Mtandao wa mateso ya tumbili duniani wafichuliwa na BBC

Uchunguzi wa BBC uliyochukuwa mwaka mzima umefichua mtandao wa unyanyasaji wa kikatili dhidi ya tumbili duniani -kutoka Indonesia hadi Marekani.
BBC ilipata mamia ya wateja nchini Marekani, Uingereza na kwingineko wakiwalipa raia wa Indonesia kuwatesa na kuwaua watoto wa tumbili wenye mikia mirefu kwenye filamu.
Mtandao huo wa kikatili ulianza kwenye YouTube, kabla ya kuhamia kwenye makundi ya faragha kwenye Telegram- programu ya ujumbe iliyosimbwa kwa njia fiche ya .
Polisi sasa wanawasaka wanunuzi hao na watu kadhaa tayari wamekamatwa.
Onyo: Makala haya yana maudhui ambayo huenda yakawaathithiri baadhi ya wasomaji
Waandishi wa habari wa BBC walijiunga kisiri katika mojawapo ya makundi makuu ya mateso ya Telegram, ambapo mamia ya watu walijadiliana na kuja na mawazo ya mateso makali na kuwaagiza watu nchini Indonesia na nchi nyingine za Asia kuyatekeleza.
Lengo la watu hao lilikuwa kuunda filamu za kawaida ambapo tumbili wa macaque wenye mikia mirefu walinyanyaswa, kuteswa na wakati mwingine kuuawa kwenye filamu.
BBC ilifuatilia watesaji nchini Indonesia, wasambazaji na wanunuzi nchini Marekani, na kuwasilisha uovu huo kwa vyombo vya usalama ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Takriban watu 20 sasa wanachunguzwa kote duniani, wakiwemo wanawake watatu wanaoishi nchini Uingereza ambao walikamatwa na polisi mwaka jana na kuachiliwa chini ya uchunguzi, na mwanamume mmoja ambaye alifunguliwa mashtaka wiki iliyopita katika jimbo la Oregon nchini Marekani
Mike McCartney, msambazaji mkuu wa video nchini Marekani anayejulikana kwa jina lake la skrini, "The Torture King", alikubali kuzungumza na BBC - na kuelezea wakati alipojiunga na kundi lake la kwanza la Telegram la kutesa tumbili.
"Walikuwa wamejiandaa kwa zana zote," McCartney alisema. "Je unataka kutumia nyundo? Unataka kutumia koleo? Je! unataka screwdriver?" Video iliyofuata ilikuwa "jambo la kusikitisha sana ambalo nimewahi kuona," alisema.

Chanzo cha picha, JOEL GUNTEN/BBC
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
McCartney, mwanachama wa zamani wa genge la pikipiki ambaye alizuiliwa gerezani kabla ya kuingia na ulimwengu wa mateso ya tumbili, aliishia kuendesha vikundi kadhaa vya Telegraph ambapo washirika wake wapenda mateso makali walisambaza video.
"Haina tofauti na pesa za dawa," alisema. "Pesa ya madawa ya kulevya hutoka kwenye mikono michafu, pesa hizi zinatokana na mikono yenye damu."
BBC pia iliwatambua washukiwa wengine wawili wakuu ambao sasa wanachunguzwa na Idara ya Usalama wa Nchi ya Marekani (DHS) - Stacey Storey, mwanamke wa miaka 40 kutoka Alabama ambaye alijulikana katika jamii kama "Sadistic", na kiongozi anayejulikana kama. "Bw Ape" - ambaye jina lake halisi hatuwezi kufichua kwa sababu za kiusalama.
"Bw Ape" alikiri katika mahojiano na BBC kwamba alihusika na vifo vya tumbili wanne na kuwatesa wengine wengi. Alikuwa ameagiza video "za ukatili wa ajabu", alisema.
Simu ya Storey ilinaswa na maajenti wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao walipata karibu video 100 za mateso, pamoja na ushahidi kwamba alilipa kwa ajili ya kuunda baadhi ya video za kikatili zaidi zilizotolewa.
Kulingana na vyanzo vya polisi, Storey alikuwa akishiriki katika kundi la mateso mapema mwezi huu. BBC ilipowasiliana naye mjini Alabama mwezi Januari, Storey alidai kuwa alidukuliwa na kukataa kuzungumzia madai hayo kwa kina.

