Vijue vizuizi vingine saba vya majini vilivyowahi kutokea duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, BBC News Persian
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Shirika la habari la Iran Tasnim limeripoti kwamba Iran imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye meli za kijeshi za Marekani katika Ghuba ya Oman, baada ya Jeshi la Wanamaji la Marekani kukamata meli ya makontena yenye bendera ya Iran, Touska.
Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) imesema manowari ya USS Spruance "iliizuia Touska" baada ya "kushindwa kutii maonyo kutoka kwa vikosi vya Marekani kwa kipindi cha saa sita. Kisha wanajeshi wa Marekani waliishambulia meli hiyo kwa helikopta na kushuka kwa kamba na kuingia Touska.
Touska ilikuwa umbali wa takriban maili 40 baharini kutoka bandari ya Chabahar, kusini-mashariki mwa Iran, baada ya kuondoka Port Klang, nchini Malaysia, tarehe 12 Aprili.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema imepewa "onyo la kusimama" baada ya kujaribu kuvuka kizuizi cha majini cha Marekani. Wafanyakazi wa Iran walikataa kutii, kwa hivyo meli yetu ya majini iliwazuia kwa kulipua chumba cha injini."
Uamuzi wa Marekani unafanana na mbinu za zamani wakati wa vita kuzuia njia za baharini ili kudhoofisha uchumi, kuvuruga biashara na kumlazimisha adui kubadilisha mwelekeo au kusalimu amri.
Historia inaonyesha ingawa hatua kama hizo zinaweza kuwa na ufanisi katika kuleta shinikizo. Kwa mfano wakati wa vita viwili vya dunia - vizuizi vya majini vilisaidia katika kudhoofisha uwezo wa nchi kuendeleza vita.
Lakini katika maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na vizuizi vya Gaza na Yemen, mbinu hiyo ilizidisha migogoro ya kibinadamu bila kutoa matokeo ya kudumu ya kisiasa.
Kizuizi cha Uingereza kwa Ujerumani

Chanzo cha picha, Historica Graphica Collection / Heritage Images / Getty Images
Kizuizi cha majini dhidi ya Ujerumani katika Vita vya Kwanza vya Dunia (1914–1919), kilianzishwa na Uingereza kwa nchi hiyo kutawala Bahari ya Kaskazini ili kudhibiti shughuli za bahari hiyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jeshi la Wanamaji la Ufalme wa Uingereza lilikagua meli na kuweka shinikizo kwa nchi zisizoegemea upande wowote, na hivyo kuizuia Ujerumani isifanye biashara ya kimataifa. Baada ya muda, orodha ya bidhaa zilizopigwa marufuku iliongezeka zaidi ya vifaa vya kijeshi hadi kujumuisha chakula na mbolea.
Mwanzoni Ujerumani ilifanikiwa kupunguza athari hizo kupitia biashara katika mataifa yasiyoegemea upande wowote na biashara ya ndani. Lakini kadri vita vilivyoendelea, uagizaji ulipungua sana, na uhaba wa pembejeo ulipunguza uzalishaji wa kilimo na viwanda.
Athari za kijamii zilikuwa kubwa. Kufikia mwaka 1916, uhaba wa chakula uligeuka kuwa mgogoro. Kile kinachoitwa "Baridi ya Turnip" ikawa ishara ya ugumu wa maisha, na wanahistoria wanakadiria maelfu ya raia walikufa kutokana na utapiamlo na magonjwa yanayohusiana nayo.
Ingawa kizuizi hicho hakikuwa sababu pekee ya kushindwa kwa Ujerumani, wanahistoria wanakiona kama sababu kubwa katika kudhoofisha uwezo wa nchi hiyo wa kuendelea na vita.
Vizuizi dhidi ya Japani

Chanzo cha picha, Galerie Bilderwelt / Getty Images
Kama taifa la kisiwa, Japan ina utegemezi mkubwa wa njia za majini. Hutegemea meli kuagiza mafuta, malighafi na chakula, na kusambaza vikosi vyake kote Pasifiki.
Kuanzia mwaka 1943, manowari za Marekani zilizidi kushambulia meli za wafanyabiashara wa Japan, huku shughuli za uwekaji wa mabomu kwenye maji zikazidi kuvuruga njia kuu za baharini.
Kufikia miaka ya mwisho ya vita, meli za wafanyabiashara za Japani zilikuwa zimeharibiwa kwa kiasi kikubwa. Tathmini zinaonyesha kuharibiwa huku kulikuwa sababu kubwa katika kuporomoka kwa uchumi wake wa wakati wa vita.
Tofauti na Ujerumani, Japani haikuwa na njia za ardhi za kukabiliana na shinikizo hilo.
Ingawa kujisalimisha kwake kulitokana na mambo mengi - ikiwa ni pamoja na mabomu ya atomiki na kuingia kwa Umoja wa Kisovieti katika vita - kukatwa kwa njia za usambazaji ya majini kulichangia pia.
Karantini ya Marekani kwa Cuba

