'Shujaa wa vita' wa Urusi aliyetoroka: 'Nilijipiga risasi na watu wangu ili tuondoke Ukraine'

 Yevgeny Korobov
    • Author, Amalia Zatari
    • Nafasi, BBC Idhaa ya Kirusi
    • Akiripoti kutoka, Astana
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Yevgeny Korobov, afisa wa zamani wa jeshi la Urusi, amesimama katikati ya chumba akiwa amevaa shati jeusi na suruali nyepesi. Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akiishi Astana, mji mkuu wa Kazakhstan, kwa karibu miaka mitatu.

Anasema kwamba wakati huu wahamiaji wengine saba au wanane wamebaki katika nyumba yake.

"Ninajaribu kadiri niwezavyo kuwasaidia watu kama mimi. Huna haja ya kunilipa, ishi tu hapa, ndio hivyo tu," anasema. "Nani mwingine atawasaidia? Baada ya yote, kuna kitu kinachotufunga. Sote ni wahamiaji. Sote tulikimbia."

Miaka minne tu iliyopita, Korobov alikuwa akipigana nchini Ukraine kuanzia Februari hadi Mei 2022.

Korobov anasema alihitimu kutoka shule ya kijeshi akiwa "afisa kijana mwenye ari"

Chanzo cha picha, Evgeny Korobov's personal archive

Maelezo ya picha, Korobov anasema alihitimu kutoka shule ya kijeshi akiwa "afisa kijana mwenye ari"

'Vita vimeanza'

Korobov alikuwa akitamani kuwa jeshini kila mara, ingawa wazazi wake walikuwa wafanyakazi wa posta. Alisoma katika chuo cha kijeshi katika eneo lake la asili la Krasnoyarsk, kabla ya kujiunga na jeshi la Urusi kama "afisa kijana aliyejaa shauku ya kutumikia". Mkataba wake ulidumu hadi 2023.

Hata hivyo, shauku yake ilipungua haraka.

"Wakati wa utumishi jeshini unakutana na dhuluma na unaanza kukata tamaa kabisa na kila kitu, na jinsi mambo yalivyo nchini Urusi," anasema.

Mapema mwaka wa 2022, Korobov alitumwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika eneo la Kursk, karibu na mpaka wa Ukraine. "Sikuamini kungekuwa na vita, lakini tulienda huko tukiwa na wasiwasi," anakumbuka.

Anaelezea alichokiona baada ya kuvuka mpaka kuingia Ukraine: "Tuliendesha gari kupitia maeneo yenye watu wengi. Watu walikuwa wakiishi maisha yao, Mtu alikuwa akijaza mafuta kwenye gari, mtu alikuwa akinywa kahawa, mtu akivuta sigara. Nasi tunaendesha gari. Vita vimeanza."

Kikosi chake kilihamia kuelekea mji mkuu Kyiv, kikisimama katika wilaya ya Brovary mashariki mwa jiji.

Korobov alikuwa akipigana nchini Ukraine kuanzia Februari hadi Mei 2022

Chanzo cha picha, Evgeny Korobov's personal archive

Maelezo ya picha, Korobov alikuwa akipigana nchini Ukraine kuanzia Februari hadi Mei 2022
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hapa ndipo ofisi ya mwendesha mashtaka wa Ukraine inasema kwamba wanajeshi wa Urusi walikuwa wametekeleza uhalifu wa kivita. Matangazo ya redio yanadai kwamba wanajeshi wa Brigedi ya 15, ambapo Korobov alikuwa na makao yake, walikuwa wameanzisha chumba cha mateso katika ofisi ya posta katika eneo la Kyiv. Waandishi wa habari pia waliripoti kuhusu kuuawa kwa raia wasiopungua watano na kikosi hicho hicho.

Korobov anadai kwamba yeye binafsi hakushuhudia uhalifu wa kivita, lakini alisikia habari zake kutoka kwa wengine.

Anasema kwamba kazi yake ilikuwa kusindikiza safu za nyuma, urambazaji na upelelezi wa njia wakati wa vita, na kwamba kwa hivyo alikuwa akisafiri kila wakati.

Kikosi chake kilikuwa karibu na Kyiv hadi mwisho wa Machi, baada ya hapo aliondoka katika eneo hilo wakati vikosi vya Urusi viliporudi nyuma kufuatia jaribio lililoshindwa la kuzingira mji mkuu wa Ukraine.

Aliporudi nyuma, Korobov aliona miji ya Kiukreni ikiharibiwa. Anasema hii ilimsababishia "hofu na kukata tamaa".

