Usitishaji wa muda mapigano Iran ni mtego?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki mbili za kusitisha mapigano kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran zimekamilika, huku kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz ukiwa suala ambalo limejadiliwa sana na kuzua hisia tofauti.
Ijumaa iliyopita Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, alichapisha kwenye mtandao wa X kuwa wamefungua mlango bahari wa Hormuz, na kuleta mvutano ndani ya serikali ya Iran na baadaye mlango huo wa bahari ulifungwa tena siku moja baadaye.

Chanzo cha picha, HAMSHAHRI
Kipindi cha ukimya
Wanasiasa nchini Iran wana mitazamo tofauti ya kisiasa ikija katika usitishwaji wa mapigano, na viongozi wengi hawapendi kutumia jina hilo.
Maafisa wa Iran wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa wanataka "dhamana ya kudumu" katika mazungumzo ya kupata amani, wakitaka kuhakikishiwa kuwa hawatashambuliwa tena.
Kulingana na viongozi wa serikali ya Iran, hakuna usitishwaji mapigano, kwa sababu kulingana na kauli ya kiongozi wa awali wa kidini Ali Khamenei, "tofauti kati ya Marekani na Jamhuri ya Kiislamu si suala la kimkakati bali ni tofauti ya kimsingi."
Mwezi Novemba mwaka uliopita, Ali Khamenei alisema kuwa Iran na Marekani zina "mgongano wa maslahi," akisisitiza kwamba "asili ya kiburi ya Marekani haikubali chochote isipokuwa kujisalimisha, hili ndilo marais wote wa Marekani walitaka lakini hawakulitamka wazi, ila rais wa sasa amelisema wazi"
Baada ya vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel, Ali Khamenei hakutaja neno "usitishaji mapigano" na, inaonekana ilikuwa makusudi, alizungumzia mara kadhaa hali ya "hakuna vita, hakuna amani."
Tarehe 10 mwezi Aprili, siku ya kwanza ya usitishaji mapigano ya sasa, katika ujumbe wa kuadhimisha siku 40 tangu kifo cha baba yake, badala ya kutumia neno "usitishaji mapigano," Mojtaba Khamenei alitumia kauli "kipindi cha ukimya kwenye uwanja wa vita."
Tafsiri hii pia imejirudia katika maandishi na misimamo ya baadhi ya makamanda wa kijeshi pamoja na wafuasi wa serikali ya Iran.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii inaleta utofauti gani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ahmad Masjedjamei, aliyekuwa Waziri wa Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu, aliungana na waandamanaji tarehe 10 mwezi Aprili na kutoa hisia zake kuhusu usitishaji mapigano.
Ingawa siku 20 zilikuwa zimepita tangu kumalizika kwa Nowruz na Eid al-Fitr, Ahmad Masjedjamei aliandika,"Nilimpa mkusanyaji taka kifurushi cha pipi. Aliniuliza kwa mshangao, 'Leo ni Eid?' Nikasema hapana, nikamwambia amani imepatikana. Alijibu, 'Kuna tofauti gani kati ya vita na amani kwa watu kama sisi?' Hakujua, na wala mimi pia sijui."
Mbali na maoni ya wananchi kuhusu vita na usitishaji mapigano,jambo moja linaloweza kukubaliwa ni kwamba usitishaji mapigano wa sasa una tofauti za msingi na muhimu ukilinganishwa na kipindi baada ya Vita vya Siku 12 na pia vita vya miaka minane vya Iran na Iraq.
Leo, usitishaji mapigano unatekelezwa licha ya kifo cha Ali Khamenei, ambaye alikuwa mkuu wa nchi na kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Idadi ya makamanda wakuu wa kisiasa, kijeshi na kiusalama pamoja na maafisa wengine wameuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel, na Iran imepata hasara kubwa za kiuchumi.
Hata hivyo, licha ya gharama kubwa za vita hivi, maafisa wa ngazi ya juu kutoka Iran na Marekani wamefanya mazungumzo ya moja kwa moja katika hatua isiyo ya kawaida, na juhudi kubwa zinaendelea ili kuongeza muda wa usitishaji mapigano na kufikia makubaliano kati ya nchi hizo mbili.
