Je, Chelsea ina shida gani?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ahmed Bahajj
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Chelsea FC, klabu bingwa duniani,wametumia zaidi ya pauni bilioni moja kuboresha timu yao, lakini bado wanahangaika kwenye matokeo, kwa nini?

Wamepoteza mechi tano mfufulizo za Ligi Kuu ya England. Walichabangwa na Newcastle, Everton, Manchester City, Manchester United na hivi punde, kichapo cha kikatili cha mabao matatu kwa nunge kutoka kwa Brighton.

Chelsea sasa wako nafasi ya 7 katika jedwali la EPL ,baada ya mechi 34 ,msimu huu pekee wamepoteza mechi 12 na kupata 9, wameshinda mechi 13 pekee na wana alama 48 ,ukumbuke kinara wa Ligi Arsenal ana alama 70..

Chanzo cha masaibu yao ni nini?

Chelsea wameshinda mechi moja tu kati ya tisa zilizopita za Ligi ya Premia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chelsea wameshinda mechi moja tu kati ya tisa zilizopita za Ligi ya Premia

Kwanza, mkakati wa umiliki na uongozi. Tangu Roman Abramovich kuondoka mwezi Machi, mwaka 2022, Todd Boehly alipochukuwa hatamu alibadilisha kabisa mfumo, akasajili vijana wengi kwa mikataba mirefu, akilenga mafanikio ya baadae, badala ya mafanikio ya haraka.

Hata hivyo, timu hii ya chipukizi imekosa uwiano na umoja kabisa.

Kuna vipaji kama Enzo Fernández na Mykhailo Mudryk, João Pedro, Cole Palmer lakini hakuna viongozi wa kutosha, hakuna mchanganyiko sahihi wa uzoefu na ubunifu.

Mfano ni juzi tu Enzo amezungumza na vyombo vya habari akisema ndoto yake ni kujiunga na Real Madrid inaonyesha roho yake haipo Chelsea.

Isitoshe kila wiki orodha ya wachezaji inabadilika na hilo linafanya kuwa vigumu kujenga mshikamano wa timu hivyo na bila mfumo uliozoeleka,, wachezaji wanaonekana kupotea.

Jambo lingine ni mabadiliko ya mara kwa mara ya makocha. Kila mara makocha wanaandikiwa na kufutwa kazi kiholela, kutoka Thomas Tuchel hadi Mauricio Pochettino—Frank Lampard Enzo Maresca,na sasa Liam Rosenior.

Hakuna mfumo unaojengwa kwa muda mrefu, inakuwa vigumu kujenga timu imara chini ya makocha tofauti wasiodumu.

Enzo Fernandez

Chanzo cha picha, Getty Images

Yote tisa mechi hushindwa uwanjani sio nje ya uwanja.

Uwanjani, Chelsea wana shida kubwa ya mashambulizi, wanatengeneza nafasi lakini hawafungi.

Msimu huu kwenye mashindano yote, wamefunga mabao 53 pekee. Mfungaji wao bora ana mabao 14 pekee katika mechi tano zilizopita hawajafunga hata bao moja kisha unatarajia kuwania ubingwa ngumu sana

Itakuwa kinaya kubwa iwapo Chelsea haitashiriki michuano ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao licha ya kuwa wao ndio klabu bingwa duniani kwa sasa.

Kwa kifupi timu haijengwi na pesa pekee bali ni muongozo imara na kwa sasa vigogo hawa wa zamani hawana uwiano, hawana utambulisho na hawana msimamo thabiti.

Lakini inasemekana kuwa kurukaruka kwa maharagwe sufuriani ndiko kuiva kwake, labda hivi karibuni Chelsea itarejea tena kwenye ubora wake.