Korobov anasema kwamba safu hizo zilikabiliwa na mashambulizi ya vikosi kadhaa vya Kiukreni.

"Tulilazimika kujibu kwa risasi," anakumbuka. "Tungefanya nini kingine? Kufa? Je, mimi ni mtu mzuri kama ningekufa? Pia nilitaka kuishi na nilitaka wanajeshi wangu wote warudi. Tulikuwa tunapigania nini? Kwa ajili ya maisha yetu. Waukraine walikuwa na adui, sisi. Tulikuwa na maadui wawili, Waukraine na makamanda wetu wenyewe."

'Shujaa wa vita'

Mwishoni mwa mwaka wa 2022, muda mfupi kabla hajaondoka Urusi na kuelekea Kazakhstan, Korobov aliamriwa na kamanda wake huko Moscow kuonekana kwenye televisheni ya Urusi."

Kabla tu ya kuondoka Urusi, Korobov aliamriwa na kamanda wake huko Moscow. Kipindi hicho kilimuonesha kama shujaa wa vita ambaye alikuwa amejeruhiwa vitani.

"Luteni Mwandamizi Yevgeny Korobov, pamoja na kundi lake, walikuwa wakisindikiza safu ya nyuma," alisema mwenyeji wa kipindi maarufu cha mazungumzo ya jioni kwenye Channel One. "Walikumbana na shambulio la kuvizia. Walipigana na vikosi vya adui. Waliwashambulia takribani wanamgambo 15 na vifaa vya adui. Wao wenyewe hawakupoteza."

Korobov anaita hadithi hiyo, iliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na wizara ya ulinzi ya Urusi, kuwa ya uwongo. Anasema kikosi chake kilikutana na shambulio la kuvizia mwanzoni mwa Machi 2022 katika eneo la Chernihiv, lakini tukio hilo lilitiwa chumvi sana.

Korobov alionekana kwenye televisheni ya Urusi kwa amri ya kamanda wake huko Moscow.

Chanzo cha picha, smotrim.ru

Maelezo ya picha, Korobov alionekana kwenye televisheni ya Urusi kwa amri ya kamanda wake huko Moscow.

"Kuangukia kwenye mtego, ndiyo. 'Uliopangwa kwa umakini', hapana kabisa. Kama maadui walikuwa wengi kuliko sisi, sijui watu wangapi walikuwa pale au ni nani aliyekuwa akifyatua risasi," Korobov anajibu.

Baada ya kuonekana kwenye vyombo vya habari, alipokea medali ya ujasiri, ambayo Korobov anasema "hakujali kabisa." "Kwa tukio lililobuniwa? Kwa vita ambavyo sikutaka kushiriki? Tayari sikuwa nataka kuhudumu jeshini, nilikuwa navumilia tu hadi mkataba wangu uishe."

Kile Korobov hakikanushi ni kwamba alijeruhiwa nchini Ukraine. Wakati wa mahojiano ya televisheni, anaonekana wazi kulemaa anapotembea.

'Hakuna namna ya kurudi'

Korobov alijeruhiwa mguuni huko Donetsk mwezi Mei 2022, kisha akaondolewa na kurejeshwa Urusi.

Wakati huo, amri ilitolewa kushambulia kijiji cha Ozerne karibu na Lyman. "Ni mara moja tu tuliweza kukikaribia; tulishambuliwa kwa kila aina ya silaha, na katika mashambulizi yaliyofuata hatukuweza hata kukaribia," anasema Korobov.

"Wakati huo nilielewa tayari kwamba hakuna uwezekano tungeachiliwa kurudi nyumbani. Na njia pekee ya kuondoka pale ilikuwa ama ukiwa umeuawa au umejeruhiwa."

Siku moja, kikosi chao kwa bahati mbaya kiliangusha droni katika maeneo yanayodhibitiwa na Ukraine. Korobov anasema kikosi chake cha watu wanne kilitumwa kuirejesha na kuambiwa na kamanda wao wasirudi bila droni hiyo, jukumu analolielezea kuwa haliwezekani.

Korobov alikimbilia Kazakhstan kwa msaada wa mradi wa Go by the Forest, ambao huwasaidia wanajeshi wa zamani wa Urusi kama yeye.
Maelezo ya picha, Korobov alikimbilia Kazakhstan kwa msaada wa mradi wa Go by the Forest, ambao huwasaidia wanajeshi wa zamani wa Urusi kama yeye.