Tangu tarehe 10 Aprili, wakati usitishaji mapigano katika vita kati ya Marekani, Israel na Iran ulipotangazwa, picha zilizosambaa zilionyesha baadhi ya wafuasi wa serikali wakipinga hatua hiyo mbele ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran. Walipaza sauti kupinga usitishaji mapigano na kudai vita viendelee
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian alisema,"Iran haitafuti vita wala machafuko, na daima inasisitiza mazungumzo na ushirikiano na nchi mbalimbali. Hata hivyo, jaribio lolote la kutulazimishia matakwa au kutushinikiza tujisalimishe litashindwa."
Aliongeza kuwa,"Katika mfumo huu, vikosi vya ulinzi viko tayari kukabiliana na vitisho, mikono iko kwenye vitufe vya mashambulizi, na mazungumzo ndiyo njia pekee ya kutatua mzozo kati ya Iran na Marekani."
Shirika la habari la Fars News Agency, chombo cha habari kinachohusishwa na Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, kiliandika Ijumaa, tarehe 18 katika makala yenye kichwa "Mtego uko wazi! kilichobaki ni mchezo", "Kukubali masharti yetu ndiyo ilikuwa njia pekee kwa Marekani kusitisha vita ili ijiandae kwa shambulio kubwa. Sisi pia tulikuwa tukijipanga, kujaza vifaa, na kujiandaa kwa vita wakati wa usitishaji mapigano, lakini katika kipindi hiki hatuwezi kushambulia moja kwa moja. Hivyo, tujiandae kwa shambulio la adui,na tuko tayari."
Usitishaji mapigano ni "mtego"
Miongoni mwa mitazamo mbalimbali kuhusu usitishaji mapigano, wapo wanaoiona kama fursa ya kufanya marekebisho ya ndani. Baadhi ya wanasiasa kama aliyekuwa rais wa Iran Hassan Rouhani, alisema kuwa"baada ya vita," sauti za wananchi lazima zisikilizwe, maandamano yashughulikiwe, na mageuzi ya kisiasa na kiuchumi yafanywe. Rouhani anaona usitishaji mapigano kama fursa adimu ya kujenga upya imani ya umma kwa serikali.
Usitishaji mapigano kati ya Iran na Iraq
Ingawa hali ya sasa nchini Iran haiwezi kulinganishwa moja kwa moja na mazingira ya vita vya miaka minane ya vita vya Iran na Iraq, bado kuna uwiano fulani wa kisiasa, kijamii na kiitikadi katika namna taifa linavyokabiliana na matokeo ya vita na usitishaji mapigano, na mustakabali wa taifa.
Tarehe 19 mwezi Julai mwaka wa 1988, ujumbe wa Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulichapishwa, na kuitwa "Kikombe cha sumu." Kwa msingi wake, Iran ilikubali Azimio la Umoja wa Mataifa, na Iran pamoja na Iraq zikakubaliana kusitisha mapigano baada ya vita vya miaka minane.
Siku hiyo hiyo, wabunge na baadhi ya maafisa wa serikali walizungumzia umuhimu wa kukubali usitishaji mapigano. Gazeti la Kayhan, kupitia makala ya Mehdi Nasiri iliyochapishwa katika matoleo mawili, lilitoa wito wa "kuuelewa hali ya sasa" ya nchi.
Katika ripoti kuhusu siku ya kwanza ya usitishaji mapigano kati ya Iran na Iraq, gazeti la Kayhan lilimnukuu Hossein Abdi Abyaneh, mkurugenzi mkuu wa sheria katika Wizara ya Mambo ya kigeni ya Iran, akisema kwamba "udhibiti na ukaguzi wa meli katika Mlango wa Hormuz na eneo la Ghuba ya Uajemi, ni haki ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na haki hii itaendelea kuwepo kwa Iran hadi amani ya kudumu itakapopatikana."

Chanzo cha picha, KEYHAN
Mgawanyiko katika jamii na katika mfumo wa utawala
Kinachojitokeza kwa sasa ni ukosefu wa uelewa kuhusu "usitishaji mapigano" katika nyanja ya kisiasa na kijamii ya Iran.
Migawanyiko imeripotiwa katika ngazi mbalimbali za utawala, kisiasa na jamii nchini Iran.
Kwa upande mmoja, usitishaji mapigano huonekana kama chombo cha kimkakati cha usimamizi wa migogoro na kuendeleza njia ya diplomasia, na kwa upande mwingine huonekana kama mtego au fursa ya adui kujipanga upya.
Usitishaji mapigano hauchukuliwi kama mwisho wa mchakato wa kupatikana kwa amani, bali kama kipindi cha mpito, kipindi ambacho mustakabali wake unategemea mazungumzo na diplomasia.















