa wa nchi wa kuzalisha umeme ili kuondoa hatari ya kutokuwepo kwa umeme wa uhakika.
Kutumia umeme kumepunguza gharama kwa karibu theluthi moja ya kile ambacho kingegharimu katika kununua dizeli, ambayo nchi jirani ya Kenya inatumia kuwezesha treni yake ya SGR, anaiambia BBC.
"Sisi ndio wa bei nafuu zaidi katika kanda hii, na barani Afrika, kwa kutazama gharama," anasema.
Sio kila mtu ana furaha
Mwenyekiti wa Umoja wa Mawakala wa Vituo vya Mabasi Dodoma, Adam Ally Mwanshinga, anasema wanachama wake wamepoteza sehemu kubwa ya biashara kutokana na reli hiyo.
Kituo cha mabasi cha kisasa katika mji mkuu – kulikuwa na shughuli nyingi, anasema, na kuongeza kuwa sasa kuna abiria wachache kila siku.
Ingawa ni bei nafuu kusafiri kwa basi, urahisi wa treni umekuwa wa kuvutia zaidi kwa wengi.
"Biashara imedorora na maisha ni magumu," anasema Mwanshinga.
“Mabasi hayawezi kujaa na biashara nyingi za hapa zilizokuwa zikinufaika na watu wengi wanaokuja hapa zinateseka,” anasema.
Hata hivyo anaonekana kukubaliana na hali hiyo, akisema maendeleo ya SGR "yamefanya vyema kwa watu wengi."
"Ndio maisha yalivyo - kuna wale wanaofaidika na wale ambao watateseka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