"Nilijua kuwa hapo ndipo mwisho, hakukuwa na njia ya kurudi," anasema. "Na nikafyatua risasi kwa wanajeshi wenzangu. Nilifyatua risasi ardhini kwa mkupuo. Niliwajeruhi wenzangu. Kisha nikajijeruhi mwenyewe, nilijipiga risasi. Nilitoa huduma ya kwanza, kisha tukatambaa kuelekea mahali pa kuhamishwa."

Hii inaashiria kuwa jeraha lililoripotiwa na kusherehekewa kwenye kipindi cha televisheni Let Them Talk lilikuwa jeraha ambalo Korobov alijisababishia mwenyewe.

BBC haiwezi kuthibitisha kwa uhuru simulizi ya Korobov, ingawa alitoa picha za mguu wake ulioumia.

Korobov na wana kikosi chake kisha walihamishwa kutoka mstari wa mbele. Alikaa hospitalini kwa mwezi mmoja na nusu, kisha akapitia hatua za urekebishaji.

Korobov alitaka kumaliza mkataba wake akiwa Urusi hadi mwaka 2023 bila kurejea Ukraine. Hata hivyo, baada ya kutangazwa kwa uhamasishaji zaidi Septemba 2022, mikataba yote ikawa ya muda usiojulikana. Mwishoni mwa mwaka huo, aliarifiwa kwamba atarudishwa Ukraine.

Kutafuta hifadhi

Korobov anasema kwamba kabla ya kuondoka Urusi, aliwasiliana na mradi wa Go By The Forest, ambao husaidia wanajeshi wa zamani wa Urusi kama yeye ambao wanaogopa kurudi kwenye vita vya Ukraine. Wanaharakati wa mradi huo kisha walimuwekea njia ya kukimbia kwenda Kazakhstan.

Hivi karibuni, alipakia begi na kuondoka Urusi.

Kesi ya jinai ya kukimbia jeshi imeanzishwa dhidi ya Korobov, na anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 gerezani. Kwa sababu hiyo, katika miezi ya mwanzo ya maisha Astana, hakutoka sana nje ya nyumba.

Baadaye, alipata kazi kwenye baa, kinyemela, kwa sababu, kama mtafutaji hifadhi, hakuruhusiwa kufanya kazi huko.

"Kazakhstan bado haijatoa hifadhi kwa raia wa Urusi, na nadhani haitatoa," anasema Korobov.

"Tunasubiri uamuzi kutoka nchi za Ulaya, hasa Ufaransa, kwa sababu kwa sasa ndiyo nchi pekee iliyokubali wanajeshi wa Urusi wanaokimbia," anasema.

Korobov anaelewa kusita kwa nchi za Magharibi kukubali wanajeshi wa Urusi wanaokimbia, lakini anaamini hii ni mojawapo ya "njia za ufanisi za kutatua mgogoro: siyo tu kusambaza silaha na kuweka vikwazo, bali pia kuwapa Warusi fursa ya kukataa kubeba silaha, kukataa kupigana."

Mwanaharakati wa haki za binadamu Artur Alkhastov amekuwa akiwasaidia wahamiaji wa Urusi huko Kazakhstan
Maelezo ya picha, Mwanaharakati wa haki za binadamu Artur Alkhastov amekuwa akiwasaidia wahamiaji wa Urusi huko Kazakhstan

BBC ilimhoji Artur Alkhastov, wakili kutoka Ofisi ya Haki za Binadamu ya Kazakhstan, ambaye amekuwa akisaidia wanajeshi wa Urusi wanaokimbia ambao walifika nchini humo katika miaka mitatu iliyopita. Sehemu ya mchakato ni kuthibitisha wanajeshi hao wa zamani, ili kuzuia mawakala wa huduma za usalama za Urusi kuingilia kikundi hicho.

Anasema kuthibitisha simulizi ya Korobov ilikuwa ngumu na ilichukua muda.

Kwa mtazamo wake, mwanajeshi wa Urusi anayekimbia vita leo yuko katika hatari kubwa zaidi kuliko wapinzani wengi wa vita au wapinzani wa kisiasa, kwa sababu mamlaka ya Urusi wanaona wanajeshi hao wa zamani kama wasaliti.

Hii inaweka wanajeshi wa Urusi wanaokimbia Kazakhstan na Armenia katika hatari, kwa sababu nchi zote mbili zina vituo vya kijeshi vya Urusi.

Korobov na wanajeshi wengine wanaokimbia wanaweza kulindwa dhidi ya kurejeshwa Urusi kwa sababu ni watafuta hifadhi, lakini hawawezi kulindwa kutokana na tishio la kubakwa, anaeleza Alkhastov.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa ana Ambia Hirsi