Chanzo cha picha, Getty Images
1962 wakati wa mgogoro wa Makombora wa Cuba Marekani iliepuka kuita hatua yake dhidi ya Cuba kuwa ni kizuizi cha majini, badala yake ilitumia neno "karantini" ili kuepuka athari za kisheria.
Chini ya Rais John F Kennedy, vikosi vya majini vya Marekani vilitumwa ili kuzuia vifaa vya kijeshi vya Usovieti kufika Cuba. Lengo lilikuwa ni kuzuia utumwaji zaidi wa makombora na kuishinikiza Moscow kuingia katika mazungumzo.
Operesheni hiyo ilidumu chini ya mwezi mmoja na ilifanya kazi kama kizuizi. Zikiwa zinakabiliwa na hatari ya makabiliano, baadhi ya meli za Kisovieti zilirudi nyuma.
Pamoja na diplomasia kali, mzozo huo uliisha kwa kuondolewa makombora ya Usovieti kutoka Cuba na, kwa siri, makombora ya Marekani kutoka Uturuki.
Ukipima lengo lililotajwa la karantini hiyo, inaonekana ilifanikiwa.
Umoja wa Mataifa dhidi ya Iraq

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kufuatia uvamizi wa Iraq nchini Kuwait mwaka 1990, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliweka vikwazo vikali, ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kuzuia usafiri wa baharini.
Udhibiti huo kutoka miaka ya 1990 na hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, ukawa sehemu muhimu ya juhudi za kuitenga Iraq kiuchumi na kuilazimisha kufuata matakwa ya kimataifa.
Ingawa Iraq haikuwa na matumizi makubwa ya baharini, lakini utekelezwaji wa sheria hii ulichangia katika kupunguza usafirishaji wa mafuta nje ya nchi. Hata hivyo, njia za ardhini ziliifanya Iraq kuepuka baadhi ya vikwazo.
Hatua hizi zilikuwa na ufanisi zikijumuishwa na vikwazo vingine na shinikizo la kijeshi.
Vikwazo vya baharini dhidi ya Yugoslavia

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati wa vita vya Balkan, vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Shirikisho ya Yugoslavia vilitekelezwa baharini kupitia operesheni za pamoja za NATO na Umoja wa Ulaya.
Katika Bahari ya Adriatic kati ya 1992 na 1996, maelfu ya meli zilikaguliwa, na mamia zilielekezwa kwingine au kusimamishwa. Jiografia na mipaka ya nchi hiyo ilifanya utekelezaji uwe rahisi.
Operesheni hizi zilipata ufanisi zaidi kwa kuongeza gharama kwa meli zinazokiuka vikwazo. Hata hiyvo hazikumaliza mgogoro wenyewe. Mchanganyiko wa shinikizo la kijeshi na kidiplomasia ulihitajika ili kufikia suluhu.
Israel dhidi ya Gaza

Chanzo cha picha, Majdi Fathi / NurPhoto via Getty Images
Kizuizi dhidi ya Gaza, kimekuwepo tangu 2007, ni sehemu ya mfumo mpana wa vikwazo vya usafiri, biashara na upatikanaji wa rasilimali dhidi ya watu wa Gaza.
Israel inasema hatua hizo ni muhimu ili kuzuia ulanguzi wa silaha. Mashirika ya kibinadamu yanasema kizuizi hicho kimeharibu vibaya uchumi na hali ya maisha ya Gaza.
Uhalali wa kizuizi hicho bado unapingwa. Katika maoni ya mwaka 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilielezea wasiwasi wake kuhusu hali katika maeneo ya Palestina.
Licha ya miaka mingi ya vikwazo, vizuizi hivyo havijazuia vurugu za mara kwa mara katika eneo hilo. Ingawa vimeleta shinikizo, havijatoa usalama wa kudumu au maafikiano ya kisiasa.
Saudi Arabia kuizingira Yemen

Chanzo cha picha, Getty Images
Tangu mwaka 2015, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia umeweka vikwazo kwenye bandari na anga za Yemen, ukilenga kupunguza mtiririko wa silaha kwa vikosi vya Houthi.
Yemen inategemea sana bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, kwa hivyo hatua hizi zimekuwa na athari ya moja kwa moja kwa raia. Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara kuhusu hatari za njaa, uhaba wa mafuta na matatizo kwenye mifumo ya afya.
Kizuizi hicho kimeongeza shinikizo kwa Wahouthi, lakini hakijaleta suluhu ya kisiasa. Badala yake, kimechangia mgogoro wa muda mrefu wa kibinadamu na kusababisha ukosoaji wa kimataifa.