Chanzo cha picha, ED OU/BBC
"Bw Ape", Stacey Storey na Mike McCartney ni walengwa watatu kati ya watano muhimu katika uchunguzi unaoendelea wa Usalama wa Taifa. Bado hawajafunguliwa mashtaka, lakini wanaweza kufungwa jela hadi miaka saba iwapo watafunguliwa mashtaka kulingana na ushahidi uliokusanywa na DHS.
Ajenti Maalum Paul Wolpert, ambaye anaongoza uchunguzi wa DHS, alisema kila mtu aliyehusika kutoka kwa vyombo vya sheria ameshtushwa sana na asili ya uhalifu unaodaiwa.
"Sijui kama kuna mtu yeyote amewahi kufikiria uhalifu kama huu unafanyika," alisema.
Mtu yeyote anayehusika katika ununuzi au kusambaza video za mateso ya tumbili anapaswa "kutarajia kubishiwa mlangoni wakati fulani," Ajenti Wolpert alisema. "Hautaponea."
Polisi nchini Indonesia wamewakamata washukiwa wawili wa mateso. Asep Yadi Nurul Hikmah alishtakiwa kwa kutesa wanyama na kuuza spishi zinazolindwa, na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. M Ajis Rasjana alihukumiwa kifungo cha miezi minane - hukumu ya juu zaidi inayotolewa kwa kutesa mnyama.

Video za kuteswa kwa tumbili bado zinapatikana kwa urahisi kwenye Telegram na sasa Facebook, ambapo BBC hivi majuzi ilipata makumi ya vikundi vinavyoshiriki maudhui yaliyokithiri, baadhi yao yakiwa na zaidi ya wanachama 1,000.
"Tumeshuhudia kuongezeka kwa maudhui haya ya kusikitisha, ya picha, ambayo yalikuwa yamefichwa lakini sasa yanasambazwa waziwazi kwenye majukwaa kama Facebook," alisema Sarah Kite, mwanzilishi mwenza wa shirika la kutoa misaada kwa wanyama la Action for Primates.
Facebook iliambia BBC kuwa imeondoa makundi yaliyoangaziwa na kampuni hiyo. "Haturuhusu unyanyasaji wa wanyama kwenye majukwaa yetu na tunaondoa maudhui haya tunapofahamu, kama tulivyofanya katika kisa hiki," msemaji alisema.
Bi Kite pia alitaka sheria za Uingereza kuimarishwa ili kurahisisha kuwashtaki watu wanaolipia video za mateso. "Iwapo mtu anahusika kikamilifu katika kusababisha maumivu hayo kwa kulipia na kutoa orodha ya mambo anayotaka kufanyiwa mnyama, kuwe na sheria kali zaidi za kuwawajibisha," alisema.
YouTube iliiambia BBC katika taarifa kwamba unyanyasaji wa wanyama "hauna nafasi" kwenye jukwaa na kampuni hiyo "inajitahidi kuondoa haraka maudhui yanayokiuka kanuni".
"Mwaka huu pekee, tumeondoa maelfu ya video na kufungia maelfu ya chaneli kwa kukiuka sera zetu za vurugu na za kutisha," ilisema taarifa hiyo.
Telegram ilisema "imejitolea kulinda faragha ya watumiaji na haki za binadamu kama vile uhuru wa kujieleza", na kuongeza kuwa wasimamizi wake "hawawezi kufuatilia vikundi vya kibinafsi".












