Sababu 4 kwa nini mazungumzo ya Iran na Marekani yako shakani

s

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Hatma ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani imeingia katika hali ya sintofahamu kubwa huku muda wa kusitisha mapigano ukikaribia kuisha. Kinachoonekana sasa si tu mkwamo wa kidiplomasia, bali pia ongezeko la kauli kali, vitisho na taarifa zinazokinzana kutoka pande zote mbili.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, bado hakuna uhakika iwapo Iran itashiriki mazungumzo yajayo yanayopangwa kufanyika kupitia upatanishi wa Pakistan. Wakati baadhi ya vyanzo vikionyesha kuwa Tehran inafikiria kushiriki, vingine vinasema huenda ikajiondoa kabisa kutokana na hali ya sasa ya mvutano.

Wakati huo huo, hali imezidi kuchanganyika baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa Makamu wa Rais wa Marekani ambaye anaongoza ujumbe wa mazungumzo hayo, JD Vance bado hajaanza safari kwenda Pakistan, kutokana na sintofahamu juu ya ushiriki wa Iran.

Katika mazingira haya, mazungumzo yanaonekana kuyumba kati ya matumaini ya kidiplomasia na hatari ya kurejea kwa mgogoro mpana zaidi. Zipo sababu nne zinazofanya mazungumzo haya kufika katika hali ya sntofahamu

Kauli za ubabe na vitisho

Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Truth Social kwamba Marekani "inaongoza vita dhidi ya Iran kwa tofauti kubwa" na kuongeza kuwa "mambo yanaenda vizuri sana" huku akisema jeshi la Marekani limefanya kazi "kwa kiwango cha kushangaza."

Kauli hizi zimeonekana na wachambuzi kama kuongeza presha ya kisiasa badala ya kutengeneza mazingira ya mazungumzo. Badala ya lugha ya upatanishi, matumizi ya neno "vita" yamezidisha wasiwasi kuhusu mwelekeo wa mgogoro huo.

Kwa upande mwingine, Iran imejibu kwa msimamo mkali zaidi, ikionyesha kuwa haitakubali mazungumzo chini ya vitisho, hali inayoongeza pengo kati ya pande hizo mbili.

Tukio la kukamatwa kwa meli ya Iran

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Mvutano uliongezeka zaidi baada ya jeshi la Marekani kukamata meli ya mizigo ya Iran iliyokuwa ikielekea bandari ya Bandar Abbas. Tukio hili lilitokea baada ya meli hiyo kudaiwa kujaribu kuvunja zuio lililowekwa na Marekani.

U.S. Central Command ilitoa picha na video zikionyesha wanajeshi wakiteka meli hiyo, hatua iliyochukuliwa kama ishara ya kuendelea kwa hatua za kijeshi hata wakati wa kusitisha mapigano.

Iran ilijibu kwa hasira, ikiitaja hatua hiyo kama "uharamia wa kijeshi" na kuonya kuwa iko tayari kujibu kwa nguvu. Ikajibu kwa kushambulia meli za kijeshi za Marekani.

Iran inaona kama kuna mzaha, 'huku mazungumzo huku unakamata meli zetu'. Tukio hili limeongeza mvutano na kupunguza uwezekano wa kuaminiana kati ya pande hizo mbili.

Iran yagawanyika kuhusu kushiriki mazungumzo

Taarifa kutoka ndani ya Iran zinaonyesha picha mchanganyiko kuhusu ushiriki wake katika mazungumzo yajayo. Baadhi ya vyanzo vya kidiplomasia vinaeleza kuwa Tehran inaendelea "kupitia kwa kina" uwezekano wa kushiriki, huku ikitathmini masharti yaliyopo.

Hata hivyo, kauli za viongozi waandamizi zimekuwa kali zaidi. Spika wa bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf alisema Iran "haitakubali mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho," akiongeza kuwa taifa hilo limekuwa likijiandaa kuonyesha "karata mpya kwenye uwanja wa vita" katika wiki mbili zilizopita.

Lakini baadaye Pakistan ikasema inazungumza na uongozi wa juu wa Iran. unaonesha dalili za kushiriki mazungumzo hayo, yaliyopangwa sasa kufanyika leo.

Mchanganyiko huu wa kauli za kisiasa unaonyesha wazi kuwa ndani ya Iran bado hakuna msimamo mmoja kuhusu kama mazungumzo yanafaa kuendelea au la. Na hicho ni kikwazo kingine.

Masuala ya zamani bado hayajapatiwa suluhisho

Licha ya matukio mapya, kiini cha mgogoro hakijabadilika. Suala la mpango wa nyuklia wa Iran na pia mlango bahari wa hormuz bado ni mzizi wa mvutano, huku kila upande ukiwa na msimamo mgumu.

Marekani inaona mpango huo kama tishio la usalama wa kimataifa, wakati Iran inauona kama haki yake ya maendeleo ya teknolojia ya kiraia. Tofauti hii imekuwepo kwa miaka mingi na bado haijapatiwa suluhisho la kudumu.

Hii ina maana kuwa hata bila mvutano mpya, mazungumzo yangekuwa magumu. Kuongezeka kwa changamoto mpya kunafanya hali kuwa ngumu zaidi mara mbili.